SERIKALI YATAIFISHA
KUNDI LINGINE LA NG’OMBE KUTOKA RWANDA
NA; MWANDISHI MAALUM –
KASULU
Kufuatia zoezi linaloendelea la oparesheni kamata mifugo
linaloongozwa na Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga
Mpina, serikali kwa mara nyingine imetaifisha kiasi cha ng’ombe 171
waliokamatwa katika kijiji cha Kakere wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Akiongea katika zoezi hilo Waziri Mpina amesema Wilaya za
mipakani mwa Nchi jirani ziko katika tishio kubwa la kuvamiwa na mifugo na
kuelekeza mwanasheria wa Wilaya ya Kasulu kuanza kuandaa utaratibu wa mahakama
kuzipiga mnada. “Hatua ya kwanza sisi kama Serikali tunataifisha ng’ombe hawa
na kufanya utaratibu wa kuzipiga mnada na mwanasheria wetu wa Serikali aanze
taratibu ambapo ng’ombe hao tutawapiga mnada kwa mujibu wa sheria ya magonjwa
ya wanyama No. 17 ya mwaka 2003.” alisema Mpina.
Mpina aliongeza kusema kuwa, ng’ombe hao kwa sasa wataendelea
kuwa chini ya Serikali mpaka taratibu zitakapo kamilika, na kuitaka kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya
Kasulu kuelendelea kwa kasi kubwa
kukamata mifugo katika mapori na kuhakikisha mifugo yote inapatikana.
Sambamba na hilo, Waziri Mpina aliwataka wananchi
kujiadhari na kuondoka katika kununua
kesi zisizokuwa za kwao kwa kuikubali mifugo kutoka nje ya nchi kuwa ni ya kwao,
kwani ni kujitaftia matatizo na kuisadia serikali katika jitahada hizi za
kukamata mifugo inayoingia ndani ya nchi kinyume na taratibu.
“Kwa hiyo wananchi
wawe namba moja kuwafichua watu hao, na wale tunaowabaini kuwa wanaitikia mifugo toka nje ya nchi kuwa
ni mali yao lazima wachukuliwe hatua.” alisisitiza Mpina.
Awali akitoa taarifa ya ng’ombe hao waliokamatwa katika Wilaya
hiyo mkuu wa wilaya hiyo Mwanahawa Mrindoko alisema ng’ombe hao ni mali ya raia wa Rwanda kwani Serikali ya wilaya
ilikuwa inawatafuta Raia wahamiaji
haramu na kuwapata, hivyo sheria
itachukua mkondo wake, na aliongeza kwa kusema kuwa kamati ya ulinzi na usalama
itaendelea na zoezi la kuwatafuta wafugaji ambao ni wahamiaji haramu.
Akiwa katika wilaya ya Kakonko Waziri Mpina aliagiza kamati
ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo
kupitia Mkuu wa Wilaya Kanali Hosea Ndagalla kuanza mara moja zoezi la
oparesheni ya kukamata mifugo toka nje ya nchi kwani tarifa za awali zinasema
kuwa Wilaya hiyo ilikuwa haijaanza kabisa kutekeleza agizo hilo na ni moja ya Wilaya
ya mpakani mwa nchi jirani ya Burundi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina, akiangalia Ng’ombe aina ya nyankole waliopo katika kijiji cha Kakere baada ya kutaifishwa na serikali. |
Waziri Mpina akiongea na wanahabari hawapo katika picha baada ya zoezi la kutaifisha kundi la ng’ombe waliovamia katika kijiji cha Kakere wilayani Kasulu. |
Ng’ombe aina ya nyankole kutoka Rwanda,
waliotaifishwa na serikali katika kijiji cha Kakere wilayani Kasulu wakisubiri
kukamilika kwa taratibu za mahakama kwa ajili ya kupigwa mnada.
|