Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba
Ndaki amesema atazungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii kuhusu kitendo cha
baadhi ya watumishi wa umma walio chini ya wizara hiyo, ambao wamekuwa
wakiielekeza mifugo kwa makusudi kuingia kwenye hifadhi za taifa ili waikamate
na kuwaonea wafugaji kwa kuwalipisha tozo pamoja na kutaifisha mifugo hiyo.
Waziri Ndaki amezungumza hayo jana
(09.02.2021) wakati akihitimisha ziara yake ya siku mbili Mkoani Kilimanjaro,
kwa kuzungumza na baadhi ya wafugaji katika Wilaya ya Siha mkoani humo mara
baada ya kutembelea Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) na Ranchi ya
West Kilimanjaro zilizopo katika wilaya
hiyo ili kujionea namna wanavyotekeleza majukumu yao.
Amesema kitendo hicho cha kifisadi
hakiwezi kuvumilika na kwamba watuhumiwa wote watatafutwa na kukamatwa ili
hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa ikiwemo kufukuzwa kazi.
“Ninajua kuna wakati tunaonewa unakuta
ng’ombe wako pembeni ya hifadhi wanapelekwa kwa lazima ndani ya hifadhi,
nimesema nazungumza na mwenzangu wa maliasili na utalii na kumwambia huo mtindo
hapana, tuwasake watu wako kwa sababu wenye tabia hiyo siyo wafugaji ni watu wa
Wizara ya Maliasili na Utalii, hao tunaanza kuwasaka mmoja mmoja maeneo yote
wanayokaa karibu na wafugaji tutawabaini na wanachokifanya ni kitendo cha
kiharamu na ufisadi kwa sababu una bunduki unamtisha mfugaji halafu unawapeleka
kwa lazima ng’ombe kwenye hifadhi hiyo na kusema umewakamata ng’ombe kwenye
hifadhi hatutaelewana.” Amesema Mhe. Ndaki
Ameongeza kuwa kitendo hicho lazima
kikemewe kwa kuwa kinarudisha nyuma uwekezaji katika Sekta ya Mifugo na kutaka
watumishi wa umma pamoja na wafugaji kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi
na kwamba lazima kukomesha hatua hiyo kwa sababu inasababisha migogoro kati ya
wafugaji na hifadhi za taifa na kwamba kuna wakati wafugaji wanaelewa maeneo ya
hifadhi, lakini wakipeleka mifugo karibu na maeneo hayo wananyanyaswa na mifugo
yao kulazimishwa kuingia ndani ya hifadhi ili ionekane wameingiza mifugo ndani
ya hifadhi.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameitaka Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO)
kufikia Jumatano ijayo, iwe imeandaa taarifa ya mifugo iliyopo kwenye ranchi
zote hapa nchini, zikiwemo za kiwango cha mifugo inayozaliwa, kufa na aina ya
mifugo iliyopo ili kuona kinachoendelea katika ranchi hizo.
Amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, kuhakikisha
anasimamia zoezi hilo ili taarifa hizo aweze kuzipata siku hiyo ya Jumatano, ikiwa
ni lengo la kuhakikisha mifugo ya serikali inakuwa na tija kwa taifa.
“Tunataka rasilimali ya mifugo
inufaishe taifa na wananchi hawa hatuwezi kuwa na rasilimali ambayo hatujui iko
kiasi gani.” Amefafanua Mhe, Ndaki.
Pia ameitaka NARCO kuhakikisha inatumia
teknolojia ya kisasa ya kuwawekea mifugo iliyopo kwenye ranchi zake ili
kudhibiti vitendo vya wizi wa mifugo ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika
ranchi zake na kuisababishia hasara za mara kwa mara.
Kuhusu uwekezaji wa NARCO katika duka
la kuuzia nyama lililopo Kata ya Sanya Juu Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro,
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameitaka kamati ya ulinzi na
usalama ya wilaya hiyo kufanya uchunguzi juu ya utendaji wa duka hilo baada ya
kutoridhishwa na taarifa zilizorekodiwa tangu kuanza kwake kazi ya uuzaji
nyama.
Waziri Ndaki ameongeza kuwa kumekuwa na
taarifa za mauzo kidogo ya nyama ambayo hayalingani na uhitaji wa nyama eneo
husika, huku akitaka mmoja wa mawakala ambaye aliwahi kuwa na utaratibu wa
kununua nyama katika Ranchi ya West Kilimanjaro kwa bei ya jumla na kwenda
kuuza kwenye duka lake kuchunguzwa na kuitaka kamati hiyo kuwachukulia hatua za
kisheria wale wote watakaobainika kuhujumu utendaji kazi wa duka.
Kwa upande wao baadhi ya wafugaji
waliohudhuria mkutano huo wamelalamikia uvamizi wa wanyamapori ambao wamekuwa
wakiingia katika maeneo yao na kuharibu mazao na malisho ya mifugo hali ambayo
imekuwa ikiwarudisha nyuma katika utendaji wao wa kazi.
Wameongeza kuwa kitendo hicho
kimeathiri kwa kiasi kikubwa malisho ya mifugo na kuiomba serikali kuangalia
hatua ambazo inaweza kuchukua ili kudhibiti kitendo hicho ambacho kimekuwa
kikiwarudisha nyuma mara kwa mara pamoja na kufanya mikakati mbalimbali ya
kuhakikisha dawa na chanjo za mifugo zinawafikia ili kudhibiti magonjwa ya
mifugo ambayo yamekuwa yakiathiri kwa kiasi kikubwa mifugo yao.
Awali kabla ya kikao hicho na baadhi ya
Wafugaji wa Wilaya ya Siha, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa
katika Ranchi ya West Kilimanjaro inayosimamiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa
(NARCO) kujionea utendaji kazi wa ranchi hiyo pamoja na kupokea taarifa ya
namna ranchi hiyo inafanya kazi kutoka kwa meneja wa ranchi hiyo Bw. Raymond
Lutege ambaye amemuambia Waziri Ndaki kuwa ranchi hiyo iko katika hatua
mbalimbali za kuhakikisha mbegu bora za mifugo wakiwemo ng’ombe na kondoo
zinapatikana ili wafugaji waweze kufuga kisasa kwa kuwa na mifugo bora.
Waziri Ndaki akiwa katika Taasisi ya
Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Kituo cha Wilaya ya Siha, mara baada ya
kusomewa taarifa ya kituo na Kaimu Mkurugenzi wa Kanda ya Kaskazini Dkt.
Athuman Nguluma, waziri huyo ameitaka TALIRI kuhakikisha tafiti inazofanya ziwe
na tija kwa wafugaji na taifa kwa ujumla ili tasnia ya ufugaji iweze kubadilika
na kuwa ya kisasa zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Siha
Mhe. Onesmo Buswelu amesema anaimani kubwa na utendaji kazi wa Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki kwa namna alivyoanza kusimamia sekta za mifugo na
uvuvi na kuonesha nia thabiti ya kutatua changamoto zilizopo katika sekta hizo.
Ameongeza kuwa serikali kupitia Wizara
ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada kuhakikisha wafugaji wananufaika
kwa kiasi kikubwa pamoja na kuondoa migogoro kati ya wafugaji na watumiaji
wengine wa ardhi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya wafugaji katika Taasisi ya Utafiti
wa Mifugo nchini (TALIRI) kituo cha Wilaya ya Siha, wakati akihitimisha ziara
yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Kilimanjaro na kuwataka wafugaji wafuge
kisasa na kuwahakikishia kuwa wizara itaendelea kusimamia maslahi ya wafugaji
nchini. (09.02.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akisalimiana na baadhi ya wafugaji wa jamii ya kimaasai
mara baada ya kuzungumza nao alipotembelea Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini
(TALIRI) kituo cha Wilaya ya Siha, wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya
siku mbili Mkoani Kilimanjarao.
(09.02.2021)
Picha ya pamoja ya Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na uongozi wa Wilaya ya Siha, na
baadhi ya kinamama wa jamii ya kimaasai mara baada ya kuzungumza na baadhi ya
wafugaji wa jamii hiyo, alipotembelea Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini
(TALIRI) kituo cha Wilaya ya Siha, wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya
siku mbili Mkoani Kilimanjaro. (09.02.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akifafanua jambo kwa Meneja wa Ranchi ya West Kilimanjaro
Bw. Raymond Lutege (wa kwanza kulia) mara baada ya Waziri Ndaki kufika katika
ranchi hiyo siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani
Kilimanjaro na kutaka ranchi zote za taifa kutumia teknolojia ya kisasa katika
kudhibiti wizi wa mifugo katika ranchi hizo. (09.02.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akipatiwa maelezo ya mbegu bora za mbuzi na
Kaimu Mkurugenzi wa Kanda ya Kaskazini wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini
(TALIRI) Dkt. Athuman Nguluma, mara baada ya Waziri Ndaki kutembelea kituo cha
taasisi hiyo kilichopo Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro wakati akihitimisha
ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo na kuitaka TALIRI ihakikishe
matokeo ya tafiti zake yanakuwa na tija kwa wafugaji. (09.02.2021)
Muonekano wa duka la kuuzia
nyama linalomilikiwa na Ranchi ya West Kilimanjaro iliyo chini ya Kampuni ya
Ranchi za Taifa (NARCO), ambalo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki
ameitaka kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Siha kufanya uchunguzi wa
utendaji kazi wa duka hilo baada ya kutoridhishwa na namna linavyoendeshwa
tangu kuanzishwa kwake. (09.02.2021)