Na Mbaraka Kambona, Mpwapwa
Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya
Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Dkt. Jonas Kizima amesema utafiti
wanaoufanya umejikita katika kutatua changamoto za mbegu bora za mifugo na
mbegu bora za malisho kwa wafugaji ili sekta ya mifugo iweze kuchangia vyema
katika pato la Taifa.
Dkt.
Kizima aliyasema hayo alipotembelea kukagua shughuli zinazofanywa na
Kituo cha TALIRI Mpwapwa kilichopo Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma Februari 18,
2021.
Alisema kuwa lengo la utafiti
wanaoufanya ni kuhakikisha wanapata mbegu bora za mifugo na kuzalisha mbego
bora za malisho ya mifugo ambazo zitakazosaidia kutatua changamoto za
upatikanaji wa mbegu bora za mifugo zinazohimili mazingira yaliyopo na malisho
inayoikabili nchi kwa sasa.
Aliongeza kuwa kwa sasa taasisi hiyo
inaendelea na kufanya Tathmini ya ubora, ustahimilivu na makuzi ya malisho ya
mifugo yatakayofaa kwa chakula cha kutosha kwa ajili ya mifugo.
Kwa mujibu wa Dkt. Kizima, matokeo
yoyote ya utafiti lazima yabadilishwe kuwa biashara kwa sababu wafugaji
wakifanya ufugaji unaoendana na mazingira yao itawasaidia kutengeneza uchumi na
kuwaongezea tija katika ufugaji wao.
“Tafiti tunazozifanya zinalenga
kuimarisha mnyororo wa thamani wa mifugo ili mchango wa sekta ya mifugo uweze
kuonekana katika uchumi wa kati,” alisema Dkt. Kizima
Dkt. Kizima alisema kuwa TALIRI
imesambaza vituo vyake katika Kanda Saba nchini ili kuwa karibu na wafugaji
kuwasaidia kutatua changamoto zao ili waweze kufanya ufugaji wenye tija.
Alisema vituo hivyo vipo katika Kanda
ya Mashariki, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini, Kanda ya
Magharibi, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Naye, Mkurugenzi, Idara ya Utafiti,
Mafunzo na Huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa alisema kuwa Wizara ya Mifugo
na Uvuvi imezihamasisha Halmashauri zote nchini kuanzisha mashamba darasa ya
malisho ili wafugaji waweze kujifunza na kupata mbegu bora za malisho kwa ajili
ya mifugo.
“Tunawahimiza wafugaji kuona umuhimu wa
kulima malisho ili yaweze kuwasaidia kupata lishe ya uhakika kwa mifugo yao na
pia kwa kulima malisho kutawapunguzia migogoro ya mara kwa mara kati yao na
wakulima,” alisema Dkt. Mwilawa
Aliongeza kuwa wanawahamasisha wafugaji hususan walio katika nyanda kame wastawishe malisho ya mifugo wakati wa masika na kuyatunza ili yaweze kuwasaidia kulisha mifugo yao wakati wa kiangazi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu,
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Dkt. Jonas Kizima akiongea na
Waandishi wa Habari (hawapo pichani) alipotembelea Kituo cha taasisi hiyo cha
TALIRI Mpwapwa kilichopo Wilayani Mpwawa kukagua shughuli zinazofanywa na kituo
hicho Februari 18, 2021.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa akiongea na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati alipokuwa anaeleza kuhusu utafiti wa malisho unaofanywa na Kituo cha Utafiti wa Mifugo (TALIRI) Mpwapwa kilichopo Wilayani Mpwapwa alipotembelea moja ya Shamba la Malisho ya mifugo la kituo hicho Februari 18, 2021. Kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi, Utafiti na Mafunzo, Dkt. Hassan Mruttu.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu,
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Dkt. Jonas Kizima (katikati-
aliyevaa suti nyeusi) akijadiliana jambo na baadhi ya Viongozi kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi na Maafisa wengine wa kituo cha TALIRI Mpwapwa alipotembelea
kituo hicho Februari 18, 2021.
Pichani ni Josho la Nunge.
Josho hilo la kihistoria lilijengwa Wilayani Mpwapwa na Wajerumani mwaka 1905 likiwa ni josho la
kwanza kujengwa Afrika Mashariki. Tangu Josho hilo lijengwe mpaka sasa lina
umri wa miaka 116 na bado linatumika likiwa katika hali nzuri kama linavyoonekana
pichani. (18.02.2020)
Baadhi ya Ng'ombe wanaofugwa katika kituo cha TALIRI Mpwapwa kilichopo Wilayani Mpwapwa wakinywa maji katika kisima kilichotengwa kando ya Josho la Nunge kwa ajili ya kunyweshea mifugo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni