Nav bar

Alhamisi, 30 Septemba 2021

MBEYA KUTENGA BAJETI YA UNYWAJI MAZIWA SHULENI

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote zilizopo mkoani kwake kutenga bajeti ya maziwa kwa wanafunzi wote wa shule za awali na msingi waliopo mkoani humo.

Homera ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha Siku ya unywaji maziwa shuleni ulimwenguni ambayo kitaifa imefanyika leo (29.09.2021) mkoani Mbeya amesema kuwa suala la unywaji maziwa shuleni kwa wanafunzi ni la lazima na si hiyari.

“Hatuwezi kusubiri wadau tu kila siku wajitoa wakati watoto ni wetu wenyewe hivyo ni lazima wakati wa kupanga bajeti zote za halmashauri zilizopo mkoani Mbeya iwekwe bajeti ya kutekeleza mpango huu na kwa sababu mimi ndo naidhinisha bajeti zote,sitopitisha bajeti yoyote ambayo haina bajeti ya kutekeleza mpango huo” Amesema Homera.

Aidha Homera amepongeza juhudi na kazi inayofanywa na Wizara ya mifugo na Uvuvi kupitia bodi ya maziwa kwa kuwa karibu na wadau mbalimbali wa tasnia ya maziwa waliopo mkoani humo ambapo amewataka wasindikaji wote wa maziwa nchini kuendelea kuwekeza katika mkoa huo.

“Mimi ninapenda sana wawekezaji na kipekee kabisa niwashukuru ASAS kwa kuamua kuja kujenga kiwanda kikubwa cha maziwa hapa, niwaombe Tanga Fresh na makampuni mengine ya maziwa kufanya hivyo pia ili kuchochea zaidi uwekezaji katika tasnia ya maziwa katika mkoa wa Mbeya” Amesisitiza Homera.

Akizungumzia hali ya uwekezaji kwenye tasnia ya maziwa nchini, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Stephen Michael amesema kuwa hadi sasa Tanzania ina jumla ya ng’ombe wa maziwa Mil. 1.2 ambao huzalisha jumla ya lita za maziwa Bil.3.1. 

“Aidha hadi kufikia Aprili 30 mwaka huu, Tanzania ilikuwa na jumla ya viwanda vya kusindika maziwa vikubwa, vidogo na vya kati 104 na kati ya hivyo 96 ndo vinafanya kazi” Amesema Michael.

Akibainisha kuhusu uwezo wa uzalishaji wa viwanda hivyo, Michael amesema kuwa viwanda vilivyopo vina uwezo uliosimikwa wa kusindika lita 865600 kwa siku lakini kutokana na uhaba wa upatikanaji wa malighafi viwanda hivyo vinasindika wastani wa asilimia 24 ya uwezo wake ambao ni sawa na lita 206849 kwa siku.

Akielezea kuhusu utekelezaji wa mpango wa unywaji maziwa shuleni, Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini (TDB) Dkt. George Msalya amesema kuwa mpango huo ulianzia mkoani Kilimanjaro mwaka 2007 kwa lengo la kuhamasisha unywaji wa maziwa nchini kwa kujenga utamaduni huo kuanzia ngazi ya shule ya awali.

“Tunafanya hivi kwa sababu mbali na maziwa kuwa lishe nzuri na kiburudisho kwa watoto, imethibitika kuwa maziwa ni mlo kamili unaoweza kujitosheleza bila kutegemea chakula kingine na ndo chakula pekee chenye virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini” Amesema Dkt. Msalya.

Aidha Dkt. Msalya amebainisha kuwa tangu kuanza kwa mpango huo takribani watoto elfu 90 kutoka shule 210 hapa nchini wamepatiwa maziwa ambapo amesema kuwa idadi hiyo imeendelea kupungua kadri miaka inavyoendelea.

“Tunaendelea kufanya jitihada kubwa katika kuwajengea uwezo wanafunzi, wazazi na walezi wao juu ya umuhimu wa maziwa ili kuhakikisha kiwango cha matumizi ya bidhaa hiyo kinaongezeka” amehitimisha Dkt. Msalya.

Maadhimisho ya Siku ya unywaji Maziwa mwaka huu yalitanguliwa na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na ugawaji maziwa katika vituo vya afya, mahabusu ya watoto na kwenye vituo vya watoto yatima.


Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera (kushoto) akimkabidhi cheti mwakilishi wa kampuni ya ASAS mkoani humo Ahmed Kasu ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa kampuni hiyo kwenye utekelezaji wa mpango wa unywaji maziwa shuleni wakati wa Maadhimisho ya Siku ya unywaji maziwa shuleni yaliyofanyika mkoani Mbeya (29.09.2021).

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera (kushoto) akimkabidhi zawadi ya begi mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mashindano ya kutunga jumbe nzuri zinazohusu unywaji maziwa shuleni wakati wa Maadhimisho ya Siku ya unywaji maziwa shuleni yaliyofanyika mkoani Mbeya (29.09.2021).


Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera akimkabidhi maziwa mmoja wa wanafunzi waliofika kwenye maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa shuleni yaliyofanyika (29.09.2021) mkoani humo, wengine pichani kutoka kushoto ni mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Stephen Michael, Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini (TDB) Dkt. George Msalya na Meneja Utawala na Fedha kutoka Kiwanda cha maziwa cha Sebadom Anati Kombeson.

 

 

MKANDARASI ATAKIWA KUFUATA TARATIBU NA KANUNI UJENZI WA MAJENGO YA MIHADHARA.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Dkt. Pius Mwambene ametaka ujenzi wa vyumba viwili vya mihadhara katika chuo hicho Tawi la Tengeru Mkoani Arusha kujengwa kwa kufuata taratibu na kanuni za ujenzi.

Dkt. Mwambene amebainisha hayo katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo katika jengo la NBC jijini Dodoma, wakati wa utiaji saini wa ujenzi wa vyumba hivyo.

Alisema anatarajia kazi ya ujenzi itatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Aliongeza kuwa mkataba unaonyesha muda wa ujenzi  uliopangwa ni miezi sita, ambapo ujenzi utaanza mwishoni mwa mwezi huu wa Septemba na kukamilika  mwishoni mwa mwezi wa Machi mwaka 2022.

Aidha Mtendaji huyo alisema kuwa gharama za ujenzi wa vyumba viwili vya mihadhara ni Shilingi Milioni 800 hadi utakapokamilika.

Awali akiongea baada ya zoezi la utiaji saini kukamilika Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Ugani na Mafunzo Dkt. Angelo Mwilawa ameitaka kampuni ya LI JUN Devolopment Co Ltd ya Moshi inayotekeleza ujenzi huo, kufuata taratibu zote zilizoainishwa kwenye mkataba ili kupata matokeo bora yenye tija.

Naye meneja wa kampuni hiyo Bw. Xu Geng Sheng amewahakikishia viongozi na wataalam wa wizara waliokuwepo kwenye tukio hilo kuwa utekelezaji wa ujenzi huo utazingatia weledi na taratibu zote zilizopo ili kupata matokeo yenye tija na hatimaye kutangaza vyema jina la kampuni.

Kwa wakati mwingine Mtendaji wa Mkuu wa LITA Dkt. Mwambene alisema vyumba hivi vinajengwa ili kupanua wigo wa udahili wa wanafunzi kukidhi uhitaji wa elimu kwa sasa hususan katika Sekta ya Mifugo.


Mwanasheria wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Mifugo, Bi. Mariam Mgendwa akitia Saini sehemu ya Mwanasheria kwenye Mkataba wa Ujenzi wa Mihadhara 2 katika Chuo cha Tengeru Arusha akishuhudiwa na Mwanasheria, Bi. Irene Likindo aliyesimama wa kwanza kulia na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Ugani na Mafunzo, Dkt. Angelo Mwilawa (wa kwanza kushoto aliyesimama), zoezi limefanyika katika ofisi ndogo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo kwenye jengo la NBC Dodoma. (29.09.2021)

 


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mfunzo ya Mifugo Tanzania, Dkt. Pius Mwambene (kulia) na Meneja wa Kampuni ya Ujenzi ya LI JUN Development (ltd) ya Moshi, Bw.Xu Geng Sheng (kushoto) wakisaini mkataba wa Ujenzi wa vyumba 2 vya Mihadhara (Lecture Theatre) vyenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 240 kila kimoja katika Kampasi ya Tengeru, ambapo ujenzi huo utakamilika ifikapo machi, 2022 na utagharimu shilingi Milioni 809,806,552.37. Hafla hii imefanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo kwenye jengo la NBC Dodoma (29.09.2021)

 

Jumatano, 29 Septemba 2021

ZIWA VICTORIA KUFANYIWA MPANGO BORA WA MATUMIZI KUKUZA UCHUMI WA BULUU


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kufanya mpango wa matumizi bora ya ziwa Victoria ambao utaainisha maeneo ambayo yatatumika kufanya ufugaji wa vizimba ili kutoa nafasi pia kwa shughuli za uvuvi wa asili kuendelea bila kuwa na muingiliano.

Ulega aliyasema hayo Septemba 27, 2021 alipotembelea eneo la Kampuni ya Kichina ya Tangreen iliyowekeza katika mradi wa ufugaji wa Samaki kwa kutumika vizimba kandokando ya ziwa Victoria, jijini Mwanza.

Alisema kuwa serikali imedhamiria kufanya hivyo ili kupunguza muingiliano wa shughuli za ufugaji wa Samaki na Uvuvi wa asili ili shughuli zote zifanyike kwa ufanisi na kuleta tija katika uchumi wa buluu.

"Mpango wa Serikali ni kuhakikisha ufugaji wa vizimba unafanyika katika maeneo maalum na sio kila mahala, tuwe na maeneo mahsusi ya kazi hii ili kutoa nafasi pia wavuvi wa asili waweze kuendelea na shughuli zao," alisema Ulega

Waziri Ulega alisema kuwa mpango huo pia utavutia wawekezaji wengi kuwekeza katika ziwa Victoria, na wao kama Serikali wanawakaribisha wawekezaji kama TanGreen kuja kuwekeza nchini.

"Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji, na hivi karibuni tumemuona akifanya jitihada kubwa kwa kuitangaza nchi yetu katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kufungua milango ya uwekezaji, na moja ya maeneo ya uwekezaji aliyokuwa akiyatangaza ni katika uchumi wa buluu," alisema Ulega

Aliongeza kuwa TanGreen imejikita katika kukuza uchumi wa buluu kwa kufuga Samaki wa vizimba na wanatarajia kuvuna Tani Elfu kumi (10, 0000) kwa mwaka, huku akisema kuwa kwa sasa nchini samaki wanaovuliwa kutoka kwenye mabwawa ni Tani Elfu Ishirini na Mbili (22,000) hivyo TanGreen wanakwenda kuzalisha nusu ya kile kinachozalishwa sasa nchini.

Aidha, alimuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salim Mkali kuhakikisha muwekezaji huyo analindwa, na kama kutakuwa na wadokozi wenye nia ya kuirudisha nyuma kampuni hiyo wawachukulie hatua kali. 

Ulega aliendelea kusema kuwa bado kunahitajio kubwa la Samaki nchini, kiasi kinachohitaji kwa mwaka ni Tani Laki Saba (700, 000) wakati uwezo uliopo kwa sasa Ni kuzalisha Tani Laki Nne (400, 000) hivyo kufanya pungufu ya Tani Laki Tatu (300,000) huku akisema ufugaji wa vizimba ukifanyika vizuri utasaidia kupunguza changamoto hiyo nchini.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Ruhumbi alisema kuwa wamejipanga kuufanya Mkoa huo kuwa mzalishaji mkubwa wa Samaki wa kufugwa katika mabwawa.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameendelea kuhamasisha uwekezaji wa mitaji na wamehamasisha mabenki kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na imeshaanza kutoa mikopo, huku akisema wanaendelea kuwashawishi wawekeza wakubwa wa mitaji kuwekeza katika ufugaji wa samaki na kukuza uchumi wa buluu.

"Hivyo unaweza kuona kuwa ushawishi tulioufanya ndio umepelekea wawekezaji wakubwa kama TanGreen kujitokeza na kwa kweli imeleta tija kwa sababu miaka mitatu iliyopita kulikuwa na vizimba 18, lakini kwa sasa tunavizimba 473 na asilimia 77 ya vizimba vyote vipo hapa ziwa Victoria," alisema Dkt. Tamatamah

Awali, Daktari wa Samaki wa Kampuni ya TanGreen, Dkt. Mugure Katwiga Mariwanda akisoma taarifa fupi ya Kiwanda hicho alisema kuwa moja ya lengo la Kampuni hiyo ni kukuza na kutangaza teknolojia ya ufugaji ikiwemo kufungua fursa ya ajira kwa vijana.

"Mhe. Naibu Waziri, pamoja na jitihada tunazoendelea nazo lakini tunakumbana na changamoto kadhaa ikiwemo uhaba wa vifaranga vya Samaki ndani ya nchi, baadhi ya wavuvi kuingia ndani ya mradi kuiba au kuharibu miundombinu," alisema Dkt. Katwiga Mariwanda

Aliongeza kwa kuiomba Serikali itoe vibali vya kuingiza vifaranga vya samaki kutoka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji yaliyopo huku akiiomba Serikali iendelee kutoa elimu kwa jamii ya wavuvi juu ya uwekezaji wa vizimba ili waache kufanya shughuli za uvuvi katika mradi huo.


Muonekano katika picha ni Nyumba ya wafanyakazi wa TanGreen na baadhi ya vizimba vya kufugia Samaki vilivyowekwa ndani ya Ziwa Victoria. Nyumba hiyo imejengwa mahususi kwa ajili ya wafanyakazi wanaosimamia vizimba hivyo ndani ya ziwa. 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiwapa chakula Samaki wanaofugwa katika sehemu ya vizimba vya Kampuni ya TanGreen vilivyowekwa ndani ya ziwa Victoria. Ulega alifanya ziara katika eneo la Kampuni hiyo ya Kichina ambayo inajishughulisha na ufugaji wa samaki kwa kutumika vizimba Septemba 27, 2021. 

 


SERIKALI YADHAMIRIA KUBORESHA BIASHARA YA MIFUGO NCHINI.

 


Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuboresha mazingira ya biashara ya mifugo, ikiwemo ujenzi wa mnada wa upili wa nyamatala ili kuendelea kuchochea uchumi wa taifa.

Hayo yalisemwa   na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Amosy Zephania, wakati akizungumza na wafanyabiashara wa mifugo wa mnada wa upili Nyamatala uliopo Wilayani Misungwi mkoani Mwanza Septemba 27,2021.

Alisema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kuhamasisha wafanyabiashara wa mifugo kukutana na wenye viwanda, wazungumze na kukubaliana bei ili kuwezesha upatikanaji wa mifugo yenye ubora ambao unahitajika kwenye viwanda na wafanyabiashara hao kupata soko zaidi.

"Lengo ni kuendelea kuona mifugo inapata thamani, ambapo watu wa viwandani wanadai kuwa mifugo wanayopelekewa haina ubora wanao wanaouhitaji." Alisema

Aliongeza kuwa wanaposema biashara, wanaanzia sokoni, Wizara pamoja na serikali kwa ujumla mpaka sasa ina viwanda vitano vikubwa vinavyotegemea malighafi za mifugo ikiwemo kiwanda cha Chobo Misungwi na Tan Choice.

"Sisi tumekuja kutoa rai kwenu, wenye viwanda waje wazungumze na nyinyi, wawaeleze wanataka mifugo ya aina gani, mifugo inenepeshwe kwa kiwango gani na watatoa bei gani, Alisema Bw. Zephania.

Mmoja wa wafanyabiashara wa mifugo mnada wa upili Nyamatala Bw. Emmanuel Mgelwa, aliipongeza serikali kuwatimizia mahitaji waliokuwa wanayataka katika mnada huo ila changamoto ni suala la ulinzi.

Naye Tabu Shindika, aliiomba serikali kuleta mnada wa mbuzi katika eneo hilo ili mtu akitaka ng'ombe, mbuzi na kondoo wapate hapo kwenye mnada wa Nyamatala.


Kaimu katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Amosy Zephania akiongea na wafugaji pamoja na wafanyabiashara wa Mifugo wa mnada wa Upili nyamatala wakati wa ziara yake Mkoani Mwanza. Lengo ni kujua changamoto zinazowakabili katika biashara yao na kujadili njia Bora za kuweza kutatua changamoto hizo kwenye mnada Huo Mkoani Mwanza. Septemba 27,2021 

ULEGA AINGILIA KATI MGOGORO SHAMBA LA SERIKALI NANGARAMO NA WANANCHI


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu kuweka utaratibu mzuri wa kugawa kwa muda sehemu ya shamba la kuendeleza Mifugo la Nangaramo na kuwapatia wananchi wanaoishi karibu na shamba hilo ili waweze kufanya shughuli zao za kilimo.

Ulega alitoa maelekezo hayo Septemba 24, 2021 kufuatia malalamiko aliyoyapata kutoka kwa wananchi wanaoishi karibu na shamba hilo kukosa maeneo ya kulima wakidai kuwa mipaka ya shamba hilo imewekwa ndani ya maeneo yao ya asili ya kilimo.

Akiwa katika shamba hilo lililopo Wilayani Nanyumbu, Mkoani Mtwara, Naibu Waziri Ulega alipata fursa ya kusikiliza kero za wananchi hao ambao wengi wao waliiomba Serikali kuwapatia sehemu ya eneo la shamba hilo ili waweze kulima zao la mpunga.

Baada ya kusikiliza malalamiko ya Wakulima hao ambao walisema maeneo yao yamechukuliwa na shamba hilo, Ulega alimuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo kupitia upya maeneo ya mipaka ya shamba hilo ili waone ni sehemu gani katika shamba hilo wanaweza kuligawa kwa muda kwa Wakulima hao.

 

"Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya asipewe mtu kipande cha kulima bila kuwa na karatasi ya makubaliano itakayothibisha muda wa kulima katika eneo hilo, maana bila kufanya hivyo kuna wachache wanaweza kugeuka huko mbele wakauza maeneo hayo wakati yeye alipewa kwa muda tu," alisema Ulega

Naibu Waziri Ulega aliendelea kusema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Samia Suluhu Hassan inatumia maarifa makubwa sana katika kuwahudumia wananchi na kuwaletea maendeleo na hivyo aliwataka wananchi hao kuendelea kulitunza shamba hilo na wasigombane na Uongozi wa shamba hilo, wakae kwa amani na upendo ili waweze kufanya shughuli zao vizuri.

"Shamba hili ni lenu Watanzania wote litunzeni, muwe na wivu na shamba hili, msimuone mtu analifanyia ubaya na nyie mkafurahia, hapana, msifanye hivyo litunzeni ni mali yenu,"alisisitiza Ulega

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Mariam Chaurembo alimuhakikishia Naibu Waziri kuwa maelekezo yake wameyapokea na watayafanyia kazi.

"Mheshimiwa Naibu Waziri tunakuahidi tutasimamia maelekezo yako na tunaamini wakati wa mvua ukifika Wakulima hawa wakianza kulima katika maeneo tutakayo wagawia lugha itakuwa tofauti hapa," alisema Chaurembo

Awali, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, Yahya Mhata alisema kuwa ni muhimu Serikali kuangalia upya mipaka ya shamba hilo ambalo sehemu kubwa kumekuwa pori bila kutumika, huku akimuomba Naibu Waziri Ulega kuona uwezekano wa kutoa baadhi ya eneo na kuwagawia Wakulima ili waweze kufanya shughuli zao za Kilimo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alitoa maelekezo ya kuboresha shamba la kuendeleza mifugo la Nangaramo kwa Meneja wa Shamba hilo (kulia kwake- aliyevaa Shari jeupe) alipotembelea katika shamba hilo Septemba 24, 2021. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Mariam Chaurembo

Sehemu ya Wananchi wanaoishi karibu na shamba la kuendeleza Mifugo la Nangaramo lililopo Wilayani Nanyumbu, Mkoani Mtwara wakiwa wanamsikiliza Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (hayupo pichani) alipotembelea Shamba hilo Septemba 24, 2021. 

 

SERIKALI KUFANYA MAPITIO SHERIA NA KANUNI SEKTA YA UVUVI NCHINI


Serikali ipo katika mchakato wa kufanya mapitio ya sheria na kanuni zinazo simamia sekta ya uvuvi nchini ili kukuza na kuendeleza viumbe maji ikiwemo ufugaji samaki kwa kutumia vizimba.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Mashimba Ndaki amebainisha hayo  September 24,2021 jijini Dodoma wakati alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya kushiriki mkutano wa kimataifa wa kukuza na kuendeleza ukuzaji viumbe maji ulifanyika kwa njia ya video.

Mashimba, alisema lengo la kupitia sheria pamoja na kanuni katika sekta hiyo ni kuhakikisha kuwa zinawezesha uvuvi wa kutumia vizimba pamoja na mabwawa.

“Sheria pamoja na kanuni zetu awali sekta hii ya uvuvi ilikuwa imemezwa na uvuvi wa majini tuu hivyo tunafanya mapitio ili kuwezesha uvuvi huu wa kutumia vizimba unakuwa na mchango katika kuongeza pato la taifa” alisema Mashimba.

Akizungumzia mkutano huo alisema lengo lake ni kuwezesha nchi washiriki kukuza na kuendeleza ukuzaji wa viumbe maji kwa kutumia uvuvi wa vizimba, mabwawa pamoja na njia nyingene.

“Pia katika mkutano huu tunaangalia changamoto pamoja na fursa zilizopo, vipaumbele na namna ya kuendeleza uvuvi wa viumbe maji” alisema Ndaki.

Alisema uvuvi huo unamchango mkubwa katika usalama wa chakula ambapo hivi sasa sekta hiyo inachangia pato la taifa kwa asilimia 1.7.

“Kwenye samaki tunapata protini kwa asilimia 21 na takwimu zinaonyesha kuwa kuna kipindi tulipanda hadi kufikia mtu mmoja kula kilo 14, kwa mwaka lakini mwaka 2020, tumeshuka hadi mtu mmoja kula kilo 8.5 kwa mwaka” alisema

Kutokana na hali hiyo alisema Taifa linatakiwa kuwa na uvuvi endelevu unaochangia usalama wa chakula na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Tumekubalina kuwa na ushirikiano  wa namna ya kupeana utaalamu wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ili kuwa na uvuvi endelevu utakao kuza pato letu lakini pia pato la dunia kupitia sekta hii” alisisitiza

Vilevie, alisema mkakati wa serikali ni kuhakikisha inafanya utafiti wa maeneo kwa ajili ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba.

 

“Ili kuwasaidia watu wanaohitaji kufuga samaki kwa njia hii serikali inafanya utafiti wa mazingira kwa ajili ya ufugaji ili kuwaondolea gharama wananchi watakao hitaji kwa kuwa gharama zake ni kubwa” alisema

Kadhalika, alisema mkakati mwingine ni kuhakikisha kuwa vituo vitano vya ukuzaji viumbe maji vinaboreshwa na kuzalisha vifaranga vya samaki kwa wingi na vyenye ubora.

“Lakini pia serikali inampango wa kuanzisha mashamba darasa kila wilaya kwa ajili ya kufundisha wakulima pamoja na wafugaji ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba na mabwawa” alisemaWaziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) September 24,2021. ofisini kwake iliyopo mji wa serikali Mtumba, jijini Dodoma mara baada ya kushiriki mkutano wa kimataifa wa kukuza na kuendeleza ukuzaji viumbe maji ulifanyika kwa njia ya video.

WAZIRI NDAKI ATEKELEZA AGIZO LA RAIS, AGAWA ENEO KWA WAFUGAJI

 

Serikali imekabidhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza eneo lenye ukubwa wa Hekta 6,000 lililotolewa kwa wananchi wa vijiji vya Mpeta na Chakuru ili ligawiwe kwa wananchi hao kwa ajili ya shughuli za ufugaji baada ya mgogoro wa muda mrefu wa wananchi hao kuvamia Hifadhi ya Ranchi ya Taifa ya Uvinza iliyopo Mkoani Kigoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amekabidhi eneo hilo (23.09.2021), akitekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ameamua eneo hilo kumegwa kutoka Hifadhi ya Ranchi ya Taifa ya Uvinza baada ya kusikia kilio cha wafugaji hao kutoka mikoa ya kanda ya ziwa kutokuwa na maeneo kwa ajili ya mifugo yao.

Waziri Ndaki alibainisha kuwa hatua hiyo inakuja kukiwa na mgogoro mkubwa baina ya wananchi hao ambao ni wafugaji, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambapo wananchi zaidi ya 5,900 wamevamia eneo la ranchi hiyo kitongoji cha Mwanduhubanhu kijiji cha Mpeta na eneo la Kazaroho Wilaya ya Uvinza na kuendesha shughuli za ufugaji na kilimo.

Kabla ya hatua ya kukabidhi eneo hilo serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, watendaji wa Halmashauri za Wilaya za Uvinza na Kasulu kutoka Idara za Ardhi, Kilimo na Mifugo ambao walifanya sensa ya kujua idadi ya wavamizi hao kupima eneo ambalo litaweza kutumika kwa wananchi, kuchora ramani upya na kugawa eneo kuondoa mgogoro huo mchakato uliochukua miezi miwili kukamilika.

Waziri Ndaki alisema awali Rais Samia alishauriwa kutoa Hekta 4,000 lakini baada ya kufanywa kwa sensa ya watu na mifugo aliamua kutoa Hekta 6,000 ili ziweze kutumiwa na wananchi hao.

“Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa eneo hili naomba kutangaza kuwa serikali haitaongeza eneo lingine na mgawanyo utafanywa kwa watu zaidi ya 5,900 waliokuwa wakihusika na mgogoro na kwamba watakaovamia eneo la ranchi ambalo siyo eneo lililomegwa na kugawiwa sheria itachukua mkondo wake.” Amesema Waziri Ndaki

 

Akitoa taarifa kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe amesema mchakato umefanyika kwa kuwa na vikao zaidi ya vitano na viongozi na wananchi waliovamia eneo hilo ambapo changamoto mbalimbali zilijitokeza.

Prof. Msoffe alisema licha ya mapendekezo na ushauri uliokuwa ukitolewa na wataalam wananchi hao pia walikuwa na mapendekezo, ushauri na maamuzi ambayo wakati mwingine yaliegemea kwenye baadhi ya makundi kuona yananufaika zaidi hivyo maamuzi mengi kuwa na changamoto ya kufikia mwisho kwa faida ya wote.

“Kwa sasa kumekuwa na idadi kubwa sana ya watu na mifugo na hiyo inatokana na ongezeko kubwa la wavamizi hao ambapo baada ya kusikia kumeanza mchakato wa sensa na upimaji baadhi ya watu waliongezeka ambao hapo awali hawakuwepo kwenye eneo hilo na wengine wameingia kwenye eneo ambalo hapo awali halikuwa kwenye mgogoro na kuanza kudai waongezewe eneo.” Alisema Mkurugenzi huyo wa NARCO.

Aliongeza kuwa eneo hilo la Hekta 6,000 limegawanywa kwa Hekta 2,500 kutoa kitongoji cha Kazaroho kijiji cha Mpeta na Hekta 3500 kitongoji cha Mwanduhubanhu kijiji cha Mpeta wilaya ya Uvinza.

Naye Mkuu wa Wilaya Uvinza, Mhe. Anafi Msabaha akizungumza katika mkutano huo amesema mgogoro huo umefikia mwisho kwa maamuzi ya Rais kutoa eneo ambalo litatumiwa na wananchi waliokuwa kwenye mgororo na kwamba wilaya itasimamia kuona taratibu za ugawaji zinafanyika kwa uwazi na wananchi ambao ni wafugaji waliohusika wanapatiwa maeneo kulingana na mgawanyo utakaofanyika.

Baadhi ya wananchi walioongea baada ya taarifa ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki kuhusu kutolewa kwa eneo hilo wameishukuru serikali kwa kukubali kuwamegea eneo hilo, huku wakidai bado eneo walilopewa haliwezi kutosheleza mahitaji na kuomba waongezewe maeneo zaidi.

Mmoja wa wananchi hao Bw. Masele Mayenga amesema eneo lililotolewa linaweza kutumika kupatia ufumbuzi wa mgogoro uliokuwepo ambapo wafugaji walikuwa wakisumbuliwa na kuondolewa eneo la Ranchi kwa kuvamia eneo hilo ambapo amesema kuwa bado eneo walilopewa haitoshelezi mahitaji yao.


Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) Prof. Peter Msoffe (aliyesimama kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Uvinza Bw. Masumbuko Kechegwa (aliyesimama kushoto) wakikabidhiana nyaraka ambapo NARCO imekabidhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Hekta 6,000 zilizomegwa kutoka kwenye Ranchi ya Uvinza kwa ajili ya wananchi ambao ni wafugaji waliovamia ranchi hiyo. Agizo la kumegwa eneo hilo limetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. (23.09.2021) 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyesimama kulia) akizungumza na wananchi wa vitongoji vya kijiji cha Mpeta Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma, kuhusu agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kumega Hekta 6,000 za Ranchi ya Taifa ya Uvinza na kugawiwa kwa wananchi waliovamia eneo hilo na kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji. (23.09.2021) 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyesimama wa pili kutoka kushoto) na Mkuu wa Wilaya Uviza Mhe. Hanafi Msabaha (wa kwanza kushoto) wakishuhudia Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) Prof. Peter Msoffe (aliyekaa kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Uvinza Bw. Masumbuko Kechegwa (aliyekaa kushoto) wakisaini nyaraka za makabidhiano ambapo NARCO inakabidhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Hekta 6,000 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi waliovamia Hifadhi ya Ranchi ya Taifa ya Uvinza iliyopo katika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma ili kumaliza mgogoro wa muda mrefu baina ya pande hizo. (23.09.2021) 


ULEGA: TUMEDHAMIRIA KUWAWEZESHA WAVUVI WAONDOKANE NA UVUVI WA KUWINDA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kuwaelimisha Wavuvi na kuwapa vifaa maalum vitakavyowasaidia kujua wapi kuna makundi ya Samaki ili waachane na Uvuvi wa kuwinda ambao umekuwa hauna tija kwao.

Ulega aliyasema hayo katika hafla fupi ya kuwakabidhi Wavuvi na Wakulima wa Mwani vifaa vya kufanyika kazi vikiwemo injini ya boti na Kamba za kulimia zao la Mwani iliyofanyika katika Kijiji cha Mchinga, Mkoani Lindi Septemba 23, 2021.

"Sasa hivi tunatumia njia ya 'Satelite' kujua mavuvi yetu yako wapi, samaki wako wapi, kifaa cha GPS kinamsaidia mvuvi kabla hajatoka Pwani kujua aende umbali gani ambako kuna makundi ya Samaki,"alisema Ulega

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwataka Wavuvi na Wakulima wa zao la Mwani kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwaletea maendeleo.

Katika hafla hiyo, Naibu Waziri Ulega aliwapatia Wavuvi injini moja ya boti yenye thamani ya Shilingi Milioni 11, na Kamba zenye thamani ya Shilingi Milioni 8 kwa Vikundi vitatu vya kina mama Wakulima wa Mwani Mkoani humo.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mama Salma Kikwete alisema kuwa anaishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha wananchi wa Jimbo lake vifaa vitakavyowasaidia kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Aliongeza kuwa yeye kama Mbunge kwa kushirikiana na wananchi ataendelea kuhakikisha maendeleo yanapatiakana kwa kasi katika Jimbo hilo la Mchinga.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akimkabidhi Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mama Salma Kikwete (kushoto) injini ya Boti yenye thamani ya Shilingi Milioni 11 kwa ajili ya kuwapa Wavuvi waitumie katika shughuli zao. Hafla ya kukabidhi injini ilifanyika Katika Kijiji cha Mchinga, Mkoani Lindi Septemba 23, 2021. 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (katikati) akikabidhi kamba za kulimia Mwani kwa wakina Mama Wakulima wa Mwani katika Kijiji cha Mchinga Mkoani Lindi Septemba 23, 2021. Kamba hizo zilizokabidhiwa zina thamani ya Shilingi Milioni 8 Kulia kwake ni Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mama Salma Kikwete. 


Mmoja wa kina Mama wanaojishughulisha na ukulima wa Mwani, Fatuma Selemani akiishukuru Serikali kwa kuwapatia vifaa vitakavyowasaidia kurahisisha utendaji kazi wao. Alitoa shukrani hizo katika hafla ya kukabidhi boti kwa Wavuvi na Kamba kwa Vikundi vya kina mama Wakulima wa Mwani iliyofanyika katika Kijiji cha Mchinga, Mkoani Lindi Septemba 23, 2021. 

 

SERIKALI YA RAIS SAMIA KUWAINUA KIUCHUMI WANANCHI WA RUANGWA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kupeleka miradi ya ufugaji Kuku, Mbuzi na  Samaki katika Wilaya ya Ruangwa ili iwasaidie  kuinua Uchumi wao.

Ulega aliyasema hayo  wakati akiongea na Viongozi wa Wilaya ya Ruangwa iliyopo Mkoani Lindi  Septemba 22, 2021.

Alisema kutokana na kasi kubwa ya maendeleo ya Wilaya hiyo inayochochewa na shughuli za uchimbaji madini Serikali imeona ni vyema kupeleka miradi hiyo kwa kina mama na vijana ili kukuza uchumi wao na kukidhi mahitaji ya mazao ya Mifugo katika Wilaya hiyo.

Naibu Waziri Ulega aliitaja miradi hiyo ambayo  itapelekwa katika Wilaya hiyo na kuwasaidia wakina mama na vijana ni pamoja  ufugaji wa kuku na ufugaji wa Samaki na Mradi wa Kopa mbuzi lipa mbuzi.

"Mwezi Oktoba tutaanza na Vikundi kumi, tutaleta Wilayani hapa kuku elfu mbili (2000) ikiambatana na semina ya kuelekeza namna ya kufuga kuku hao kibiashara," alisema Ulega

Aidha, Waziri Ulega alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma kutafuta eneo zuri ambalo watalitumia kuanza kufanya ufugaji wa Samaki.

"Sasa tafuteni eneo na kikundi kimoja kizuri ili tuje kuweka shamba darasa la ufugaji wa samaki, kikundi hicho kitakuwa kinavuna Samaki hao na watawafundisha na wengine kuhusu ufugaji huo wa samaki," aliongeza Ulega

Waziri Ulega alimuahidi Mkuu wa Wilaya hiyo kuwa atapeleka wataalamu wa shughuli ya ufugaji wa Samaki ili kuwasaidia wananchi hao.

Naye, Mkuu wa Wilaya hiyo alisema kuwa kufuatia kuchipuka kwa shughuli za madini Wilayani humo kumepelekea kuongezeka kwa mahitaji mbalimbali muhimu ikiwemo mahitaji ya nyama, mayai, Samaki na maziwa ambayo mengi yamekuwa yakiagizwa katika maeneo mengine ya nchi na hivyo alimuomba Naibu Waziri kuona hizo fursa na kuwawezesha wananchi wa Wilaya hiyo ili waweze kuzitumia.

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiongea na Wafugaji na Wakulima wa Kijiji cha Nangurugai Kilichopo Wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi Septemba 22, 2021. Lengo la ziara yake hiyo ni kusikiliza kero za Wakulima na Wafugaji na kuzitatua. Sehemu ya Wananchi wa Kijiji cha Nangurugai wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (hayupo pichani) alipokuwa akiongea nao Septemba 22, 2021. Ulega alikwenda katika Kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake Wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi. 


NACHINGWEA YATAKIWA KUSIMAMIA MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI KWA WAKULIMA NA WAFUGAJI


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Hashim Komba kuhakikisha anawapanga Wakulima na Wafugaji katika maeneo waliyopangiwa ili kuondosha migogoro inayoikabili Wilaya hiyo.

Ulega aliyasema hayo wakati akiongea na Wakulima na Wafugaji wa Kata za Matekwe, Kilimarondo, Kiegei na Mbondo alipofanya ziara katika Wilaya hiyo ya Nachingwea, Mkoani Lindi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za Wakulima na Wafugaji Septemba 21, 2021.

Alisema kuwa ili Wilaya hiyo iondokane na migogoro ya Wakulima na Wafugaji ni lazima Serikali isimamie mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao tayari wanao.

"Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya mfugaji au mkulima anayefanya shughuli katika eneo ambalo hakupangiwa mtoe mpeleke katika eneo analopaswa kufanya shughuli zake, ni lazima tusimamie utaratibu tuliojiwekea kwa mujibu wa sheria," alisema Ulega

kuhusu tatizo la maji ya kunyweshea Mifugo linalowasumbua Wafugaji wa maeneo hayo, Ulega alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametenga Shilingi Milioni 480 kwa ajili ya kujenga Bwawa la kunyweshea Mifugo litakalojengwa katika Kijiji cha Matekwe Kilichopo Wilayani humo ili Wafugaji wawe na maji ya uhakika wakati wa kiangazi.

"Sio bwawa tu, Rais Mama Samia atawajenge Josho kwa ajili ya kuogeshea mifugo, Milioni 18 zitatolewa kwa ajili ya kazi hiyo, Sasa nitashangaa sana nikiona wafugaji mnaendelea kuzagaa," alisisitiza Ulega

Aidha, alitumia fursa hiyo pia kuwaonya Wakulima na Wafugaji hao kuacha vitendo vya kujichukulia Sheria mkononi kwani havifai na vinahatarisha amani katika jamii.

Naye Mkuu wa Wilaya wa Nachingwea, Hashim Komba alimuhakikishia Naibu Waziri Ulega kuwa maelekezo yote aliyoyatoa atayafanyia kazi na kisimamia sheria ili utaratibu ufuatwe.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiongea na Wafugaji na Wakulima wa Kata za Matekwe, Kilimarondo, Kiegei na Mbondo alipofanya ziara katika Wilaya ya Nachingwea iliyopo Mkoani Lindi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za Wakulima na Wafugaji Septemba 21, 2021. Katika Mkutano huo Naibu Waziri alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Hashim Komba (kushoto) kuhakikisha anasimamia Mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuwapanga Wafugaji na Wakulima katika maeneo husika. 


Sehemu ya Wafugaji na Wakulima waliohudhuria Mkutano wa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (hayupo pichani) alipokuwa akiongea nao katika Kijiji cha Kilimarondo, Wilayani Nachingwea, Mkoani Lindi Septemba 21, 2021. 


SERIKALI KUENDELEA KUHAMASISHA ULAJI WA NYAMA NCHINI.

 

Wizara ya Mifugo na Uvuvi   imesema  bado ulaji wa nyama nchini Tanzania  ni mdogo ambapo kwa sasa ulaji ni kilo 15 kwa mtu tofauti na tafiti za shirika la chakula Duniani  linaloelekeza kila mtu atumie kilo 50 kwa mwaka. 

Akizungumza,  Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Amosy Zephania  katika ziara yake ya kikazi  katika  shamba la kuku la Irvine  wilayani siha Mkoani Kilimanjaro Septemba 21,2021 ambapo  alisema kuwa  kutokana na hali hiyo serikali inatarajia kuendelea kutoa elimu kwa watanzania kuona umuhimu wa ulaji wa nyama .

“Sensa ya mifugo ya mwaka 2019/2020 inanyesha katika kaya zinazijishughulisha na kilimo na ufugaji  Tanzania ni zaidi ya milioni saba, kaya zaidi ya milioni nne sawa na asilimia 55. 3 wanafuga kuku kuanzia 10 na kuendelea, hii inaonyesha jinsi tunavyozungumza kuku tu, nazungumzia maisha ya watanzania kwanzia ngazi ya chini  hadi juu, "amesema 

Alisema ni wajibu wa Kampuni hiyo kuhamasisha  wananchi kujikita katika ufugaji wa kuku  hali itakayo peleka ongezeko la ulaji wa nyama kwa watanzania.

" Toeni elimu kwa jamii, jitanganezi, zipo pesa katika kila halmashauri nchi nzima fikeni huko, zungumzeni   na wakurugenzi wakopesheni kuku vijana, kinamama, watu wenye ulemavu, uwezo wa kulipa  upo, kwa kufanya hivyo tutawafikia watanzania wengi zaidi na ulaji wa nyama utaongezeka, "amesema

Kwa upande wake meneja masoko na uendelezaji wa biashara wa Kampuni hiyo nchini, Jeremia  Kilato alisema wanazalisha vifaranga zaidi laki 220 kwa wiki, ingawa wanatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia zaidi ya laki 290 kwa wiki. 

" Tunajivunia uzalishaji wa kisasa na wenye ubora wa kimataifa, lakini kwa sasa tunakabiliwa na changamoto, ni ongezeko kubwa la uhitaji wa vifaranga hasa katika kipindi hichi cha  Uviko 19, Kampuni imeweka mikakati  ya kuweza   kununua  mashine mpya itakayoongeza uzalishaji kutoka 220 hadi 290,"amesema.

Alisema, wanatarajia kuendelea  kusambaza vifaranga katika  Wilaya zote na Mikoa yote ambapo hadi sasa tayari wamesambaza  katika mikoa 13.

Kwa upande wake meneja wa kituo cha uwekezaji Kanda ya Kaskazini, Bw. Daudi Riganda alisema mwekezaji huyo yupo kihalali na yupo kwenye hatua za mwisho.


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Amosy Zephania akiongea na watendaji wa shamba la irvine's (hawapo pichani) lililopo Mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani huko September 21,2021 lengo ni kuona namna wanaendesha shughuli zao na kisikiliza changamoto zinazowakabili na kuzifanyia kazi.

 

Meneja wa nchi wa shamba ufugaji wa kuku Irvine’s, Bw. Darryl Combe akieleza namna shamba lao lilivyoanza hadi kufikia sasa na malengo yao katika kuendelea kukuza shamba ilo wakati wa ziara ya Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Amosy Zephania (hayupo pichani) kwenye shamba hilo Mkoani Kilimanjaro Septemba 21,2021.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Amosy Zephania (waliokaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Uongozi wa shamba la irvine's wa pili kutoka kushoto ni Bw. Darryl Combe na wa pili kutoka kulia ni Bw. Fabio Stella pamoja na watumishi wa shamba hilo na watumishi kutoka Wizara ya Mifugo na uvuvi, mara baada ya kutembelea shamba hilo lililopo Siha Mkoani Kilimanjaro. Septemba 21,2021.

SERIKALI KUJENGA BWAWA LA MIL. 480 LIWALE


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema katika bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali itajenga bwawa la kunyweshea Mifugo lenye thamani ya Shilingi Milioni 480 katika Kijiji cha Kimambi, Wilayani Liwale, Mkoani Lindi.

Ulega aliyasema hayo Septemba 20, 2021 alipofanya ziara katika Wilaya ya Liwale, Mkoani Lindi kwa lengo la kusikiliza kero za Wafugaji na Wakulima ili kuzitatua.

Alisema ujenzi wa bwawa hilo utasaidia kutatua changamoto ya maji ambayo inawakabili wafugaji wa maeneo hayo na utasaidia pia kutatua migogoro baina yao na wakulima Wilayani humo.

"Rais Samia Suluhu Hassan anakwenda kuwajengea bwawa lenye thamani ya Shilingi Milioni 480 hapa Kimambi, ujenzi wa bwawa hilo utasaidia kuwaondosha katika migogoro," alisema Ulega

Naibu Waziri Ulega alisisitiza kuwa  pesa hizo zipelekwe kufanya kazi iliyopangiwa ya ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo huku akiwataka viongozi wa Wilaya hiyo kuhakikisha pesa hizo zinatumika vizuri.

Aidha, alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewapa pia Majosho mawili katika Kijiji cha Kimambi na Kijiji cha Luwele.

"Sasa kwa sababu huku mifugo  imekuwa mingi sana, Mimi nakuongezeeni Josho lingine hapa ili mifugo mingi iweze kuogeshwa ," aliongeza Ulega

Naye, Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea pesa hizo huku akisema kuwa bwawa hilo likikamilika hawatarajii tena kuona migogoro katika Vijiji vilivyotengwa kwa ajili ya Wafugaji Wilayani humo.

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiongea na Wafugaji na Wakulima wa Kijiji cha Kimambi, Wilayani Liwale, Mkoani Lindi (hawapo pichani) alipofanya ziara katika Wilaya hiyo Septemba 20, 2021 kwa lengo la kutatua kero zao. Katika ziara hiyo Ulega alisema Serikali itajenga bwawa la kunyweshea Mifugo Kijijini hapo lenye thamani ya Shilingi Milioni 480.  Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Judith Nguli.

 

Sehemu ya Wakulima na Wafugaji wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (hayupo pichani) alipokuwa akiongea nao katika Kijiji cha Kimambi,  Wilayani Liwale Mkoani Lindi Septemba 20, 2021. 

 


*ULEGA AWATAKA WAFUGAJI PWANI KUVUNA MIFUGO YAO*


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka Wafugaji wa Mkoa wa Pwani kuanza kuvuna Mifugo yao na kuiuza kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kuwaongezea kipato na kupunguza migogoro kati yao na watumiaji wengine wa ardhi.

Ulega aliyasema hayo Septemba 19, 2021 wakati akiongea na Wafugaji na Wakulima wa Wilaya ya Rufiji alipofanya ziara Wilayani humo ya kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Alisema ni muhimu viongozi wa Wilaya za Rufiji, Mkuranga na Kibiti kukaa na wadau wa mifugo kutengeneza mkakati wa kuhamasisha uvunaji wa mifugo yao kwakuwa soko la kuuza lipo mkoani humo na bado hawajalitumia ipasavyo.

"Hapa Mkoa wa Pwani tuna Kiwanda cha Nyama cha TanChoice lakini pamoja na kiwanda hicho kuwepo hakuna mifugo inayopelekwa pale kutoka ukanda wetu huu wa Pwani," alisema Ulega

Aliongeza kwa kusema kuwa ili faida ya uwepo wa kiwanda hicho ionekane ni vyema wadau wote wa mifugo mkoani humo waanze uvunaji mkubwa na kupeleka kuiuza kiwandani hapo.

"Tunatamani kuona mifugo inatoka katika ukanda huu wa Pwani na kwenda kuuzwa jijini Dar es Salaam ambapo ndipo kwenye biashara kubwa ya nyama, msione fahari kukaa na makundi makubwa ya mifugo ambayo mwisho wa siku yakaonekana kuwa ni kero na hayana faida," aliongeza Ulega

Kuhusu kuboresha huduma za Mifugo, Waziri Ulega alisema kuwa katika Bajeti ya Mwaka huu 2021/ 2022 Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kununua Pikipiki 300 na itazigawa kwa Maafisa Ugani nchi nzima ili waweze kutoa huduma ya mifugo kwa ufanisi.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowelle alisema kuwa kufuatia migogoro mingi iliyoibuka katika Wilaya yake ameanzisha zoezi la sensa ya Mifugo na Wafugaji ili waweze kujua idadi yao halisi na kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi kulingana na mahitaji.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akimsikiliza Mwenyekiti wa Kijiji cha Chumbi C, Muhidin Mtopa (katikati) alipokuwa akimuonesha moja ya eneo lililotengwa na Serikali kwa ajili ya Wafugaji Kijijini hapo lakini baadhi ya Wafugaji wamebadirisha eneo hilo kuwa makazi na mashamba ya mpunga. Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, kitendo hicho kimesababisha migogoro ya wakulima na wafugaji kuendelea kushamiri katika Kijiji hicho. Naibu Waziri Ulega alitembelea Kijiji hicho Kilichopo Wilayani Rufiji Mkoani Pwani Septemba 19, 2021.Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiongea na Wafugaji na Wakulima wa Wilaya ya Rufiji(hawapo pichani) alipofanya ziara Wilayani humo Septemba 19, 2021 kwa lengo la kusikiliza kero zao na kuzitatua. Naibu Waziri Ulega pamoja na mambo mengine aliwataka wafugaji wa Mkoa wa Pwani kwa ujumla kuvuna Mifugo yao ili kujiongezea kipato na kupunguza migogoro ya mara kwa mara kati yao na watumiaji wengine wa ardhi. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowelle. 

WAHUSIKA VYETI VYA VIFO VYA ZAIDI YA NG'OMBE 270 WASAKWA*


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameagiza maafisa mifugo na madaktari wa mifugo, Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, walioandika au kushuhudia vyeti vya vifo vya ng’ombe zaidi ya 270 ambao walikamatwa na uongozi wa Pori la Hifadhi la Maswa kusakwa na kufikishwa katika Baraza la Veterinari Tanzania ili kuchunguzwa.

Waziri Ndaki amebainisha hayo (16.09.2021) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya za Itilima na Meatu ambapo akiwa katika Wilaya ya Itilima aliarifiwa baadhi ya wafugaji walioshinda kesi Mahakama ya Rufaa mwaka 2019, baada ya ng’ombe wao kudaiwa kuingia katika Pori la Hifadhi la Maswa mwaka 2017, kurejeshewa ng’ombe 51 pekee huku uongozi wa pori hilo ukiwaarifu ng’ombe zaidi ya 270 walikufa, bila wafugaji hao kushuhudia mizoga ya ng’ombe hao wala vyeti vya vifo ambavyo inaelezwa viliandikwa na maafisa mifugo ambao pia hawakushudia mizoga hiyo.

Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa sasa inafuatilia taarifa za wafugaji kote nchini, ambao mifugo yao ilikamatwa na baadaye wafugaji hao kushinda kesi lakini mifugo hiyo haijareshwa kwao wala fedha walizolipishwa faini, kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kutaka taarifa hiyo ambayo wizara inakusanya ili kuifikisha kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa ajili ya maamuzi zaidi.

“Maafisa mifugo na madaktari wa mifugo nchi nzima mnapaswa kujua nyie ni madaktari wa mifugo siyo kukaa kwenye meza na kuandika vyeti vya vifo vya ng’ombe bila kushuhudia vifo hivyo, baadhi yenu wanafanya kazi kiholela.” Amesema Mhe. Ndaki

“Hili jambo siyo dogo ni kubwa nimeagizwa na Rais nije kufuatilia masuala haya watu wameshinda kesi lakini ng’ombe hawajarudishwa kwa wenyewe, nimeambiwa nifuatilie nipeleke orodha yote kwa waziri mkuu ili taarifa itolewe.” Amefafanua Mhe. Ndaki

Kuhusiana na ng’ombe zaidi ya 270 ambao hawajulikani walipo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amemjulisha afisa mifugo Mkoa wa Simiyu kwamba wizara inataka kujua aliyeandika vyeti vya vifo vya ng’ombe hao ambavyo havijulikani vilipo na wala ushahidi wa kuwa ng’ombe hao walikufa, huku akionya maafisa mifugo na madaktari watakaobainika kuendelea kufanya kazi bila kufuata taratibu za kazi zao Baraza la Veterinari Tanzania halitasita kufuta usajili wao.

Aidha, Waziri Ndaki amewaelekeza wakuu wa Wilaya za Itilima na Meatu kufikia Siku ya Jumanne (21.09.2021) wawe wamefikisha taarifa rasmi wizarani juu ya idadi ya mifugo iliyokuwa imekamatwa na kurejeshwa kwa wafugaji, idadi ambayo haijarudishwa pamoja na majina ya wafugaji ambao wanadai mifugo yao baada ya kushinda kesi mahakamani kwa madai kuwa mifugo yao iliingia katika Pori la Hifadhi la Maswa.

Katika nyakati tofauti akiwa katika Wilaya za Itilima na Meatu baadhi ya wafugaji wamelalamikia kitendo cha baadhi ya maafisa wa serikali, kutoheshimu maamuzi ya mahakama ambapo ndiyo chombo cha mwisho katika kutoa haki kwani maamuzi yametolewa siku nyingi lakini baadhi ya wafugaji hawajui hatma ya mifugo yao iliyokamatwa hali iliyosababisha kuwa na maisha duni.

Pia wamemuomba Waziri Ndaki kuwa, serikali iangalie namna ya kuwaruhusu wafugaji kuvuna malisho katika maeneo ya hifadhi badala ya malisho hayo kuchomwa moto ili wafugaji wawe wanayavuna na kuyatunza kwa ajili ya mifugo yao.

Wamebainisha kuwa wamekuwa wakipata shida ya malisho kutokana na baadhi ya maeneo kuwa na ukame, hali ambayo inawapa wakati mgumu kwa mifugo yao kuwa na malisho ya uhakika.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amewahimiza wafugaji kuiwekea mifugo yao hereni za kieletroniki ambazo zinatambua mfugo ulipo kuanzia ngazi ya taifa hadi kijiji hali ambayo itasaidia kuzuia wizi na upotevu wa mifugo.

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), akizungumza na baadhi ya wafugaji wa vijiji vya Shishani na Lungalumbogo vilivyopo Kata ya Migato katika Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu juu ya taarifa ya wafugaji ambao hawajarejeshewa mifugo yao licha ya kushinda kesi mahakamani kwa madai ya kuingiza mifugo katika Pori la Hifadhii la Maswa na kuagiza kusakwa kwa maafisa mifugo na madaktari wa mifugo wa Wilaya ya Bariadi, walioandika au kushuhudia vyeti vya vifo vya ng’ombe zaidi ya 270 waliokuwa wamekamatwa kwa madai ya kuingia kwenye Hifadhi ya Pori la Maswa. Waziri Ndaki ameagiza maafisa hao kufikishwa katika Baraza la Veterinari Tanzania kwa ajili ya uchunguzi zaidi. (16.09.2021) 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), (aliyejifunga shuka) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Itilima Mhe. Faiza Sileiman, wakati alipokuwa akiwasili katika vijiji vya Shishani na Lungalumbogo vilivyopo Kata ya Migato na kupokelewa na wafugaji wa kabila la kisukuma waliokuwa wakiimba moja ya nyimbo za kabila hilo kwa ajili ya mapokezi ya Waziri Ndaki alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Simiyu kufuatilia taarifa ya wafugaji ambao hawajarejeshewa mifugo yao licha ya kushinda kesi mahakamani kwa madai ya kuingiza mifugo katika Pori la Hifadhi la Maswa. (16.09.2021) 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) (kulia), akibadilisha mawazo na Bw. Praisegod Zakaria Afisa Sheria kutoka Bodi ya Nyama nchini (anayemfuata), Dkt. Benezeth Lutege Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Udhibiti wa Magonjwa yaenezwayo na Wadudu pamoja na Bw. Shigi Magese Afisa Sheria kutoka wizarani. Waziri Ndaki aliwasili katika vijiji vya Shishani na Lungalumbogo vilivyopo Kata ya Migato Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo kufuatilia taarifa ya wafugaji ambao hawajarejeshewa mifugo yao licha ya kushinda kesi mahakamani kwa madai ya kuingiza mifugo katika Pori la Hifadhi la Maswa. (16.09.2021)