Na Mbaraka Kambona, Kigoma
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba
Ndaki amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo katika mpango
wa kuwa na mkakati endelevu wa kudhibiti uvuvi haramu na kuachana na utaratibu
wa kuendesha oparesheni za muda mfupi.
Ndaki alisema hayo wakati akiongea na
Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi ulipo katika Ziwa
Tanganyika Mkoani Kigoma Aprili 24, 2021.
Akiongea na wavuvi hao Ndaki alisema
kuwa lengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuwa na udhibiti wa uvuvi haramu
ambao utakuwa endelevu utakaoshirikisha wahusika wenyewe wanaofanya shughuli za
uvuvi na viongozi wa eneo husika kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya hadi
Mkoa.
“Tunataka kuja na mkakati endelevu wa
namna ya kudhibiti uvuvi haramu, tuusike sote, kuanzia Wataalamu, Viongozi wa
ngazi zote na wananchi wanaohusika na uvuvi wenyewe,” alisema Ndaki huku
akiongeza kuwa
“Uvuvi haramu unatishia rasilimali zetu
za uvuvi, tusiulee, tuwashirikishe wahusika ili waone kuwa uvuvi haramu ni kitu
kisichokubalika”.
Kwa Mujibu wa Ndaki anasema
walichokigundua katika mkakati wa kutumia oparesheni za muda mfupi ni kwamba
matokea yanakuwa ya muda mfupi na operesheni hizo zikiisha matukio ya uvuvi
haramu yanaendelea tena kwa sababu operesheni hizo zinahusisha wataalamu kutoka
Wizarani na sio wahusika wenyewe wa eneo husika.
‘‘Ulinzi wa rasilimali za uvuvi sio
jukumu la watu wa makao makuu peke yake, ni jukumu letu sote, tuone umuhimu wa
kutunza rasilimali zetu na wote tukubaliane kuwa uvuvi haramu haukubaliki na
tukikukamata sheria itachukua mkondo wake,” alisisitiza Ndaki
Kuhusu baadhi ya viongozi
wanaolalamikiwa kuhusika na vitendo vya uvuvi haramu alisema kuwa kiongozi au
mtaalamu yeyote mwenye dhamana ya masuala ya uvuvi atakayepatikana kuhusika na
vitendo vya uvuvi haramu na yeye atakuwa haramu na atashughulikiwa kama
wahalifu wengine.
Aliongeza kuwa kiongozi yeyote
aliyepewa dhamana ya kusimamia masuala ya uvuvi na eneo lake linafanya uvuvi
haramu, wataanza kumchukulia hatua huyo kiongozi na wengine wote watakaokuwa
wanahusika kwa namna moja au nyingine kwa kutokuwajibika kwao.
Ndaki alisema kuwa hatalegeza nati hasa
linapokuja suala la uvuvi haramu na kuwataka wananchi na viongozi wa ngazi zote
kushirikiana kwa pamoja kupiga vita uvuvi haramu huku akiwahimiza kuwafichua
wale wote wanaohusika na vitendo vya uvuvi haramu katika maeneo yao.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akijadiliana jambo na Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) Katika Mkutano wa Waziri huyo na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni