Nav bar

Jumanne, 7 Desemba 2021

FISH4ACP ITACHOCHEA ONGEZEKO LA PATO LA TAIFA KUPITIA SEKTA YA UVUVI-DKT. TAMATAMAH

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa Mradi wa FISH4ACP utasaidia kuongeza nguvu kwenye maboresho ambayo sekta ya Uvuvi inaendelea kuyafanya hivi sasa  kwa ajili ya  kuongeza mchango wa sekta 

Dkt. Tamatamah ameyasema hayo  (06.12.2021) wakati akifungua warsha ya siku mbili ya ukamilishaji mpango wa maboresho ya mnyororo wa thamani wa dagaa na samaki aina ya mgebuka kutoka Ziwa Tanganyika iliyofanyika kwenye ukumbi wa “Kigoma Social Hall” uliopo Manispaa ya Kigoma.

“Lakini pia mradi huu utakuwa na mchango mkubwa katika kutoa ajira hasa kupitia maboresho ya mnyororo wa thamani ya mazao yanayotoka  Tanganyika, utapunguza umasikini miongoni mwa wavuvi na wadau wote watakaohusika kwenye mnyororo huo na kubwa zaidi utaongeza kiwango cha ulaji wa samaki ambao kwa mujibu wa Shirika la Kilimo na Chakula Uliwenguni (FAO) kila Mtanzania anakula kiasi cha kilo 8.5 kwa mwaka hivyo naamini mpaka kukamilika kwa mradi huu angalau kila Mtanzania atakuwa anakula kilo 10.5 kwa mwaka” Amesema Dkt. Tamatamah.

Dkt. Tamatamah ameongeza kuwa katika kuboresha shughuli za Uvuvi wa Ziwa Tanganyika Serikali kupitia kanuni ya Uvuvi ya mwaka 2020, Serikali ilipunguza viwango vya tozo ya usafirishaji wa dagaa inayoenda nje kutoka dola za Marekani 1.5 hadi 0.5 kwa kilo na kwa upande wa Migebuka kutoka Dola za Marekani 0.5 hadi 0.3  jambo ambalo anaamini litahamasisha sana biashara ya mazao hayo ya uvuvi katika masoko ya nje.

“Lakini pia kwa kutambua kuwa  uvuvi endelevu na ulinzi wa rasilimali za uvuvi unategemea uwepo wa taarifa sahihi zinazopatikana kwa wakati za idadi na mtawanyo wa samaki katika vyanzo husika na hapa niishukuru tena Serikali ya awamu ya sita kwa kutenga fedha za utafiti wa utambuzi wa wingi na mtawanyiko wa samaki katika bahari ya Hindi na Ziwa Tanganyika na huu ndo utakuwa utafiti wa kwanza kufanyika tangu nchi yetu ipate uhuru” Amesisitiza Dkt. Tamatamah.

Akizungumza kwa niaba ya Shirika la Chakula na Kilimo Ulimwenguni (FAO), Mwakilishi mkazi wa Shirika hilo kwa upande wa Afrika Mashariki Martin Van Der Knaap amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) katika kusimamia hatua mbalimbali za utekelezaji wa mpango huo ambapo kwa niaba ya Shirika lake  ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakati wote wa utekelezaji wa mpango huo.

“Miaka kadhaa iliyopita Umoja wa Ulaya uliomba miswada mbalimbali itakayolenga kwa undani kuhusu mnyororo wa thamani wa samaki na mazao mengine ya uvuvi katika maeneo mbalimbali na ni miswada 12 tu kati ya zaidi ya 40 ndo ilikubaliwa kuwezeshwa fedha kwa ajili ya utekelezaji ukiwemo huu unaohusu mradi wa FISH4ACP hivyo FAO tunaishukuru sana EU kwa kukubali kufadhili mradi huu ambao umeonekana kutekelezwa vizuri zaidi  Tanzania ukilinganisha na maeneo mengine” Amesema Martin.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara yake imejipanga kuelekeza nguvu katika uvuvi wa bahari kuu ambao unatarajiwa kuboresha uchumi wa mvuvi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

 “Kiukweli eneo ambalo kama sekta bado hatujaliwekea nguvu kubwa ni kwenye upande wa Uvuvi wa bahari na tumegundua moja ya changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya Uvuvi ni uwekezaji mdogo kwenye upande wa Uvuvi wa bahari kuu hasa kutoka sekta binafsi hivyo kwa hivi sasa tumeleekeza nguvu yetu kwenye sera ya uendelezaji wa miundombinu ambapo jambo la kwanza ni ujenzi wa bandari za uvuvi na tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia shilingi bilioni 50.72 ambayo tutaanza kujengea bandari ya Uvuvi huko Kilwa Masoko” Amesema Dkt. Tamatamah.

Dkt. Tamatamah amesema kuwa Serikali imeamua kuwekeza zaidi kwenye uvuvi wa bahari kuu kwa sababu mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea hivi sasa yamesababisha samaki wengi kutopatikana kwenye ukanda wa pwani huku wengi  wakikimbilia katikati ya bahari (deep sea) hivyo ni lazima zifanyike jitihada za kuhakikisha uvuvi kwenye ukanda huo unaendelea.

“ Mbali na Ujenzi wa bandari, Serikali pia kupitia mpango wa tatu wa maendeleo ya Taifa , inatarajia kununua meli 4 za uvuvi ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa suala la Uvuvi wa bahari kuu na kwa mwaka huu wa fedha kupitia Shirika la “IFARD” tutanunua meli mbili  na nyingine mbili tutanunua kabla ya mpango kukamilika mwaka 2025/2026” Amesisitiza Dkt. Tamatamah.

Katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wahisani mbalimbali wanaofadhili miradi ya sekta ya uvuvi, Serikali imetenga fedha zitakazotumika  kwa ajili ya utafiti wa wingi na mtawanyo wa rasilimali za Uvuvi kwa upande wa bahari ya Hindi na Ziwa Tanganyika ambapo kwa mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi milioni 800 zimeshatolewa kwa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) kwa ajili ya utekelezaji wa Utafiti huo.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) Dkt. Ismail Kimirei wakifuatilia maoni ya mmoja wa wadau wa  Uvuvi wa Ziwa Tanganyika wakati wa  warsha ya siku mbili ya ukamilishaji mpango wa maboresho ya mnyororo wa thamani wa dagaa na samaki aina ya mgebuka kutoka Ziwa Tanganyika iliyofanyika kwenye ukumbi wa “Kigoma Social Hall” uliopo Manispaa ya Kigoma  (06.12.2021).Sehemu ya wadau wa Uvuvi wa Ziwa Tanganyika wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah (hayupo pichani) wakati akifungua warsha ya siku mbili ya ukamilishaji mpango wa maboresho ya mnyororo wa thamani wa dagaa na samaki aina ya mgebuka kutoka Ziwa Tanganyika iliyofanyika kwenye ukumbi wa “Kigoma Social Hall” uliopo Manispaa ya Kigoma  (06.12.2021).

 

Jumapili, 5 Desemba 2021

WAFUGAJI WATAKIWA KUTUMIA MFUMO WA UTAMBUZI WA MIFUGO KIELEKTRONIKI

 

Serikali imewataka wafugaji Wilayani Mufindi kutumia vyema fursa iliyotolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi   ya utambuzi wa mifugo kwa mfumo wa kielektroniki ili kuondokana na changamoto ya wizi wa mifugo hiyo uliokuwa ukijitokeza mara kwa mara.

Rai hiyo ilitolewa Disemba 4, 2021 na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bw. Saad Mtambule wakati wa uzinduzi wa zoezi la utambuzi, usajili na ufatiliaji mifugo kwa kuweka hereni maalum sikioni zenye namba zinazotolewa na Wizara.

Alisema katika kipindi cha hivi karibuni Wilaya hiyo ilikumbwa na wimbi la wizi wa Ng'ombe ambapo ilikuwa ni vigumu kutambua kutokana na kukosa Alama  maalum za kuwatambulisha.

"Tulikuwa na changamoto ya wizi wa mifugo kwa muda mrefu sana na ilikuwa ni jambo gumu kutambua mifugo ikipotea katika kijiji kimoja na kuipata katika kijiji kingine kwa hiyo kupitia utambuzi huu utakuwa umekomesha kabisa wizi kwa sababu mifugo yote itakua inatambulika" alisema

Akizungumzia mfumo huo wa utambuzi Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na ustawi wa Wanyama kutoka wizara ya mifugo na uvuvi (Mifugo), Dkt. Annette Kitambi alibanisha kuwa  hereni zitakazotumika zitakuwa za kisasa ambazo zitawekwa namba na hazitachubuka.

Alisema hereni hizo zitakuwa na namba 12 zikianzia na namba ya nchi, mkoa, wilaya na kata  husika inayopatikana mifugo hiyo ambapo pia zitawekwa taarifa zote muhimu ambazo zitasajiliwa katika mtandao.

"Huu mfumo hereni zitakuwa na namba 12 ambapo katika usajili tutapiga picha ya ng'ombe na namba zilizopo katika hereni kwa hiyo kutakuwa na picha mbili ambazo zitasaidia kutambua mifugo ni ya nani na hata ikitokea imeibiwa itakuwa rahisi kupatikana kwa sababu itaweza kufuatiliwa kama zinavyofuatiliwa simu zikiibiwa" alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji nchini, Jeremiah Wambura aliishukuru Wizara kwa kuanzisha mfumo huo ambao pamoja na kusaidia katika kudhibiti wizi wa mifugo pia utasaidia Serikali kujua idadi ya mifugo iliyopo na kupanga utaratibu mzuri  wa maeneo ya malisho kutokana na mahitaji ya mifugo iliyopo.


Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Bw. Saad Mtambule akiongea na wafugaji wa Halmashauri hiyo wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo Disemba 04, 2021 Mkoani Iringa. 

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na ustawi wa wanyama, Dkt. Annette Kitambi akisisitiza suala la uwekaji hereni Mifugo na umuhimu wa utambuzi usajili na ufuatiliaji wa mifugo  kwa wafugaji wa Wilaya ya Mufindi wakati wa  uzinduzi wa  mwongozo huo  Mkoani Iringa. Disemba 04, 2021. 

Mwenyekiti wa wafugaji Tanzania, Bw. Jeremiah Wambura akihamasisha wafugaji kupokea zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwani lina manufaa kwao na litasaidia kudhibiti wizi na upotevu wa Mifugo yao. Disemba 04,2021 Mkoani Iringa

 


Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bw. Saad Mtambule avalisha hereni kwenye sikio la ng'ombe wa kwanza kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mara baada ya uzinduzi wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo Disemba 04, 2021 Mkoani Iringa. 

Jumapili, 28 Novemba 2021

TAASISI ZA FEDHA ZAHIMIZWA KUTOA MIKOPO KWA WAVUVI NA WAFANYABIASHARA WA DAGAA

Taasisi za kifedha nchini zimehimizwa kutoa mikopo kwa wavuvi na wafanyabiashara wa dagaa kwa kuwa zao hilo lina tija kiafya na kiuchumi.


Hayo yamesemwa leo (26.11.2021) na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega wakati alipotembelea mwalo wa Igombe wilayani Ilemela mkoa wa Mwanza baada ya kufika kwenye moja ya banda linalotumika kukaangia dagaa na kukutana na wafanyabiashara hao.


Naibu Waziri Ulega amesema kuwa umefika wakati wa taasisi za kifedha pamoja na Halmashauri kuanza kuliangalia kundi hilo ambalo likiwezeshwa litaweza kuwahakikishia watanzania kuondokana na utapiamlo lakini pia kuongeza kipato kwa wahusika na taifa kwa ujumla.


“Dagaa ni zao la kimkakati kutokana na umuhimu wake kiafya na kiuchumi ndio maana tunaendelea kuzihamasisha taasisi za kifedha kuwakopesha wavuvi na wafanyabiashara wa dagaa ili waweze kuvua dagaa wengi kwa kutumia zana za kisasa, kuwahifadhi katika mazingira mazuri na kusafirishwa katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi,” alisema Naibu Waziri Ulega


Halmashauri kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotokana na makusanyo ya mapato ya ndani zimeshauriwa kuanza kuliangalia kundi hilo linalojishughulisha na mnyororo wa thamani wa dagaa kwanza kwa kuwakopesha ili waweze kuboresha mazingira wanayofanyia kazi kuanzia kwenye utengenezaji wa vichanja kwa ajili ya kuanikia dagaa, kukaangia hadi kwenye maghala ya kuhifadhia.


Lakini pia Naibu Waziri Ulega amewasihi wafanyabiashara hao kuwa waaminifu hasa kwenye urejeshaji wa mikopo kwani kumekuwepo na tatizo la baadhi ya vikundi kusumbua kwenye urejeshaji wa mikopo waliyopatiwa. Vilevile amewataka kuzingatia ubora katika uandaaji wa dagaa hao ili wanapopelekwa sokoni kusiwe na tatizo lolote.


Pia amewataka wataalam kutoka katika Halmashauri kuwa jirani na wafanyabiashara hao ili wawasaidie katika kuwashauri namna ya kupanga mipango yao itakayowasaidia waweze kujinyanyua kiuchumi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akionja dagaa waliokuwa wanakaangwa katika mwalo wa Igombe ambapo amezisihi taasisi za kifedha pamoja na Halmashauri kutoa mikopo kwa wafanyabiashara hao wa dagaa ili waweze kuboresha mazingira na mitaji yao kwa kuwa biashara hiyo inalipa. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Hassan Masala. (26.11.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza na Wavuvi katika mwalo wa Kayenze wilayani Ilemela mkoani Mwanza mara baada ya kusikiliza kero zao ambapo ameendelea kuwasisitiza kutumia zana sahihi za uvuvi. (26.11.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akimuangali samaki aina ya sangara mwenye uzito zaidi ya kilo 40 wakati alipotembelea Kampuni ya Y & P inayozalisha barafu na kugandisha samaki Jijini Mwanza. Mhe. Ulega amewahimiza wamiliki wa Kampuni hiyo kuongeza kasi katika kukamilisha taratibu zilizobaki ili waanze kuchakata samaki. (26.11.2021)


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Dkt. Anthony Diallo akizungumza na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) wakati alipotembelea Ofisi za CCM Mkoa kwa ajili ya kusaini kitabu cha wageni. Kuanzia kushoto ni Katibu wa CCM Mkoa, Ndg. Julius Peter akifuatiwa na MNEC, Ndg. Jamal Babu. (26.11.2021)

Ijumaa, 26 Novemba 2021

ZALISHENI NYAVU KWA KUZINGATIA UBORA - ULEGA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amekitaka kiwanda cha kuzalisha nyavu za kuvulia dagaa cha Ziwa Net kuzalisha nyavu hizo kwa kuzingatia ubora.

 

Naibu Waziri Ulega ameyasema hayo leo (25.11.2021) wakati alipotembelea kiwanda hicho kwa lengo la kuona namna uzalishaji wa nyavu hizo unavyokwenda ambapo uongozi wa kiwanda hicho umetakiwa kuzingatia ubora katika uzalishaji wa nyavu lakini pia kuhakikisha wanazalisha nyavu za kutosha ili wavuvi wasipate shida kuzitafuta.

 

Kwa upande mwingine Naibu Waziri Ulega amempongeza mwekezaji huyo wa Kiwanda cha Ziwa Net kwa uamuzi wake wa kujenga kiwanda hicho lakini pia kwa kutoa ajira nyingi kwa wanawake ambapo kati ya waajiriwa 18 wanaweke ni 15. Vilevile amewasihi kuhakikisha wanazingatia misingi ya ajira na kuhakikisha hakuna unyanyasaji wa watumishi. Lakini pia amewashauri kuendelea kuwekeza katika utengenezaji wa nyavu za aina nyingine zikiwemo za kuvulia samaki pamoja na nyavu maalum za kutengenezea vizimba vya samaki.

 

Vilevile amewasihi uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha wanajitangaza lakini pia kuwaalika wadau kuja kuona namna nyavu zinavyozalishwa ili pia waweze kutoa maoni yao kuhusu nyavu hizo.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kali amesema uwepo wa kiwanda hicho ni muhimu sana kwa wavuvi kwa kuwa itawarahisishia upatikanaji wa nyavu kwa bei nafuu. Lakini pia itapunguza uvuvi haramu kwa kuwa wavuvi watakuwa wakitumia nyavu sahihi.

 

Meneja Masoko wa kiwanda cha Ziwa Net, Bi. Christina Melkior amesema lengo la kuanzishwa kwa kiwanda hicho ni kurahisisha upatikanaji wa nyavu za dagaa kwa wavuvi, kukuza na kutangaza zana bora za uvuvi pamoja na kufungua fursa ya ajira kwa vijana watakao ajiriwa katika kiwanda hicho. Pia amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha vipande 66 vyenye urefu wa mita 75 na upana wa mita 3.2 kwa siku ambapo uzalishaji kwa mwezi ni vipande 2000.

 

Naibu Waziri Ulega pia ametembelea mwalo wa Ihale kukagua maendeleo ya ujenzi wa mwalo huo na kuzungumza na wavuvi, Kituo cha kupumzisha Mifugo cha Lamadi wilayani Busega mkoa wa Simiyu na kiwanda cha kuchakata mabondo cha Pesca Perch wilayani Magu mkoa wa Mwanza.

Picha ya pamoja ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega na Viongozi na watumishi wa kiwanda cha Ziwa Net kilichopo katika Kijiji cha Kanyama wilayani Magu mkoa wa Mwanza mara baada ya kutembelea kiwanda hicho. (25.11.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akisikiliza maelezo ya namna nyavu za kuvulia dagaa zinavyotengenezwa wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza nyavu cha Ziwa Net kilichopo katika Kijiji cha Kanyama wilayani Magu mkoa wa Mwanza. (25.11.2021)


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi Robert Luhumbi (kulia) akizungumza na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ofisini kwake ambapo amemueleza mipango waliyonayo ya kuhakikisha wanaongeza uzalishaji wa samaki kupitia ufugaji kwa kutumia vizimba. Mhe. Ulega alifika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kusaini kitabu cha wageni kabla ya kuanza ziara yake ya kikazi ya siku mbili. (25.11.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akikagua ujenzi wa mwalo wa Ihale wilayani Busega mkoa wa Simiyu ambapo amemtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha ujenzi huo kwa wakati. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Gabriel Zacharia na Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Busega, Mhe. Simon Songe. (25.11.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na wananchi wa Kijiji cha Ihale wilayani Busega mkoa wa Simiyu mara baada ya kukagua mwalo wa Ihale ambapo amewataka wananchi kushirikiana na serikali katika kulinda rasilimali za uvuvi. (25.11.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akikagua miundombinu iliyopo katika Kituo cha kupumzishia Mifugo cha Lamadi wilayani Busega mkoa wa Simiyu ambapo amewaagiza Viongozi kuendelea kulilinda eneo hilo na kwamba uangaliwe uwezekano wa kukiboresha Kituo hicho ili kiweze kufanya kazi kama zamani. (25.11.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiangalia mabondo wakati alipotembelea kiwanda cha kuchakata mabondo cha Pesca Perch kilichopo wilayani Magu mkoa wa Mwanza. (25.11.2021)

Alhamisi, 25 Novemba 2021

UWEKEZAJI KWENYE DAGAA NI MUHIMU KIAFYA NA KIUCHUMI

Uwekezaji kwenye zao la dagaa ni muhimu kiafya kwa kuwa utasaidia wananchi kuondokana na utapiamlo lakini pia utawanyanyua wananchi kiuchumi.

 

Hayo yamesemwa leo (24.11.2021) na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega wakati alipotembelea mialo ya Igabilo na Rushara iliyopo wilayani Bukoba mkoa wa Kagera kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wavuvi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, Ndugu Shaka Hamdu Shaka.

 

Naibu Waziri Ulega amesema dagaa watasaidia sana kuondoa utapiamlo kwa kuwa wana protini, madini ya chuma na madini mengine ambayo ni muhimu kwa afya ya binadamu. Pia amesema itawashangaza sana watu endapo maeneo ambayo kuna dagaa wengi watoto wawe na tatizo la utapiamlo. Hivyo wavuvi wamehimizwa kutumia njia bora za uanikaji wa dagaa ikiwa ni pamoja na kuwahifadhi vizuri ili wasipoteze ubora.

 

Vilevile wavuvi na wafanyabiashara wa dagaa wamehimizwa kuwekeza katika zao hilo ili waweze kuvua kwa wingi, waweze kuwahifadhi kwa kuzingatia ubora na kuwasafirisha katika maeneo yote ya nchi ili wananchi wengi waweze kununua dagaa kitu ambacho kitawaongezea kipato hasa ikizingatiwa kuwa watu wengi wanahusika katika mnyororo mzima wa thamani wa dagaa.

 

Akiwa katika mialo hiyo, Naibu Waziri Ulega aliwasihi wavuvi kujiunga kwenye ushirika ili waweze kuunganishwa na taasisi za fedha ambapo itakuwa ni rahisi kwa wao kupata mikopo ambayo itawasaidia kuweza kununua zana bora za uvuvi na kuanza kuvua kisasa.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiangalia dagaa waliokuwa wameanikwa chini wakati alipotembelea mwalo wa Igabilo wilayani Bukoba mkoa wa Kagera kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wavuvi. Mhe. Ulega amewata wavuvi hao kuacha kuanika dagaa chini badala yake watumie vichanja. (24.11.2021)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na Wavuvi na wafanyabiashara katika mwalo wa Rushara Kemondo wilayani Bukoba mkoani Kagera ambapo licha ya kusikiliza na kutatua kero walizokuwa nazo, amewataka kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili waweze kuunganishwa na taasisi za kifedha na kupata mikopo. (24.11.2021)


Wavuvi katika mialo ya Igabilo na Rushara wilayani Bukoba mkoa wa Kagera kwa nyakati tofauti wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (hayupo pichani) wakati alipotembelea mialo hiyo kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wavuvi hao. (24.11.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiukagua mwalo wa Rushara wilayani Bukoba mkoa wa Kagera wakati alipokwenda kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wavuvi. (24.11.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Kagera mara baada ya kumaliza mazungumzo nao wakati alipofika Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kusaini kitabu cha wageni. Wa tatu kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Meja Jenerali Charles Mbuge. (24.11.2021)

Jumatano, 24 Novemba 2021

NAIBU WAZIRI ULEGA AWATAKA WAFUGAJI KULIMA MALISHO

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka wafugaji hapa nchini kulima malisho kwa ajili ya mifugo yao.


Naibu Waziri Ulega ameyasema hayo leo (23.11.2011) wakati alipotembelea shamba la malisho ya mifugo kwenye kitalu cha NARCO ambacho kinatumiwa na Kampuni ya Kahama Fresh wilayani Karagwe mkoa wa Kagera.


Akiwa katika shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 400, Naibu Waziri Ulega amesema wafugaji wanatakiwa kulima malisho na kuacha kutegemea malisho ya asili peke yake. Lakini pia amesema ipo fursa kubwa kupitia kilimo cha malisho kwa wafugaji na wasio wafugaji kwani kufanya biashara ya malisho ya mifugo kutawawezesha kujinyanyua kiuchumi.


Naibu Waziri Ulega ametembelea kuona ujenzi unaoendelea wa kiwanda cha vyakula vya mifugo pamoja na kiwanda cha maziwa, ambapo ameipongeza Kampuni ya Kahama Fresh kwa kuamua kufanya uwekezaji huo. Vilevile ametembelea kuona mifugo inayomilikiwa na Kampuni hiyo ambapo amesema kuwa mwekezaji huyo ameonesha mfano mzuri wa matumizi ya ardhi aliyokodoshiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na kuwataka wawekezaji wengine kufuata taratibu wanazopewa.


Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Kahama Fresh, Bw. Josam Ntangeki amesema kwa upande wa kiwanda wanatarajia kiwe kimekamilika ifikapo mwezi Machi, 2021. Lakini kwa sasa wanaendeleo kutoa mitamba kwa ajili ya maziwa kwa wafugaji wadogo ambao ndio watakuwa wakipeleka maziwa kwenye kiwanda hicho kitakapo kamilika.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza jambo baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Bukoba kwa ajili ya kufanya ziara ya siku mbili mkoani Kagera ambapo amepokelewa na viongozi na wataalam kutoka Sekta ya Uvuvi wakiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi, Bw. Ezra Mutagwaba (wa pili kutoka kulia). (23.11.2021)


Mkurugenzi wa Kampuni ya Kahama Fresh, Bw. Josam Ntangeki (kushoto) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) kuhusu ujenzi unaoendelea wa Kiwanda cha kutengeneza Chakula cha Mifugo pamoja na kiwanda cha maziwa kinachojengwa katika Kijiji cha Kihanga wilayani Karagwe mkoa wa Kagera. (23.11.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akiwa kwenye moja ya shamba la malisho ya mifugo linalomilikiwa na Kampuni ya Kahama Fresh ambapo ameendelea kuwahimiza wawekezaji wengine kujenga tabia ya kupanda malisho kwa ajili ya mifugo yao. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kahama Fresh, Bw. Josam Ntangeki na wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Karagwe, Ndg. Pascal Rwamgata. (23.11.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akiwaangalia ng’ombe waliokuwa wanatoka kuogeshwa kwenye moja ya josho linalotumia mashine katika moja ya Kitalu cha NARCO kinachotumiwa na Kampuni ya Kahama Fresh kilichopo wilayani Karagwe mkoa wa Kagera. (23.11.2021)


Picha ya pamoja ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) na Viongozi na Wataalam kutoka WMUV, Chama cha Mapinduzi na baadhi ya wawekezaji mara baada ya kumaliza kutembelea mifugo inayomilikiwa na Kampuni ya Kahama Fresh. Mhe. Ulega amempongeza Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Bw. Josam Ntangeki kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kupitia sekta ya mifugo. (23.11.2021)Jumanne, 16 Novemba 2021

HALMASHAURI ZAHIMIZWA KUZINGATIA MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI

Halmashauri zote nchini zimehimizwa kuzingatia mipango bora wa matumizi ya ardhi ikiwemo  kuweka njia za Mifugo zitazowawezesha kwenda  kwenye Malisho, maji na kwenye Masoko Ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Rai hiyo ilitolewa na  Kaimu Mkuu wa Kitengo cha mazingira Wizara ya Mifugo na uvuvi  Sekta ya Mifugo, Bw. Yusuf Selenge katika mafunzo ya  ufugaji endelevu unaokabili mabadiliko ya tabia nchi yaliyofanyika Mkoani Geita Novemba 15, 2021.

Akiongea katika mafunzo hayo alisema kuwa  asilimia kubwa ya migogoro inatokana na baadhi ya vijiji kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi na kusabisha njia za kupitisha mifugo ikitumika kwa matumizi mengine.

“hii programu itasaidia sana kwa sababu imehimiza matumizi bora ya ardhi kwa hiyo Halmashauri wanatakiwa kutafuta wafadhiri na mapato yao ya ndani kuweza kutekeleza mpango huo kwa sababu njia za kupitisha mifugo zilikuwepo lakini zimevamiwa kwa matumizi mengine," alisema

Kuhusu mradi wa  utekelezaji wa mradi wa ufugaji endelevu,  Selenge alibainisha kuwa programu hiyo inatekelezwa katika sekta tatu za kilimo, mifugo na uvuvi ambapo kwa sasa mafunzo hayo yanatolewa kwa maafisa  katika Halmashauri ambao watawajibika kufikisha elimu kwa wakulima na wafugaji ngazi za vijiji.

Aliongeza kwa kusema kuwa  programu hiyo ilianza kutekelezwa tangu 2015 hadi 2025 ambapo utekelezaji wake unafanyika katika mamlaka ya Serikali za mitaa kupitia kwa maafisa sita katika halmashauri ambao watawajibika kufikisha elimu kwa wakulima na wafugaji.

“Halmashauri ndio wanachukua elimu hii na kuifikisha ngazi ya kata na kijiji, maafisa tunaofanya nao ni sita kwenye Halmashauri ambao ni Afisa  Mazingira, Afisa mifugo na uvuvi, Afisa kilimo na umwagiliaji, Afisa malisho, Afisa mipango pamoja na Afisa maendeleo ya jamii,” aliongeza

Aidha Bw. Selenge aliwahimiza  maafisa hao wa Halmashauri kuhakikisha wanawaelimisha  wafugaji njia bora ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo kuwashauri wananchi kuhimilisha Mifugo yao, kulima Malisho, kuyaboresha, kuyahifadhi, na kuvuna maji.

Naye, Afisa Mazingira kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Jeremiah Legela alisema kuwa pamoja na mambo mengine mafunzo hayo yatasaidia kuboresha mifugo ikiwemo kutoweka chapa katika mifugo ambayo imekuwa ikiharibu ngozi na kupunguza ubora.

Aliongeza  kuwa mpango wa sasa ni kutumia njia ya kisasa ikiwemo kuweka hereni katika masikio na kuiacha ngozi ya mifugo zikiwa na ubora ambapo unahitajika katika soko hasa viwanda vya ngozi vilivyopo nchini.

Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Bi. Mpelwa James  alibainisha kuwa faida waliyoipata katika mafunzo hayo watahakikisha inawafikia wafugaji ili kuhakikisha wanashiriki kulinda mazingira hasa katika vyanzo vya maji.

“kitu ambacho nimeondoka nacho hapa cha kwenda kufanya kwa wafugaji ambao wana mifugo mingi zaidi ya elfu moja ni kuwahimiza na kuwashirikisha kufanya tathimini za kimazingira ili kukabiliana na ya athari za mabadiriko ya tabia ya nchi kwa sababu wasipofanya hivyo kutakuwa na hatari ya kukosa malisho,” alisema

Aliongeza kuwa hatua hiyo itawaongezea uelewa wananchi juu ya mabadiriko ya tabia ya nchi na itawajengea uwezo  wa kuhimili mabadiliko hayo ili waweze kuwa na uhakika wa kupata chakula cha mifugo na kwenye kaya zao kutokana na uzalishaji wenye tija.


Afisa mazingira kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Jeremiah Legela akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi (hawapo pichani) yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya mji wa Geita Mkoani Geita Novemba 15, 2021. 


Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya mji wa Geita Mkoani Geita Novemba 15, 2021. 

 

Kaimu Mkuu wa kitengo cha mazingira Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo) Bw. Yusuf Selenge (wa nne kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya  watendaji wa Halmashauri ya geita mara baada ya mafunzo mafupi ya kuongeza uelewa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi  kwa watendaji hao yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya mji wa Geita Mkoani Geita Novemba 15, 2021. 


Jumatano, 10 Novemba 2021

WAVUVI WATAKIWA KUKATA BIMA YA JAHAZI

Waziri  wa Mifugo  na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wavuvi  kukata bima ya jahazi ili iwasaidie kuwakinga wanapokumbwa na majanga wakati wakitekeleza majukumu yao ya kila siku.

Mhe. Ndaki ameyasema hayo wakati akizindua bima ya Jahazi kwa wavuvi iliyoandaliwa na benki ya NMB kwa kushirikiana na Britam Insurance katika tukio lililofanyika jijini Mwanza Oktoba 31, 2021.

Amesema siku za nyuma bima ilikuwa inawaangalia wavuvi wakubwa pekee na kwamba kwa sasa NMB na Britam wamekuja na aina mpya ya kuwasaidia wavuvi wadogo na wa kati.

"Niwapongeze na kuwashukuru sana benki ya NMB pamoja na washirika wao kuja na hii bima ya jahazi ambayo sasa wavuvi na wote katika Sekta ya Uvuvi wataweza kufanya kazi zao kwa kujiamini kwa kuwa endapo watakumbwa na janga watakuwa na uhakika wa kinga ya vyombo vyao wakitambua kuwa bima ipo na watarejea katika kazi zao," amesema Mhe. Ndaki.

Ameongeza kuwa kwa kutegemea bima kunaongeza kujiamini na kujiamini huko kunaongeza ari ya kufanya kazi zaidi ambapo mwisho wake kunaongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

Aidha ametaka  wavuvi kuendelea  kupewa elimu ya bima ili waijue na kufanya maamuzi kwa kuwa ni njia sahihi ya kuwasaidia katika kipindi chote wanapokuwa katika shughuli zao.

Amesema  NMB  imedhamiria kuwainua kiuchumi  wakulima, wafugaji na sasa ni zamu ya wavuvi na kwamba serikali inatambua mchango wao katika kuhakikisha makundi hayo yananufaika na mikopo inayotolewa na benki hiyo.

Amesema sekta ambazo zilikuwa zinaonekana kuwa na 'risk'  kwa sasa zianze kufikiwa na  kukatiwa bima kwa kuwa zina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.

Waziri Ndaki amesema  kuwa  sekta ya uvuvi imetoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 202,000 na zaidi ya watanzania   milioni 4.5 wameendelea kutegemea kupata kipato chao kupitia Sekta ya uvuvi na kwamba inachangia asilimia 1.7 ya pato la taifa hivyo ni kundi muhimu ambalo linatakiwa kusaidiwa ili liweze kupiga hatua.

Naye Afisa Mkuu wa wateja binafsi na biashara kutoka benki ya NMB, Bw. Filbert Mponzi amesema bima hiyo inawalenga wavuvi wadogo na wa kati hapa nchini na itakuwa bima yenye kusaidia sana wavuvi kama wao binafsi na waliowaajiri lakini pia itahusisha vyombo vyao ambavyo wanatumia wakiwa katika shughuli za Uvuvi.

Amesema wavuvi watakata bima ya asilimia tatu ya chombo husika cha shughuli ya Uvuvi na kwamba wataweza kukingwa na majanga ya ajali, kuungua mitumbwi ama boti, kuvamiwa, kugongwa au kugonga vyombo vingine  pamoja na watu watakaokuwa ndani ya vyombo hivyo.

Aidha bima iyo itatoa gharama za matibabu kwa mvuvi pamoja na kulipwa fidia kutokana na  ajali yoyote itakayompata atakapokuwa majini kwa ajili ya shughuli za Uvuvi ama kando kando ya ziwa, mto, bwawa na bahari.

Mpozi amewataka wavuvi kufika katika Ofisi  za NMB kwa ajili ya kukata bima ambayo itawakinga na majanga mbalimbali wanapokuwa katika shughuli zao za Uvuvi.

Akizungumza katika uzindizi Huo, meneja wa kampuni ya  bima ya Britam kanda ya Ziwa, Bw. Said Kadabi amesema bima hiyo itawasaidia wavuvi kuinuka kiuchumi kwa kuwa sasa watafanya kazi zao kwa kujiamini

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), akiongea na  wavuvi, wawakilishi kutoka benki ya NMB na wawakilishi kutoka kampuni ya Britam Insurance (hawapo pichani) katika hafla ya uzindizi wa Bima ya jahazi kwa wavuvi na kuwasihi wavuvi kuchangamkia fursa hiyo kwani itaboresha ufanyaji kazi na kuwaimarisha zaidi. Oktoba 31, 2021 Jijini Mwanza. 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) (kushoto) akishuhudia utiaji saini wa mkataba Kati ya Benki ya NMB na kampuni ya Britam Insurance leo kwenye uzindizi wa Bima ya jahazi kwa wavuvi Mkoani Mwanza, kulia ni Mkuu wa Idara ya Bima, Bw. Martine Massawe. Oktoba 31, 2021 

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji wa Benki ya NMB, watendaji wa kampuni ya Britam Insurance, viongozi wa Mkoa wa Mwanza na wadau wa uvuvi mara baada ya uzindizi wa Bima ya jahazi kwa wavuvi Mkoani humo Oktoba 31, 2021. 

 


SERIKALI YAGAWA VIFARANGA 2600 KWA VIKUNDI VYA KINAMAMA MKURANGA

Katika jitihada za kuwakwamua kiuchumi wananchi hususan kinamama, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imegawa Vifaranga 2600 kwa  mashamba darasa mawili  katika kata ya Vikindu na Kimanzichana vilivyopo wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.

Akizungumza mara baada ya kugawa vifaranga hivyo Novemba 9, 2021,  Kaimu Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Idara ya utafiti na  mafunzo, Dkt. Hassan  Mruttu  alisema vifaranga hivyo vitakaa katika mashamba hayo  kwa  wiki nne kabla ya kusambazwa katika vikundi 17 vya Wilaya hiyo.

Alisema   pamoja na kuwepo kwa vifaranga hivyo, pia vikundi hivyo vitapewa chakula cha kuvikuza  pamoja na wataalamu wa kusaidia ukuaji wa kuku katika Wilaya hiyo.

"Tumepokea vifaranga 2600, tumegawa katika mashamba darasa mawili  katika kikundi cha Kisawani na kikundi cha tujikomboe  hivi vitakaa hapa kwa wiki 4 na baadaye tutavisambaza kwa vikundi 17, ili kuwasaidia wakinamama kujikwamua kiuchumi," alisema Dkt. Mruttu

“Kuna tofauti kubwa kati ya mashamba ya mfano na mashamba darasa, hili ni shamba darasa, kwanzia Novemba 10, wataalamu watakuwa hapa na baada ya hapa tu nategemea wana kikundi wa vikundi hivi viwili mkawe waalimu kwa vikundi hivyo vingine 17,"alisema

Kwa upande wake Afisa mifugo na uvuvi wa Wilaya hiyo Bi. Anna Kiria aliwataka   wanakikundi kuongeza umakini katika kufuatilia mafunzo ili kuleta matokeo chanya katika uzalishaji.

" Vifaranga  hawa wanaitaji  usafi wa kutosha, umakini na kujitolea,   tutapewa mafunzo tuzingatie, na  mwisho tutapewa vyeti vitakavyotufanya na sisi kwenda kuwafundisha wenzetu," alisema Anna

 

Alisema halmashauri hiyo itafuatilia kwa ukaribu kuona kila mmoja anatimiza wajibu wake, na haitamvumlia mwana kikundi atakayekuwa sababu ya kukwamisha shughuli hiyo ya maendeleo.

Aidha mwenyekiti wa kikundi cha Kisawani kata ya Vikindu, Bi.Sintaweza  Omary, aliipongeza serikali ya awamu ya sita huku akiiomba kuongeza jitihada katika kuwasaidia wakinamama vijijini.

"Mradi huu utaenda kukuza uchumi wa wakinamama wa Mkuranga, hivyo tunamshukuru  Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hasan kwa kuwa kumbuka wakinamama na tunamuomba asichoke katika kuhakikisha wanajikwamua kupitia asilimia 10 zitolewazo katika halimashauri, "alisema


Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya utafiti na Mafunzo Dkt. Hassan Mruttu akiongea na wanakikundi wa kisawani (hawapo pichani) mara baada ya kuwasili kwa vifaranga kwa ajili ya mashamba darasa kwenye Wilaya ya mkuranga Mkoani Pwani  Novemba 09, 2021.

Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Mkuranga, Bi. Anna Kiria (kulia) akikabidhi vifaranga kwa mwenyekiti wa kikundi cha kisawani kata ya vikindu Wilaya ya Mkuranga Bi. Staweza Omary (kushoto) nyuma yao ni baadhi ya wanakikundi wa kisawani na watendaji kutoka Wizara ya Mifugo na uvuvi. Novemba 09, 2021.

Baadhi ya vifaranga vilivyowekwa kwenye Banda la kikundi cha kisawani kata ya Vikindu, Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani. Novemba 09, 2021


Katibu wa Mbunge wa jimbo la Mkuranga, Bi. Zuwena Mtulia (kushoto) akiweka maji kwenye vyombo vya kunywea maji vifaranga nje ya jengo la shamba darasa la  kikundi cha kisawani kata ya Vikindu Wilaya ya mkuranga mkoani Pwani, Novemba 09, 2021.

BILIONI 50 KUANZISHA UJENZI WA BANDARI YA UVUVI KILWA MASOKO

Serikali imetenge fedha shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ambayo itajengwa Wilayani Kilwa mkoani Lindi.

 

Hayo yamesemwa leo (09.11.2021) na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah wakati wa makabidhiano ya eneo hilo la mradi kwa Mshauri Elekezi wa kampuni ya Sering kutoka nchini Italia, kwa ajili ya kukamilisha kandarasi ya upembuzi yakinifu utaopelekea kujulikana kwa gharama za mradi huo na kutangaza zabuni ya ujenzi wa bandari hiyo.

 

Dkt. Tamatamah amesema kuwa ujenzi wa bandari ya uvuvi ni moja ya mkakati wa serikali katika kuhakikisha inaendelea kukuza sekta ya uvuvi hasa katika kuhamasisha uwekezaji na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi  katika pato la taifa.

 

“Ujenzi huu wa bandari ya uvuvi unakwenda sambamba na ununuzi wa meli mbili (2) kubwa za uvuvi  ambazo zitafanya uvuvi katika bahari kuu   lakini serikali pia inalifufua Shirika la Uvuvi (TAFICO) ambalo ndilo litakalokuwa likisisimamia meli hizo,” alisema Dkt. Tamatamah

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Zainabu Kawawa amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalam watakaofika kwa ajili ya kukamilisha mradi huo na kuhakikisha wanaanza kujipanga kutumia fursa zitakazojitokeza kutokana na uwepo wa mradi huo.

 

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kilwa, Kaimu Shekh Mkuu wa Kilwa, Muhidini Matata ameishukuru serikali kwa kuamua kujenga bandari ya uvuvi wilayani Kilwa kwa kuwa itawaletea manufaa mengi kiuchumi. Lakini pia ameiomba serikali kuendelea kupeleka miradi mbalimbali itakayowasaidia wananchi kunyanyuka kiuchumi.

 

Kwa upande wa Mshauri Elekezi Bw. GABRIEL anayeiwakilisha Kampuni Sering Ingegneria kutoka Italia,anasema wanafuraha kubwa kwa kupata nafasi ya kushiriki katika mradi huu muhimu kwa wakazi wa Kilwa na Tanzania kwa ujumla.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Zainabu Kawawa wakikata utepe kama ishara ya kukabidhi mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kwa mshauri elekezi Kampuni ya Sering Ingegneria kutoka Italia kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu. (09.11.2021)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa wakati alipomtembelea ofisini kwake ambapo alimuelezea mpango ulipo kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi. (09.11.2021)


Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Zainabu Kawawa akizungumza na baadhi ya viongozi na wananchi wa Kilwa Masoko ambao walifika kwenye makabidhiano ya ujenzi wa bandari ya uvuvi kwa Mshauri Elekezi Kampuni ya Sering Ingegneria kwa ajili ya kufanya Upembezi Yakinifu ambapo amewataka viongozi na wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalam watakaofanya kazi hiyo. (09.11.2021)


Baadhi ya viongozi na wataalam kutoka Wizarani, Mkoa na Wilaya ya Kilwa wakitembelea eneo la mradi wa ujenzi wa bandari ya Uvuvi. (09.11.2021)


Baadhi ya viongozi na wataalam wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa kuhusu mradi wa ujenzi wa bandari ya uvuvi katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Maendeleo Kilwa Masoko. (09.11.2021)

Ijumaa, 29 Oktoba 2021

LITA YATAKIWA KUENDELEA KUTOA MAFUNZO YA MUDA MFUPI KWA WAFUGAJI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki ameiagiza Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kuendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wafugaji ili wafuge kisasa.

 

Waziri Ndaki ameyasema hayo leo (28.10.2021) alipotembelea Kampasi ya Tengeru iliyopo mkoani Arusha kwa lengo la kufungua bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 ambalo litasaidia kupunguza changamoto ya miundombinu iliyopo.

 

“Wafugaji bado wanahitaji kupatiwa elimu ya ufahamu ili waweze kuelewa faida na hasara za kuendelea na njia ya ufugaji wa asili na njia bora za ufugaji wa kisasa utakaoweza kuwaletea tija ambapo kwa kuwatumia wataalam tunaowafundisha na waliopo katika maeneo mbalimbali tutaweza kubadilisha fikra za wafugaji wetu,” alisema Waziri Ndaki

 

Pia LITA imetakiwa kusaidia kutatua changamoto ya malisho kwa wafugaji kwa kutoa elimu juu ya umiliki wa maeneo na upandaji malisho. Waziri Ndaki amesema kupitia mashamba yao ya malisho ambayo hutumika kuwafundishia wanafunzi, pia wanaweza kuyatumia mashamba hayo kama mashamba darasa ambapo wafugaji watapata fursa ya kwenda kujifunza.

 

Aidha, amewashauri Bodi na Viongozi wa LITA kuangalia namna ya kutoa elimu ambayo itawasaidia wahitimu wa vyuo hivyo kwenda kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea kuajiriwa. Hili pia amewaeleza wanafunzi baada ya kufungua bweni la wasichana kuwa ni lazima wasome kwa nguvu wakilenga kujiajiri.

 

Waziri Ndaki ameipongeza Bodi na Uongozi mzima wa LITA kwa kazi nzuri wanayoifanya ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu kama bweni la wasichana licha ya changamoto walizonazo. Pia amewaahidi kuwa wizara itaendelea kutenga fedha za maendeleo katika bajeti kwa ajili ya kuendelea kutatua changamoto walizonazo zikiwemo za miundombinu, mitambo na vifaa mbalimbali na kwamba wizara itaangalia namna ya kuwasaidia ili kutatua changamoto ya usafiri kwa kununua basi la chuo.

 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya LITA, Prof. Malongo Mlozi amesema majukumu ya LITA ni kutoa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya Stashahada na Astashahada, kutoa huduma za ushauri na mafunzo ya muda mfupi kwa wafugaji, maafisa ugani pamoja na wadau wengine katika sekta, kufanya tafiti na huduma za ushauri ili kujitathmini na kuboresha mafunzo yanayotolewa na kuzalisha na kutunza aina mbalimbali za mifugo na malisho bora kwa ajili ya mafunzo na kuhudumia jamii ya watanzania.

 

Mtendaji Mkuu wa Wakalaya ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo, Dkt. Pius Mwambene amesema wakala imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo ongezeko la udahili kutoka 798 mwaka 2012/13 hadi wanafunzi 3,592 mwaka 2020/21, ongezeko la ufikiaji wafugaji kutoka 267 mwaka 2012/13 hadi 2,104 mwaka 2020/21. Pamoja na mafanikio hayo bado wakala inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za miundombinu, upungufu wa walimu na watumishi wengine, uhaba wa fedha za maendeleo, usafiri, mitambo, lakini pia baadhi ya wanafunzi wasaidiwe kupata fursa ya mikopo.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akifungua bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 katika Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mkoani Arusha ambapo amewataka wanafunzi hao kutunza miundombinu hiyo vizuri. (28.10.2021)

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Mhe. Mhandisi. Richard H. Ruyango (kushoto) akitoa taarifa fupi ya Wilaya kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipofika ofisini kwake kwa ajili ya kusaini kitabu cha wageni. (28.10.2021)

Mwenyekiti wa Bodi ya LITA, Prof. Malongo Mlozi (kushoto aliyesimama) akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya bodi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipotembelea Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mkoani Arusha kwa lengo la kufungua bweni la wasichana lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 80. Prof. Mlozi amesema moja ya jukumu walilokuwa nalo ni kuhakikisha kuna kuwa na ongezeko la wanafunzi hivyo kufunguliwa kwa bweni hilo kutasaidia sana. Taarifa hiyo imesomwa katika ofisi ya meneja Kampasi ya Tengeru mkoani Arusha. (28.10.2021)

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene akitoa taarifa ya Wakala hiyo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipotembelea Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mkoani Arusha kwa ajili ya kuzindua bweni la wasichana. Dkt. Mwambene amesema licha ya mafanikio wanayoyapata bado wakala inakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa miundombinu, mitambo, upungufu wa walimu na watumishi wengine, uhaba wa fedha za maendeleo, usafiri, mitambo, lakini pia baadhi ya wanafunzi wasaidiwe kupata fursa ya mikopo. (28.10.2021)

Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani (WMUV), Dkt. Angello Mwilawa akitoa maelezo kuhusu aina ya malisho ya mifugo yaliyopandwa katika shamba la chuo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipotembelea moja ya shamba la malisho katika Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru. (28.10.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akipanda mti nje ya bweni la wasichana kwenye Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mara baada ya kulifungua. (28.10.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mara baada ya kufungua bweni la wasichana ambapo amewasihi kusoma kwa bidii huku wakilenga zaidi kwenda kujiajiri mara baada ya kuhitimu masomo yao. (28.10.2021)