Nav bar

Jumamosi, 31 Desemba 2022

ULEGA AKIZUNGUMZA NA WANANCHI WA KIJIJI CHA MTEPELEA WILAYANI KILWA MKOANI LINDI

 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Mtepela kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, ambapo aliwahimiza kupima, kuyatangaza na kumilikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ya Mifugo ili yaweze kulindwa na kuepusha migogoro ya mara kwa mara. (29/12/2022)

Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza katika kikao cha Kamati ya Mawaziri wa Kisekta Mkoani Lindi. Pamoja na mambo mengine alitoa rai kwa viongozi wa mkoa huo kulinda misitu ambayo imeendelea kuteketezwa na wakulima wa zao la ufuta kwa kuwa jambo hilo lisiposimamiwa ipasavyo litaleta madhara makubwa ya kimazingira. (29/12/2022)

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Angeline Mabula (Mb) (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack na waheshimiwa mawaziri, naibu mawaziri na wakuu wa wilaya. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (wanne waliosimama) pia alishiriki ziara hiyo Mkoani Lindi. (29/12/2022)

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Angeline Mabula (Mb) (wanne kutoka kulia) akiwa na waheshimiwa mawaziri na naibu mawaziri walipofika kwenye Kijiji cha Mtepela Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wapili kutoka kulia) ni miongoni mwa viongozi walioshiriki ziara hiyo. (29/12/2022)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


 

KIKAO CHA KAMATI YA MAWAZIRI WA KISEKTA MKOANI MTWARA

 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Abdallah Ulega (Mb.) akitoa salaam za Wizara wakati wa kikao cha Kamati ya Mawaziri wa Kisekta Mkoani Mtwara Disemba 28, 2022. Pamoja na mambo mengine alisisitiza umuhimu wa kupima, kuyalinda, kuyatangaza na kutoa Hati kwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji.


Sehemu ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta (meza kuu), baadhi ya Wabunge wenyeji na wataalam walipowasili Wilaya ya Nanyumbu - Kijiji cha Mbangara kutatua migogoro ya ardhi Disemba 28,2022.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb.),  akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed(kushoto) muda mfupi baada ya kuwasili Ofisi za Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kikao cha Kamati ya Mawaziri wa Kisekta kuhusu migogoro ya Vijiji 975, Disemba 28,2022.

Sehemu ya Wananchi wa Kijiji cha Mbangara - Mbuyuni Wilaya ya Nanyumbu, Mtwara wakisikiliza kwa makini maelezo ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta kuhusu utatuzi wa Migogoro ya maeneo yao,  Disemba 28, 2022.

Jumanne, 27 Desemba 2022

SAUTI YETU WIKI HII

 


VIFARANGA 62,730 VYAZUILIWA KUINGIA NCHINI

Na Mbaraka Kambona,


Wakaguzi wa Mifugo na Mazao yake kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi walio katika kituo cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wamevizuia vifaranga vya kuku wa mayai 62,730 ambavyo ni mali ya Kampuni ya Phoenix Farms Limited ya Mkuranga, Pwani vilivyofikishwa uwanjani hapo vikitokea nchini Ubeligiji bila ya kuwa na vibali.


Akitoa taarifa ya zuio la vifaranga hivyo wakati akiongea na Waandishi wa Habari jijini Disemba 24, 2022, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga alisema Vifaranga hivyo vilivyowekwa kwenye makasha 697, stakabadhi yake ya mauziano  ya mzigo inaonesha vina gharama ya shilingi 200,262,706.


“Mkurugenzi wa Kampuni pamoja na Wakala wa Mmiliki wa vifaranga hivyo walikiri kutokuwa na kibali cha kuingiza vifaranga hivyo na kwa msingi huo amevunja Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Sura ya 156 na Kanuni za Udhibiti wa Usafirishaji wa Wanyama na Mazao yake ya GN. Na. 28/2007,” alisema Prof. Nonga


Alisema kutokana na tafsiri hiyo vifaranga hivyo vimezuiliwa kuingizwa nchini kwa kuwa ni mzigo hatarishi huku akifafanua kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeutaka uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Tawi la Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam kuielekeza Kampuni ya Phoenix Farms Limited kuvirudisha vifaranga hivyo nchini Ubeligiji kwa sababu vinaweza kuhatarisha usalama wa kuku hapa nchini.


“Vilevile, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kampuni ya Phoenix Farms Limited tunamuelekeza kuviondosha vifaranga hivyo katika maeneo ya uwanja wa ndege na kuvirudisha alikovitoa,”aliongeza


Aidha, alisema kuwa Mwaka 2006 Tanzania iliweka zuio la uingizaji wa kuku na mazao yake kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege duniani na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa salama dhidi ya ugonjwa huo ambao umeathiri nchi nyingi duniani.


Pof. Nonga alitoa wito kwa watanzania wote hususan wadau wa kuku kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo ya kudhibiti kuingia na kuenea kwa magonjwa ya kuku nchini hususan Ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege ili kulinda usalama wa kuku, na ndege wengine pamoja na afya ya jamii ya watanzania kwa ujumla.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga akiwaonesha Waandishi wa habari (hawapo pichani) makasha  yaliyotumiwa kubebea vifaranga 62,730 vilivyoingizwa nchini bila kibali. Akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, Prof. Nonga alitoa tamko la kuzuia vifaranga hivyo visiingie nchini Disemba 24, 2022.

Ijumaa, 23 Desemba 2022

SEMINA KUHUSU MASUALA YA SUMUKUVU YAFANYIKA KWA WAKUU WA IDARA NA VITENGO WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI (SEKTA YA MIFUGO)

 

Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwillawa akiongea na wajumbe (hawapo pichani) wa semina ya wakuu wa Idara wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi masuala yanayohusu  sumukuvu, wakati alipokuwa akifunga semina hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa African Dream, Dodoma 22.12.2022.

Muwasilisha Mada, Dkt. Jamal Kusaga akiwasilisha mada kuhusu hali ya sasa ya sumukuvu nchini, kwenye semina ya kuwapatia wakuu wa Idara wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi masuala yanayohusu sumukuvu, semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa African Dream, Dodoma. 22.12.2022.

Mkufunzi wa chuo cha Kilimo (MATI) cha Ilonga, Ms. Mariam Joseph akiwasilisha mada inayohusu "Njia iliyopendekezwa  ya kuzingatia jinsia wakati wa kudhibiti sumukuvu kwenye Semina ya kuwapitisha wakuu wa Idara masuala yanayohusu Sumukuvu, Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa African Dream, Dodoma. 22.12.2022.

Afisa TEHAMA kutoka sekta ya Mifugo, Bi Priscilla Joseph (aliyesimama) akichangia mada kwenye semina ya wakuu wa Idara wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi masuala yanayohusu Sumukuvu  iliyofanyika katika ukumbi wa African Dream, Dodoma. 22.12.2022.

Sehemu ya wajumbe waliohudhuria semina ya kuwapatia wakuu wa Idara wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi masuala yanayohusu sumukuvu, semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa African Dream, Dodoma. 22.12.2022.


CHANJO DHIDI YA UGONJWA WA HOMA YA MAPAFU YA NG'OMBE

 


MABORESHO YA MWONGOZO WA UWEKEJI HERENI YATAMFIKIA KILA MDAU-NDAKI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.  Mashimba Ndaki amebainisha kuwa Wizara yake inaendelea kufanya maboresho ya Mwongozo unaosimamia zoezi la uwekaji wa hereni za kielektroniki kwenye mifugo ili kufanya zoezi hilo kuwa shirikishi kwa pande zote zinazohusiana na sekta ya ufugaji.


Mhe. Ndaki ameyasema hayo jana (20.12.2022) wakati akifunga mkutano wa Wadau wa sekta ya Mifugo uliofanyika kwa siku mbili kwenye jengo la PSSSF, Makole jijini Dodoma ambapo amebainisha kuwa mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuboresha mwongozo huo utakabidhiwa kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu ili atoe hatma ya zoezi hilo.


“Kwenye maboresho ya mwongozo huu tutamfikia kila mdau anayehusika na sekta ya mifugo kwa nafasi yake ili baada ya kukamilika kwake kusiwe na malalamiko ya baadhi ya wadau kutoshirikishwa” Amesisitiza Mhe. Ndaki.


Mhe. Ndaki ametoa rai kwa wafugaji wote walioshiriki kwenye mkutano huo kuwafikishia wafugaji wenzao elimu waliyoipata kupitia mada mbalimbali zilizowasilishwa wakati wote wa mkutano huo ili waweze kutekeleza kwa pamoja maazimio yaliyofikiwa.


“Ni lazima wote kwa pamoja tuelewe sekta ya Mifugo inapaswa kwenda kwenye mwelekeo mpya, hatuwezi kuwa walewale kwa sababu tunalazimishwa kubadilika sasa hivi kwa namna yoyote ile kutokana na mazingira tuliyopo, mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la watu” Amesema Mhe. Ndaki.


Akizungumzia kuhusu marufuku ya uingizwaji wa vifaranga vya kuku kutoka nje, Mhe. Ndaki amesema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo ili kuwalinda wawekezaji na wafanyaiashara wa ndani ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan zinazolenga kuongeza idadi ya wawekezaji nchini.


“Lakini natoa rai kweu mhakikishe mnaboresha mazao yenu ili yawe shindani kwenye masoko ya ndani na nje kwa sababu hivi sasa tupo kwenye ushirikiano wa Afrika Mashariki na hivi karibuni tutaingia kwenye sarafu moja hivyo ni lazima mjipange” Ameongeza Mhe. Ndaki.


Akizungumzia ubora wa nyama inayozalishwa hapa nchini na namna inavyokubalika katika masoko ya nje, Mkurugenzi wa Kiwanda cha kusindika nyama cha Eliya kilichopo mkoani Arusha Bw. Irfhan Virjee amesema kuwa kwa sasa nyama inayozalishwa hapa nchini na kusafirishwa kwenye masoko ya nje ina ubora na kuhitajika hasa kwenye soko la nchi za falme za kiarabu  kiasi cha kushindwa kukidhi mahitaji ya soko hilo.


Naye Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la kimataifa la Heifer ambao ni moja wa wadau wakubwa kwenye sekta ya Mifugo nchini Bw. Mark Tsoxo amesema kuwa ili kufanikisha  mwelekeo mpya wa sekta ya Mifugo ni lazima Serikali na wadau wote kufanya mabadiliko ya teknolojia na mifumo inayoratibu sekta hiyo.  


“Jambo jingine ni muhimu kuhakikisha kwenye mwelekeo huu mpya wa sekta ya Mifugo tunawajumuisha kwa kiasi kikubwa vijana ambao wanakadiriwa kufikia asilimia 31 ya idadi ya watu wote nchini  na wanawake ambao ni asilimia 51 ya idadi ya watu wote waliopo nchini, kinyume na hapo tutatengeneza changamoto kubwa wakati tukitekeleza mwelekeo huu” Amesisitiza Bw. Tsoxo.


Mkutano huo wa wadau wa sekta ya Mifugo ulifunguliwa Disemba 19 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambapo wadau mbalimbali walioshiriki mkutano huo walifanikiwa kutoa maoni mbalimbali yaliyolenga kutekeleza kauli mbiu ya Mkutano huo ya “ Mwelekeo Mpya wa Sekta ya Mifugo nchini”

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda akifafanua moja ya maazimio yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa wadau wa sekta ya Mifugo uliofanyika Disemba 19-20, 2022 kwenye jengo la PSSSF Makole, jijini Dodoma.


Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Mbaraka Stambuli akisoma maazimio yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa wadau wa sekta ya Mifugo uliofanyika Disemba 19-20, 2022 kwenye jengo la PSSSF Makole, jijini Dodoma.


MAFUNZO REJEA KWA WATAALAM WA MIFUGO


 Afisa Mifugo Mtafiti Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Felister Kimario akizungumzia juu ya uboreshaji wa kosaafu za mbari za mifugo na umuhimu wake katika kukuza sekta ya mifugo wakati wa siku ya pili ya mafunzo rejea ya siku mbili yaliyokuwa yakifanyika katika Mji wa Hai Mkoani Kilimanjaro yakihusisha baadhi ya maafisa ugani kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara. (20.12.2022)



Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi katika Halmashauri ya Mji wa Handeni Mkoani Tanga Bw. Zakaria Swai akifafanua juu ya muhtasari ya yaliyojadiliwa katika siku ya kwanza ya mafunzo rejea ya siku mbili yaliyokuwa yakifanyika katika Mji wa Hai Mkoani Kilimanjaro yakihusisha baadhi ya maafisa ugani kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara. (20.12.2022)


Afisa Mifugo Daraja la Pili kutoka Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) kilichopo Mkoani Arusha Bw. Samwel Kakungu akielezea umuhimu na hatua mbalimbali zinazofuatwa za uhimilishaji na umuhimu wa njia hiyo kwa wafugaji katika kupata mbegu bora za mifugo yao wakati wa siku ya pili ya mafunzo rejea ya siku mbili yaliyokuwa yakifanyika katika Mji wa Hai Mkoani Kilimanjaro yakihusisha baadhi ya maafisa ugani kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara. (20.12.2022)


Afisa Mifugo Msaidizi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Sebastian Shilangila akiwafahamisha maafisa ugani juu ya matumizi ya ugani kiganjani kwa kutumia simu janja pamoja na kompyuta wakati wa siku ya pili ya mafunzo rejea ya siku mbili yaliyokuwa yakifanyika katika Mji wa Hai Mkoani Kilimanjaro yakihusisha baadhi ya maafisa ugani kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara. (20.12.2022)


Afisa Utafiti Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Grace Masolwa akifafanua juu ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ugani kwa kutumia mfumo wa M-Kilimo wakati wa siku ya pili ya mafunzo rejea ya siku mbili yaliyokuwa yakifanyika katika Mji wa Hai Mkoani Kilimanjaro yakihusisha baadhi ya maafisa ugani kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara. (20.12.2022)

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Ugani) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Samwel Mdachi akiwaelekeza baadhi ya maafisa ugani namna ya kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika mfumo wa M-Kilimo na ugani kiganjani kwa kutumia simu janja, wakati wa siku ya pili ya mafunzo rejea ya siku mbili yaliyokuwa yakifanyika katika Mji wa Hai Mkoani Kilimanjaro yakihusisha baadhi ya maafisa ugani kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara. (20.12.2022)

Baadhi ya maafisa ugani kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara wakiwa kwenye mafunzo rejea ya siku mbili yaliyofanyika katika Mji wa Hai Mkoani Kilimanjaro ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa kwao na maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo imeandaa mafunzo hayo ili kuwakumbusha maafisa ugani majukumu yao na namna ya kuwahudumia wafugaji. (20.12.2022)


Afisa Mfawidhi Kanda ya Kaskazini Dkt. Raphael Mwampashi akifafanua juu ya udhibiti wa magonjwa ya mifugo kwa maafisa ugani wakati wa mafunzo rejea ya siku mbili yaliyokuwa yakifanyika katika Mji wa Hai Mkoani Kilimanjaro yakihusisha baadhi ya maafisa ugani kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara. (20.12.2022)

CHANJO DHIDI YA UGONJWA WA HOMA YA MAPAFU YA MBUZI

 


CHANJO DHIDI YA UGONJWA WA KIMETA KWA NG'OMBE, MBUZI NA KONDOO


 

MAJALIWA ATOA DIRA YA KUBORESHA SEKTA YA MIFUGO NCHINI

◼️ Aagiza Msomera kutumika kama darasa la Ufugaji nchini 


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka wadau wa Sekta ya Mifugo kuboresha mifumo ya ufugaji  ili kufanya shughuli hiyo kwa tija ambapo amesisitiza umuhimu wa sekta hiyo kwa Serikali na Mwananchi mmoja mmoja.


Mhe. Majaliwa ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Mifugo uliolenga kujadili mwelekeo mpya wa sekta hiyo nchini  uliofanyika katika moja ya kumbi zilizopo jengo la PSSF jijini Dodoma leo (19. 12.2022).


Mhe. Majaliwa amesema kuwa licha ya kiasi kidogo cha mchango wa asilimia 7 kwenye pato la Taifa unaotolewa na sekta ya Mifugo, bado ushiriki wa wadau kwenye mabadiliko ya kuelekea kwenye ufugaji wa kisasa upo chini hivyo ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanahamasisha zaidi jamii ili  kuboresha Sekta ya Ufugaji ikiwemo kutatua  changamoto  mbalimbali zinazowakumba wafugaji pamoja  na mifugo yenyewe.


“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana mapenzi ya dhati na Sekta ya Mifugo na anatamani kuona inaleta mapinduzi ya kiuchumi kwa kukuza zaidi pato la wananchi, kutoa ajira na kuchangia pato la Taifa bila kuathiri mazingira na maendeleo ya sekta nyingine hivyo ni lazima wafugani waachane na huu utaratibu wa kufuga kwa kuhamahama kwa sababu pia unachangia kwa kiasi kikubwa kupoteza ubora wa nyama, Sisi kule Lindi kiasi kikubwa cha nyama tunayokula huwa haina ubora kwa sababu haiivi vizuri kutokana na mifugo inayopatikana kule kuwa imekomaa sana kwa sababu ya kutembezwa umbali mrefu” Amesema Mhe. Majaliwa.  


Kutokana na dhamira hiyo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Mifugo na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya tathmini ya maeneo ya ufugaji yaliyopo katika maeneo yao na kiasi cha mifugo kinachoweza kufugwa na endapo mifugo itazidi uwezo wa eneo husika, wafugaji waelekezwe kuvuna mifugo yao.


 “Wafugaji wahamasishwe kuvuna mifugo yao kwa wakati ili kuwawezesha kupata bei nzuri sokoni pamoja na kupunguza changamoto za malisho hususan wakati wa ukame. Kwa ujumla kasi ya uvunaji wa mifugo nchini bado ipo chini ya asilimia 10 ikilinganishwa na viwango bora vya uvunaji wa mifugo kitaifa ambavyo ni kati ya asilimia 20 na 25.” Amesisitiza Mhe. Majaliwa


Aidha Mhe. Majaliwa amezielekeza Wizara ya Ardhi na Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe zinashirikiana na wadau wa sekta ya mifugo katika kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya vijiji na kutenga maeneo ya malisho ya pamoja, ranchi za vijiji na vitalu kwa ajili ya wafugaji binafsi ambapo amesisitiza vijiji vyenye ardhi ya kutosha, vitenge maeneo ya Ranchi za Vijiji yenye ukubwa wa kati ya hekta 200 na 500 ambazo zitatumika kwa utaratibu wa kuwapanga wafugaji kutoka ndani ya kijiji husika.


“Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo inamiliki Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ihakikishe maeneo yote ya NARCO yaliyoko kwenye mikoa yetu, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa kwanza mtambue maeneo hayo yanamilikiwa na nani na mjue yapo katika wilaya gani na yana ukubwa upi na je matumizi ni sahihi kama Serikali inaotaka” Amesema Mhe. Majaliwa.


Katika hatua nyingine Mhe. Majaliwa amewataka wafugaji wote nchini kutumia kijiji cha Msomera kama darasa la Ufugaji nchini kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali kwenye shughuli za Ufugaji kijijini hapo.


“Kule Msomera tumepima kabisa maeneo na tumeyagawa kwenye vitalu na mengine tumeyaacha yatumike kwa yule ambaye angependa kuzunguka kidogo na mifugo yake, lakini pia tumeweka miundombinu ya kisasa kabisa ya majosho na mabwawa ya kunyweshea mifugo yenye mabirika ya kutosha huku pia wataalam wakiwatembelea na kutoa  maelekezo kwa wafugaji waliopo pale nini kifanyike kwa mujibu wa kalenda ya ufugaji” Amebainisha Mhe. Majaliwa.


Awali, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki alisema lengo la mkutano huo mbali na  kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya mifugo kujadili kwa kina na uwazi kuhusu mwelekeo mpya wa sekta ya mifugo nchini pia utawajengea uwezo wafugaji ili wafuge kwa tija na kibiashara kama wawekezaji kwenye sekta ya mifugo.


“Sekta ya Mifugo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, hivyo watatumia mkutano huo kujadili namna ya ufugaji bora pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hivyo nina Imani sote tutatoa maoni yetu kwa ukamilifu ili yaweze kutusaidia kutekeleza mabadiliko tunayotarajia” Amehitimisha Mhe. Ndaki 


Mkutano huo unaofanyika kwa siku mbili unalenga kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji ili kuipa fursa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutekeleza kwa ufanisi maeneo 7 yaliyopo kwenye mpango wa mabadiliko ya sekta hiyo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (kulia) akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa wadau wa sekta ya Mifugo tukio lililofanyika leo (19.12.2022) kwenye moja ya kumbi zilizopo jengo la PSSF, Makole jijini Dodoma.

Baadhi ya Wakuu wa Mikoa yenye idadi kubwa ya wafugaji  (mbele) wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa wadau wa sekta ya Mifugo tukio lililofanyika leo (19.12.2022) kwenye moja ya kumbi zilizopo jengo la PSSF, Makole jijini Dodoma.

MAFUNZO REJEA KWA MAAFISA UGANI YATAJWA KUTATUA CHANGAMATO ZA SEKTA YA MIFUGO

Na. Edward Kondela


Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepongezwa kwa kutoa mafunzo rejea kwa maafisa ugani kote nchini ikiwa ni njia mojawapo ya mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo nchini.


Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Mhe. Juma Irando amebainisha hayo leo (19.12.2022) wakati akifungua mafunzo rejea ya siku mbili kwa maafisa ugani kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara ambapo amesema baadhi ya maafisa hao wanaohudhuria mafunzo wanatakiwa kuwashirikisha maafisa wengine pamoja na wafugaji juu ya mafunzo hayo ili sekta ya mifugo iwe na tija zaidi.


Mhe. Irando amesema sekta ya mifugo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali hali inayosababisha baadhi ya wafugaji kutofuga kibiashara hivyo mafunzo rejea yanayotolewa na wizara hiyo yataleta matokeo chanya kwa maafisa ugani ambao wanategemewa kuwahudumia wafugaji.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Bw. David Lekei amesema wafugaji katika wilaya hiyo wameanza kubadilika na kufuga kibiashara kwa kuwashirikisha maafisa ugani ili kuwapatia mafunzo ya ufugaji wenye tija.


Bw. Lekei amesema wafugaji wa Wilaya ya Hai wameanza kutambua juu ya uchaguzi wa mbegu bora za mifugo pamoja na malisho ambayo yatakuwa na matokeo mazuri ya mazao yatokanayo na mifugo yao ikiwemo nyama na maziwa.


Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Ugani) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi amesema lengo la mafunzo rejea kwa maafisa ugani nchini ambapo wizara imepanga kuwafikia maafisa hao 800 kuanzia ngazi ya kijiji, kata na halmashauri katika mwaka huu wa fedha ni kuwajengea uwezo katika utendaji wao wa kazi.

Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Mhe. Juma Irando akizungumza leo (19.12.2022) Mjini Hai, wakati akifungua rasmi mafunzo rejea ya siku mbili kwa baadhi ya maafisa ugani (hawapo pichani) kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara ambapo amesema baadhi ya maafisa hao wanaohudhuria mafunzo wanatakiwa kuwashirikisha maafisa wengine pamoja na wafugaji juu ya mafunzo hayo kwa kuwa ni nia ya serikali kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo nchini. (19.12.2022)

kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Bw. David Lekei akizungumza leo (19.12.2022) Mjini Hai, wakati wa kufunguliwa rasmi mafunzo rejea ya siku mbili kwa baadhi ya maafisa ugani (hawapo pichani) kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara ambapo amesema wafugaji katika wilaya hiyo wameanza kubadilika na kufuga kibiashara kwa kuwashirikisha maafisa ugani ili kuwapatia mafunzo ya ufugaji wenye tija pamoja na kuchagua mbegu bora za mifugo na malisho. (19.12.2022)

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Ugani) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Samwel Mdachi akifafanua juu ya mwendelezo wa jitihada za wizara kuwaongezea uwezo maafisa ugani ili kuwasaidia wafugaji katika kutatua changamoto zinazowakabili, ambapo amesema katika mwaka huu wa fedha wizara imepanga kuwafikia maafisa ugani 800 kote nchini. Bw. Mdachi amebainisha hayo leo (19.12.2022) katika Mji wa Hai, Mkoani Kilimanjaro wakati wa ufunguzi wa mafunzo rejea ya siku mbili kwa baadhi ya maafisa ugani kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara. (19.12.2022)

Afisa Tawala Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. John Kusaja akitoa maelezo ya mambo ya msingi ya kuzingatiwa kwa maafisa ugani wakiwa kwenye mafunzo rejea ya siku mbili yanayofanyika katika Mji wa Hai Mkoani Kilimanjaro yakihusisha baadhi ya maafisa hao kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara. (19.12.2022)

Picha ya pamoja ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Mhe. Juma Irando baada ya kufungua rasmi mafunzo rejea ya siku mbili kwa maafisa ugani kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara. Mafunzo hayo yanatolewa na maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi. (19.12.2022)

CHANJO DHIDI YA UGONJWA WA MDONDO (TEMAVAC)

 


Jumatano, 21 Desemba 2022

MKUTANO WA WADAU WA SEKTA YA MIFUGO

 


MAFUNZO KWA MAAFISA UGANI


 Afisa Tawala Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. John Kusaja akitoa maelezo ya mambo ya msingi ya kuzingatiwa kwa maafisa ugani (hawapo pichani) wakiwa kwenye mafunzo rejea ya siku mbili yaliyofanyika katika Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora yakihusisha baadhi ya maafisa hao kuanzia ngazi ya kata kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma pamoja na wadau wengine kutoka sekta binafsi. (16.12.2022)

Afisa Mifugo Mtafiti Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Felister Kimario akifafanua kwa maafisa ugani waliohudhuria mafunzo rejea ya siku mbili yaliyofanyika katika Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, juu ya kuboresha mbari za mifugo na ufugaji kibiashara. Mafunzo hayo yalihudhuriwa na baadhi ya maafisa ugani kuanzia ngazi ya kata kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma pamoja na wadau wengine kutoka sekta binafsi. (16.12.2022)

Afisa Mifugo Msaidizi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Sebastian Shilangila akiwafahamisha maafisa ugani juu ya matumizi ya mfumo wa M-Kilimo wakati wa mafunzo rejea ya siku mbili yaliyofanyika katika Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, yaliyohudhuriwa na baadhi ya maafisa ugani kuanzia ngazi ya kata kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma pamoja na wadau wengine kutoka sekta binafsi. (16.12.2022)

Afisa Utafiti Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Grace Masolwa akifafanua juu ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ugani kwa maana ya ugani kiganjani wakati wa mafunzo rejea ya siku mbili yaliyofanyika katika Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, yaliyohudhuriwa na baadhi ya maafisa ugani kuanzia ngazi ya kata kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma pamoja na wadau wengine kutoka sekta binafsi. (16.12.2022)

Afisa Mifugo Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Atupele Mohamed akiwaelekeza baadhi ya maafisa ugani namna ya kutumia mfumo wa M-Kilimo na ugani kiganjani kwa kutumia simu janja, wakati wa mafunzo rejea ya siku mbili yaliyofanyika katika Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, yaliyohudhuriwa na baadhi ya maafisa ugani kuanzia ngazi ya kata kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma pamoja na wadau wengine kutoka sekta binafsi. (16.12.2022)

Afisa Mfawidhi kutoka Kituo cha Mifugo Kanda ya Tabora Bi. Adelina Mkumbukwa akiwakumbusha maafisa ugani juu ya umuhimu wa kudhibiti magonjwa ya mifugo na namna ya kuwaelekeza wafugaji, ufugaji bora unaozingatia udhibiti wa magonjwa. Bi. Mkumbukwa alikuwa akieleza hayo wakati wa mafunzo rejea ya siku mbili yaliyofanyika katika Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, yaliyohudhuriwa na baadhi ya maafisa ugani kuanzia ngazi ya kata kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma pamoja na wadau wengine kutoka sekta binafsi. (16.12.2022)

WAWEKEZAJI WATAKIWA KUTOA FURSA ZA AJIRA KWA WAZAWA

Na Mbaraka Kambona, Pwani

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wawekezaji katika sekta ya mifugo kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira kwa vijana ili waweze kufaidika moja kwa moja na uwekezaji wao unaofanyika hapa nchini.

Waziri Ndaki alitoa kauli hiyo wakati akizindua rasmi ujenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL) unaofanyika katika Kata ya Vigwaza, Halmashauri ya Chalinze, mkoani Pwani Disemba 15, 2022.

Alisema ni muhimu sana kwa wawekezaji kutoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi wenye ujuzi na hata wale wasio na ujuzi wakafikiriwe kupewa fursa za ajira ndogo ndogo ili waweze kufaidika na uwekezaji unaoendelea kufanyika katika sekta ya mifugo.

"Ndugu zangu, kiwanda hiki kipo miongoni mwa watu hapa Vigwaza, ni wazi kuwa wananchi watakuwa na matumaini kutokana na uwepo wa  kiwanda hiki, naamini mtawapa kipaumbele mtakapoanza uzalishaji wenu, nimeambiwa mtaajiri watu 1500 na kuna watu 300 pia watapata ajira ambazo sio za moja kwa moja, niwaombe sana mtilie maanani watu wa hapa kwa wenye ujuzi na hata wale ambao hawana ujuzi,"  alisema Ndaki

Aidha, Mhe. Ndaki aliwakumbusha  wawekezaji hao kuzingatia wajibu kwa jamii, kwa maana kufanya shughuli za maendeleo kwa jamii inayowazunguka ili wananchi waone faida ya uwepo wa uwekezaji katika maeneo yao.

"Mtakapoanza uzalishaji niwaombe mfikirie pia wajibu kwa jamii, baada ya kupata faida mrudishe  kwa jamii inayowazunguka hapa, muangalie mahitaji ya jamii inayowazunguka na mkatoa mchango wenu katika kutatua changamoto za wananchi,"aliongeza Ndaki

Halikadhalika, aliwataka wananchi na wafugaji kwa ujumla kutumia fursa ya uwepo wa kiwanda hicho kujiongezea kipato ikiwemo kunenepesha mifugo yao ili waweze kuuza katika kiwanda hicho.

Kiwanda hicho kitapokamilika na kuanza uzalishaji kitakuwa na uwezo wa kuchinja Ng'ombe 2000, Mbuzi na Kondoo  7000 kwa siku.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) akipiga makofi baada ya kuzindua rasmi ujenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL) unaofanyika Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 15, 2022. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL), Bi. Mariam Ng'hwani.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akisalimiana na Mbunge wa Chalinze, ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwan Kikwete(katikati) muda mfupi baada ya kufika katika eneo linalojengwa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL) lililopo Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 15, 2022.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na Wananchi walishiriki katika hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL) uliofanyika Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 15, 2022. Kiwanda hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuchinja Ng'ombe 2000 kwa siku.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL), Bi. Mariam Ng'hwani (kushoto) akimueleza jambo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kulia) alipokuwa akikagua eneo la ujenzi wa kiwanda hicho kinachojengwa  Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 15, 2022.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL), Bi. Mariam Ng'hwani (kushoto) akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) sehemu ambayo kiwanda hicho kinajengwa alipokuwa akikagua shughuli za ujenzi alipotembelea eneo la ujenzi Disemba 15, 2022.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Abattoirs Limited (UMAL), Bi. Mariam Ng'hwani akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki ramani ya ujenzi wa kiwanda hicho muda mfupi baada ya kufika katika eneo la ujenzi lililopo Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 15, 2022.