Nav bar

Jumanne, 31 Januari 2023

MWELEKEO MPYA

 




ENEO LA KITARAKA KUTUMIKA KIMKAKATI KUZALISHA MIFUGO KIBIASHARA

Na Mbaraka Kambona, Singida


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amesema kuwa Serikali imedhamiria kulitumia eneo la kupumzishia mifugo la Kitaraka lililopo wilayani Manyoni, Singida  liweze kutumiwa na vijana watakao hitimu mafunzo katika vituo atamizi kwa ajili ya kufanya shughuli za uzalishaji wa mifugo  kibiashara ili kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.


Mhe. Ulega alibainisha hayo wakati wa kikao baina yake na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba (kushoto) alipokutana nae katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida Januari 30, 2023. 


Wakati wa mazungumzo yao, Mhe. Ulega alimueleza Mkuu wa Mkoa huyo kuwa lengo la ziara yake ni kujadiliana nae kuhusu dhamira ya Serikali ya kutaka kulitumia eneo la kitaraka kwa ajili ya kufanya shughuli za uzalishaji wa mifugo ili kuwawezesha vijana  kujipatia ajira lakini pia kuzalisha malighafi ya uhakika kwa ajili ya viwanda vya nyama na kuifanya sekta ya mifugo  kuchangia ipasavyo katika pato la taifa na la mtu mmoja mmoja.


 Alisema kuwa kupitia programu ya vituo atamizi iliyoanzishwa na serikali kwa ajili ya kuwafundisha vijana ufugaji wa kisasa, Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 19 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kufuga kibiashara kwa ajili ya kuuza  ndani na nje ya nchi.


“Progaramu hii ya vituo atamizi ni ya miaka 3(2022/23-2024/25) na hizi bilioni 19 zinatolewa na wadau mbalimbali ambapo serikali inatoa bilioni 6.3, na bilioni 12.6 zitachangiwa  na wadau wengine kutoka sekta binafsi”,alisema Ulega


Aliongeza kwa kusema kuwa mpango huo wa kutumia eneo la Kitaraka unatarajiwa kuzalisha robota 500,000 za malisho ya mifugo na kunenepesha ng’ombe 8000 kwa wakati mmoja.


Aidha, alifafanua kuwa eneo hilo la Kitaraka limekaa kimkakati kwa ajili ya unenepeshaji wa mifugo kwasababu ndani ya eneo hilo kuna kituo cha treni ya mwendokasi (SGR) hivyo itarahisisha usafirishaji wa malighafi kutoka hapo kwenda maeneo mengine ya soko.

Aidha, Naibu Waziri alimuomba Mkuu wa Mkoa, uongozi wa halmashauri, na wananchi wa Singida kwa ujumla kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa dhati  katika kufanikisha adhma ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza ajira kwa vijana kupitia sekta ya mifugo.


“Serikali ya Mhe Rais, Dkt. Samia imejielekeza ipasavyo ktk kutumia fursa za sekta za Mifugo,uvuvi na kilimo katika kuajiri Vijana na kuongeza uzalishaji nchini hivyo naomba mtoe ushirikiano wa kutosha ili adhma hii iweze kutimia kama ilivyokusudiwa”, alifafanua Mhe. Ulega

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akiongea na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba (hayupo pichani) alipokutana nae katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Mkoani Singida Januari 30, 2023.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba (kushoto) muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Mkoani Singida Januari 30, 2023.


WAFUGAJI WANAOHAMA BONDE LA MTO KILOMBERO WASIZUIWE-NDAKI

◼️ Awashangaa watendaji wanaowawekea vikwazo 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amewaagiza viongozi na watendaji wote mkoani Morogoro kutowazuia wafugaji wanaohama kutoka bonde la Mto Kilombero ambapo amesema kuwa kufanya hivyo ni kukwamisha utekelezaji wa agizo la Serikali linalowataka wafugaji na wakulima kuondoka kwenye bonde hilo.


Mhe. Ndaki amesema hayo jana (27.01.2023) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Nakaguru iliyopo  Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro ambao ulijumuisha wafugaji na wakulima wanaozungukwa na bonde la Mto Kilombero.


“Tangazo la Serikali la kuondoka kwenye  bonde la mto Kilombero ni sahihi na sisi wafugaji tunapaswa kuliheshimu kwa sababu ni lazima tuondoke kwenye bonde hilo kwa sababu ni tuna wajibu wa kulinda maeneo tengefu, oevu na yale yote yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo lakini cha kushangaza naambiwa kuna baadhi ya watendaji wanawazuia wafugaji wanaotaka kuhamia kwenye maeneo mengine waliyoyapata mbali na hapa, Tuwape vibali waondoke” Amesisitiza Mhe. Ndaki.


Katika kutekeleza agizo hilo, Mhe. Ndaki amewasisitiza viongozi wa maeneo yenye wafugaji wanaopaswa kuhama, kuhakikisha wanawatafutia wafugaji hao maeneo ya kuhamia ili zoezi hilo la kuwahamisha lisiathiri shughuli zao za ufugaji.


“Najua kuna maeneo ambayo mliyatenga kama maeneo ya malisho lakini kwa bahati mbaya yamevamiwa na watumiaji wengine wa ardhi, hakikisheni mnawaondoa wavamizi hao na kugawa maeneo hayo kwa wafugaji watakaohama kwenye bonde hilo” Ameongeza Mhe. Ndaki.


Akielezea namna watakavyotekeleza maagizo hayo Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Danstan Kyoba ameahidi kukutana na viongozi na watendaji mbalimbali wa Wilaya hiyo kwa ajili ya kuanza kutenga maeneo ambayo watahamia wafugaji na wakulima wanaoondoka kwenye bonde la mto Kilombero.


“Ndani ya siku 100 mimi na timu ya wataalam wangu tutatembelea kwenye vijiji vyote vinavyoguswa na mpango huu wa kuondoka kwenye bonde hilo ili tukubaliane maeneo watakayohamia lakini kwanza tutekeleze agizo la kuondoka” Ameongeza Mhe. Kyoba.


Bonde la Mto Kilombero linazungukwa na vijiji 23 vilivyopo Wilayani Kilombero ambavyo ni Luwembo, Maulanga, Miwangani, Namwawala, Idandu, Kalenga, Kikwambi, Mofu, Miyomboni, Nakagulu, Ijia, Isago, Luvilikila, Mkangawalo, Chita, Melela, Chisano, Karangekelo, Msolwa, Miembeni, Kibugasa na Ngalimila.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wafugaji wa Wilaya ya Kilombero jana (27.01.2023) kwenye Mkutano uliofanyika ukumbi wa shule ya sekondari Nakaguru iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro ambapo alisisitiza suala la  kuondoka kwa wafugaji waliopo kwenye bonde la Mto Kilombero.

Sehemu ya wafugaji na wakulima wa Wilaya ya Kilombero wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati wa Mkutano baina yake na wao uliofanyika jana (27.01.2023) kwenye Ukumbi wa shule ya sekondari Nakaguru iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro.

BILIONI 60 ZAWEKEZWA SEKTA YA UVUVI, NCHI ZA ULAYA ZAHAMASIKA KATIKA UFUGAJI SAMAKI

Na. Edward Kondela


Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewekeza Shilingi Bilioni 60 katika Sekta ya Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2022-2023 ili kuinua kipato cha wananchi kupitia sekta hiyo.


Akizungumza jijini Mwanza (26.01.2023) kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah wakati wa ujio wa mabalozi nane kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya kwenye Kampasi ya Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA), Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Prof. Mohammed Sheikh amesema fedha hizo zimewekezwa kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kwa kununua boti na wavuvi wadogo waweze kufika kwenye maji ya kina kirefu kuvua samaki ili kuongeza kipato.


Prof. Sheikh amebainisha hayo baada ya ziara ya siku moja ya mabalozi hao katika Kampasi ya FETA iliyopo katika Kata ya Nyegezi, Wilaya ya Nyamagana ili kushuhudia majukumu mbalimbali ya FETA na mradi wa ufugaji samaki wanaoufadhili.


Ameongeza kuwa ujio wa mabalozi hao ni wa kawaida ili kujionea namna utekelezaji wa miradi hiyo ambayo wanashirikiana na serikali ili kuwaondoa wavuvi katika uvuvi wa kutumia zana za zamani za uvuvi na kutumia njia ya vizimba kwa kufuga samaki wengi na kujipatia kipato zaidi.


Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) Dkt. Semvua Mzighani amesema ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba unakua kwa kasi na serikali imewekeza pesa, hivyo FETA inawashauri vijana kuchangamkia fursa kupitia Ziwa Victoria.


Dkt. Mzighani ameongeza kuwa FETA inatoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi na kuwashauri wanaohitaji kujifunza namna ya kufuga samaki kwa njia ya vizimba kujiunga na FETA kwenye mafunzo ya muda mfupi ili kujifunza jinsi ya kutengeneza vizimba, namna ya kuviweka ziwani, kupata mbegu bora za samaki, namna ya kukuza samaki na kuwahifadhi ili wasiharibike baada ya kuwavua.


Amefafanua kuwa kumekuwa na muitikio mkubwa wa watu kujifunza namna ya kufuga samaki kupitia vizimba na tayari wapo ambao wameanza kuwekeza kwenye Ziwa Victoria lakini anawasihi watu wengi zaidi kujitokeza hususan vijana kuchangamkia fursa hiyo.


Naye mmoja wa wafugaji samaki kwa njia ya vizimba katika Ziwa Victoria ambaye amepata elimu FETA Bw. Mpanju Elpidius amewaasa vijana wenzake kuchangamkia fursa hiyo kwa kuanza na kidogo walichonacho ili waweze kufikia malengo yao.


Ameipongeza serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutenga fedha ya kuwakopesha vijana kwa masharti nafuu ili kufuga samaki kwa njia ya vizimba na kuziomba benki zilizopo nchini kuiga mfano wa serikali kwa kuwaamini vijana na kuwakopesha kwa masharti nafuu ili kuwekeza kwenye fursa mbalimbali ikiwemo ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba.


Baadhi ya mabalozi kutoka nchi za ulaya waliotembelea miradi inayotekelezwa na FETA ukiwemo wa utoaji elimu ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba kwenye Ziwa Victoria, wamesema wameridhishwa na namna fedha walizowekeza zinavyotumika na kuhamasisha vijana kujitokeza kwa wingi na kuiomba serikali kuwasimamia ili waweze kutumia fedha hiyo kwa malengo yanayotarajiwa.


Umoja wa Nchi za Ulaya umewekeza Shilingi Milioni 800 kwa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA), kwa ajili ya kukuza Sekta ya Uvuvi kupitia ufugaji samaki ambapo wanawekeza kwenye miundombinu, mitaala na kuwawezesha wakufunzi kupata elimu zaidi kwenye ukuzaji viumbemaji kwa njia ya kisasa katika kipindi cha miaka minne ambapo hadi sasa mradi huo umetekelezwa kwa miaka miwili ili kuvutia tasnia ya ufugaji samaki.

Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Prof. Mohammed Sheikh (wa kwanza kulia), akizungumza na mmoja wa mabalozi kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya waliotembelea Kampasi ya Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) iliyopo Kata ya Nyegezi jijini Mwanza, kushuhudia majukumu mbalimbali ya FETA na mradi wa ufugaji samaki wanaoufadhili. Kulia kwa Prof. Sheikh ni Mtendaji Mkuu wa FETA Dkt. Semvua Mzighani. (26.01.2023)

Mabalozi nane kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya wakikagua shughuli za ufugaji samaki katika Kampasi ya Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) iliyopo Kata ya Nyegezi jijini Mwanza, wakati wakikagua miradi mbalimbali ya Sekta ya Uvuvi wanayoifadhili hapa nchini kupitia FETA. (26.01.2023)

Mabalozi nane kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya wakishuka kutoka kwenye boti baada ya kushuhudia mradi wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba kwenye Ziwa Victoria jijini Mwanza, ambao ni moja ya miradi inayofadhiliwa na umoja huo hapa nchini kupitia Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA). (26.01.2023)

Baadhi ya mabalozi kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya na watumishi wa Jeshi la Polisi nchini wakishuhudia njia mojawapo ya ukaushaji samaki kwenye vichanja, wakati wa ziara ya siku moja ya mabalozi nane kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya waliotembelea Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Nyegezi jijini Mwanza kujionea miradi wanayoifadhili kupitia wakala hiyo hapa nchini yenye thamani ya Shilingi Milioni 800 kwa miaka minne ambapo hadi sasa utekelezaji wake umefikia miaka miwili. (26.01.2023)

Picha ya pamoja ya mabalozi nane kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya na baadhi ya wafanyakazi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo wakati wa ziara ya siku moja ya mabalozi hao jijini Mwanza kutembelea miradi inayofadhiliwa na umoja huo hapa nchini katika Sekta ya Uvuvi kupitia Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA). (26.01.2023)


TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MRADI WA SWIOFISH

 

Mkurugenzi Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei  akiongea wakati wa kikao cha kupokea taarifa za utekelezaji wa mradi wa  SWIOFIC-Nairobi Convention  kilichofanyika Mkoani Tanga Januari 27,2023 lengo likiwa ni pamoja na kuwezesha ushirikiano katika masuala ya usimamizi wa mazingira na Uvuvi Ili kuimarisha usalama wa Chakula kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na kuimarisha maisha ya jamii za wavuvi kwa ujumla.

Afisa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Bi. Julieth Evance akiwasilisha muhtasari wa kikao kilichopita cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa SWIOFIC-Nairobi Convention kwa wajumbe wa kamati hiyo (hawapo pichani) kilichofanyika Mkoani Tanga Januari 27,2023

Mratibu wa mradi wa SWIOFIC -Nairobi Convention Bi. Ulrika Gunnartz akiwasilisha mada wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kilichofanyika  Mkoani Tanga Januari 27, 2023

Meneja wa Taasisi ya hifadhi za Bahari na maeneo Tengefu (MPRU) Dkt.Sware Semesi akiuliza maswali wakati  wa kikao cha kupokea taarifa za utekelezaji wa mradi wa SWIOFIC - Nairobi Convention kutoka kwa wataalam wa mradi huo  kilichofanyika Mkoani Tanga Januari 27, 2023.

Mkurugenzi Msaidizi uendelezaji wa rasilimali za Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Merisia Mparazo akichangia hoja wakati  kikao cha kupokea taarifa za utekelezaji wa mradi wa SWIOFIC-Nairobi Convention  kilichofanyika Mkoani Tanga Januari 27,2023 lengo likiwa ni pamoja na kuwezesha ushirikiano katika masuala ya usimamizi wa mazingira na Uvuvi Ili kuimarisha usalama wa Chakula kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na kuimarisha maisha ya jamii za wavuvi kwa ujumla.

Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Bi. Asha Churu (wa pili kutoka kulia) akionyesha eneo la mwalo wa Kwale Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei (wa tatu kutoka kulia)  walipoenda kutembelea  Januari 27,2023.

Mkurugenzi Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa  Uvuvi Tanzania (TAFIRI) (wa tatu kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa kamati ya wataalam wa mradi wa SWIOFIC -Nairobi Convention na baadhi ya wavuvi wa mwalo wa Kwale mara baada ya kutembelea mwalo huo Mkoani Tanga Januari 27, 2023.

Ijumaa, 27 Januari 2023

UTEKELEZAJI WA MWELEKEO MPYA WA SEKTA YA MIFUGO NCHINI

 


HERI YA SIKU YA KUZALIWA

 





​WAFUGAJI WANAOVAMIA MASHAMBA YA WAKULIMA NI WAHALIFU WASHUGHULIKIWE - NDAKI

Kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wakulima kwenye mikutano ya hadhara aliyoifanya jana (26.01.2023) kwenye kata za Ulaya na Mbwade Wilayani Kilosa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameagiza wafugaji wote wanaovamia mashamba ya wakulima hao wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria.


Mhe. Ndaki amesema kuwa pamoja na kuwa ufugaji ni shughuli halali kama zilivyo nyingine, inapaswa kufanyika kwa kufuata taratibu na sheria bila kuathiri watumiaji wengine wa ardhi.


"Yaani mkulima amelima mazao yake afu kwa makusudi mfugaji anaenda kulisha mifugo yake, huo ni uhalifu na matukio ya aina hii yakithibitishwa kuwa ni kweli basi naomba Mwenyekiti wa Chama cha wafugaji usihangaike hata kunipigia simu kwa sababu na mimi ntasisitiza watu hao wachukuliwe hatua za kisheria" Amesisitiza Mhe. Ndaki.


Aidha Mhe. Ndaki ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Kilosa kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya Sheria wataalam wote wanaopokea rushwa ili kuchochea migogoro hiyo ya wakulima na wafugaji.


"Lakini pia changamoto nayoiona hapa ni wafugaji kutoainishiwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho hivyo ninawaagiza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa mkakae na watu wenu ili muainishe na kuorodhesha maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo na kuyawasilisha ofisini kwangu ili yatangazwe kwenye gazeti la Serikali na hatimaye kurasimishwa rasmi.


Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kilosa Mhe. Palamagamba Kabudi ameishukuru Serikali kwa kuwatengea fedha za kuanzisha mashamba darasa 3 ya malisho ya mifugo ambapo ameongeza kuwa yatawasaidia kuondokana na changamoto ya ukosefu wa malisho ya mifugo hasa msimu wa kiangazi.


"Lakini jambo la pili Wilaya yetu mbali na kuwa na wafugaji ina wafugaji wanaofanya kilimo pia hivyo naomba Wizara iwasaidie hasa kwenye eneo la ugani kwa sababu idadi yao haiendani na wataalam wa ugani waliopo " Amesema Mhe. Kabudi. 


Awali mmoja wa Wakulima walioshiriki kwenye Mkutano huo Bw. Omary Walii alisema kuwa kumekuwa na kiwango cha ongezeko la uvamizi wa wafugaji kwenye maeneo ya wakulima huku akibainisha uharibifu unaofanywa na wafugaji wa kata ya Mbwade kwenye skimu ya umwagiliaji iliyopo kwenye kijiji cha Chanzulu.


Akizungumzia hoja hiyo, mmoja wa wafugaji wa kijiji cha Mbwade Bw. Sozia Zakayo amesema kuwa sababu kubwa inayowafanya kuingia kwenye maeneo ya wakulima ni hali ya mabadiliko ya tabia nchi ambayo inaiathiri mifugo yao hasa kwenye upande wa maji ambapo alimuomba Mhe. Ndaki kuwajengea lambo litakalowatosheleza kupata huduma ya maji wakati wote wa msimu wa kiangazi.


Ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki Mkoani Morogoro inaendelea tena leo ambapo atafanya mkutano na wananchi wa Wilaya ya Kilombero huku lengo la Ziara hiyo likiwa ni kuhamasisha utekelezaji wa Mwelekeo mpya wa sekta ya Mifugo kupitia Mpango wa mabadiliko wa Sekta hiyo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa tatu kutoka kulia) akiongozana na wafugaji wa kijiji cha Mbwade kwenda kukagua shamba darasa la malisho lililopo kijijini hapo muda mfupi baada ya kuwasili katika eneo hilo lililopo Kilosa mkoani Morogoro jana (26.01.2023)

Sehemu ya wananchi wa Kata ya Ulaya iliyopo Kilosa Mkoani Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati wa Mkutano baina yao jana (26.01.2023).

Sehemu ya wananchi wa Kata ya Ulaya iliyopo Kilosa Mkoani Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati wa Mkutano baina yao jana (26.01.2023).

SEKTA YA MIFUGO YAWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MAAGIZO KUHUSU MRADI WA UJENZI WA BWAWA KWA AJILI YA KUNYWESHEA MAJI MIFUGO KATOKA KIJIJI CHA CHAMAKWEZA WILAYANI CHALINZE MKOANI PWANI

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma akitoa maelezo mafupi kabla ya kufunga kikao cha kuwasilisha kwa Kamati taarifa ya Utekelezaji wa Maagizo kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kijiji cha Chamakweza kilichopo Chalinze Mkoani Pwani kilichofanyika jijini Dodoma leo Januari 25, 2023.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akijibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati wa Kikao cha kuwasilisha kwa Kamati hiyo Taarifa ya Utekelezaji wa Maagizo kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kijiji cha Chamakweza kilichopo Chalinze Mkoani Pwani. Uwasilishaji wa taarifa hiyo umefanyika jijini Dodoma leo Januari 25, 2023.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akieleza jambo wakati wa Kikao cha kuwasilisha kwa Kamati ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji taarifa ya Utekelezaji wa Maagizo kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kijiji cha Chamakweza kilichopo Chalinze Mkoani Pwani kilichofanyika katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma leo Januari 25, 2023.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo), Bw. Tixon Nzunda akitoa ufafanuzi wa  baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati wa Kikao cha kuwasilisha kwa Kamati hiyo Taarifa ya Utekelezaji wa Maagizo kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kijiji cha Chamakweza kilichopo Chalinze Mkoani Pwani. Uwasilishaji wa taarifa hiyo umefanyika jijini Dodoma leo Januari 25, 2023.

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Prof. Patrick Ndekidemi akichangia hoja wakati wa  Kikao cha kuwasilisha kwa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji taarifa ya Utekelezaji wa Maagizo kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kijiji cha Chamakweza kilichopo Chalinze Mkoani Pwani kilichofanyika jijini Dodoma leo Januari 25, 2023.


Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini, Mhe. Charles Mwijage akichangia hoja wakati wa  Kikao cha kuwasilisha kwa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji taarifa ya Utekelezaji wa Maagizo kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kijiji cha Chamakweza kilichopo Chalinze Mkoani Pwani kilichofanyika jijini Dodoma leo Januari 25, 2023.

Sehemu ya Viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Sekta ya Mifugo  wakichukua taarifa wakati wa Kikao cha  kuwasilisha kwa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Taarifa ya Utekelezaji wa Maagizo kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kijiji cha Chamakweza kilichopo Chalinze Mkoani Pwani. Uwasilishaji wa taarifa hiyo umefanyika leo Januari 25, 2023.

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali ya Vyakula vya Wanyama Dkt. Asimwe Rwiguza akiwasilisha  kwa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Taarifa Utekelezaji wa Maagizo kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kijiji cha Chamakweza kilichopo Chalinze, mkoani Pwani. uwasilishaji wa taarifa hiyo umefanyika jijini Dodoma leo Januari 25, 2023.



DKT. TAMATAMAH AKUTANA NA UJUMBE WA UBALOZI WA UINGEREZA KUTOKA SHIRIKA LA FEDHA LA UINGEREZA (UK EF)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (katikati) akiwa kwenye mazungumzo na ujumbe wa Ubalozi wa Uingereza kutoka Shirika la Fedha la Uingereza (UK EF) katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma juu ya ushirikiano baina ya wizara na shirika hilo kwenye ujenzi wa bandari ya uvuvi katika eneo la Kilwa Masoko, Wilaya ya Kilwa, Mkoani Lindi. (25.01.2023)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah akiuonesha ujumbe wa Ubalozi wa Uingereza kutoka Shirika la Fedha la Uingereza (UK EF), (hawapo pichani) mchoro wa bandari ya uvuvi inayojengwa katika eneo la Kilwa Masoko, Wilaya ya Kilwa, Mkoani Lindi kwa thamani ya Shilingi Bilioni 266 ambapo ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Mwezi Septemba Mwaka 2024. Mazungumzo na ujumbe huo juu ya ushirikiano katika ujenzi wa bandari ya uvuvi baina ya wizara na shirika hilo, yamefanyika katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma. (25.01.2023)


Baadhi ya viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) wakiwa kwenye kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah wakati wa mazungumzo na ujumbe wa Ubalozi wa Uingereza kutoka Shirika la Fedha la Uingereza (UK EF) katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma juu ya ushirikiano baina ya wizara na shirika hilo kwenye ujenzi wa bandari ya uvuvi katika eneo la Kilwa Masoko, Wilaya ya Kilwa, Mkoani Lindi. (25.01.2023)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (wanne kutoka kushoto mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe wa Ubalozi wa Uingereza kutoka Shirika la Fedha la Uingereza (UK EF) na baadhi ya viongozi wa wizara Sekta ya Uvuvi, baada ya mazungumzo juu ya ushirikiano baina ya wizara na shirika hilo katika ujenzi wa bandari ya uvuvi inayojengwa katika eneo la Kilwa Masoko katika Wilaya ya Kilwa, Mkoani Lindi. Mazungumzo na ujumbe huo juu ya ushirikiano katika ujenzi wa bandari ya uvuvi baina ya wizara na UK EF, yamefanyika katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma. (25.01.2023)

SERIKALI YAPOKEA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA UVUVI


Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) imepokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa usimamizi wa pamoja wa rasilimali za uvuvi na mazingira ya bahari SWIOFIC -Nairobi Convention  unaofadhiliwa na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa (SIDA)

Akizungumza mara baada ya kupokea ripoti hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimirei, amesema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa miaka mitano tangu 2019 na unatarajiwa kumalizika mwezi Disemba 2023

Amesema lengo la mradi kuwezesha ushirikiano katika masuala ya usimamizi wa mazingira, kuimarisha rasilimali za Uvuvi na kuboresha maisha ya jamii za wavuvi kwa ujumla

"Mradi huu unafanyika kwa majaribio kwa upande wa Tanzania, Madagascar na Msumbiji, baada ya hapo matokeo yatakayotokana na mradi huu yatatumika kama mfano katika nchi nyingine hasa katika nchi za Magharibi mwa Bahari ya Hindi ambako utatekelezwa mradi mkubwa zaidi" amesema

Ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita inaendelea na jitihada za kuboresha mazingira ya uvuvi hasa Ukanda wa Pwani ikiwemo kuanzisha miradi mikubwa ya kuendeleza miradi ambayo imekwisha muda wake

"Nia ni kuona uzalishaji katika dhana pana ya uchumi wa bluu inafanya kazi na wananchi wetu wanapata maboresho kwa maana ya kupata kipato na lishe bora kwa kuzingatia usalama wa chakula ili kuinua uchumi wao binafsi na uchumu wa taifa kwa ujumla

Aidha amebainisha kuwa pamoja na mambo mengine Serikali imeendelea na jitihada za kuboresha sekta ya uvuvi ikiwemo kuanzisha ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko na Zanzibar

Amewataka wananchi na wavuvi kuwa tayari kupokea fursa zote zinazoletwa kupitia miradi mbalimbali ili kuungana na Serikali ya awamu ya sita ambayo imejikita pia katika kuendeleza kutekeleza miradi hiyo pindi inapomalizika.


Mkurugenzi Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei akiongea wakati wa kufungua  kikao cha kupokea taarifa za utekelezaji wa mradi wa  SWIOFIC- Nairobi Convention  kilichofanyika Mkoani Tanga Januari 26,2023 lengo likiwa ni pamoja na kuwezesha ushirikiano katika masuala ya usimamizi wa mazingira na Uvuvi Ili kuimarisha usalama wa Chakula kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na kuimarisha maisha ya jamii za wavuvi kwa ujumla.

Mkurugenzi Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa kamati ya wataalam wa mradi wa SWIOFIC -Nairobi Convention mara baada ya kikao cha kupokea taarifa za utekelezaji wa mradi huo kilichofanyika Mkoani Tanga Januari 26, 2023.


Jumatano, 25 Januari 2023

​SERIKALI YATAKA USIMAMIZI MZURI ZAIDI WA SEKTA YA UVUVI, KUFIKIA MALENGO ENDELEVU

Serikali imedhamiria kuimarisha usimamizi  wa rasilimali za uvuvi nchini ili kuwezesha Sekta ya uvuvi kuendelea kuchangia katika kuleta maendeleo endelevu ikiwa ni miongoni mwa sekta za kiuchumi zinazotoa ajira, kuimarisha usalama wa chakula, maisha ya watu pamoja na  kuongeza mapato ya nje na ndani ya nchi.


Hayo yamesemwa Januari 24,2023 mjini Tanga na Mkurugenzi Msaidizi wa  Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Merisia Mparazo wakati wa ufunguzi wa kikao cha kamati ya wataalam wa  mradi wa SWIOFIC -Nairobi Convention.


Alisema kuwa mradi huo unahakikisha kwamba kunakua na ushirikino  katika usimamizi wa  masuala ya Bahari na mazingira yake pamoja na rasilimali za Uvuvi zilizomo nchini.


Aidha alibainisha kuwa sekta hiyo imeajiri zaidi ya watu milioni 4.5 wanaojihusisha na shughuli za uvuvi na zile zinazohusiana  na uvuvi wakati takribani 194,804 ni ajira za moja kwa moja kwa wavuvi na watu 31,998 wameajiriwa katika tasnia  ya ukuzaji  viumbe maji.


Aliongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ina jukumu la kusimamia na kuendeleza rasilimali za uvuvi nchini kwa kuhakikisha ustawi wa jamii ya wavuvi.


Alisema Serikali itaimarisha usimamizi wa rasilimali za Uvuvi na kuboresha maisha ya jamii za wavuvi katika Wilaya ya Nkinga kupitia mradi wa SWIOFIC -Nairobi Convention.


"Lengo la mradi linaendana na sera ya taifa ya uvuvi ya mwaka 2015 inayoeleza kuwa rasilimali za uvuvi zinaendelezwa, zinasimamiwa, zinahifadhiwa na kutumika kwa uendelevu kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya binadamu", alisema.


Mkurugenzi Msaidizi uendelezaji wa rasilimali za Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Merisia Mparazo akiongea wakati wa kufungua  kikao cha wataalam wa mradi wa SWIOFIC-Nairobi Convention  kilichofanyika kwenye Wilaya ya Nkinga Mkoani Tanga Januari 24,2023 lengo likiwa ni pamoja na kuwezesha ushirikiano katika masuala ya usimamizi wa mazingira na Uvuvi Ili kuimarisha usalama wa Chakula kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na kuimarisha maisha ya jamii za wavuvi kwa ujumla.


Mratibu wa mradi wa SWIOFIC -Nairobi Convention Bi. Ulrika Gunnartz akiwasiliasha mada wakati wa kikao cha kamati ya wataalam wa mradi huo kilichofanyika kwenye Wilaya ya Nkinga Mkoani Tanga Januari 24, 2023


Mratibu wa Sekta ya Uvuvi kitaifa kutoka Shirika la chakula na kilimo la umoja wa Mataifa (FAO), Bi. Olivia Mkumbo (wa pili kutoka kushoto) akiwasilisha mada wakati wa kikao cha kamati ya wataalam wa mradi wa SWIOFIC -Nairobi Convention kilichofanyika kwenye Wilaya ya Nkinga Mkoani Tanga Januari 24,2023


Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Bw. Tumaini Chambua akiwasilisha mada wakati wa  kikao cha kamati ya wataalam wa mradi wa SWIOFIC -Nairobi Convention kilichofanyika kwenye Wilaya ya Nkinga Mkoani Tanga Januari 24,2023 lengo likiwa ni pamoja na kuwezesha ushirikiano katika masuala ya usimamizi wa mazingira na Uvuvi Ili kuimarisha usalama wa Chakula kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na kuimarisha maisha ya jamii za wavuvi kwa ujumla.


Afisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais ambae pia ni Afisa kiungo wa Nairobi Bi. Magdalena Ngotolainyo akiwasilisha  mada wakati wa kikao cha kamati ya wataalam wa mradi wa SWIOFIC -Nairobi Convention kilichofanyika kwenye Wilaya ya Nkinga Mkoani Tanga Januari 24,2023 lengo likiwa ni pamoja na kuwezesha ushirikiano katika masuala ya usimamizi wa mazingira Ili kuimarisha usalama wa Chakula, kushughulikia mabadiliko ya tabia nchi na kuimarisha maisha ya  jamii za wavuvi kwa ujumla.


Sehemu ya washiriki wa kikao cha kamati ya wataalam wa mradi wa SWIOFIC -Nairobi Convention wakisikiliza kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa na wawezeshaji (hawapo pichani) wa kikao hicho kilichofanyika kwenye Wilaya ya Nkinga Mkoani Tanga Januari 24,2023.

 

Mkurugenzi wa huduma za Mifugo nchini Prof. Hezron Nonga akifafanua jambo wakati wa kikao cha wadau mbalimbali wa sekta ya Mifugo waliokutana leo (24.01.2023)  kwenye ukumbi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi uliopo eneo la Mtumba jijini Dodoma ili kujadili rasimu ya Mwongozo ulioboreshwa wa Utambuzi wa Mifugo.


Sehemu ya wadau wa sekta ya Mifugo wakipitia rasimu ya Mwongozo ulioboreshwa wa utambuzi wa Mifugo wakati wa kikao cha kujadili rasimu hiyo kilichofanyika leo (24.01.2023) kwenye Ukumbi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi uliopo eneo la Mtumba jijini Dodoma.

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YAWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO ILIYOGHARAMIWA KWA FEDHA ZA MKOPO KUTOKA SHIRIKA LA FEDHA LA KIMATAIFA (IMF) KUPITIA DIRISHA LA EXTENDED CREDIT FACILITY (ECF) KWA KIPINDI CHA NUSU MWAKA KUANZIA JULAI HADI DISEMBA 2022 KWENYE KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakati Wizara ilipowasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo iliyogharamiwa kwa fedha za Mkopo kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kupitia dirisha la Extended Credit Facility (ECF) kwa kipindi cha Nusu Mwaka kuanzia Julai hadi Disemba 2022. (23.01.2023)


Katibu Mkuu Waziri wa Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda (wa pili kutoka kushoto) akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoulizwa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakati Wizara ilipowasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo iliyogharamiwa kwa fedha za Mkopo kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kupitia dirisha la Extended Credit Facility (ECF) kwa kipindi cha Nusu Mwaka kuanzia Julai hadi Disemba 2022. (23.01.2023)


Katibu Mkuu Waziri wa Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakati Wizara ilipowasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo iliyogharamiwa kwa fedha za Mkopo kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kupitia dirisha la Extended Credit Facility (ECF) kwa kipindi cha Nusu Mwaka kuanzia Julai hadi Disemba 2022. (23.01.2023)


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakifuatilia wasilisho la taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo iliyogharamiwa kwa fedha za Mkopo kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kupitia dirisha la Extended Credit Facility (ECF) kwa kipindi cha Nusu Mwaka kuanzia Julai hadi Disemba 2022. (23.01.2023)