Nav bar

Jumanne, 7 Desemba 2021

FISH4ACP ITACHOCHEA ONGEZEKO LA PATO LA TAIFA KUPITIA SEKTA YA UVUVI-DKT. TAMATAMAH

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa Mradi wa FISH4ACP utasaidia kuongeza nguvu kwenye maboresho ambayo sekta ya Uvuvi inaendelea kuyafanya hivi sasa  kwa ajili ya  kuongeza mchango wa sekta 

Dkt. Tamatamah ameyasema hayo  (06.12.2021) wakati akifungua warsha ya siku mbili ya ukamilishaji mpango wa maboresho ya mnyororo wa thamani wa dagaa na samaki aina ya mgebuka kutoka Ziwa Tanganyika iliyofanyika kwenye ukumbi wa “Kigoma Social Hall” uliopo Manispaa ya Kigoma.

“Lakini pia mradi huu utakuwa na mchango mkubwa katika kutoa ajira hasa kupitia maboresho ya mnyororo wa thamani ya mazao yanayotoka  Tanganyika, utapunguza umasikini miongoni mwa wavuvi na wadau wote watakaohusika kwenye mnyororo huo na kubwa zaidi utaongeza kiwango cha ulaji wa samaki ambao kwa mujibu wa Shirika la Kilimo na Chakula Uliwenguni (FAO) kila Mtanzania anakula kiasi cha kilo 8.5 kwa mwaka hivyo naamini mpaka kukamilika kwa mradi huu angalau kila Mtanzania atakuwa anakula kilo 10.5 kwa mwaka” Amesema Dkt. Tamatamah.

Dkt. Tamatamah ameongeza kuwa katika kuboresha shughuli za Uvuvi wa Ziwa Tanganyika Serikali kupitia kanuni ya Uvuvi ya mwaka 2020, Serikali ilipunguza viwango vya tozo ya usafirishaji wa dagaa inayoenda nje kutoka dola za Marekani 1.5 hadi 0.5 kwa kilo na kwa upande wa Migebuka kutoka Dola za Marekani 0.5 hadi 0.3  jambo ambalo anaamini litahamasisha sana biashara ya mazao hayo ya uvuvi katika masoko ya nje.

“Lakini pia kwa kutambua kuwa  uvuvi endelevu na ulinzi wa rasilimali za uvuvi unategemea uwepo wa taarifa sahihi zinazopatikana kwa wakati za idadi na mtawanyo wa samaki katika vyanzo husika na hapa niishukuru tena Serikali ya awamu ya sita kwa kutenga fedha za utafiti wa utambuzi wa wingi na mtawanyiko wa samaki katika bahari ya Hindi na Ziwa Tanganyika na huu ndo utakuwa utafiti wa kwanza kufanyika tangu nchi yetu ipate uhuru” Amesisitiza Dkt. Tamatamah.

Akizungumza kwa niaba ya Shirika la Chakula na Kilimo Ulimwenguni (FAO), Mwakilishi mkazi wa Shirika hilo kwa upande wa Afrika Mashariki Martin Van Der Knaap amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) katika kusimamia hatua mbalimbali za utekelezaji wa mpango huo ambapo kwa niaba ya Shirika lake  ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakati wote wa utekelezaji wa mpango huo.

“Miaka kadhaa iliyopita Umoja wa Ulaya uliomba miswada mbalimbali itakayolenga kwa undani kuhusu mnyororo wa thamani wa samaki na mazao mengine ya uvuvi katika maeneo mbalimbali na ni miswada 12 tu kati ya zaidi ya 40 ndo ilikubaliwa kuwezeshwa fedha kwa ajili ya utekelezaji ukiwemo huu unaohusu mradi wa FISH4ACP hivyo FAO tunaishukuru sana EU kwa kukubali kufadhili mradi huu ambao umeonekana kutekelezwa vizuri zaidi  Tanzania ukilinganisha na maeneo mengine” Amesema Martin.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara yake imejipanga kuelekeza nguvu katika uvuvi wa bahari kuu ambao unatarajiwa kuboresha uchumi wa mvuvi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

 “Kiukweli eneo ambalo kama sekta bado hatujaliwekea nguvu kubwa ni kwenye upande wa Uvuvi wa bahari na tumegundua moja ya changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya Uvuvi ni uwekezaji mdogo kwenye upande wa Uvuvi wa bahari kuu hasa kutoka sekta binafsi hivyo kwa hivi sasa tumeleekeza nguvu yetu kwenye sera ya uendelezaji wa miundombinu ambapo jambo la kwanza ni ujenzi wa bandari za uvuvi na tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia shilingi bilioni 50.72 ambayo tutaanza kujengea bandari ya Uvuvi huko Kilwa Masoko” Amesema Dkt. Tamatamah.

Dkt. Tamatamah amesema kuwa Serikali imeamua kuwekeza zaidi kwenye uvuvi wa bahari kuu kwa sababu mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea hivi sasa yamesababisha samaki wengi kutopatikana kwenye ukanda wa pwani huku wengi  wakikimbilia katikati ya bahari (deep sea) hivyo ni lazima zifanyike jitihada za kuhakikisha uvuvi kwenye ukanda huo unaendelea.

“ Mbali na Ujenzi wa bandari, Serikali pia kupitia mpango wa tatu wa maendeleo ya Taifa , inatarajia kununua meli 4 za uvuvi ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa suala la Uvuvi wa bahari kuu na kwa mwaka huu wa fedha kupitia Shirika la “IFARD” tutanunua meli mbili  na nyingine mbili tutanunua kabla ya mpango kukamilika mwaka 2025/2026” Amesisitiza Dkt. Tamatamah.

Katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wahisani mbalimbali wanaofadhili miradi ya sekta ya uvuvi, Serikali imetenga fedha zitakazotumika  kwa ajili ya utafiti wa wingi na mtawanyo wa rasilimali za Uvuvi kwa upande wa bahari ya Hindi na Ziwa Tanganyika ambapo kwa mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi milioni 800 zimeshatolewa kwa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) kwa ajili ya utekelezaji wa Utafiti huo.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) Dkt. Ismail Kimirei wakifuatilia maoni ya mmoja wa wadau wa  Uvuvi wa Ziwa Tanganyika wakati wa  warsha ya siku mbili ya ukamilishaji mpango wa maboresho ya mnyororo wa thamani wa dagaa na samaki aina ya mgebuka kutoka Ziwa Tanganyika iliyofanyika kwenye ukumbi wa “Kigoma Social Hall” uliopo Manispaa ya Kigoma  (06.12.2021).Sehemu ya wadau wa Uvuvi wa Ziwa Tanganyika wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah (hayupo pichani) wakati akifungua warsha ya siku mbili ya ukamilishaji mpango wa maboresho ya mnyororo wa thamani wa dagaa na samaki aina ya mgebuka kutoka Ziwa Tanganyika iliyofanyika kwenye ukumbi wa “Kigoma Social Hall” uliopo Manispaa ya Kigoma  (06.12.2021).

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni