Na. Edward Kondela
Chama cha Wafugaji wa Kuku wa
Nyama nchini (TABROFA) kimetakiwa kuwa
na ushirikiano ili kutokomeza changamoto wanazozipata wafanyabiashara wa kuku
hasa mawakala wasiotambulika wanaouza vifaranga vya kuku wa nyama pamoja na
vyakula vya kuku kwa bei ya juu katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza katika mkutano wa
wafanyabiashara na wazalishaji wa vifaranga vya kuku wa nyama jijini Dar es
Salaam, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema mawakala
wanaotumiwa na wenye viwanda vya kutotolesha vifaranga kama hawajasajiliwa wakamatwe.
“Kuanzia sasa mawakala wa wauzaji wa
vifaranga vya kuku pamoja na chakula cha kuku nataka wafuatiliwe na waeleze
wapi walisajiliwa”. Amesema Mhe.Ndaki.
Aidha, Mhe. Ndaki amewataka wafugaji
wote wanaouza kuku wa nyama
kujisajili Bodi ya Nyama nchini
(TMB) kwa ajili ya biashara kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa
atakayekaidi.
Pia, waziri huyo amewataka wafugaji wa
kuku wa nyama kuanza kuuza kuku kwa uzito badala ya kukadiria ili waweze
kuendana na gharama halisi za ufugaji na kupata faida ili ufugaji uwe na tija
kwao na kutaka TABROFA kusimamia hilo na kuwachukulia hatua wafugaji
watakaoenda kinyume na hilo.
Ameongeza kuwa sekta ya ufugaji ni
muhimu kwa pato la nchi na kuwataka wataalamu wa mifugo kufanya tafiti za
mifugo kwa kuwalenga wafugaji wenyewe kwa kubaini changamoto zao sio kuwatumia
wasomi.
“Tuache kufanya tafiti kwa kuwatumia
bwana shamba na bibi shamba ambao hawafikishi ujumbe kwa wafugaji kuhusu elimu dhidi ya tafiti zilizofanyika,”
ameeleza.
Naye Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Bw.
Imani Sichwale amewataka wafugaji hao kuacha kufuga kuku kwa mazoea bali wafuge
kitaalamu kwa kuweka bajeti ya ufugaji kwa lengo la kukuza tasnia yao.
Hata hivyo Bw. Sichwale amesema kuwa
nyama inasoko nje ya nchi kuliko kuku kwa sababu haijapata vigezo vya uuzaji
nje ya nchi.
Amesema asilimia 80 ya wafugaji wa kuku
wa nyama ni wanawake hivyo amewataka kushikilia tasnia hiyo kwa lengo la
kuondoa umaskini kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha
Wafugaji wa Kuku wa Nyama nchini (TABROFA) Bw. Costa Mrema amesema katika
tafiti walizozifanya zimebaini kuwa ulaji wa kuku wa nyama Tanzania ni kati ya
kuku laki 9 hadi milioni 1.2 kwa wiki.
“Idadi hiyo 70% ya walaji wa kuku wa
nyama ni katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ikifuatiwa na mikoa ya Arusha,
Mwanza, Kilimanjaro na Dodoma”. Amesema Bw. Mrema.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza katika mkutano wa wafanyabiashara na wazalishaji wa vifaranga vya kuku wa nyama jijini Dar es Salaam, ambapo ameagiza kuchukuliwa hatua kwa mawakala wa kuku wasiotambulika pamoja na kuagiza Chama cha Wafugaji wa Kuku wa Nyama nchini (TABROFA) kuwataka wanachama wake kuuza kuku kwa uzito badala ya kukadiria. (17.02.2021)
Kaimu Msajili wa Bodi ya
Nyama nchini (TMB) Bw. Imani Sichalwe akiwataka wafugaji wa kuku kujisajili
katika bodi hiyo ili kufanya shughuli ya ufugaji kuwa rasmi kwao na kuweza
kupata fursa mbalimbali zinazojitokeza pamoja na kusaidiwa kutatua changamoto
zinazowakabili. (17.02.2021)
Mkurugenzi Msaidizi Ukaguzi
wa Nyama na Mazao Yake kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Gibonce Kayuni,
akiwataka wafugaji wa kuku wa nyama (hawapo pichani) kuweka kumbukumbu sahihi
za ufugaji, kushirikisha wataalamu na kuishirikisha wizara katika msaada wa
kisheria mara wanapopata hasara kutokana na kuuziwa vifaranga visivyo na
sifa. Dkt. Kayuni amebainisha hayo katika
mkutano wa wafanyabiashara na wazalishaji wa vifaranga vya kuku wa nyama jijini
Dar es Salaam. (17.02.2021)
Mtendaji Mkuu Wakala ya
Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Dkt. Pius Mwambene akizungumza katika
mkutano wa wafanyabiashara na wazalishaji wa vifaranga vya kuku wa nyama jijini
Dar es Salaam na kuwataka wafugaji kujiunga LITA ili wapatiwe elimu bora ya
ufugaji. (17.02.2021)
Baadhi ya wafugaji wa kuku
wa nyama jijini Dar es Salaam, wakionesha mzani unaoweza kupima kuku kwa mara
moja kuanzia Kilogramu mbili hadi 300 na kuiomba serikali kusimamia azma yao ya
kuuza kuku kwa uzito badala ya bei ya kukadiria ambayo imekuwa ikiwapa hasara
kubwa na kushindwa kuendelea na ufugaji. (17.02.2021)
Baadhi ya washiriki wa
mkutano wa wafanyabiashara na wazalishaji wa vifaranga vya kuku wa nyama jijini
Dar es Salaam, wakisikiliza hoja mbalimbali ambazo zilikuwa zikiwasilishwa
ambapo mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Mashimba Ndaki. (17.02.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni