Nav bar

Alhamisi, 29 Aprili 2021

MIFUGO YA TANZANIA YAHITAJIKA VIETNAM NA WAZIRI NDAKI AWAALIKA WAVIETNAM KUFUGA SAMAKI

Na. Edward Kondela

 

Balozi wa Vietnam nchini Tanzania Mhe. Nguyen Nam Tien amesema atawasilisha serikalini vigezo vinavyopaswa kufuatwa na wafanyabishara wa hapa nchini ili waweze kusafirisha mifugo na nyama kwenda nchini Vietnam, kutokana na nchi hiyo kuwa na uhitaji mkubwa wa nyama.

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amebainisha hayo leo (28.04.2021) ofisini kwake katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, mara baada ya kuwa na mazungumzo mafupi na balozi huyo aliyefika ofisini kwa Waziri Ndaki ili kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam na kupeana uzoefu katika sekta za mifugo na uvuvi.

 

Mhe. Ndaki amesema Balozi Tien amesema nchi ya Vietnam ina uhitaji mkubwa wa nyama kwa kuwa wana ng’ombe wasiozidi Milioni Sita hivyo kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa hiyo endapo watakidhi vigezo vya kusafirisha mifugo na nyama nchini humo.

 

“Tunaweza kutumia fursa hii kusafirsha ng’ombe au nyama na kwamba wataleta orodha ya vitu vinavyohitajika ili kama nchi tuweze kupeleka ng’ombe au nyama.” Amesema Mhe. Ndaki

 

Aidha, Waziri Ndaki amewaomba wawekezaji kutoka Vietnam kuwekeza hapa nchini katika viwanda vya maziwa kwa kuwa maziwa yaliyopo bado ni mengi kulinganisha na viwanda vilivyopo, pamoja na kuwekeza katika viwanda vya kuchakata ngozi za mifugo kwa kuwa kiasi kikubwa cha ngozi kimekuwa kikiharibika.

 

Kuhusu Sekta ya Uvuvi, Waziri Ndaki amesema amemuomba Balozi wa Vietnam hapa nchini Mhe. Nguyen Nam Tien kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini humo ili kuja kuwekeza katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na mabwawa kwa kuwa nchi hiyo inafanya vizuri katika sekta hiyo.

 

Amefafanua kuwa lengo la serikali ya Tanzania ni kuwekeza zaidi katika ufugaji wa samaki ili idadi ya samaki wanaopatikana kwa njia ya maji ya asili kwa maana ya kwenye Bahari ya Hindi, maziwa na mabwawa iweze pia kupatikana kwa njia ya ufugaji wa kutumia vizimba na mabwawa.

 

“Tumewaomba kupata utaalamu wao wa ufugaji samaki, lakini pia kama tunaweza kupata wawekezaji kutoka kwao, tuna fursa kubwa na kama wizara tunataka tupate samaki nusu wanaotoka kwenye maji ya asili na nusu wengine wapatikane kwa njia ya kufuga.” Amesema Mhe. Ndaki.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akifafanuliwa jambo na Balozi wa Vietnam nchini Tanzania Mhe. Nguyen Nam Tien, wakati balozi huyo alipofika katika ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ili kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam. (28.04.2021)


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa Vietnam nchini Tanzania Mhe. Nguyen Nam Tien, wakati balozi huyo alipofika katika ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ili kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam. Katika mazungumzo yao Balozi Tien amewakaribisha wafanyabiashara wa Tanzania kusafirisha mifugo na nyama nchini Vietnam kutokana na nchi hiyo kuwa na uhitaji mkubwa wa nyama. (28.04.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiagana na Balozi wa Vietnam nchini Tanzania Mhe. Nguyen Nam Tien, wakati balozi huyo alipofika katika ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ili kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam ambapo katika Sekta ya Uvuvi, Waziri Ndaki amemuomba Balozi Tien kuwakaribisha wawekezaji kutoka Vietnam ili waje hapa nchini kuwekeza katika ufugaji wa samaki wa kutumia vizimba na mabwawa kutokana na nchi ya Vietnam kufanya vizuri katika sekta hiyo. (28.04.2021)

UVUVI HARAMU KUDHUBITIWA BWAWA LA MUNGU

Serikali kwa kushirikiana na wadau imepanga kudhibiti Uvuvi haramu kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo Mkoani Kilimanjaro.

 

Haya yamesemwa na Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah leo (28.04.2021) baada ya kumalizika kwa kikao cha ujirani mwema kilichojadili kuhusu ulinzi na usimamizi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu. Kikao hicho kiliwajumuisha Viongozi na Wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wilaya za Mwanga, Moshi na Simanjiro kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Kindoroko wilayani Mwanga.

 

Dkt. Tamatamah amesema kupitia kikao hicho wamejadili kwa kina kuhusu tatizo la Uvuvi haramu unaofanyika kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu na kutoka na maazimio ambayo Wizara na Halmashauri zilizoshiriki pamoja na wadau watakwenda kuyasimamia utekelezaji wake lengo likiwa ni kudhibiti shughuli za uvuvi haramu katika bwawa hilo. Moja ya maazimio hayo ni pamoja na udhibiti wa uuzwaji wa samaki wadogo kwenye masoko yanayosimamiwa na halmashauri.

 

“Samaki wadogo wanavuliwa pasipo halali na huwa wanauzwa kwenye masoko ambayo yapo chini ya halmashauri, hivyo tumekubaliana wote kuwa baada ya siku saba halmashauri zihakikishe samaki hao hawauzwi tena katika masoko na hii itasaidia kuwafanya wavuvi kupunguza au kuacha kuvua samaki hao kwa kuanza kukosa wanunuzi,” alisema Dkt. Tamatamah.

 

Dkt. Tamatamah amesema sera ya uvuvi ya mwaka 2015 imekasimu majukumu ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi kwa serikali kuu kwa maana ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya TAMISEMI kupitia Halmashauri na majukumu mengine yamekasimiwa kwa wavuvi na wadau wengine.

 

Vilevile amesema kuwa Wizara inayojukumu la kutunga sera, sheria na kanuni lakini TAMISEMI kupitia halmashauri zinaowajibu wa kuzisimamia na kuhakikisha kwamba utekelezaji wake unafuatwa. Lakini kwa upande wa wavuvi wanaowajibu wa kushiriki katika ulinzi shirikishi wa rasilimali za uvuvi kwa kuwa wao ndio wanufaika wa kwanza.

 

Mkutano huo umewahusisha wadau wa pande zote kwa maana ya wizara, halmashauri na wadau ili kuwa na mkakati wa pamoja badala ya kila mmoja kuwa na mkakati wake kuhusu udhibiti wa uvuvi haramu na kuhakikisha rasilimali za uvuvi kwenye bwawa la Nyumba ya Mungu zinalindwa na kusimamiwa.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Thomas Apson amesema moja ya changamoto iliyojitokeza katika udhibiti wa uvuvi haramu ni kwamba kila wilaya ilikuwa ikifanya doria kwa wakati wake hivyo wavuvi wakiona doria inafanyika katika wilaya moja wanakimbilia kwenye wilaya nyingine. Lakini kutokana na makubaliano ya kikao, sasa utawekwa utaratibu mzuri wa doria zinazofanyika ili kutotoa tena nafasi kwa wavuvi kufanya uvuvi haramu.

 

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mhe. Zephania Chaula amesema moja ya changamoto iliyopo ni ya uingizwaji wa zana haramu za uvuvi kupitia mipakani. Hivyo ameziomba mamlaka zinazohusika kuhakikisha zana hizo hazipitishwi kwani hiyo ni moja ya njia ya kudhibiti uvuvi haramu hapa nchini.

 

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Emmanuel Bulayi amesema kwamba wizara inaendelea kuwahamasisha wavuvi kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili waweze kuunganishwa na taasisi za fedha kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ambazo zipo tayari kuwakopesha na hivyo wataweza kununua zana sahihi na zenye ubora kwa ajili ya kufanyia shughuli za uvuvi.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na wajumbe wa Kikao cha ujirani mwema (hawapo pichani) kilichojadili kuhusu usimamizi shirikishi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu ambacho kimejumuisha Viongozi na Wataalam kutoka Wizara na Halmashauri za Wilaya ya Mwanga, Moshi Vijijini na Simanjiro. Kikao kimefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Kindoroko wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro. (28.04.2021)


Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi (aliyesimama) akifafanua jambo wakati wa Kikao cha ujirani mwema kilichojumuisha Viongozi na Wataalam kutoka Wizara, Halmashauri za Wilaya ya Mwanga, Moshi Vijijini na Simanjiro kuhusu usimamizi shirikishi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu ikiwa ni pamoja na udhibiti wa uvuvi haramu. Kikao kimefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Kindoroko wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro. (28.04.2021)

Baadhi ya Viongozi na Wataalam kutoka Wizara na Halmashauri za Wilaya ya Mwanga, Moshi Vijijini na Simanjiro wakisikiliza mada kwenye Kikao cha ujirani mwema kilichojadili kuhusu usimamizi shirikishi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu. Kikao kimefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Kindoroko wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro. (28.04.2021)


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) akisaini kitabu cha wageni kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mwanga wakati alipofika wilayani hapo kushiriki kikao cha ujirani mwema kilichojadili kuhusu usimamizi shirikishi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Thomas Apson na kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi. (28.04.2021)


Jumatatu, 26 Aprili 2021

SERIKALI YAMALIZA MGOGORO WA ARDHI BAINA YA WANANCHI NA NARCO

Na Mbaraka Kambona, Kigoma

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameielekeza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kutenga Ekari Elfu Kumi na Tano (15000) na wazigawe kwa Wananchi wa Vijiji viwili vya Mpeta na Chakulu vilivyopo Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma ili kutatua mgogoro wa ardhi wa muda mrefu baina ya wananchi hao na Kampuni hiyo.

 

Ndaki alitoa maelekezo hayo Aprili 25, 2021 katika ziara yake Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma kwa lengo kutatua mgogoro huo wa ardhi kufuatia wananchi wa vijiji hivyo kuvamia maeneo ya Ranchi ya Uvinza na kuishi humo kinyume na taratibu.

 

Akiongea na wananchi wa vijiji hivyo kwa nyakati tofauti, Waziri Ndaki alisema kuwa Serikali imeamua kufikia maamuzi hayo ili wananchi hao waweze kujikita katika shughuli za maendeleo na kuachana na migogoro ya kila siku ambayo haina tija yoyote.

 

“Hatupendi tuendelee na migogoro kwenye maeneo yetu, tunataka tumalize migogoro ili tuanze kufanya shughuli za maendeleo, kila mwananchi afanye shughuli yake bila bughudha yoyote,” alisema Ndaki

 

Aliongeza kuwa baada ya ugawaji wa maeneo hayo kukamilika Mkuu wa Wilaya ya Uvinza na timu yake watakwenda kufanya tathmini katika maeneo hayo na kuyafanyia mchakato wa kuyarasimisha ili kuwa Kijiji au Kitongozi.

 

Alisisitiza kuwa pamoja na wananchi hao kuvunja Sheria, Serikali imeangalia maslahi mapana na ndio maana imeamua kutoa sehemu ya eneo katika ranchi hiyo ili wananchi hao waweze kuishi kwa utulivu na kuendelea na shughuli zao huku akiwaonya kuwa wasijaribu tena kuingia katika ranchi hiyo baada ya kugawa ekari hizo na atakayefanya hivyo anatafuta kesi.

 

 

“Ranchi ni eneo la kufugia mifugo na sio eneo la kuishi watu au kulima humo, atakayejaribu kuingia tena ananitafuta kesi, tumewapa maeneo hayo ili mkae humo, atakayetaka kufuga aje sisi tutampa eneo la kukodisha kwa bei ya Serikali ili aweze kufuga kisasa, kulima malisho na kuongeza tija ya mifugo yake,” alisisitiza Ndaki

 

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mwanamvua Mrindoko baada ya kumshukuru Waziri Ndaki kwa uamuzi huo naye aliwasisitiza wananchi hao kutoendelea kuvamia maeneo ya ranchi hiyo ili kuepukana na migogoro isiyo na tija na badala yake watumie maeneo hayo waliyopewa kujiletea maendeleo yao.

 

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chakulu, Mohamed Baswage aliishukuru Serikali kwa tamko hilo la kuwapa eneo wananchi wa Kijiji hicho huku akisema kuwa uamuzi huo utawasaidia wao kusukuma maendeleo yao kwa pamoja wakishirikiana na Serikali.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akiagana na mmoja kati ya Wazee wanaoishi katika Kijiji cha Mpeta aliyejitokeza kuhudhuria mkutano wa Waziri huyo na Wananchi wa Kijiji hicho uliofanyika Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma Aprili 25, 2021. Katika Mkutano huo, Waziri Ndaki aliamua Ekari zaidi ya Elfu Nane ( 8000) zimegwe kutoka katika Ranchi ya Uvinza ili wakabidhiwe wananchi wanaoishi katika eneo la Mwandulubhantu lililopo katika kijiji cha Mpeta ili wazitumie  kwa makazi na shughuli nyingine za maendeleo.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mpeta ambapo alieleleza  kuwa zaidi ya  Ekari  Elfu Kumi na Nne (14000) zitegwe kutoka katika Ranchi ya Uvinza na zigawiwe kwa wananchi wanaoishi katika eneo la Mwandulubhantu na Kazaroho  ili wazitumie kwa makazi na shughuli nyingine za kimaendeleo. Waziri Ndaki  alitembelea Wilaya ya Uvinza iliyopo Mkoani Kigoma Aprili 25, 2021na kufanya maamuzi hayo kwa lengo la kumaliza mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya wananchi hao na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akiongea na Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Masele Shilagi muda mfupi baada ya kusikiliza maombi ya Wananchi wa Kijiji cha Chakulu waliovamia  maeneo ya Ranchi ya Uvinza ambapo Waziri Ndaki alielekeza kiasi cha Ekari Elfu Tano (5000) zitengwe kutoka katika Ranchi  hiyo na zigawiwe  kwa wananchi  wanaoishi katika eneo la Kazaroho lililopo katika kijiji cha Chakulu  ili wazitumie kwa makazi na shughuli nyingine za maendeleo. Waziri Ndaki alitoa maelekezo hayo alipofanya ziara Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma Aprili 25, 2021.


Wananchi wa Kijiji cha Mpeta wakiagana kwa furaha na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati kulia) muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa Waziri huyo na Wananchi wa Kijiji cha Mpeta uliofanyika Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma Aprili 25, 2021.




ULEGA ATAKA KUCHANGAMKIWA KWA SOKO LA KAA NA JONGOO BAHARI!

Na. Edward Kondela

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewataka wananchi wanaofanya shughuli zao katika Ukanda wa Bahari ya Hindi kuchangamkia fursa ya ufugaji viumbe maji wakiwemo kaa na jongoo bahari ambao wamekuwa na soko kubwa nje ya nchi.

 

Akizungumza mwishoni mwa wiki (24.04.2021) katika Kijiji cha Tawalani kilichopo kata ya Manza iliyopo Wilaya ya Mkinga, Mkoani Tanga, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani humo, Mhe. Ulega amesema Ukanda wa Bahari ya Hindi bado haujatumiwa vyema katika kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hivyo wananchi kujikita zaidi katika uvuvi na kutojishughulisha na ufugaji wa viumbe maji ambao wamekuwa wakitakiwa nchi mbalimbali.

 

Mhe. Ulega amebainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekuwa akizungumzia sana Sekta ya Uvuvi kuwekeza kwenye uchumi wa bluu, hivyo wananchi hususan wanaofanya shughuli za uvuvi wanatakiwa kuongeza wigo wa shughuli za kiuchumi katika Ukanda wa Bahari ya Hindi zikiwemo za ufugaji wa viumbe maji hususan kaa na jongoo bahari pamoja na kilimo cha zao la mwani.

 

“Shughuli za uchumi ziwe nyingi sana, rais anataka twende na uchumi wa bluu, anataka tufanye kazi twende baharini tufanye kazi lakini huku pwani tutengeneze vizimba kwa ajili ya shughuli mbalimbali mfano kunenepesha kaa na majongoo bahari na tufunge Kamba kwa ajili ya kulima mwani.” Amesema Mhe. Ulega

 

Ameongeza kuwa ni wakati sasa kwa wananchi wa ukanda huo kuondoa umasikini kwa kuendeleza shughuli za uvuvi, ufugaji wa viumbe maji pamoja na kilimo cha mwani ili waweze kuongeza mapato na kuwa na wigo mpana zaidi wa kuongeza kipato kwa mwaka.

 

Akisoma taarifa ya Kikundi Shirikishi cha Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) mwishoni mwa wiki (24.04.2021) katika Kijiji cha Tawalani, katibu wa kikundi hicho Bw. Salehe Ally Sua amesema katika kipindi cha miezi kumi wamepata tani 52 za mwani na kuziuza kwa Shilingi Milioni 52 ambapo kwa sasa wamefanikiwa kupata soko la uhakika ambalo wanauza Shilingi 1,250 kwa kilogramu moja.

 

Aidha, amesema kupitia kilimo hicho kipato cha mtu mmoja mmoja kimeweza kuongezeka na kujikomboa kiuchumi hali ambayo imewasaidia kujipatia maendeleo na kumudu mahitaji mbalimbali ya kijamii.

 

Licha ya mafanikio hayo Bw. Sua amesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya mabadiliko ya hali ya hewa ambayo imekuwa ikiharibu zao hilo na kupanda na kushuka kwa bei ya zao mwani katika masoko mbalimbali hali ambayo inawafanya wakulima kushindwa kuweka mipango stahiki ya kilimo hicho pamoja na ukosefu wa vifaa kwa ajili ya kilimo hicho.

 

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Ulega amesema wizara itatoa Shilingi Milioni Nne kwa ajili ya kununua kamba za kilimo cha mwani na kuelekeza fedha au kamba zenye thamani ya hiyo pesa ziwasilishwe haraka katika kikundi hicho.

 

Amesema fedha hizo ziwe chachu kwa ajili ya kukuza kilimo hicho na kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi itazidi kutoa misaada mbalimbali kwa vikundi vinavyojishughilisha na kilimo cha zao la mwani kwa kutoa vifaa zikiwemo kamba ili kuongeza uzalishaji wa zao la mwani hali ambayo pia inaweza kuchochea uwepo wa viwanda vya kuzalisha bidhaa zitokanazo na mwani.

 

Akiwa katika ziara hiyo ya kikazi ya siku moja Mkoani Tanga, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ametoa msaada wa injini mbili za boti kwa ajili vikundi vya uvuvi vya Upendo Beach Group na Songambele.

 

Injini hizo zenye thamani ya shilingi Milioni 30 ambapo kila moja ina thamani ya Shilingi Milioni 15, Naibu Waziri Ulega amewataka wavuvi hao kutotumia vifaa hivyo kwa kujiingiza katika uvuvi haramu bali watumie kwa ajili ya uvuvi unaofuata sheria na kanuni na kwamba serikali bado inaendelea kuweka mazingira mazuri ya uvuvi kwa kuondoa tozo ambazo zimekuwa kero kwao.

 

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa injini hizo, viongozi wa vikundi hivyo wamesema wamefurahishwa na msaada huo ambao utakuwa na tija kwao katika kuongeza kiwango cha uvuvi na kutumia muda mfupi baharini na kuwataka wavuvi wengine kujiunga katika ushirika ili waweze kupata misaada mbalimbali kutoka kwa wadau ikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kulia) akiwa ameshikana mkono na Mwenyekiti wa kikundi cha Upendo Beach Bw. Mzee Makole, wakati Naibu Waziri Ulega akikabidhi msaada wa injini ya boti yenye thamani ya Shilingi Milioni 15 kwa ajili ya kukiimarisha kikundi hicho kwenye shughuli za uvuvi. Naibu Waziri Ulega amekabidhi msaada huo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi akiwa nje ya jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga wakati alipofika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella na kwanza kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mhe. Ummy Mwalimu. (24.04.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kulia) akiwa ameshikana mkono na Mwenyekiti wa kikundi cha ushirika Songambele Bw. Selemani Haruna Kuzu kilichopo Wilayani Mkinga wakati akimkabidhi msaada wa injini ya boti yenye thamani ya Shilingi Milioni 15 kwa ajili ya kukiimarisha kikundi hicho kwenye shughuli za uvuvi. Naibu Waziri Ulega amekabidhi msaada huo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi akiwa nje ya jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga wakati alipofika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella. (24.04.2021)

Katibu wa Kikundi Shirikishi cha Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika Kijiji cha Tawalani, kilichopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga Bw. Salehe Ally Sua akifafanua jambo juu ya zao la mwani kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella na Katibu Tawala wa mkoa huo Bi. Judica Omari, wakati Naibu Waziri Ulega alipofika katika kijiji hicho kuhamasisha kilimo cha zao la mwani na kutoa ahadi ya wizara ya kutoa msaada wa Shilingi Milioni Nne kwa ajili ya kununulia kamba maalumu ya kupandia zao hilo ambazo ameagiza zifike katika kikundi hicho ndani ya muda mfupi. (24.04.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na baadhi ya wananchi (hawapo pichani) wanaofanya shughuli zao katika Ukanda wa Habari ya Hindi kuchangamkia fursa ya ufugaji viumbe maji wakiwemo kaa na jongoo bahari ambao wamekuwa na soko kubwa nje ya nchi. Naibu Waziri Ulega alikuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Tawalani kilichopo kata ya Manza iliyopo Wilaya ya Mkinga, Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani humo. (24.04.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Viumbe Maji Baharini kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (aliyevaa suti nyeusi) Dkt. Hamisi Nikuli kuhakikisha anaharakisha mchakato wa kufikisha Shilingi Milioni Nne au kamba maalum kwa ajili ya kilimo cha mwani zenye thamani ya fedha hiyo kwa Kikundi Shirikishi cha Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika Kijiji cha Tawalani, kilichopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga ikiwa ni mchango wa Wizara ya Mifugo na Uvu kuhakikisha kilimo cha mwani kinakuwa na tija zaidi. (24.04.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Viumbe Maji Baharini kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (aliyevaa suti nyeusi) Dkt. Hamisi Nikuli kuhakikisha anaharakisha mchakato wa kufikisha Shilingi Milioni Nne au kamba maalum kwa ajili ya kilimo cha mwani zenye thamani ya fedha hiyo kwa Kikundi Shirikishi cha Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika Kijiji cha Tawalani, kilichopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga ikiwa ni mchango wa Wizara ya Mifugo na Uvu kuhakikisha kilimo cha mwani kinakuwa na tija zaidi. (24.04.2021)


Jumapili, 25 Aprili 2021

ULEGA - “MKIRUHUSU MIFUGO IPITE NJIA ZA PANYA NCHI ITAKOSA MAPATO”

Na. Edward Kondela

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewataka wananchi wa Kijiji cha Horohoro Kijijini Kata ya Duga katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, kutoruhusu mifugo ipitishwe kinyemela mpakani kwenda nchi jirani badala yake wawafichue wanaofanya hivyo ili kuwadhibiti kwani serikali inakosa mapato.

 

Mhe. Ulega aliyasema hayo mwishoni mwa wiki (24.04.2021) wakati alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo kwa kutembelea eneo lenye ekari 23 ambapo kutajengwa mnada wa mifugo kijijini hapo na kusema kuwa mnada huo utakuwa chachu ya kuinua maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

 

Alisema lazima wananchi wilayani hapo kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri wa kudhibiti mifugo kupitishwa kinyemela kwenda nje ya nchi ili kuiwezesha serikali kukusanya mapato hatua ambayo itakuwa ni chachu kubwa kwao kuwezesha maendeleo.

 

“Niwaambie tu kwamba lazima hivi sasa tujipange kwa ujio wa fursa za mnada huu kwani baada ya miaka miwili eneo hili litakuwa na picha tofauti na ilivyokuwa hapo awali na litafungua ukurasa mpya wa maendelea kwenye eneo lenu na tumekubaliana wizarani jambo hilo litaanza mwezi wa tano, wazee wa duga mtupe ushirikiano kwa vijana wetu ambao watakuja kufanya kazi hapa.“ Alisema Mhe. Ulega

 

“RC Shigella utakuwa umeacha alama kwa hili na nyinyi wananchi RC ametoa rai mnada huo usigeuke kuwa ni dude ambalo litakuwa limekaa halina shughuli za kufanya watu wanapitisha mifugo njia za panya na nyie mnawaona na hamtoi taarifa kuzuia jambo hilo.” Alifafanua Mhe. Ulega

 

Naibu Waziri huyo alisema mnada huo ukianza kufanya kazi, eneo hilo litakuwa na shughuli mbalimbali ambazo zitawasaidia kuwaingizia vipato mbalimbali vya kimaendeleo hali ambayo itasaidia kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

 

“Lakini niwaambie kwamba mkiacha watu wanapitisha mifugo kwa njia ya panya hakuna nchi inachokipata na wananchi hamuwezi kupata chochote hapo ni sehemu nzuri ya kuhakikisha mnapaombea na kupiga dua, sala tuweze kuinua uchumi wetu watu wa Mkinga.” Alisema

 

Aidha alisema mnada huo utaanza mwezi Mei mwaka huu, huku akiwataka wakazi wa eneo la Kata ya Duga kuwapa ushirikiano watumishi ambao watapelekwa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo ya kuhakikisha wanakusanya ushuru wa serikali.

 

Aliwataka pia wafugaji wa eneo hilo kuhakikisha wanafuga kisasa ili waweze kuwa na ng’ombe wenye tija zaidi kutokana na kwamba watanzania wapo kwenye mazingira mazuri ya kufuga kisasa tofauti na nchi nyingine.

 

“Mhe. Rais wetu Samia Suluhu Hassan anataka kuona ng’ombe wenye kilo 500 diwani wa Kata ya Duga na wengine tunataka tukimbie mchakamchaka tufikie lengo la Rais anataka kuona tunauza nyama inatupa tija, mfugaji anabadilika anapata kipato na nchi inapata mapato ya kutosha.” Alisema.

 

Naibu Waziri huyo alisema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella alibainisha kuwa mkoa unataka kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo lakini hayo yote hayawezi kufanikiwa ikiwa baadhi ya watu wanapitisha ng’ombe kwenda nje ya nchi kinyemela kwa kutumia njia zisizo rasmi.

 

Alifafanua kuwa ili kuongeza mapato ya serikali kupitia mifugo, katika mwaka ujao wa fedha 2021/2022 Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga kutumia Shilingi Bilioni 4 na Milioni 400 kwa ajili ya kujenga minada mbalimbali nchini ukiwemo wa Kijiji cha Horohoro Kijijini kata ya Duga katika Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga.

 

Alisema ujenzi huo unatokana na takwa la kisheria la magonjwa ya wanyama namba 17 ya mwaka 2003 ambayo inataka kufanyika hayo huku akieleza kuwa wizara ina mipango mingi ya kuhakikisha wanawasaidia wafugaji kuhusu sehemu za malisho.

 

Awali akizungumza katika eneo hilo la mnada Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella alisema moja ya tatizo kubwa lililopo eneo la mpakani ni kutokuwa na mnada wa uhakika kwa ajili ya wafanyabiashara na wafugaji wa mifugo, ndiyo maana serikali ya Mkoa wa Tanga na Wizara ya Mifugo na Uvuvi zinataka kusiwe na ufugaji wa kuhamahama.

 

Mhe. Shigella alisema hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa bungeni hivi karibuni,  ameeleza nia yake ya kutaka kuona wafugaji matajiri na siyo wa kuhamahama na ili kuweza kujenga mazingira wezeshi ya eneo la kuuzia mifugo kwani bila kufanya hivyo, wafanyabiashara  wamekuwa wakienda kuwalangua wafugaji kwenye mazizi yao  na hivyo kujikuta hawanufaiki ipasavyo.

 

“Kuna soko kubwa nchini Kenya ambapo baadhi ya wafugaji na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu walikuwa wanasafirisha mifugo kwenda Kenya na baadhi ya watumishi wa serikali wasiokuwa waaminifu ndio walikuwa wanaongoza mchakato huo wa kusafirisha mifugo bila kupitia kwenye taratibu mahsusi zilizopo.” Alisema Mhe. Shigella

 

Hata hivyo alisema anaishukuru wizara kwa kuliona hilo na kuunda  kamati na kuweza kubaini  uwepo wa changamoto walizokuwa wanalalamikia wafanyabiashara na wananchi wa Kijiji cha Horohoro Kijijini kwani kubwa walilokuwa nalo ni mifugo kupitishwa kwenye njia isiyokuwa rasmi, kutokana na kutokuwa na eneo maalumu ambalo mifugo kabla haijasafirishwa inatakiwa ipumzishwe mahali ambapo itakaguliwa magonjwa na kukusanywa kwa tozo kabla ya kusafirishwa kwenda nchi jirani.

 

Kwa upande wake Afisa Biashara wa Minada kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Basil Mataba alisema wizara ina jumla ya minada ya upili 14 na minada 11 ya mpakani ambapo mnada wa Kijiji cha Horohoro Kijijini mara utakapoanza kufanya kazi utakuwa wa 12.

 

Bw. Mataba alisema wanategemea Mwezi Mei mwaka huu mnada wa Kijiji cha Horohoro Kijijini utaanza kufanya kazi hivyo kuondoa adha ambazo walikuwa wakizipata wafanyabiashara na wafugaji kutorosha mifugo kwenda nje ya nchi ili kuuza mifugo yao.

 

Alibainisha hadi sasa eneo hilo la mnada tayari shughuli mbalimbali zinaendelea ikiwemo ya kufyeka nyasi na tayari kibanda cha kukusanyia ushuru kimeshasimikwa wakati wakiendelea na ujenzi wa eneo hilo huku akieleza kwamba wizara itaendelea na hatua za ununuzi wa vifaa kwa ajili ya uzio wa awali.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akifafanua juu ya ujenzi wa mnada wa Kijiji cha Horohoro Kijijini katika Kata ya Duga iliyopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, kwa mkuu wa mkoa huo Mhe. Martine Shigella na katibu tawala wa mkoa Bi. Judica Omari. (24.04.2021)



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa kwanza kulia) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella pamoja na viongozi wengine wa mkoa huo, wakati Naibu Waziri Ulega alipotembelea eneo unapowekwa mnada wa mifugo katika Kijiji cha Horohoro Kijijini kilichopo kata ya Duga Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga na kuwataka wafanyabiashara na wafugaji kutotorosha mifugo kwenda nje ya nchi kwa njia zisizo rasmi kwani serikali inapoteza mapato. (24.04.2021)


Muonekano wa kibanda cha ushuru kilichosimikwa katika eneo la mnada wa Kijiji cha Horohoro Kijijini uliopo Kata ya Duga Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga ambapo shughuli mbalimbali zinaendelea ikiwemo ya kufyeka nyasi. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ametembelea eneo hilo na kusisitiza kuwa mnada huo utaanza kufanya kazi Mwezi Mei mwaka huu. (24.04.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Kulia), Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Thobias Mwilapwa wakibadilishana mawazo, mara baada ya Naibu Waziri Ulega kufika katika ofisi za mkuu wa mkoa huo kabla ya kuanza ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Tanga. (24.04.2021)


SERIKALI KUJA NA MKAKATI ENDELEVU KUDHIBITI UVUVI HARAMU

Na Mbaraka Kambona, Kigoma

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo katika mpango wa kuwa na mkakati endelevu wa kudhibiti uvuvi haramu na kuachana na utaratibu wa kuendesha oparesheni za muda mfupi.

 

Ndaki alisema hayo wakati akiongea na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi ulipo katika Ziwa Tanganyika Mkoani Kigoma Aprili 24, 2021.

 

Akiongea na wavuvi hao Ndaki alisema kuwa lengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuwa na udhibiti wa uvuvi haramu ambao utakuwa endelevu utakaoshirikisha wahusika wenyewe wanaofanya shughuli za uvuvi na viongozi wa eneo husika kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya hadi Mkoa.

 

“Tunataka kuja na mkakati endelevu wa namna ya kudhibiti uvuvi haramu, tuusike sote, kuanzia Wataalamu, Viongozi wa ngazi zote na wananchi wanaohusika na uvuvi wenyewe,” alisema Ndaki huku akiongeza kuwa

 

“Uvuvi haramu unatishia rasilimali zetu za uvuvi, tusiulee, tuwashirikishe wahusika ili waone kuwa uvuvi haramu ni kitu kisichokubalika”.

 

Kwa Mujibu wa Ndaki anasema walichokigundua katika mkakati wa kutumia oparesheni za muda mfupi ni kwamba matokea yanakuwa ya muda mfupi na operesheni hizo zikiisha matukio ya uvuvi haramu yanaendelea tena kwa sababu operesheni hizo zinahusisha wataalamu kutoka Wizarani na sio wahusika wenyewe wa eneo husika.

 

‘‘Ulinzi wa rasilimali za uvuvi sio jukumu la watu wa makao makuu peke yake, ni jukumu letu sote, tuone umuhimu wa kutunza rasilimali zetu na wote tukubaliane kuwa uvuvi haramu haukubaliki na tukikukamata sheria itachukua mkondo wake,” alisisitiza Ndaki

 

Kuhusu baadhi ya viongozi wanaolalamikiwa kuhusika na vitendo vya uvuvi haramu alisema kuwa kiongozi au mtaalamu yeyote mwenye dhamana ya masuala ya uvuvi atakayepatikana kuhusika na vitendo vya uvuvi haramu na yeye atakuwa haramu na atashughulikiwa kama wahalifu wengine.

 

Aliongeza kuwa kiongozi yeyote aliyepewa dhamana ya kusimamia masuala ya uvuvi na eneo lake linafanya uvuvi haramu, wataanza kumchukulia hatua huyo kiongozi na wengine wote watakaokuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine kwa kutokuwajibika kwao.

 

Ndaki alisema kuwa hatalegeza nati hasa linapokuja suala la uvuvi haramu na kuwataka wananchi na viongozi wa ngazi zote kushirikiana kwa pamoja kupiga vita uvuvi haramu huku akiwahimiza kuwafichua wale wote wanaohusika na vitendo vya uvuvi haramu katika maeneo yao.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiongea na Wavuvi wa Mwalo wa Kibirizi ambapo alisema kuwa Serikali ipo katika mipango ya kuandaa mkakati shirikishi na endelevu wa kupambana na uvuvi haramu nchini. Ndaki alifanya Mkutano na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi uliopo Mkoani  Kigoma. (24.04.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akijadiliana jambo na Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) Katika Mkutano wa Waziri huyo na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akisisitiza jambo wakati akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi katika Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Wavuvi hao uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Magese Bulayi akiongea na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi wakati alipokuwa akijibu baadhi ya Maswali yaliyoulizwa na wavuvi hao katika Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Wavuvi uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Mstahiki Meya, Manispaa ya Kigoma Mjini, Baraka Lupoli akiongea na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi wakati wa Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Wavuvi hao uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Sehemu ya Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi wakifuatilia matukio yanayoendelea  katika Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki na Wavuvi hao uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng'enda akiongea na Wavuvi wa Mwalo wa Kibirizi katika Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Baadhi ya Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi waliojitokeza kumsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (hayupo pichani) katika Mkutano baina ya Waziri huyo na Wavuvi wa Mwalo wa Kibirizi uliofanyika leo Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Mchakataji Mazao ya Uvuvi, Prisca Steven akitoa kero zinazowashumbua Wachakataji wa Mazao ya Uvuvi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) katika mkutano wa waziri huyo na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika mwalo wa Kibirizi uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)





Jumamosi, 24 Aprili 2021

TALIRI YATAKIWA KUFANYA TAFITI ZITAKAZOLETA TIJA SEKTA YA MIFUGO.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), kufanya tafiti zitakazo lisaidia taifa kupiga hatua kupitia sekta ya mifugo.

 

Prof. Ole Gabriel, aliyasema hayo wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya jiji  Mkoani Dodoma Aprili 23, 2021.

 

Akizungumza na Wajumbe wa baraza hilo Prof. Ole Gabriel alisema  kuwa, hakuna Taasisi nyingine ambayo Wizara hiyo inaweza kuitegemea katika suala la utafiti zaidi ya TALIRI, hivyo ni lazima ifanye tafiti zitakazo boresha sekta ya mifugo nchini na kuchangia pato la taifa.


“Tusibakie kujisifu tuu kuwa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa idadi kubwa ya mifugo lazima tujisifie kwa namna tutavyoweza kutumia sekta hii kukuza uchumi wa taifa” alisema Prof. Ole Gabriel

 

Alisema kuwa tafiti ndizo zinaweza kulisadia taifa kutoka hapa lilipo na kupiga hatua kufikia nchi ambazo zimefanikiwa katika sekta ya mifugo.

 

“Kama Rais alivyokuwa akitoa hotuba yake bungeni alisema ng'ombe wetu akichinjwa nyama yake haiwezi kuzidi kilo 150 hii yote ni kutokana  na kutokuwa na utafiti wa mbegu bora ambazo zitaweza kutoa kiasi cha kutosha cha nyama” alisema Prof. Ole Gabriel

 

Aidha alisema kuwa, TALIRI inatakiwa kufanya tafiti ya mbegu bora za ngombe ili kuwa na uhakika wa nyama ya kutosha pamoja na maziwa.

 

“Lazima sekta hii ya mifugo tui ‘link’ na Tanzania ya viwanda hivyo basi tunatakiwa kuhakikisha kuwa ng'ombe wetu wanatoa nyama ya kutosha na iliyo bora, maziwa mengi, ngozi, pembe pamoja na kwato” alisema Prof. Ole Gabriel

 

Kadhalika alisema kuwa kama sekta ya mifugo itashindwa kuwa na bidhaa zitokanazo na mazao ya mifugo bora, hata malighafi kwa ajili ya viwanda hazita kidhi viwango.

 

Aliongeza kuwa ni wakati sasa kwa Taasisi hiyo kukaa mguu sawa silaha begani ili kuzalisha mifugo bora na kukuza sekta ya mifugo.

 

Vile vile, aliiagiza TALIRI kuhakikisha wanakuwa wabunifu katika kuangalia changamoto mpya zinazohusu wafugaji   ili kuzifanyia kazi mara moja.

 

Kwa upande  wake Mwenyekiti  wa baraza hilo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Dk. Jonas Kizima, alisema kuwa kikao hicho ni cha pili kwa baraza hilo na moja ya kazi yake ni kupitia bajeti yake.

 

“Pamoja na kupitia bajeti pia mweshimiwa Katibu Mkuu tutakuwa na maazimio ambayo tutayaandika na kukuletea wewe ikiwa ni sehemu ya utekelezaji alisema Kizima.

 

Kwa upande wao Wajumbe wa baraza la wafanyakazi TALIRI wamemshukuru Katibu Mkuu (Mifugo) kwa kuweza kufika na kushiriki nao na  kuahidi kuwa wamepokea maelekezo yake na watahakikisha wanayafanyia kazi na kuyasimamia vizuri Ili kuongeza tija na ufanisi katika kazi zao za kitafiti.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiongea na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) (hawapo pichani) wakati wa kikao cha baraza la wanyakazi hao kulichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. (23.04.2021)

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi, Dkt. Jonas Kizima (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa Taasisi hiyo na watumishi kutoka WMUV mara baada ya kikao cha Baraza la Wafanyakazi kulichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. (23.04.2021)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akisalimiana na watumishi wa Wizara pamoja na watumishi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kufungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TALIRI. (23.04.2021)