Nav bar

Jumatano, 27 Agosti 2025

UTAFITI WA WINGI WA SAMAKI ZIWA TANGANYIKA UMEANZA RASMI

Na. Stanley Brayton, WMUV

 Kigoma 

Agosti 27, 2025

Nchi zilizopo ukanda wa Ziwa Tanganyika ambazo ni Tanzania, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi, zimezindua rasmi zoezi la Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki katika Ziwa Tanganyika, ambao zoezi hilo linalenga kutambua wingi wa mazao ya Uvuvi katika Ziwa hilo.

Akizungumza katika Hafla ya Uzinduzi wa Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki Ziwa Tanganyika, leo Agosti 27, 2025 Mkoani Kigoma, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede amesema Serikali imeelekeza kufanya Tathmini ya wingi wa Samaki waliopo katika Ziwa Tanganyika ili kujua wametawanyikaje na kwenye maeneo yapi, pamoja na kujua Takwimu sahihi za wingi wa Samaki katika Ziwa hilo.

“Utafiti huu utahusisha mazao ya Uvuvi aina ya Migebuka, Dagaa au Samaki wanaoelea wa tabaka la juu, ili kusaidia uwekezaji wenye tija kwa takwimu na kuvutia wawekezaji.” ameseama Dkt. Mhede

Aidha, Dkt. Mhede ameweka bayana kuwa zoezi hilo halifanywi tu kwa ajili ya kuandika ripoti, bali kwa ajili ya ushahidi wa kusaidia katika uundaji wa Sera, ikiwemo kujua namna ya kuendeleza Ziwa, kuhifadhi Ziwa na Rasilimali zake au matumizi ya Rasilimali hizo.

Vilevile, Dkt. Mhede amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imejipanga kikamilifu kwa kuandaa Wataalamu wa kutosha ili kuhakikisha Utafuti huo unakamilika kwa mafanikio.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh amesema, katika miaka ya Tisini Tanzania ilifanya Utafiti kama huo, na kubaini kuwa wingi wa Samaki ulikuwa ni Tani 303,645, na kwamba ongezeko la watu, mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la nguvu ya Uvuvi uenda ndio vimefanya mazao hayo kupungua kutokana na uhitaji kuongezeka zaidi.

Prof. Sheikh amesema tangu wakati huo hakuna tathmini kama hiyo ya kikanda iliyofanyika kutokana na uhaba wa rasilimali, na mwaka 1995, Tanzania ilikadiriwa kuwa tani 157,493, na iIdadi hiyo ilipungua hadi tani 144, 690 kwa mwaka 2022, na baadae ilipungua zaidi hadi tani 84,094 katika utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI).

Halikadhalika, Prof. Sheikh, amesema suala la kufanya Utafiti wa wingi wa Samaki katika Ziwa Tanganyika utasaidia kujua idadi ya Samaki waliopo katika Ziwa, ili kuweka Mipango mathubuti ya Usimamizi  wa Rasilimali za Uvuvi na kuhakikisha uendelevu. 

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimerei amesema Mafunzo ya Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki katika Ziwa Tanganyika  yamefanyika kwa siku kumi, ikijumuisha kuweka sawa mitambo ya kufanyia Utafiti na kuandaa Mpango kazi wa Utafiti huo.

Pia, Dkt. Kimerei ameweka bayana kuwa Watafiti waliopata Mafunzo wataondoka kesho kwenda Burundi kwa ajili ya kuanza kazi hiyo ya Utafiti.

Dkt. Kimerei amesema Utafiti huu ni muhimu kwani unasaidia katika kuhuisha Takwimu za wingi na mtawanyiko wa Samaki katika Ziwa Tanganyika na kuwezesha Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wanachama wa nchi za Ziwa Tanganyika kuweka Mikakati Madhubuti ya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Ziwa hilo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, akihutubia wadau wa Sekta ya Uvuvi, wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki Ziwa Tanganyika, Agosti 27, 2025, Kigoma.

Mkurugenzi wa Uvuvi - Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh, akielezea hali ya Utafiti ya wingi wa Samaki katika miaka ya nyuma, wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki Ziwa Tanganyika, Agosti 27, 2025, Kigoma.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimerei, akikaribisha wadau wa Sekta ya Uvuvi na kutoa Muhtasari wa Jumla wa Tathmini ya Hifadhi ya Samaki Kanda ya Ziwa Tanganyika, wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki Ziwa Tanganyika, Agosti 27, 2025, Kigoma.

Afisa Uvuvi Mwandamizi ambaye ni Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Bw. Martin Van der Knaap, akielezea juu ya Utafiti wa wingi wa Samaki Ziwa Tanganyika, wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki Ziwa Tanganyika, Agosti 27, 2025, Kigoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (wa pili kulia), akitoa Cheti kwa mmoja wa washiriki wa Warsha ya Mafunzo, wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki Ziwa Tanganyika, Agosti 27, 2025, Kigoma.

Picha ni baadhi ya wadau wa Sekta ya Uvuvi wakiwa katika Hafla ya Uzinduzi wa Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki Ziwa Tanganyika, Agosti 27, 2025, Kigoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (wa pili kulia), akielezewa namna Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki Ziwa Tanganyika unavyofanyika, wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki Ziwa Tanganyika, Agosti 27, 2025, Kigoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (alivaa suti nyeusi), akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa Sekta ya Uvuvi, wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki Ziwa Tanganyika, Agosti 27, 2025, Kigoma.






ELIMU YA ULINZI WA RASILIMALI ZA UVUVI YAFIKA RORYA

Na, Hamisi Hussein, Rorya - MARA

Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi  kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Kimansa  Bugomba amesema ulinzi wa rasilimali za sekta ya uvuvi utasaidia kuongeza upatikanaji wa mazao ya uvuvi  na kuchochea uchumi wa wananchi na  pato la Taifa.

Akitoa elimu ya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi kwa ukanda wa Ziwa Victoria Agosti 26, 2025, kwa Wavuvi na wachakataji wa mazao ya uvuvi katika Mwalo wa Isegere uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara Bw. Bugomba  amesema wajibu wa kulinda rasilimali za uvuvi ni jambo shirikishi baina ya wadau na serikali kutokana na umuhimu wake kiuchumi.

"Wizara yetu kwa mwaka 2025/2026  katika vipaumbele tulivyonavyo ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi kwa kutumia teknolojia, ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi, kwa hiyo 

sisi serikali na nyie wadau wa uvuvi tunawajibika kulinda rasilimali hizo ili sote tunufaike kiuchumi" alisema Bugomba.

Awali, akiwa Ofisini Kwake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Dkt. Khalfanis Ilekizemba aliiambia timu ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa sekta ya uvuvi inachangia shilingi bilioni 1.8  kwenye mapato ya halmashauri na kuahidi kuiunga mkono Wizara hiyo  juu ya ulinzi na usimamizi wa rasilimali hiyo.

"Tunashukuru Wizara kuendelea kuelimisha juu ya ulaji wa samaki kwa jamii zetu na sisi tutatoa ushirikiano kuanzia kwenye ulinzi wa rasilimali za Uvuvi, na kuhimiza watu wetu wale samaki".alisema Dkt. Ilekizemba.

Akiwa kwenye Mwalo huo wa Isegere  Mfawidhi wa Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kituo cha Mkoa wa Mara Bw. Yohana Mirumbe aliwambia wavuvi, wamiliki wa vyombo vya uvuvi na wadau wote wanahusika katika mnyororo wa thaman wa sekta ya uvuvi kuzingatia sheria na taratibu za ukataji wa leseni na matumizi sahihi ya zana za uvuvi ili kuondokana na uvuvi haramu.

Alisema kuna baadhi ya wavuvi hutumia nyavu zinazoruhusiwa kisheria lakini wanazitumia kuvua maeneo yasiyoruhusiwa akitolea mfano kutumia wavu wa kuvulia dagaa kwenda kuvulia samaki aina ya Sangara akisisitiza kuwa ni kosa kisheria.

Naye Afisa Uvuvi Mkuu  ambaye anasimamia udhibiti ubora na masoko (QC) mkoani Mara Bw. Mkinze  Rajabu alielezea vigenzo vya ubora wa mazao ya uvuvi yanakidhi ushindani wa soko ambapo aliwaelimisha wadau wa uvuvi njia za kudhibiti ubora na jinsi ya kuongeza thaman ya Mazao ya Uvuvi.

Baadhi ya wavuvi na wachakataji wa mazao ya uvuvi katika mwalo  huo wameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutoa elimu hiyo pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuiomba serikali kuongeza jitihada za ufutiliaji na  usimamizi wa sheria za uvuvi  ili kutokomeza uvuvi haramu katika ukanda wa Ziwa Victoria.

Kaimu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Kimansa Bugomba akitoa mafunzo ya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi  na udhibiti wa uvuvi haramu Ukanda wa Ziwa Victoria kwa wadau wa uvuvi  wa Mwalo wa Isegere uliyopo  Rorya, Mkoani Mara Agosti 26, 2025.

Kaimu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Kimansa Bugomba akitoa mafunzo ya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi  na udhibiti wa uvuvi haramu Ukanda wa Ziwa Victoria kwa wadau wa uvuvi  wa Mwalo wa Isegere uliyopo  Rorya, Mkoani Mara Agosti 26, 2025.

Kaimu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Kimansa Bugomba (Watatu, Kulia) akimwelezea Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya  Dkt. Khalfanis Ilekizemba ( Wakwanza, Kushoto) Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2025/2026 wakati wa utoaji mafunzo ya kudhibiti uvuvi haramu kwa wadau wa uvuvi  wa Mwalo wa Isegere uliyopo  Rorya, Mkoani Mara Agosti 26, 2025.

Mfawidhi wa Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Mkoa wa Mara Bw. Yohana Mirumbe akitoa mafunzo  juu ya umuhimu wa kuzingatia  Zana za Uvuvi zinazokubarika kisheria na athari za uvuvi haramu  Ukanda wa Ziwa Victoria kwa wadau wa uvuvi  wa Mwalo wa Isegere uliyopo  Rorya, Mkoani Mara Agosti 26, 2025.



Jumatatu, 25 Agosti 2025

ELIMU YA ULINZI WA RASILIMALI ZA UVUVI ZIWA VICTORIA YAANZA KUTOLEWA KWA WAVUVI

Na. Hamis Hussein

Timu ya Watalam wa Udhibiti Ubora na Masoko ya Mazao ya Uvuvi (QC) na Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza utoaji wa elimu ya Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi, Uhifadhi bora wa Mazao ya Uvuvi na Umuhimu wa ulaji wa mazao ya Uvuvi  kwa wadau wa sekta ya uvuvi Ukanda wa Ziwa Victoria ili kudhibiti uvuvi haramu na kulinda rasilimali zilizopo ndani ya ziwa hilo.

Timu hiyo ilianza utoaji elimu hiyo  kwa wadau hususan  Wavuvi na Wachakataji wa mazao ya uvuvi  Agosti 23, 2025  katika mialo ya Wilaya za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza mara baada ya kikao kazi cha kujadili mikakati ya pamoja ya kudhibiti uvuvi haramu ukanda wa Ziwa Victoria.

Akizungumza katika Mwalo wa Kayenze Kubwa uliopo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza Afisa Uvuvi Mwandamizi Bw. Hamprey Tilla aliwahimiza wavuvi kufuata sheria za uvuvi na kuuunga mkono jitihada za serikali kwa kuwa mabalozi na wadau muhimu katika kutafuta mikakati ya pamoja ya kudhibiti uvuvi haramu.

"Ndugu zangu sisi tunaongezeka lakini ziwa haliongezeki, tufuate sheria lakini sote kwa pamoja, nyie wavuvi, serikali na wadau wengine wote tunawajibu wa kulinda rasilimali hizi ndani ya ziwa letu"

Kwa upande wake Afisa Uvuvi Mkuu Bi. Gedrude Migodela aliwahimiza wadau hao wa uvuvi juu umuhimu wa matumizi ya miundombinu bora ya kuhifadhia mazao ya Uvuvi ili yaweze kukidhi vigenzo vya kimaabara  kabla ya kuingizwa sokoni.

"Ni muhimu tukatumia njia bora kuhifadhi mazao yetu kwa sababu mazao haya yakipelekwa maabara yakibainika kuwa na changamoto zitokanazo na uhifadhi wake yatakosa soko" alisema Bi Migodela.

 Akiwa kwenye Mwalo wa Shadi Wilayani Nyamagana Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Kudhibiti na Kusimamia Rasilinali za Uvuvi (FRP) Mwanza  Bw. Hamad Stima aliwahimiza wadau wa uvuvi katika eneo hilo juu ya umuhimu wa utunzaji wa rasiliamli za uvuvi kwa ajili kulinda uchumi na afya za wananchi.

Pia, timu hiyo iliwakumbusha na kuwahimiza wadau hao juu ya umuhimu wa ulaji wa mazao ya uvuvi ambapo Afisa Uvuvi Mwandamizi Bi. Grace Kakama alisema familia nyingi  za wavuvi zimekuwa hatuzitumii mazao ya uvuvi kama sehemu ya chakula chao kwa ajili protini.

Baadhi ya Wavuvi waliuliza maswali mbalimbali wakati wakipokea elimu hiyo kutoka kwa wataalam wa wizara na kuiomba serikali kufanya sensa ya wavuvi wote nchini kujua idadi yao ili waweze kupangiwa maeneo maalum  ya kufanya shughuli za uvuvi, kupunguza idadi ya boti  ikiwa ni sehemu ya maoni yao kuhusu utunzaji wa rasilimali za Uvuvi kwenye ziwa hilo.

Zoezi la utiaji elimu hiyo linaendelea leo Agosti 24, 2025 kwa mialo iliyopo Wilaya Ukerewe kwa Mkoa wa Mwanza na  kisha mialo ya Mkoa wa Mara na Simiyu.

Nahodha Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi  Bw. Dickson Stoah akitoa elimu ya Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi katika Ukanda wa Ziwa Victoria  wakati wa timu ya Wataalam ilitembelea Mwalo wa Kayenze Kubwa Ilemela Jijini Mwanza Agosti 23, 2025.

Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi  Bw. Hamphrey Tillia  akitoa elimu ya umuhimu wa kufuata Sheria za Uvuvi katika Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi katika Ukanda wa Ziwa Victoria  wakati wa timu ya Wataalam ilipotembelea Mwalo wa Kayenze Kubwa Ilemela Jijini Mwanza  Agosti 23, 2025.

Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi  Bi. Getrude Migodela  akitoa elimu ya Uhifadhi Bora wa Mazao ya Uvuvi na Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi katika Ukanda wa Ziwa Victoria  wakati wa timu ya Wataalam ilipotembelea Mwalo wa Kayenze Kubwa Ilemela Jijini Mwanza  Agosti 23, 2025.

Wadau wa Uvuvi katika Mwalo wa Kayenze wakisikiliza kwa makini  elimu ya Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi katika Ukanda wa Ziwa Victoria, Uhifadhi Bora wa Mazao ya Uvuvi na Umuhimu wa Ulaji wa Mazao ya Uvuvi iliyokuwa ikitolewa na timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilipotembelea Mwalo huo Jijini Mwanza  Agosti 23, 2025.

Mdau wa Uvuvi katika Mwalo wa Kayenze akiuliza masuali  na kutoa maoni wakati wa Wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakitoa elimu ya Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi katika Ukanda wa Ziwa Victoria, Uhifadhi Bora wa Mazao ya Uvuvi na Umuhimu wa Ulaji wa Mazao ya Uvuvi wakati wa timu ya Wataalam ilipotembelea Mwalo wa Kayenze Kubwa Ilemela Jijini Mwanza  Agosti 23, 2025.

Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi  Bi. Grace Kakama akitoa elimu ya Uhifadhi Bora wa Mazao ya Uvuvi na Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi katika Ukanda wa Ziwa Victoria  wakati wa timu ya Wataalam ilipotembelea Mwalo wa Shadi, Nyamagana  Jijini Mwanza  Agosti 23, 2025.







MIFUGO NA UVUVI YAIONESHA UBABE ARDHI

Na. Stanley Brayton, WMUV

Dodoma 

Agosti 20, 2025

⬛  Yaipiga Ardhi kipigo cha goli 3-1 bila huruma 

⬛ Kamba Wanaume yawatoa povu Ardhi, yashinda mivuto yote miwili, huku wanawake washinda kwa mvuto moja 

⬛  Mpira wa Pete wanawake washinda kwa goli 16-7


Wizara ya Mifugo na Uvuvi yaibuka kidedea Maandalizi ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) kwa kuipiga Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi goli 3-1, mechi ambayo imechezwa katika Viwanja vya Kilimani, leo Agosti 23, 2025.

Ambapo magoli ya upande wa Mifugo na Uvuvi yalifungwa na wachezaji Hema Mugenyo (1), Joseph Onesmo (2) kwa kipindi cha kwanza, na kwa upande wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kipindi cha kwanza goli lilifungwa na mchezaji Cleophace Simon.

Aidha, Mifugo na Uvuvi imeibuka kidedea mbele ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa Wanaume kushinda mivutano yote miwili na wanawake kushinda kwa mvuto mmoja huku mvuto mmoja watoshana nguvu.

Vilevile, kwa upande wa Mpira wa Pete, wanawake Wizara ya Mifugo na Uvuvi yaishinda Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi goli 16-7.

Picha ni wachezaji wa Kamba wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi  kwa upande wa Wanawake wakiwa kwenye mstari kabla ya kusalimiana na Mgeni Rasmi, wakati wa BONANZA la Maandalizi ya SHIMIWI, yaliofanyika katika Viwanja vya Kilimani, Agosti 23, 2025 Dodoma.

Picha ni wachezaji wa Kamba wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa upande wa Wanaume wakiwa tayari kwa ajili ya kuvuta kamba, wakati wa BONANZA la Maandalizi ya SHIMIWI, yaliofanyika katika Viwanja vya Kilimani, Agosti 23, 2025 Dodoma.

Picha ni wachezaji wa mpira wa miguu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiwa kwenye picha ya pamoja kabla ya kuanza mechi dhidi ya Wizara ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wakati wa BONANZA la Maandalizi ya SHIMIWI, yaliofanyika katika Viwanja vya Kilimani, Agosti 23, 2025 Dodoma.

Picha ni wachezaji wa Mpira wa Pete Wizara ya Mifugo na Uvuvi upande wa wanawake wakiwa kwenye mchuano dhidi ya Wizara ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wakati wa BONANZA la Maandalizi ya SHIMIWI, yaliofanyika katika Viwanja vya Kilimani, Agosti 23, 2025 Dodoma.


BI. KABYEMERA AWATAKA WANAMICHEZO KUINGIA KAMBINI KABLA YA KWENDA SHIMIWI

Na. Stanley Brayton, WMUV

Dodoma 

Agosti 23, 2025

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Lucy Kabyemera, amewataka wanamichezo wa Wizara wanaoshiriki Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) kuweka kambi mapema ili kuweza kujiandaa vizuri katika michuano hiyo ya SHIMIWI ili kuweza kuleta makombe na Mataji na kuongeza sifa ya Wizara.

Amezungumza hayo leo Agosti 23, 2025, kwenye Uwanja wa Kilimani Mkoani Dodoma, wakati wa BONANZA la kujiandaa na Michuano ya SHIMIWI.

Aidha, Bi.Kabyemera amewataka wanamichezo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wanamichezo wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kudumisha Umoja na ushikamano katika kuhakikisha mazoezi yanafanyika vizuri na kwa uweledi ili kuibuka vinara katika michuano hiyo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Lucy Kabyemera, akizungumza na kuwapa nasaha wanamichezo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wanamichezo wa Wizara ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kabla ya kufanya Ufunguzi wa Bonanza la kujiandaa na Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI), yaliyofanyika katika Viwanja vya Kilimani, Agosti 23, 2025 Dodoma.

Wanamichezo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wanamichezo wa Wizara ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Lucy Kabyemera, kabla ya kufanya Ufunguzi wa Bonanza la kujiandaa na Michezo ya, yaliyofanyika katika Viwanja vya Kilimani, Agosti 23, 2025 Dodoma.


WADAU WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUDHIBITI UVUVI HARAMU ZIWA VICTORIA

Na Hamisi Hussein - Mwanza.

Serikali Kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema ulinzi wa rasilimali za uvuvi katika ukanda wa Ziwa Victoria ni suala linalohitaji ushirikiano wa pamoja baina yake na wadau wote wanaohusika kwenye mnyororo wa thamani wa  sekta ya uvuvi.

Akizungumza wakati wa Kufungua Kikao cha kujadili mikakati ya kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi kwa ukanda wa Ziwa Victoria  kilichofanyika Ukumbi wa Nyakahoja  jijini Mwanza Agosti 22, 2025 Naibu  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Edwin Mhede alisema wadau wa sekta ya uvuvi kwa kushirikiana  na serikali kuhakikisha uvuvi haramu unadhibitiwa kwa kuja na mikakati ya pamoja ikiwemo elimu.

“Ni lazima tuungane na kuwa na mikakati ya pamoja kupiga vita vitendo hivi. Sio jukumu la Serikali Kuu pekee; ni wajibu wa kila mdau wa sekta hii wakiwemo wavuvi, wachakataji, wasafirishaji, wamiliki wa viwanda vya zana  za uvuvi, wauzaji na wasambazaji wa zana za uvuvi pamoja na Serikali za mitaa. Ni ukweli usiopingika kuwa samaki hawa wakitoweka, hakuna hata mmoja atakayesalia katika biashara ya samaki na mazao ya uvuvi” alisema Dkt. Mhede Aliwahimiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uvuvi Tanzania Prof. Mohammed Sheikh amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza matumizi ya teknolojia za kulinda rasilimali za Uvuvi ikiwemo mitambo ya  kuhifadhi mazao ya uvuvi.

"Kipindi cha masika asilimia 40 ya mazao ya uvuvi hupotea, kwa sasa tumeanza kuja na mitambo ya kisasa ya kuhifadhi mazao ya Uvuvi yasipotee, pia boti za uvuvi tutaziwekea vifuatilizi kwa ajili ya usalama wa maisha ya wavuvi na rasilimali zake", Alisema Prof. Sheikh.

Kwa upande  wake Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Peter Kasele alisema mkoa huo unashirikiana na wataalamu wa Wizara kwa kufanya doria pamoja na kutoa elimu .

Baadhi wa wadau wa sekta ya Uvuvi wakiwemo wavuvi, wachakataji, wasafirishaji, wamiliki viwanda vya zana za uvuvi wamesema udhibiti wa uvuvi haramu utafanikiwa iwapo serikali itasimamia sheria za uvuvi pamoja ulimishaji kufanyika kwa njia ya vyombo vya habari ambapo elimu hiyo ianishe jinsi uvuvi haramu utakavyowaathiri  serikali iendelee ujadili mikakati ya pamoja ya kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya uvuvi katika ukanda wa Ziwa Victoria .

Aidha kwa Mwaka 2024/2025 jumla ya tani 528,750.09 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.42 za mazao y Uvuvi zilivunwa kati ya hizo, tani 486,789.21 zenye thamani ya Shilingi trilioni 3.41 zilivunwa kutoka kwenye Maji ya asili na tani 43, 497.95 zenye thamani ya shilingi bilioni 12.25 zilitokana na ukuzaji viumbe maji.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede akifungua Kikao cha wadau wa sekta ya uvuvi cha kujadili mikakati ya pamoja ya kudhibiti uvuvi haramu ukanda wa ziwa victoria kilichofanyika Ukumbi wa Nyakahoja, Jijini Mwanza Agosti 22, 2025.

Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Peter Kasele akieleza jinsi mkoa huo unavyoshirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufanya doria na kutoa elimu kwa wavuvi ili kukabiliana na uvuvi haramu wakati wa kikao cha wadau wa sekta ya uvuvi cha kujadili mikakati ya pamoja ya kudhibiti uvuvi haramu ukanda wa ziwa victoria kilichofanyika Ukumbi wa Nyakahoja, Jijini Mwanza  Agosti 22, 2025.

Mkurugenzi wa Uvuvi Nchini Prof. Mohammed Sheikh akielezea hali ya uzalishaji wa mazao ya uvuvi na jitihada za Wizara ya Mifugo na Uvuvi kudhibiti uvuvi haramu wakati wa kikao cha wadau wa sekta ya uvuvi cha kujadili mikakati ya pamoja ya kudhibiti uvuvi haramu ukanda wa ziwa victoria kilichofanyika Ukumbi wa Nyakahoja, Jijini Mwanza Agosti 22, 2025.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede (KatiKati, waliokaa) akiwa katika Picha ya Pamoja na Wadau wa sekta ya Uvuvi mara baada ya kumalizika kwa kikao cha wadau wa sekta ya uvuvi cha kujadili mikakati ya pamoja ya kudhibiti uvuvi haramu ukanda wa ziwa victoria kilichofanyika Ukumbi wa Nyakahoja, Jijini Mwanza Agosti 22, 2025.






Ijumaa, 22 Agosti 2025

MHE. DKT. KIJAJI AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA BANDARI YA UVUVI KILWA MASOKO

Na. Omary Mtamike

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametembelea na kukagua hatua mbalimbali za ujenzi wa Bandari ya Uvuvi unaoendelea Kilwa Masoko mkoani Lindi Agosti 21,2025 kama inavyoonekana pichani chini👇👇👇









CHANJA ZENYE THAMANI YA MILIONI 117 ZATOLEWA KWA WAVUVI KILWA

Na. Omary Mtamike

◼️ Zina uwezo wa kukausha tani 3.7 za dagaa kwa siku

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) imewawezesha wavuvi wa dagaa waliopo eneo la Kilwa Kivinje mkoani Lindi Chanja 40 za kisasa za kuanikia dagaa zenye thamani ya shilingi Mil. 117.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi chanja hizo iliyofanyika Agosti 21,2025  Wilayani Kilwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa tukio hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali unaolenga kuondokana na changamoto ya upotevu wa mazao ya Uvuvi baada ya kuvunwa na kuhakikisha dagaa zinazovuliwa kwenye eneo hilo zinakaushwa kwenye mazingira yanayozingatia usalama wa chakula.

“Natambua kuwa hapo awali dagaa mnaovua hapa walikuwa wakiharibika kutokana na kukaushiwa kwenye miundombinu isiyo rafiki na wakati mwingine walikuwa wakikutwa na mchanga au matope jambo ambalo mbali na kupunguza thamani ya mazao hayo sokoni lilikuwa likihatarisha afya za walaji hivyo hatua hii itamaliza changamoto hizo zote” Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.

Aidha Mhe. Dkt. Kijaji amewataka wanufaika wa miundombinu hiyo kuhakikisha wanaitunza na kuitumia kama ilivyokusudiwa ili iweze kuwanufaisha kwa muda mrefu zaidi na kukidhi malengo ya kutolewa kwake.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack ameishukuru Serikali na Shirika la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa kuwawezesha wavuvi wa mkoa wake miundombinu hiyo ambapo mbali na kuahidi kusimamia matumizi yake amewataka wavuvi hao kuhakikisha wanakuza uchumi wao kupitia chanja hizo.

“Ndoo moja ya dagaa wabichi sasa inauzwa kati ya shilingi elfu 40 hadi elfu 45 na dagaa wavuvi wetu wanauza kwenye nchi za Rwanda, Congo na Burundi hivyo hatukuwa na tatizo la soko bali ilikuwa namna ya kuongeza thamani ya mazao yetu jambo ambalo leo limeanza kushughulikiwa kupitia ugawaji wa chanja hizi” Ameongeza Mhe. Telack.

Mbali na Chanja hizo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha mazingira ya shughuli za Uvuvi nchini ikiwa ni pamoja na kujenga masoko na maghala ya kuhifadhia samaki, vyumba vya kuhifadhi ubaridi, mitambo ya kuzalisha samaki na teknolojia za ukaushaji wa mazao ya uvuvi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto)akifungua turubai linalotumika kulinda ubora wa dagaa wakati wa mvua muda mfupi kabla ya kukabidhi chanja za kisasa za kuanikia dagaa kwa wavuvi wa dagaa waliopo Kilwa mkoani Lindi Agosti 21,2025. Kulia anayeshuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede akiwaeleza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack (katikati) namna nyavu za kisasa za kuanikia dagaa zinavyoweza kulinda ubora wa mazao hayo muda mfupi kabla  Mhe. Dkt. Kijaji hajazikabidhi kwa wavuvi wa dagaa waliopo Kilwa Kilivinje Agosti 21, 2025.

Pichani juu ni chanja za kuanikia dagaa zilizokuwa zinatumiwa na Wavuvi wa Kilwa Kivinje hapo awali na chini ni chanja za Kisasa walizopewa Wavuvi hao Agosti 21,2025.