Nav bar

Jumanne, 24 Mei 2022

KAMBAMITI KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA KUKUZA SEKTA YA UVUVI - DKT. TAMATAMAH

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amesema Rasilimali ya samaki aina ya kambamiti  ni muhimu katika kutoa ajira, kipato, chakula na lishe, na  kuliingizia Taifa fedha za kigeni kama aina nyingine za samaki na hivyo kuchangia katika kupunguza umaskini kwa wananchi.


Dkt. Tamatamah aliyasema hayo wakati wa kikao na wakuu wa idara, Taasisi na Vitengo  wa sekta hiyo kujadili juu ya rasimu ya mpango wa usimamizi wa zao la kambamiti kilichofanyika jijini Dodoma Mei 23, 2022.


Alisema wote tunafahamu kuwa, kabla ya mwaka 2007, uvuvi wa kambamiti ulikuwa ukifanywa na wavuvi wote wakubwa na wadogo, na mwaka 2007 uvuvi huo ulifungwa kwa wavuvi wakubwa kufuatia taarifa za utafiti zilizothibitisha kuendelea kupungua kwa rasilimali hiyo na hivyo kutisha uendelevu wake.


Hivyo kufuatia changamoto hiyo mwaka 2012, Serikali iliandaa mpango wa usimamizi wa rasilimali ya kambamiti wa miaka mitano ulioanza kutekelezwa mwaka 2013 na kuisha muda wake  mwaka 2017 ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali ya kambamiti. 


"kupungua kwa rasilimali ya kambamiti kulihusishwa na changamoto mbalimbali ikiwa  kuongezeka kwa vyombo vya uvuvi,  uvuvi usiozingatia sheria na taratibu pamoja na mabadiliko ya tabia, hivyo Serikali kupitia  Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) iliendelea kufanya utafiti ili kutoa taarifa za kisayansi kuhusu hali halisi ya kuongezeka kwa rasilimali." Alisema Dkt. Tamatamah


Dkt. Tamatamah aliongeza kuwa Wizara kupitia Idara ya Uvuvi iliona umuhimu wa kuufanyia mapitia ili uweze kuendana na hali iliyopo ya mabadiliko ya kisera, kiteknolojia na miongozo mbalimbali ya kiusimamizi.


“Mchakato wa kufanya mapitio ulianza mwaka 2019/2020 kwa ufadhili wa mradi wa SWIOFish unaofadhiliwa na Benki ya Dunia chini ya uratibu wa mtaalamwa uvuvi Bw. Yahya Mgawe kwa kushirikiana na kamati ya kitaifa ya kusimamia uvuvi wa kambamiti kama uvuvi wa kipaumbele kwenye mradi wa SWIOFish. Alisema Dkt. Tamatamah.


Aidha Dkt. Tamatamah amempongeza Mtaalam wa Uvuvi aliyeongoza mchakato wa maandalizi ya rasimu hiyo na kamati ya kitaifa ya kusimamia uvuvi wa kambamiti kwa kusimamia kikamilifu zoezi hilo hadi kupatikana kwa rasimu ya mpango wa usimamizi wa uvuvi wa kambamiti utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2022 chini ya ufadhili wa benki ya dunia.


Rasilimali ya kambamiti hupatikana katika ukanda wa bahari ya hindi hususan kwenye maeneo ya maingilio ya mito. Mikoa inayoongoza kwa kuwa na rasilimali hiyo ni Pwani (Bagamoyo, Kibiti, Mkuranga), Lindi (Kilwa), na Tanga (Pangani)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa tatu kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi mara baada ya kikao kifupi cha kupitia, kujadili na kupitisha rasimu ya mpango wa Usimamizi wa Rasilimali ya kambamiti kilichofanyika kwenye ukumbi wa NBC Jijini Dodoma. Mei 23, 2022.


Sehemu ya washiriki wakiwa kwenye kikao cha kupitia, kujadili na kupitisha rasimu ya mpango wa Usimamizi wa Rasilimali ya kambamiti kilichofanyika kwenye ukumbi wa NBC Jijini Dodoma. Mei 23, 2022


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni