Nav bar

Jumanne, 31 Januari 2023

WAFUGAJI WANAOHAMA BONDE LA MTO KILOMBERO WASIZUIWE-NDAKI

◼️ Awashangaa watendaji wanaowawekea vikwazo 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amewaagiza viongozi na watendaji wote mkoani Morogoro kutowazuia wafugaji wanaohama kutoka bonde la Mto Kilombero ambapo amesema kuwa kufanya hivyo ni kukwamisha utekelezaji wa agizo la Serikali linalowataka wafugaji na wakulima kuondoka kwenye bonde hilo.


Mhe. Ndaki amesema hayo jana (27.01.2023) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Nakaguru iliyopo  Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro ambao ulijumuisha wafugaji na wakulima wanaozungukwa na bonde la Mto Kilombero.


“Tangazo la Serikali la kuondoka kwenye  bonde la mto Kilombero ni sahihi na sisi wafugaji tunapaswa kuliheshimu kwa sababu ni lazima tuondoke kwenye bonde hilo kwa sababu ni tuna wajibu wa kulinda maeneo tengefu, oevu na yale yote yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo lakini cha kushangaza naambiwa kuna baadhi ya watendaji wanawazuia wafugaji wanaotaka kuhamia kwenye maeneo mengine waliyoyapata mbali na hapa, Tuwape vibali waondoke” Amesisitiza Mhe. Ndaki.


Katika kutekeleza agizo hilo, Mhe. Ndaki amewasisitiza viongozi wa maeneo yenye wafugaji wanaopaswa kuhama, kuhakikisha wanawatafutia wafugaji hao maeneo ya kuhamia ili zoezi hilo la kuwahamisha lisiathiri shughuli zao za ufugaji.


“Najua kuna maeneo ambayo mliyatenga kama maeneo ya malisho lakini kwa bahati mbaya yamevamiwa na watumiaji wengine wa ardhi, hakikisheni mnawaondoa wavamizi hao na kugawa maeneo hayo kwa wafugaji watakaohama kwenye bonde hilo” Ameongeza Mhe. Ndaki.


Akielezea namna watakavyotekeleza maagizo hayo Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Danstan Kyoba ameahidi kukutana na viongozi na watendaji mbalimbali wa Wilaya hiyo kwa ajili ya kuanza kutenga maeneo ambayo watahamia wafugaji na wakulima wanaoondoka kwenye bonde la mto Kilombero.


“Ndani ya siku 100 mimi na timu ya wataalam wangu tutatembelea kwenye vijiji vyote vinavyoguswa na mpango huu wa kuondoka kwenye bonde hilo ili tukubaliane maeneo watakayohamia lakini kwanza tutekeleze agizo la kuondoka” Ameongeza Mhe. Kyoba.


Bonde la Mto Kilombero linazungukwa na vijiji 23 vilivyopo Wilayani Kilombero ambavyo ni Luwembo, Maulanga, Miwangani, Namwawala, Idandu, Kalenga, Kikwambi, Mofu, Miyomboni, Nakagulu, Ijia, Isago, Luvilikila, Mkangawalo, Chita, Melela, Chisano, Karangekelo, Msolwa, Miembeni, Kibugasa na Ngalimila.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wafugaji wa Wilaya ya Kilombero jana (27.01.2023) kwenye Mkutano uliofanyika ukumbi wa shule ya sekondari Nakaguru iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro ambapo alisisitiza suala la  kuondoka kwa wafugaji waliopo kwenye bonde la Mto Kilombero.

Sehemu ya wafugaji na wakulima wa Wilaya ya Kilombero wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati wa Mkutano baina yake na wao uliofanyika jana (27.01.2023) kwenye Ukumbi wa shule ya sekondari Nakaguru iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni