Nav bar

Ijumaa, 23 Desemba 2022

MAJALIWA ATOA DIRA YA KUBORESHA SEKTA YA MIFUGO NCHINI

◼️ Aagiza Msomera kutumika kama darasa la Ufugaji nchini 


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka wadau wa Sekta ya Mifugo kuboresha mifumo ya ufugaji  ili kufanya shughuli hiyo kwa tija ambapo amesisitiza umuhimu wa sekta hiyo kwa Serikali na Mwananchi mmoja mmoja.


Mhe. Majaliwa ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Mifugo uliolenga kujadili mwelekeo mpya wa sekta hiyo nchini  uliofanyika katika moja ya kumbi zilizopo jengo la PSSF jijini Dodoma leo (19. 12.2022).


Mhe. Majaliwa amesema kuwa licha ya kiasi kidogo cha mchango wa asilimia 7 kwenye pato la Taifa unaotolewa na sekta ya Mifugo, bado ushiriki wa wadau kwenye mabadiliko ya kuelekea kwenye ufugaji wa kisasa upo chini hivyo ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanahamasisha zaidi jamii ili  kuboresha Sekta ya Ufugaji ikiwemo kutatua  changamoto  mbalimbali zinazowakumba wafugaji pamoja  na mifugo yenyewe.


“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana mapenzi ya dhati na Sekta ya Mifugo na anatamani kuona inaleta mapinduzi ya kiuchumi kwa kukuza zaidi pato la wananchi, kutoa ajira na kuchangia pato la Taifa bila kuathiri mazingira na maendeleo ya sekta nyingine hivyo ni lazima wafugani waachane na huu utaratibu wa kufuga kwa kuhamahama kwa sababu pia unachangia kwa kiasi kikubwa kupoteza ubora wa nyama, Sisi kule Lindi kiasi kikubwa cha nyama tunayokula huwa haina ubora kwa sababu haiivi vizuri kutokana na mifugo inayopatikana kule kuwa imekomaa sana kwa sababu ya kutembezwa umbali mrefu” Amesema Mhe. Majaliwa.  


Kutokana na dhamira hiyo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Mifugo na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya tathmini ya maeneo ya ufugaji yaliyopo katika maeneo yao na kiasi cha mifugo kinachoweza kufugwa na endapo mifugo itazidi uwezo wa eneo husika, wafugaji waelekezwe kuvuna mifugo yao.


 “Wafugaji wahamasishwe kuvuna mifugo yao kwa wakati ili kuwawezesha kupata bei nzuri sokoni pamoja na kupunguza changamoto za malisho hususan wakati wa ukame. Kwa ujumla kasi ya uvunaji wa mifugo nchini bado ipo chini ya asilimia 10 ikilinganishwa na viwango bora vya uvunaji wa mifugo kitaifa ambavyo ni kati ya asilimia 20 na 25.” Amesisitiza Mhe. Majaliwa


Aidha Mhe. Majaliwa amezielekeza Wizara ya Ardhi na Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe zinashirikiana na wadau wa sekta ya mifugo katika kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya vijiji na kutenga maeneo ya malisho ya pamoja, ranchi za vijiji na vitalu kwa ajili ya wafugaji binafsi ambapo amesisitiza vijiji vyenye ardhi ya kutosha, vitenge maeneo ya Ranchi za Vijiji yenye ukubwa wa kati ya hekta 200 na 500 ambazo zitatumika kwa utaratibu wa kuwapanga wafugaji kutoka ndani ya kijiji husika.


“Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo inamiliki Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ihakikishe maeneo yote ya NARCO yaliyoko kwenye mikoa yetu, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa kwanza mtambue maeneo hayo yanamilikiwa na nani na mjue yapo katika wilaya gani na yana ukubwa upi na je matumizi ni sahihi kama Serikali inaotaka” Amesema Mhe. Majaliwa.


Katika hatua nyingine Mhe. Majaliwa amewataka wafugaji wote nchini kutumia kijiji cha Msomera kama darasa la Ufugaji nchini kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali kwenye shughuli za Ufugaji kijijini hapo.


“Kule Msomera tumepima kabisa maeneo na tumeyagawa kwenye vitalu na mengine tumeyaacha yatumike kwa yule ambaye angependa kuzunguka kidogo na mifugo yake, lakini pia tumeweka miundombinu ya kisasa kabisa ya majosho na mabwawa ya kunyweshea mifugo yenye mabirika ya kutosha huku pia wataalam wakiwatembelea na kutoa  maelekezo kwa wafugaji waliopo pale nini kifanyike kwa mujibu wa kalenda ya ufugaji” Amebainisha Mhe. Majaliwa.


Awali, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki alisema lengo la mkutano huo mbali na  kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya mifugo kujadili kwa kina na uwazi kuhusu mwelekeo mpya wa sekta ya mifugo nchini pia utawajengea uwezo wafugaji ili wafuge kwa tija na kibiashara kama wawekezaji kwenye sekta ya mifugo.


“Sekta ya Mifugo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, hivyo watatumia mkutano huo kujadili namna ya ufugaji bora pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hivyo nina Imani sote tutatoa maoni yetu kwa ukamilifu ili yaweze kutusaidia kutekeleza mabadiliko tunayotarajia” Amehitimisha Mhe. Ndaki 


Mkutano huo unaofanyika kwa siku mbili unalenga kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji ili kuipa fursa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutekeleza kwa ufanisi maeneo 7 yaliyopo kwenye mpango wa mabadiliko ya sekta hiyo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (kulia) akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa wadau wa sekta ya Mifugo tukio lililofanyika leo (19.12.2022) kwenye moja ya kumbi zilizopo jengo la PSSF, Makole jijini Dodoma.

Baadhi ya Wakuu wa Mikoa yenye idadi kubwa ya wafugaji  (mbele) wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa wadau wa sekta ya Mifugo tukio lililofanyika leo (19.12.2022) kwenye moja ya kumbi zilizopo jengo la PSSF, Makole jijini Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni