Nav bar

Jumanne, 24 Mei 2022

KAMBAMITI KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA KUKUZA SEKTA YA UVUVI - DKT. TAMATAMAH

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amesema Rasilimali ya samaki aina ya kambamiti  ni muhimu katika kutoa ajira, kipato, chakula na lishe, na  kuliingizia Taifa fedha za kigeni kama aina nyingine za samaki na hivyo kuchangia katika kupunguza umaskini kwa wananchi.


Dkt. Tamatamah aliyasema hayo wakati wa kikao na wakuu wa idara, Taasisi na Vitengo  wa sekta hiyo kujadili juu ya rasimu ya mpango wa usimamizi wa zao la kambamiti kilichofanyika jijini Dodoma Mei 23, 2022.


Alisema wote tunafahamu kuwa, kabla ya mwaka 2007, uvuvi wa kambamiti ulikuwa ukifanywa na wavuvi wote wakubwa na wadogo, na mwaka 2007 uvuvi huo ulifungwa kwa wavuvi wakubwa kufuatia taarifa za utafiti zilizothibitisha kuendelea kupungua kwa rasilimali hiyo na hivyo kutisha uendelevu wake.


Hivyo kufuatia changamoto hiyo mwaka 2012, Serikali iliandaa mpango wa usimamizi wa rasilimali ya kambamiti wa miaka mitano ulioanza kutekelezwa mwaka 2013 na kuisha muda wake  mwaka 2017 ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali ya kambamiti. 


"kupungua kwa rasilimali ya kambamiti kulihusishwa na changamoto mbalimbali ikiwa  kuongezeka kwa vyombo vya uvuvi,  uvuvi usiozingatia sheria na taratibu pamoja na mabadiliko ya tabia, hivyo Serikali kupitia  Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) iliendelea kufanya utafiti ili kutoa taarifa za kisayansi kuhusu hali halisi ya kuongezeka kwa rasilimali." Alisema Dkt. Tamatamah


Dkt. Tamatamah aliongeza kuwa Wizara kupitia Idara ya Uvuvi iliona umuhimu wa kuufanyia mapitia ili uweze kuendana na hali iliyopo ya mabadiliko ya kisera, kiteknolojia na miongozo mbalimbali ya kiusimamizi.


“Mchakato wa kufanya mapitio ulianza mwaka 2019/2020 kwa ufadhili wa mradi wa SWIOFish unaofadhiliwa na Benki ya Dunia chini ya uratibu wa mtaalamwa uvuvi Bw. Yahya Mgawe kwa kushirikiana na kamati ya kitaifa ya kusimamia uvuvi wa kambamiti kama uvuvi wa kipaumbele kwenye mradi wa SWIOFish. Alisema Dkt. Tamatamah.


Aidha Dkt. Tamatamah amempongeza Mtaalam wa Uvuvi aliyeongoza mchakato wa maandalizi ya rasimu hiyo na kamati ya kitaifa ya kusimamia uvuvi wa kambamiti kwa kusimamia kikamilifu zoezi hilo hadi kupatikana kwa rasimu ya mpango wa usimamizi wa uvuvi wa kambamiti utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2022 chini ya ufadhili wa benki ya dunia.


Rasilimali ya kambamiti hupatikana katika ukanda wa bahari ya hindi hususan kwenye maeneo ya maingilio ya mito. Mikoa inayoongoza kwa kuwa na rasilimali hiyo ni Pwani (Bagamoyo, Kibiti, Mkuranga), Lindi (Kilwa), na Tanga (Pangani)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa tatu kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi mara baada ya kikao kifupi cha kupitia, kujadili na kupitisha rasimu ya mpango wa Usimamizi wa Rasilimali ya kambamiti kilichofanyika kwenye ukumbi wa NBC Jijini Dodoma. Mei 23, 2022.


Sehemu ya washiriki wakiwa kwenye kikao cha kupitia, kujadili na kupitisha rasimu ya mpango wa Usimamizi wa Rasilimali ya kambamiti kilichofanyika kwenye ukumbi wa NBC Jijini Dodoma. Mei 23, 2022


NDAKI AZINDUA ZOEZI LA UUZAJI MADUME BORA YA NG'OMBE NCHINI

Na Mbaraka Kambona, 


Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imezindua zoezi la uuzaji wa madume bora ya ng'ombe aina ya Borani ili kuwawezesha Wafugaji nchini kuboresha mifugo yao ili iwe na tija zaidi kuliko hivi sasa ambapo wengi wana makundi makubwa ya ng'ombe huku tija yake ikiwa ni ndogo.


Hafla fupi ya uzinduzi wa zoezi hilo la uuzaji wa madume bora ya ng'ombe aina ya Borani ilifanyika katika Ranchi ya Kongwa iliyopo Wilayani Kongwa, jijini Dodoma Mei 21, 2022.


Wakati akizindua zoezi hilo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi alisema anaimani kuwa uuzaji wa madume hayo bora kutasaidia wafugaji wengi kupata mbegu bora itakayosaidia kuboresha ufugaji wao.


Alisema kuwa wafugaji ni vyema kutumia fursa hiyo vizuri na kuchangamkia madume hayo huku akiwataka kuamini kuwa na mifugo michache iliyobora ndio utajiri kuliko kuwa na kundi kubwa la ng'ombe ambalo tija yake ni ndogo.


Aliendelea kuwakumbusha wafugaji kuwa wakiendelea kuamini kuwa na makundi makubwa ya ng'ombe ndio ufahari jambo hilo halitawasaidia kwa sababu hali ya  mabadiliko ya tabia nchi hairuhusu hilo lakini pia hakuna ardhi ya  kutosha ya kumuwezesha kila mfugaji kuwa na kundi kubwa la mifugo.


"Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametupa kazi ya kuhakikisha kwamba ng'ombe hawa wanakuwa na tija na kumsaidia mtanzania kuongeza kipato chake na kuchangia kwa sehemu kubwa katika pato la nchi yetu", alisema


Hivyo, aliitaka Kampuni ya NARCO kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu na kuendelea kuuza madume bora mengi kwa bei nzuri ili wafugaji wengi waweze kuyapata kwa urahisi madume hayo na kuboresha mifugo yao.


"Sasa muanze kufikiria namna ambavyo mtazalisha madume haya kwa wingi ili muwe mnayauza kila baada ya miezi sita na tukifanikiwa kufanya hivyo mabadiliko kwa wafugaji wetu yatakwenda kwa haraka sana ," alisisitiza


Waziri Ndaki aliongeza kwa kusema kuwa Serikali imedhamiria kuboresha mifugo ili wafugaji wanufaike na mifugo yao kwa kupata masoko ya uhakika ya kuuza mifugo yao na mazao yake ndani na nje ya nchi.


Aidha, alisema kuwa Serikali imepanga kufanya kampeni kubwa ya uhimilishaji wa mifugo itakayofikia wafugaji wote nchini ili wapate mifugo itakayokuwa na tija katika maisha yao na nchi kwa ujumla.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe alisema wameanza kuuza madume 197 kutoka katika Ranchi za Kongwa, West Kilimanjaro na Kalambo  na yote wamelenga yauzwe kwa wananchi ili waweze kuboresha mifugo yao.


Alisema madume hayo ya Borani yanafaa sana kwa ajili ya uzalishaji wa nyama huku akisema kuwa dume mmoja  anaweza kuzalisha majike mpaka hamsini hivyo kupitia madume hayo itaongeza idadi kubwa ya ng'ombe bora kwa wafugaji.


"Dume wa miaka 2 ambaye atakupa huduma kwa zaidi ya miaka 10 atauzwa kwa shilingi Milioni 3 na dume wa miaka 3 na kuendelea atauzwa kwa shilingi Milioni 3.5", alisema


Naye Mwenyekiti wa Wafugaji wa Wilaya ya Kongwa, Mshando Parutu alisema kuwa hatua hiyo iliyochukuliwa na NARCO ni muhimu kwa mustakabali wa wafugaji nchini huku akiwaomba Wafugaji kuchangamkia fursa hiyo ili kuboresha namna ya ufugaji wao.


Mmoja wa Wafugaji aliyenunua ng'ombe hao, Ibrahim Matiko alisema kuwa kilichomvutia kununua ng'ombe hao ni kuwa kupitia madume hayo ya Borani atapata mbegu iliyobora itakayosaidia kubadilisha mifugo yake ya asili kuwa ya kisasa yenye tija kubwa zaidi.


Pichani ni baadhi ya ng'ombe bora aina ya Borani wanaouzwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO). Uzinduzi wa zoezi la uuzaji wa ng'ombe hao ulifanyika katika Ranchi ya Kongwa, Wilayani Kongwa, jijini Dodoma Mei 21, 2022.


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe (kulia) akimueleza jambo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) katika hafla fupi ya kuzindua zoezi la uuzaji wa madume bora ya ng'ombe aina ya Borani iliyofanyika kwenye Ranchi ya Kongwa, Wilayani Kongwa, jijini Dodoma Mei 21, 2022. Wakati akizindua zoezi hilo, Mhe. Ndaki alimtaka Prof. Msoffe kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu ili kuwawezesha Wafugaji kuboresha Mifugo yao kupitia madume hayo.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akifurahia jambo na mmoja wa Wafugaji waliohudhuria hafla fupi ya uzinduzi wa uuzaji wa madume bora ya ng'ombe aina ya Borani iliyofanyika kwenye Ranchi ya Kongwa, Wilayani Kongwa, jijini Dodoma Mei 21, 2022.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akiwakagua Ng'ombe aina ya Borani walioandaliwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa NARCO kwa ajili ya kuuzwa kwa Wafugaji katika hafla fupi ya uuzaji ng'ombe hao iliyofanyika katika Ranchi ya Kongwa, Wilayani Kongwa, jijini Dodoma Mei 21, 2022.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akiwa amekata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa zoezi la uuzaji wa madume ya ng'ombe  bora aina ya Borani lililofanyika katika Ranchi ya Kongwa, Wilayani Kongwa, jijini Dodoma Mei 21, 2022.

Baadhi ya Wafugaji waliohudhuria hafla fupi ya uzinduzi wa uuzaji wa madume bora ya ng'ombe aina ya Borani wakikagua ng'ombe hao ambao wanauzwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kwa bei ya kuanzia shilingi Milioni 3 hadi Milioni 3.5. Zoezi hilo la kuuza madume kwa mtindo huo linatajwa kuwa ndio la kwanza tangu kampuni hiyo ianze kazi hapa nchini.

MIRADI YA MAENDELEO MKURANGA IPO KATIKA HATUA NZURI - NZUNDA

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda jana tarehe 20 Mei 2022 alifanya ziara ya kukagua miradi ya Maendeleo inayotekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Mkoani Pwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga na kuridhishwa na kiwango cha utekelezaji wa miradi hiyo mbali ya mapungufu madogomadogo aliyoelekeza kurekebishwa mara moja kabla ya kukamilisha miradi hiyo 30 Mei 2022 .


"Nakupongeza kwa kazi nzuri unayoendelea kufanya pamoja na kwamba ulipatwa na changamoto ya ajali lakini unaendela vizuri na utekelezaji wa mradi huu."

Alisema Nzunda alipokuwa anakagua ujenzi wa kisima katika kijiji cha Matanzi.


Miradi inayotekelezwa Katika Halmashauri ya Mkuranga inayosimamiwa Moja kwa moja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) ni pamoja na ujenzi wa Mnada wa Kisasa wa upili unaojengwa katika kijiji cha Chamgoi wenye thamani ya Tsh. 

300, 274, 584.09 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 45.75.


Aidha, mradi mwingine alioutembelea Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo ni ujenzi wa kisima kirefu cha kunyweshea Mifugo Maji, kisima hicho kinajengwa katika Kijiji cha Matanzi ambapo gharama za ujenzi ni Tsh. 162,309,590.00 ambapo ujenzi wa kisima hicho umefika asilimia 80. 


Vile vile katika Kijiji cha Tundu, Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga  linajengwa Josho lenye thamani ya Tsh.29, 719,500.00 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 70.


Pamoja na kuendelea Vizuri kwa utekelezaji wa Miradi hiyo ya Maendeleo Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Nzunda ameelekeza wakandarasi hao kufanya kazi usiku na mchana ili ifikapo tarehe 30/05/2022  wawe wamemaliza utekelezaji wa Miradi hiyo,vinginevyo kuanzia tarehe 01/06/2022 kama watakuwa hawajamaliza miradi hiyo,wakandarasi hao wataanza kukatwa "LIQUIDATION"kulingana na makubaliano ya Mkataba.


"Fanyeni kazi usiku na mchana,maana siwezi kuwaongezea Muda wa ziada wa utekelezaji wa Miradi hii, ikifika tarehe 01/06/2022 kama mtakuwa hamjakamilisha utekelezaji wa miradi hii nitaanza kuwataka Liquidation". Alisema Nzunda.


Aidha, Nzunda ameelekeza halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kusimamia miradi hiyo ya Maendeleo kwa ukaribu  na kutoa fikra potofu kuwa miradi hiyo ni ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwani wanufaika wa Miradi hiyo ni wananchi wa maeneo husika.


"Simamieni Miradi hii na kuhakikisha kuwa inatekelezwa kwa kiwango kilichokusudiwa  na inakamirika kwa wakati na kwa muda uliopangwa ili wananchi hawa waweza kupata huduma kwa wakati".Alisema Nzunda.


Nzunda alisema kuwa kwa sasa Wizara imeandaa mpango mkakati wa Mabadiliko ya Sekta ya Mifugo ambapo mpango huo utaanza utekelezaji wake mwaka wa fedha 2022/2023, maeneo Muhimu yaliyotiliwa Mkazo katika mpango Mkakati huo ni pamoja na uzalishaji wa Mifugo ya kisasa na yenye tija, uhamasishaji wa uzalizaji wa Malisho, uchimaji wa Malambo na Visima Virefu vya maji kwa kushirikiana na Sekta binafsi.


Aidha, Maeneo mengine yatakayotiliwa mkazo pia ni maeneo ya Utafiti wa mbari za Mifugo, huduma za ugani kwa Sekta ya Mifugo, Masoko pamoja na maeneo yote ya Ranchi za Taifa NARCO ambayo hayatumiki pamoja na holding Ground kuyatafutia namna bora ya kuweza kukodisha kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili yaweza kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Bi. Anna Kiria alimshukuru Katibu Mkuu Mifugo kwa uamuzi wa kupeleka Miradi hiyo ya maendeleo katika Wilaya hiyo, alisema kuwa miradi hiyo itaboresha Ustawi wa Sekta ya Mifugo na Mazao yake pamoja na kurahisisha biashara ya Mifugo.


Vilevile Kiria alisema kuwa changamoto kubwa iliyopekekea kuchelewa kukamilika kwa Miradi hiyo ni pamoja na barabara kutopitika kipindi cha mvua na kupelekea kushindwa kwa mkandarasi kupeleka vifaa vya ujenzi eneo la mradi.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo)Bw.Tixon Nzunda (Kushoto) akisikiliza maelezo ya ujenzi wa Mradi wa kisima kutoka kwa mkandarasi  Bw.Buddy Muhammed (aliyesimama Kulia) unaojengwa katika kijiji cha Matanzi Wilayani Mkuranga.Wengine katika Picha ni kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mkuranga pamoja na wananchi wa kijiji cha Matanzi.


Hiyo ni Miundombinu ya Mabirika ya Kunyweshea maji Mifugo katika kisima cha matanzi kilichopo Wilayani Mkuranga mkoani Pwani.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda akizungumza na Wananchi waliojitokeza katika mnada wa Upili wa Chamgoi jana tarehe 20/05/2022 Mkuranga alipofanya ziara katika Wilaya hiyo. Lengo la ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayosimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo)


Mwonekano wa Kisima cha kunyweshea Mifugo maji katika kijiji cha  Matanzi Wilayani Mkuranga.Lengo la utekelezaji wa Mradi huu wa Kisima ni kusogeza huduma karibu kwa Wafugaji na wananchi wa maeneo husika.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda akiwasili Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga na kupokelewa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo jana tarehe 20/05/2022.Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Bi.Veronica Kinyemi.


Baadhi ya Miundombinu inayojengwa katika mnada wa Upili wa Chamgoi katika halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga.
SERIKALI YAFICHUA ILIVYOPATA MWAROBAINI WA MAGONJWA YA MIFUGO NA MASOKO.

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka wazi namna ilivyofanikiwa kupata suluhu ya changamoto ya ukosefu wa masoko ya mazao ya Mifugo na uhaba wa chanjo za magonjwa mbalimbali ya Mifugo.


Hayo yamebainishwa leo (20.05.2022)  na Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia afya ya jamii ya veterinari, udhibiti wa pembejeo, mifugo na mazao yake kutoka Wizarani hapo ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu (Mifugo)  Dkt. Stanford Ndibalema wakati wa hotuba yake ya kufunga mafunzo ya Siku 3 ya mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi unaojulikana kama “ Mifugo Management Information System (MIMIS)”  kwa wataalam na wadau waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya Mifugo na Uvuvi yaliyokuwa yaliyofanyika kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.


Dkt. Ndibalema amesema kuwa mara baada ya kukamilika kwa Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika nchi za falme za kiarabu, Wizara yake ilipokea wakaguzi ambao walifika katika Viwanda vya kusindika nyama vilivyopo hapa nchini ikiwa ni pamoja na kiwanda cha Chobo kilichopo mkoani Mwanza, Elia kilichopo mkoani Arusha na Tanchoice kilichopo mkoani Pwani.


“Baada ya ukaguzi ule walikubali kuanza kuagiza nyama kutoka Kiwanda cha Tanchoice na Elia na kutoa maoni kadhaa ya kuboresha kwa viwanda vingine ambapo maoni hayo yameshaanza kufanyiwa kazi”  Amesema Dkt. Ndibalema.


Mbali na uwepo wa soko katika nchi za Jamhuri ya falme za kiarabu, Dkt. Ndibalema amesema kuwa tayari nchi za  China, Qatar na Oman zimeshafungua soko la nyama inayozalishwa hapa nchini na wafanyabiashara wa zao hilo wameshaanza kunufaika na fursa hiyo.


Akizungumzia kuhusu hali ya upatikanaji wa kinga  za magonjwa mbalimbali ya Mifugo Dkt. Ndibalema ameeleza kuwa hivi sasa idadi ya  vifo vya mifugo  vinavyotokana na kupe imepungua kwa kiasi kikubwa hasa baada ya Serikali kuanza kutoa bure dawa za kuogeshea mifugo hiyo.


“Sasa kazi iliyobaki ni kwa Halmashauri na kamati za majosho kuhakikisha dawa zote zinazotolewa na Serikali zinaelekezwa kwenye majosho kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji kukinga mifugo yao” Ameongeza Dkt. Ndibalema.


Dkt. Ndibalema amebainisha kuwa hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali katika kulinda afya ya mifugo ni kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa kampuni kutoka nchini India ambayo imejenga kiwanda kikubwa cha kutengeneza chanjo mbalimbali za mifugo kinachojulikana kama “Heister” kilichopo Kibaha mkoani Pwani.


“Kwa sasa Kiwanda hicho kinatengeneza chanjo 3 ambazo ni ile ya homa ya mapafu ya ng’ombe, homa ya mapafu ya mbuzi na chanjo ya Sotoka ya mbuzi na kondoo na kwa kwa Serikali yetu ni sikivu inapokea maoni ya kuboresha eneo lolote ambalo mfugaji au mdau wetu yoyote anadhani linapaswa kurekebishwa” Amesema Dkt. Ndibalema.


Wakizungumzia matarajio yao baada ya kuanza kutumia mfumo huo, baadhi ya wadau walioshiriki mafunzo hayo wamesema kuwa mfumo huo utawasaidia kurahisisha kazi zao, kuongeza faida kwenye biashara zao za mazao ya mifugo na kuokoa muda ambao watautumia kufanya shughuli nyingine za maendeleo.


Mafunzo hayo ya Siku 3 yamelenga kuongeza ufanisi wa biashara ya mazao yanayotokana na mifugo na vyakula samaki na utekelezaji wa mfumo huo unatarajiwa kuanza mapema mwezi juni mwaka huu.


Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi  (Mifugo) ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia afya ya jamii ya veterinari, udhibiti wa pembejeo, mifugo na mazao yake kutoka Wizarani hapo Dkt. Stanford Ndibalema akieleza jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya ufugaji nchini wakati wa hotuba yake ya kufunga mafunzo ya Siku 3 ya mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi  kwa wataalam na wadau waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya Mifugo na Uvuvi yaliyokuwa yaliyofanyika kwa siku 3  (Mei 18-20, 2022)  kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.


Baadhi wa washiriki wa mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi wakimsikiliza Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi  (Mifugo) Dkt. Stanford Ndibalema (hayupo pichani)  wakati wa hotuba yake ya kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku 3 (Mei 18-20, 2022) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.


WIZARA YAAHIDI KUANZA KUFANYA MAFUNZO KWA WAELIMISHA RIKA.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi, sekta ya uvuvi imeahidi kuanza kufanya mafunzo mbalimbali kwa waelimisha rika ambao watakuwa kiungo muhimu katika kutekeleza jitihada za kutokomeza Ukimwi, MSY na homa ya Ini mahala pa kazi.


Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alipokuwa akizindua kamati ya VVU, Ukimwi na magonjwa sugu yasiyoambukizwa(MSY) mahali pa kazi, tukio hilo limefanyika leo (20.05.2022) kwenye ukumbi wa ofisi za wizara NBC, Dodoma. 


" Sote tunafahamu kuwa Afya ya watumishi ndio msingi mkuu wa uendeshaji wa Taasisi yeyote. Hivyo, suala la afua za UKIMWI na MSY Mahali pa kazi lisipopewa kipaumbele, Utumishi wa umma unaweza kujikuta unapoteza nguvu kazi kutokana na magonjwa na vifo", amesema Dkt. Tamatamah.


Dkt. Tamatamah ameishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora (OR-MUUUB), Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambao wameshirikiana na wizara kuwezesha kufanyika kwa uzinduzi huo.


Aidha, Dkt. Tamatamah amesema kutokana na umuhimu wa ustawi wa watumishi, Wizara imeona ni vema ikaendelea na jitihada za kujenga uelewa juu ya maambukizi na udhibiti VVU,  UKIMWI, MSY na homa ya ini ili kuhakikisha hali ya uelewa wa kina miongoni mwa watumishi inaongezeka. 


Pia, Dkt. Tamatamah amemalizia kwa kusema ratiba ya majukumu iliyopo itazingatiwa ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa watumishi wote wa wizara, kuhamasisha upimaji wa VVU, MSY na homa ya ini na kuanza chanjo ya homa ya ini pamoja na kuendeleza Jogging Club, Utaratibu wa  Basi darasa na Mazoezi ya viungo.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya VVU/UKIMWI, Magonjwa sugu yasiyoambukizwa (MSY) na homa ya ini mahala pa kazi, mara baada ya kuzindua kamati hiyo, (kuli kwake) ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Amos Machilika, uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Wizara zilizopo ofisi za NBC, leo tarehe 20.05.2022.


Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Wizara ya Mifugo na uvuvi, sekta ya uvuvi, Amos Machilika wa kwanza kushoto akisikiliza kwa makini mwongozo na waraka wa kudhibiti VVU, Ukimwi na MSY mahala pa kazi yanayotolewa na mwakilishi kutoka Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania,(hayupo pichani) wapili ni Dkt. Hafidhi Ameir mwakilishi kutoka TACAIDS,  tarehe 20.05.2022.

Sehemu ya wajumbe wa kamati ya VVU, Ukimwi na magonjwa sugu yasiyoambukizwa (MSY) wakifatilia hotuba ya katibu Mkuu wa sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah (hayupo pichani) alipokuwa akizindua kamati hiyo, leo 20.05.2022.


ULEGA AHIMIZA ZAO LA DAGAA KWENDA KIMATAIFA

Na Mbaraka Kambona,


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Kusafirisha Mizigo (DHL) nchini Tanzania, Bi. Fatma Abubakar kujadiliana namna Serikali na shirika hilo watakavyoweza kushirikiana  kufungua zaidi masoko ya Kimataifa ya  zao la Dagaa na Mwani.


Waziri Ulega alikutana na Mkurugenzi Mtendaji huyo wa DHL  jijini Dodoma Mei 19, 2022.


Akizungumza katika majadiliano yao hayo, Waziri Ulega alisema zao la dagaa kwa muda mrefu limekuwa likiuzwa katika nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Amerika lakini biashara hiyo imekuwa ikifanywa kienyeji sana jambo ambalo limesababisha nchi na watu wake kutokuona tija kubwa ya zao hilo.


"Pamoja na dagaa kuuzwa katika masoko ya nje bado watu wanafanya kienyeji sana, tunatakiwa tuwekeze katika kuliongezea thamani zao la dagaa na kulifungasha vizuri ili liweze kuthaminika katika masoko ya kimataifa na litanunuliwa kwa wingi kuliko ilivyo hivi sasa", alisema


Aliongeza kwa kusema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na dagaa kwa wingi kuanzia baharini na katika maji baridi isipokuwa bado halijawekewa mnyororo wa thamani mzuri ili kulipa heshima yake na kuweza  kuwainua wananchi.


 "Tuweke mipango mizuri ya masoko ya dagaa na mwani ili kusudi tuweze kuona namna tunavyoweza kushirikiana katika kuyaboresha mazao hayo na kuyatafutia masoko ya uhakika nje ya nchi", alifafanua


Alisisitiza kwa kusema kuwa ni muhimu sasa zao la dagaa likapata hadhi yake,  mnyororo wa thamani wa zao hilo uimarishwe ili Wafanyabiashara waondokane na uuzaji wa dagaa katika magunia na waanze  kuwaweka katika vifungashio vizuri vitakavyovutia biashara ya kimataifa.


Aidha,  alisema ni muhimu kuanza kuelimisha  Vikundi vya Ushirika vya uvuvi ambavyo tayari vipo kwani kwa  kufanya hivyo itakuwa rahisi kuwafikia Wafanyabiashara hao  na kuwaelekeza namna ya  kuboresha biashara zao ili ziweze kukidhi masoko ya kimataifa.Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Kusafirisha Mizigo (DHL), Bi. Fatma Abubakar alisema kuwa walianza kuwawezesha Wafanyabiashara wa dagaa katika ukanda wa Ziwa Tanganyika lakini wanakusudia kuupeleka mradi huo pia mkoani Mwanza ili Wafanyabiashara mkoani humo waweze kujua namna ya kufanya ili waweze kuuza dagaa wao nje ya nchi. 


"Kwa upande wetu sisi tunapenda tufanye kazi pamoja  ili tuweze kuwasaidia wafanyabiashara wetu wa Tanzania na waweze kujikimu kimaisha", alisema Abubakar


Kuhusu zao la Mwani, Abubakar alisema kwa sasa wameanzisha mradi wa kuwawezesha wakulima wa mwani  waliopo Visiwani Zanzibar na  wanategemea kuendelea kuwaelimisha ili zao hilo liweze kuwafaidisha zaidi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akiongea na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la kusafirisha mizigo (DHL), Tanzania, Bi. Fatma Abubakar walipokutana ofisini kwake jijini Dodoma Mei 19, 2022.


Sehemu ya timu ya maafisa kutoka Shirika la Kimataifa la kusafirisha mizigo ( DHL) wakifuatilia mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega na Mkurugenzi Mtendaji wa DHL Tanzania, Bi. Fatma Abubakar (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma Mei 19, 2022.


KATIBU MKUU NZUNDA AKABIDHI MAGARI MAWILI KWA VITUO VYA WAKALA YA MAABARA YA VETERINARI TANZANIA

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Tixon Nzunda leo Mei 19,2022 amekabidhi magari mawili kwa vituo vya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania kwenye mikoa ya Arusha na Tabora.


Magari hayo yamenunuliwa na Wakala ya Maabara yya Veteinari Tanzania (TVLA) kwa kutumia fedha za mapato ya ndani kama ilivyopangwa katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2021/20022.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya makabidhiano ya magari hayo katika Ofisi za TVLA Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Nzunda amevitaka vituo ambavyo vimekabidhiwa magari hayo waende wakayatumie magari hayo kwa shughuli za TVLA kwaajili ya mafunzo kwa wafugaji na wadau wao wanaozalisha chakula cha mifugo ili waweze kuongeza tija na kuongeza mapato zaidi kwa taasisi.

"Tumieni magari haya kwaajili ya kutangaza shughuli za taasisi na shughuli za mifugo na kuwafikia wafugaji kwa ukaribu zaidi ili tuweze kutoa chanjo kwa wakati, chanjo zikiwa salama na kuwafikia wadau wengi zaidi lakini kuongeza wigo wa utoaji wa chanjo kwenye mifugo yetu". Amesema Bw.Nzunda.

Amesema sula la chanjo kwa mifugo na sula la uogeshaji wa mifugo halitakuwa jambo la hiari ni jambo la lazima kwasababu ni lazima tulinde ustawi wa wanyama, tulinde ustawi wa wananchi kwasababu mifugo ni chakula kwahiyo lazima iwe na afya bora ili iweze kukidhi viwango vya kitaifa na kimataifa katika mazao yatokanayo na mifugo kwa maana ya nyama na maziwa.

Aidha amevitaka vyama vya wafugaji na taasisi za wafugaji kuunda ushirika kwaajili ya kutafuta fedha ya chanjo lakini pia kuogesha mifugo ili Tanzania iwe mahali salama ili tuendelee kupata masoko makubwa zaidi ya ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt..Stella Bitanyi amesema magari hayo mawili yamenunuliwa kwa thamani ya shilingi Milioni 207 fedha ambazo ni mapato ya ndani.

Ameeleza kuwa malengo ya ununuzi wa magari hayo ni kwenda kutekeleza shughuli za Wakala katika vituo hivyo ambazo ni pamoja na kuwezesha utoaji huduma kwa wafugaji, kuwafikia wafugaji kwaajili ya utoaji wa elimu na mafunzo , shughuli za vituo za kila siku pamoja na kuwezesha uhamasishaji na uuzaji wa bidhaa za Wakala.

"Changamoto waliokuwa wanaipitia ya kukosa usafiri wa uhakika kwa sasa itaenda kwisha na hivyo tunatarajia kuongezeka kwa ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Wakala katika vituo vyao". Amesema Dkt.Stella.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Tixon Nzunda akikata utepele kuzindua na kukabidhi magari mawili kwenye vituo viwili vya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA). Hafla hiyo imefanyika leo Mei 19,2022 katika Ofisi za TVLA Jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Tixon Nzunda akitambulishwa watumishi wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) katika hafla ya makabidhiano ya magari mawili kwa vituo vya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwenye mikoa ya Arusha na Tabora.Hafla hiyo imefanyika leo Mei 19,2022 katika Ofisi za TVLA Jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Tixon Nzunda akipata picha ya pamoja na watumishi wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) katika hafla yya akabidhiano magari mawili kwa kwa vituo vya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwenye mikoa ya Arusha na Tabora.Hafla hiyo imefanyika leo Mei 19,2022 katika Ofisi za TVLA Jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Tixon Nzunda (kulia) akimkabidhi funguo ya gari mmoja wa wawakilishi wa kituo cha Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania Mkoa wa Tabora hafla hiyo imefanyika leo Mei 19,2022 katika Ofisi za TVLA Jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Tixon Nzunda (kulia) akimkabidhi funguo ya gari mmoja wa wawakilishi wa kituo cha Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania Mkoa wa Arusha hafla hiyo imefanyika leo Mei 19,2022 katika Ofisi za TVLA Jijini Dar es Salaam.WAFUGAJI ACHENI KUTOROSHA MIFUGO KWENDA NCHI JIRANI-NZUNDA

Katibu Mkuu Mifugo Bw.Tixon Nzunda amekemea Vikali tabia ya wafugaji kutorosha Mifugo na kwenda kuuza nchi jirani ya Kenya kwa kukwepa kulipa Ushuru na  tozo halali za serikali.


"Wafugaji wetu wanatorosha Mifugo na kwenda kuuza nchi jirani, kwa kukwepa kulipa tozo na Ushuru halali wa Serikali,wanapitisha Mifugo hiyo katika njia zisizo rasmi,na kibaya zaidi kuna baadhi ya watumishi wa Umma na Polisi wasiokuwa waaminifu wanashiriki utoroshaji huo. Alisema Nzunda"


Hayo ameyasema jana 17 May 2022 alipokuwa Mkoani Tanga akikagua miradi mbalimbali ya  Maendeleo ya Sekta Mifugo.


Nzunda amesema kuwa Tanzania ni nchi ya pili barani Africa kuwa na Mifugo mingi ikitanguliwa na Ethiopia, lakini Sekta hiyo ya Mifugo inachangia asilimia 7.1 tu katika pato la Taifa,amewaasa wafugaji hao na watumishi wa Serikali wasiokuwa waaminifu wanaoshiriki zoezi la utorosha Mifugo nje ya nchi kuacha mara moja.


"Unajua Sekta hii ya Mifugo inaweza kuchangia katika pato la taifa hata kwa asilimia 15 mpaka 20, kama wafugaji wetu wakikubali kubadili fikra zao na kuanza kufuga kisasa wakaacha mtindo wa Sasa wa uswagaji wa Mifugo, kwani Botswana wanamaajabu gani, wanamifugo michache lakini inachangia katika pato la taifa kwa asilimia nyingi kuliko sisi wenye Mifugo Mingi" Alisema Nzunda.


Aidha, Nzunda amesema kuwa kwa muda wa Miezi mitatu tangu ateuliwe kuongoza Sekta ya Mifugo, ametengeneza Mpango Makakati wa kubadilisha Sekta ya Mifugo Nchini ambapo kwa sasa suala la kuogesha,kuchanja na kuzalisha Malisho ya Mifugo kwa wafugaji litakuwa sio jambo la hiari tena,bali ni lazima.


"Wafugaji ni wawekezaji kama wawekezaji wengine,mpango huu mkakati wa kubadilisha Sekta ya Mifugo unawataka wafugaji wachanje ,waogeshe ,walime Malisho na wachimbe malambo na Visima vya maji kwa ajili ya Mifugo yao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, lengo ikiwa ni kupata Mifugo bora itakayotupatia nyama bora ili tuweze kuuza nyama hiyo nje ya  nchi kwa sababu Masoko yapo" Alisema nzunda.


Vilevile, Nzunda amesema kuwa kwa mwaka fedha 2022/2023 Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) itaanza utekelezaji wa Mkataba wa kazi "performance Contract" hii itasaidia kwa maafisa ugani  kuhakikisha wanakuwa na Registaya wafugaji walio wahudumia kwa wiki, Mwezi na mfugaji huyo atatakiwa kusaini katika regista hiyo kukubali kuwa amepokea huduma hiyo, hii itasaidia watumishi kutokufanya kazi kwa Mazoea. 


Pia, katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) amewataka Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha zinasimamia miradi yote ya Maendeleo inayopelekwa kwenye mamlaka hizo na Wizara za kisekta ili kuhakikisha wanawabana wakandarasi wanaotekeleza Miradi hiyo ili wasifanye kazi chini ya kiwango.


"Miradi yote inayoletwa na Wizara hizi za kisekta au na Serikali kuu, hakikisheni Sekretarieti ya Mkoa na Halmashauri miradi hiyo mnaisimamia vyema maana ni kwa wafaida ya wananchi wa maeneo husika"


Kwa Upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Bi.Pili mnyema alimshukuru Katibu Mkuu Mifugo kwa kutembelea mkoa huo na kufanya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo ya Sekta ya Mifugo na kuahidi kushirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa kuanza kuifuatilia kwa Ukaribu miradi hiyo.


Aidha, Bi Mnyema alikiri uwepo wa changamoto ya wafugaji kutoroshaji Mifugo nje ya nchi katika mkoa huo,na alisema kuwa wao kama mkoa wanajitahidi kufanya doria ili kuzuia utoroshwaji huo wa mifugo lakini shida kubwa ni uhaba wa vitendea kazi kwa ajili ya  utekelezaji wa kazi hiyo ya doria.


Awali Nzunda alitembelea kiwanda cha Maziwa cha Tanga, alikagua mradi wa  mnada wa Mpakani wa Horohoro unaoendelea kutekelezwa na kampuni ya V. J. MISTRY na kumwagiza Mkandalasi huyo kufanya kazi kwa kasi vinginevyo ifikapo 15 june 2022 ataanza kukatwa "liquidation"

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixson Nzunda akiagana na Mkurugenzi Mtendani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Bi.Veronica Zahara (Kushoto) mara baada ya kumaliza ukaguzi wa mnada wa Mpakani wa Horohoro jana tarehe 17/05/2022 Mkoani Tanga.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda (kushoto) akionyeshwa Ramani ya Mnada wa Mpakani wa Horohoro mkoani Tanga na Site Eng.Rweshogora jana tarehe 17/05/2022 baada ya kutembelea Mnada huo.Lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi ya maendeleo ya Sekta ya Mifugo.

Mwonekano wa Mnada wa Mpakani wa Horoboro uliopo Mkoani Tanga.

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kuanza kutumia mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi unaojulikana kama “ Mifugo Management Information System (MIMIS)” ambao unalenga kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara za Mifugo, kukata na kuhuisha leseni za wataalam wa Mifugo na vibali vinavyohusu uingizaji, uzalishaji na uuzaji  wa vyakula vya samaki.


Hayo yamebainishwa leo na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Mifugo Dkt. Charles Mhina alipokuwa akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo huo kwa wadau na wataalam kutoka sekta za  Mifugo na Uvuvi yaliyofanyika leo (18.05.2022) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.


“Uwepo wa mfumo huu utatusaidia kuokoa muda wa kushughulikia vibali lakini pia utaongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuokoa fedha za Serikali  kwa sababu “Control Number” itazalishwa pale mtu anapofanya maombi tofauti na sasa ambapo mtu anaweza kukimbia  na kitabu cha kukusanyia mapato na baadae kuendelea kukitumia kwa manufaa yake binafsi” Amesema Dkt. Mhina.


Dkt. Mhina amepongeza namna mfumo huo unavyoweza kuchakata taratibu zote zinazohusu vibali kwa wakati mmoja tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kila hatua ilikuwa na mfumo wake hali iliyokuwa ikisababisha usumbufu kwa watumiaji na kusababisha kuchelewesha upatikanaji wa vibali hivyo.


“Kupitia mfumo huu sasa hatutahitaji kujua zilipo karatasi zake za kibali ila tutaangalia tutahitaji tu kufahamu namba ya kibali chake ambayo ni lazima itaonekana kwenye mfumo lakini pia kwa mdau anayenunua ng’ombe wake wakati anawaweka kwenye zizi anaweza kuanza taratibu za kuomba kibali cha kuwasafirisha kupitia mtandao na ndani ya muda mfupi atakuwa ameshapata kibali chake” Ameongeza Dkt. Mhina.


Dkt. Mhina amezipongeza pande zote zilizoshiriki kutengeneza mfumo huo kwa kuziwezesha simu ndogo za mkononi kutumika kwenye mfumo huo jambo ambalo amebainisha kuwa litawawezesha wadau wengi zaidi kuutumia.


Akizungumzia hali ilivyokuwa kabla ya kuanza utekelezaji wa mfumo huo, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia afya ya jamii ya veterinari, udhibiti wa pembejeo, mifugo na mazao yake Dkt. Stanford Ndibalema amesema kuwa hapo awali mfanyabiashara yoyote aliyekuwa anataka kusafirisha mazao ya mifugo alilazimika kuiandikia Wizara barua na mchakato wote ulichukua muda usiopungua wiki mbili.


Naye Mkurugenzi wa kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa upande wa sekta ya Mifugo, Baltazari Kibola ameainisha maeneo ambayo mfumo huo utayaangazia kuwa ni pamoja na eneo la usafirishaji wa mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi, utoaji wa vibali kwa wafanyabiashara wa vyakula vya mifugo na usajili wa wadau waliopo chini ya bodi za nyama na maziwa.


“Lakini pia mfumo huu sasa utaanza kuwasajili kwa njia ya mtandao wataalam wa vitu vinavyohusika na utoaji wa huduma za mifugo kama vile maabara au kliniki za mifugo ambazo zinaratibiwa na Baraza la Veterinari nchini na ikumbukwe hapo awali wataalam hawa walikuwa wanalazimika kupeleka maombi yao Wizarani ndipo mchakato wa kuyashughulikia uanze” Ameongeza Kibola.


Kwa upande wake Mtaalam wa mifumo kutoka kampuni iliyoratibu utengenezwaji wa mfumo huo inayojulikana kama “Trade Mark East Africa” (TMEA) James Temu amesema kuwa kukamilika kwa mfumo huo kutawafanya wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya Mifugo na Uvuvi kupata huduma zote stahiki popote walipo ndani ya muda mfupi.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Charles Mhina (kulia) akifafanua umuhimu wa Mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi unaojulikana kama “ Mifugo Management Information System (MIMIS)” wakati akifungua mafunzo ya mfumo huo kwa wadau na wataalam kutoka sekta za  Mifugo na Uvuvi yaliyofanyika leo (18.05.2022) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa upande wa sekta ya Mifugo, Baltazari Kibola.


Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Prof. Hezron Nonga (kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (Maji baridi) Dkt. Iman Kapinga wakinukuu sehemu ya hotuba ya   Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Charles Mhina (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi unaojulikana kama “ Mifugo Management Information System (MIMIS)”   kwa wadau na wataalam kutoka sekta za  Mifugo na Uvuvi yaliyofanyika leo (18.05.2022) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.


Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi unaojulikana kama “ Mifugo Management Information System (MIMIS)” wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Charles Mhina (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya mfumo huo leo (18.05.2022) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.


BILIONI 5 KUTUMIKA KULINDA HIFADHI ZA BAHARI NCHINI

Na Mbaraka Kambona, 


Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) wamekubaliana kutekeleza Mradi wa kulinda na  kutunza baianuai ya ukanda wa Bahari ya Hindi katika Wilaya ya Mkinga iliyopo Mkoani Tanga.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki alibainisha hayo baada ya kufanya kikao kifupi na Mwakilishi wa shirika hilo nchini, Dkt. Katrina Bornemann kilichofanyika ofisini kwake  jijini Dodoma Mei 18, 2022.


Alisema lengo la mradi huo ambao utagharimu shilingi za kitanzania bilioni 5 ni kuhakikisha maeneo ya bahari pamoja na ukanda wa pwani Wilayani Mkinga yanalindwa na kuhifadhiwa ili yaweze kuwa endelevu na kuleta maendeleo kwa wananchi.


"GIZ wamekubali kutoka kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni 5 kwa ajili ya kutunza mazalia ya samaki, maeneo tengefu na fukwe za bahari ili maeneo hayo yaweze kuwa na tija zaidi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla", alisema


Aliongeza kwa kusema kuwa  wameshakubaliana mradi huo utaanza mara moja na tayari shirika hilo limeshaidhinisha kiasi hicho cha pesa kitumike katika mradi huo utakaodumu kwa miaka 5.


"Tunalishukuru shirika hili la GIZ kwa kuamua kushirikiana nasi katika kutunza baianuai ya bahari nchini, ahadi yetu ni kuwa tutatekeleza mradi huu kwa ustadi na weledi mkubwa kuhakikisha kwamba matokeo yanayotarajiwa yanapatikana na yanaonekana hasa kwa wananchi wetu ambao wataguswa na mradi huu", alibainisha


Mwakilishi wa shirika hilo la GIZ hapa nchini, Dkt. Katrina Bornemann alifika jijini Dodoma kuonana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kuutambulisha mradi huo ili uweze kuanza kutekelezwa mapema kama ilivyokusudiwa.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akipatiwa maelezo kuhusu mradi wa kutunza baianuai unaotarajiwa kutekelezwa hapa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo kutoka nchini Ujerumani (GIZ), Dkt. Katrina Bornemann (kulia) walipokutana jijini Dodoma Mei 18, 2022. Kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akiagana na Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo kutoka nchini Ujerumani (GIZ), Dkt. Katrina Bornemann (kulia) muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo yao jijini Dodoma Mei 18, 2022. Kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah.


SERIKALI YAWATANGAZIA VITA WAVUVI HARAMU

Na Mbaraka Kambona, Mwanza


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema serikali sasa itawekeza nguvu kubwa kukomesha uvuvi haramu katika ziwa viktoria baada ya hatua kadhaa zilizochukuliwa hapo awali ikiwemo kuwashirikisha wavuvi wa kanda ya ziwa kutokuzaa matunda.


Ndaki alitoa kauli hiyo alipokuwa akiongea na wadau wa sekta ya uvuvi katika kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo wavuvi wanaofanya shughuli zao katika ziwa Viktoria kilichofanyika Mkoani Mwanza Mei 16, 2022.


Alisema mwaka jana serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya uvuvi waliandaa mpango shirikishi ambao ulianisha kila mdau na jukumu lake katika ulinzi wa rasilimali za uvuvi katika ziwa viktoria lakini matokeo yake wadau hao hawakujali na sasa uvuvi haramu umeongezeka maradufu.


“Uvuvi haramu sasa hivi ni mkubwa kwenye ukanda wetu wa ziwa viktoria, na sisi wizara tumepewa jukumu la kusimamia rasilimali hizi, Mhe. Rais atatushangaa sana kuona wizara iliyopewa dhamana ya kuhakikisha rasilimali hizi zinalindwa, hazilindwi, sasa wakati tunatafuta mbinu endelevu ya kulinda rasilimali hizi, kuanzia sasa kwenda mbele tutatumia nguvu kuzuia uvuvi haramu”, alisema


Aliongeza kwa kusema kuwa serikali haitavumilia watu wachache wenye kutaka kujinufaisha wao binafsi  huku akiongeza kuwa watawashughulikia wale wote wanaojihusisha na uvuvi haramu kuanzia wavuvi, wasambazaji wa nyavu zisizo halali, na watakamata vyombo vyote vitakavyotumika kubebea au kuhifadhi mazao yaliyovuliwa kwa njia ya haramu katika mikoa yote inayozunguka ukanda wa ziwa viktoria.


Aidha, Waziri Ndaki aliwaeleza wadau wa uvuvi katika kikao hicho kuwa serikali imepokea changamoto zao na watazifanyika kazi lakini nguvu kubwa kwa sasa itawekwa katika kupambana na uvuvi haramu kwa sababu kama rasilimali za uvuvi zikitoweka hizo changamoto nyingine kama za tozo na utafutaji wa masoko hazitakuwa na maana yoyote.


Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia sekta ya uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa serikali imesikiliza kilio cha wavuvi kuhusu tozo na imezishughulikia kwa kiasi kikubwa na hivi karibuni michakato ikikamilika serikali itatoa maelekezo ambayo anaamini yatakuwa na nafuu kubwa kwa wavuvi.


Changamoto kubwa zilizowasilishwa na wadau wa sekta ya uvuvi kwa serikali ni pamoja na uvuvi haramu, matumizi yasiyosahihi ya taa za kuvulia samaki, mlundikano wa tozo kwa mazao ya uvuvi na uhaba wa masoko ya mazao ya uvuvi.


Wadau walioshiriki kikao hicho ni pamoja na viongozi kutoka serikalini, wawakilishi kutoka katika Benki, wavuvi wa Dagaa, wavuvi wa Sangara, wachakataji wa mazao ya uvuvi, wawakilishi wa vyama vya ushirika,wazalishaji wa zana za uvuvi, wafanyabiashara wa taa za sola, wafanyabiashara wa mabondo na wafugaji wa samaki kwenye vizimba.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Sekta ya Uvuvi muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Viktoria kilichofanyika Mkoani Mwanza Mei 16, 2022.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na Wadau wa Sekta ya Uvuvi katika kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Viktoria kilichofanyika Mkoani Mwanza Mei 16, 2022.


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akifafanua baadhi ya mambo katika kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Viktoria kilichofanyika Mkoani Mwanza Mei 16, 2022.

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Emmanuel Bulayi akijibu hoja zilizoibuliwa na wadau wa Sekta ya Uvuvi katika kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Viktoria kilichofanyika Mkoani Mwanza Mei 16, 2022.


Mmoja wa Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Viktoria, Bw. Sospeter Kabongo akionesha moja ya taa ambazo haziruhusiwi kisheria kutumia kuvulia Samaki  na hivyo kumuomba Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki kukomesha matumizi ya taa hizo katika kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Viktoria kilichofanyika Mkoani Mwanza Mei 16, 2022.SEKTA YA UVUVI KUANDAA DAFTARI LA VIASHIRIA HATARISHI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Sekta ya Uvuvi imeanza kuandaa daftari la viashiria hatarishi katika sekta ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001 iliyofanyiwa marekebosho mwaka 2010 katika sura 348.


Akifungua warsha hiyo leo (16.05.2022) Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Bw. Amosi Machilika amesema kuwa lengo la kuandaa daftari la viashiria hatarishi ni kuiwezesha Sekta ya Uvuvi pamoja na wadau wake wanaotekeleza Sera, Mipango, Mikakati na Programu mbalimbali za kisekta kuweza kufikia Malengo yaliyokusudiwa kwa kiwango kikubwa kwa sababu viashiria hatarishi vitakuwa vimewekewa mikakati ya kudhibitiwa kabla ya kutokea na kukwamisha juhudi za Sekta.


Machilika amesema kuwa watendaji wa sekta ya uvuvi wanajukumu la kubaini viashiria hatarishi vinavyoikabili sekta, kubuni mikakati Madhubuti ya kudhibiti viashiria hivyo na kuandaa daftari la viashiria hatarishi.


Pia amesema kuwa Wakuu wa Idara na Vitengo wanao wajibu wa kuhakikisha kwamba shughuli za sekta zinatekelezwa katika maeneo wanayoyasimami kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali ya usimamizi wa fedha za umma, ununuzi, rasilimali watu, mishahara na mikataba, kwa kusimamia haya kikamilifu kutaiwezesha sekta kufikia malengo yake yaliyokusudiwa.


Vilevile Machilika amesema kuwa matarajio ya Sekta ya Uvuvi kwenye warsha hiyo ni kuwawezesha washiriki kupata uelewa mpana kuhusu viashiria hatarishi, kuvichambua kwa umakini na kuviwekea mikakati ya kuvidhibiti au kuviepuka ili kufikia malengo ya Sekta ya Uvuvi.


Aidha, Machilika amesema kuwa Sekta ya Uvuvi imekuwa kwa asilimia 2.5 ambapo mchango wa Sekta ya Uvuvi kwenye Pato la Taifa ni asilimia 1.8 ikilinganishwa na asilimia 1.7 ya mwaka 2020. Ongezeko hilo limetokana na usimamizi Madhubuti wa shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji. Hivyo sekta ya uvuvi imemamua kuandaa kitabu kitakachosaidia kubaini viashiria hatarishi sna kuvifanyia kazi ili kuyafikia malengo yaliyowekwa.


Naye Msaidizi wa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Abraham Msechu amesema kuwa uwepo wa daftari la viashiria hatarishi una faida zake lakini seta ya uvuvi inatakiwa kuhakikisha inalitumia daftari hilo na sio kuishia kwenye kuliandaa.


Akizungumza kabla ya kufunguliwa kwa warsha hiyo, Mkaguzi Mkuu wa Ndani Sekta ya Uvuvi, Costantino Nyilawila alisema kuwa warsha hiyo imeandaliwa kwa ajili ya kuandaa daftari ambalo litasaidia kubaini viashiria hatarishi na kuweka mikakati ya kukabiliana navyo ikiwa ni pamoja na kuvidhibiti. 


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Bw. Amosi Machilika akifungua warsha na Mkutano wa kazi wa Wakuu wa Idara, Vitengo na Wataalam wa Wizara hiyo kuhusu maandalizi ya Daftari la Viashiria Hatarishi (Risk Register) kwenye ukumbi wa Hoteli ya Parklane Jijini Dodoma. (16.05.2022)


Msaidizi wa Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Serikali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Abraham Msechu akielezea umuhimu wa warsha na Mkutano wa kazi wa Wakuu wa Idara, Vitengo na Wataalam wa Sekta ya Uvuvi kuhusu maandalizi ya Daftrai la viashiria hatarishi (Risk Register) kwenye ukumbi wa Hoteli ya Parklane Jijini Dodoma. (16.05.2022)


Mkaguzi Mkuu wa Ndani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Uvuvi, Bw. Constantino Nyilawila akizungumza kabla ya ufunguzi wa Warsha na Mkutano wa kazi wa Wakuu wa Idara, Vitengo na Wataalam wa Sekta hiyo kuhusu maandalizi ya Daftari la viashiria hatarishi (Risk Register) kwenye ukumbi wa Hoteli ya Parklane Jijini Dodoma. (16.05.2022)


Baadhi ya Wakuu wa Idara, Vitengo na Wataalam wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa Warsha na Mkutano wa kazi kuhusu maandalizi ya Daftari la Viashiria Hatarishi (Risk Register) uliofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Parklane Jijini Dodoma. (16.05.2022)

Mwezeshaji wa Masuala ya Usimamizi wa Vihatarishi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Sacko Mwakalobo akiwasilisha mada wakati wa warsha ya Wakuu wa Idara, Vitengo na Wataalam wa Sekta ya Uvuvi kuhusu maandalizi ya Daftrai la viashiria hatarishi (Risk Register) kwenye ukumbi wa Hoteli ya Parklane Jijini Dodoma. (16.05.2022)


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Bw. Amosi Machilika (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha na mkutano wa kazi wa kuandaa Daftari la Viashiria Hatarishi (Risk Register) mara baada ya ufunguzi kwenye ukumbi wa Hoteli ya Parklane Jijini Dodoma. (16.05.2022)