Na. Edward Kondela
Serikali imesema
itahakikisha inachukua hatua ya kuwepo kwa taratibu maalum zilizo wazi kwenye
biashara ya mabondo ya samaki ili kujiridhisha upatikanaji wake hadi kufika
viwandani kwa ajili ya kuchakatwa.
Akizungumza (05.03.2024)
jijini Mwanza na wamiliki wa viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi katika jiji
hilo, wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo Uvuvi Prof. Riziki
Shemdoe, Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh amesema serikali
itahakikisha inaweka utaratibu ili kujiridhisha namna ya upatikanaji wa
mabondo.
Prof. Sheikh amebainisha
hayo baada ya baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi
kulalamika kuwa baadhi ya wavuvi wamekuwa wakivua samaki ambao wako chini ya
viwango vinavyotakiwa viwandani wakiwa na lengo la kuuza mabondo kwenye viwanda
vya kuchakata mabondo hayo na kuharibu mazalia ya samaki.
Ameongeza kuwa lazima
kuwepo utaratibu maalum kujua upatikanaji wa mabondo hadi kufika kwenye viwanda
kwa ajili uchakataji ili samaki wanaovuliwa wawe ni wale ambao wana viwango
vinavyotakiwa viwandani kwa ajili ya kuchakatwa.
Kuhusu uvuvi wa dagaa kwa
kutumia taa za solar na zana zingine za uvuvi ambapo inaelezwa wavuvi wamekuwa
wakivua hadi dagaa ambao wanatakiwa kuwa chakula cha samaki aina ya sangara,
Prof. Sheikh amesema serikali itaendelea kufanya taifiti zaidi kwa
kuishirikisha Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ili kuwa na matokeo
sahihi.
Amesema kuwa serikali
kupitia TAFIRI ni lazima ifanye tafiti za kujiridhisha matokeo yaliyotolewa
awali kama yana athari yoyote kabla ya kuwa na matokeo mengine na kuyatolea
ufafanuzi ili kuwa na matokeo yasiyokuwa na utata.
Prof. Sheikh amewataka pia
wafanyabiashara kuzidi kushirikiana na serikali katika juhudi za kukuza Sekta
ya Uvuvi kwa kuunga mkono maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kurasimisha sekta hiyo ili iwe endelevu.
Nao baadhi ya wamiliki wa
viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi jijini Mwanza, wameiomba serikali kupitia
Wizara ya Uvuvi kuzidi kuchukua hatua katika kupambana na uvuvi haramu ili
samaki wazidi kuzaliana kwa wingi na kuongeza wingi wa samaki katika viwanda.
Aidha, wamesema ni muhimu
kulinda soko la nje katika kuuza mazao ya uvuvi ili kuliongezea taifa mapato
zaidi na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa.
Katika kikao hicho ambacho
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikiwazungukia wadau mbalimbali wa Sekta ya
Uvuvi kupata maoni yao ya namna ya kulinda rasilimali za uvuvi, imesema itakuwa
inafanya vikao mara kwa mara ili kutatua changamoto zinazowakabili.
Kabla ya kikao hicho
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh alifika katika ofisi ya Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala wa mkoa huo Bw.
Balandya Elikana kuhusu hali ya Sekta ya Uvuvi Mkoani Mwanza ambapo aliarifiwa
kuwa uongozi wa mkoa umekuwa ukihakikisha unalinda rasilimali za uvuvi ili
ziwanufaishe wananchi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.
Mkurugenzi wa Idara ya
Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh akizungumza leo
(05.03.2024) jijini Mwanza na wamiliki wa viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi
katika jiji hilo, wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo Uvuvi Prof.
Riziki Shemdoe, ambapo amesema serikali itahakikisha inaweka utaratibu ili
kujiridhisha namna ya upatikanaji wa mabondo ya samaki. (05.03.2024)
Katibu Tawala Mkoa wa
Mwanza Bw. Balandya Elikana (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed
Sheikh (wa pili kutoka kushoto) na watendaji wengine kutoka wizarani na Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa, mara baada ya Prof. Sheikh kufika katika ofisi hizo na
kuzungumza na katibu tawala huyo namna ya kulinda rasilimali za uvuvi kabla ya
kufanya kikao na wamiliki wa viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi jijini
Mwanza, akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe.
(05.03.2024)
Mkurugenzi wa Idara ya
Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh (mwenye koti
jeusi, mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watendaji
kutoka wizarani na wamiliki wa viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi jijini
Mwanza, baada ya kuahirisha kikao ambapo Prof. Sheikh alipata fursa ya
kusikiliza maoni na changamoto zinazowakabili wamiliki hao, akimwakilisha
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe. (05.03.2024)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni