SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Mb) amesema kwa sasa mahitaji ya maziwa nchini yameongezeka, hivyo kuna haja ya serikali kuongeza Mitamba ya Ng’ombe wa Maziwa ili kuongeza uzalishaji utakaokidhi Soko la Maziwa.
Katika ziara yake Kwenye Shamba la Kuzalisha Mifugo la Kitulo Mkoani Njombe Leo Mei 02, 2026 Mhe. Dkt. Bashiru amesema kwa sasa wafugaji wamepata mwamko wa kufuga kisasa lakini uhitaji wa mbegu bora za ng’ombe wa maziwa bado ni mkubwa ukilinganisha na uzalishaji.
“Wananchi wamehamasika kufuga kisasa, sio wote lakini idadi iliyopo inaridhisha, eneo la ufugaji wa ngombe wa maziwa linavutia kwa sababu mahitaji ya maziwa hapa nchini ni makubwa kuliko uzalishaji wetu, lakini ili kuongeza uzalishaji wa maziwa hapa ndio tunaweza kupata suluhu kwenye eneo la mbegu bora hapa nchini, watu wanaenda Zambia, Kenya, Africa Kusini watu wanahangaika kupata mbegu bora” alisema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha, aliongeza kwa kumuagiza Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha kuwa kupitia Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi kupeleka ng’ombe wa maziwa takriban 3,000 ili kuongeza uzalishaji wa shamba hilo.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulia sekta ya Mifugo Dkt. Fabian Madele kwa Niaba ya Katibu Mkuu amesema ili kutimiza malengo ya serikali ya kulinda rasilimali za mifugo nchini ni wataalam na wadau wote wa sekta hiyo kushirikiana katika kutimiza azima hiyo licha ya changamoto zinazolikabili shamba hilo.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Mhe. Rabson Mahenge amesema Halmashauri hiyo imekuwa ikishirikiana na Shamba hilo kulinda dhidi ya wavamizi ili kuendelea kutimiza malengo ya shamba hilo ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa mifugo bora hususani ng’ombe wa maziwa na nyama.
Shamba la Mifugo Kitulo lina ukubwa wa hekta 4,875.641 kwa sasa shamba hilo lina uwezo wa kubeba ng’ombe 1500 huku uwezo wake ni kubeba Ng’ombe 4,500 kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa.


Maoni
Chapisha Maoni