Nav bar

Jumatano, 29 Septemba 2021

SERIKALI YA RAIS SAMIA KUWAINUA KIUCHUMI WANANCHI WA RUANGWA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kupeleka miradi ya ufugaji Kuku, Mbuzi na  Samaki katika Wilaya ya Ruangwa ili iwasaidie  kuinua Uchumi wao.

Ulega aliyasema hayo  wakati akiongea na Viongozi wa Wilaya ya Ruangwa iliyopo Mkoani Lindi  Septemba 22, 2021.

Alisema kutokana na kasi kubwa ya maendeleo ya Wilaya hiyo inayochochewa na shughuli za uchimbaji madini Serikali imeona ni vyema kupeleka miradi hiyo kwa kina mama na vijana ili kukuza uchumi wao na kukidhi mahitaji ya mazao ya Mifugo katika Wilaya hiyo.

Naibu Waziri Ulega aliitaja miradi hiyo ambayo  itapelekwa katika Wilaya hiyo na kuwasaidia wakina mama na vijana ni pamoja  ufugaji wa kuku na ufugaji wa Samaki na Mradi wa Kopa mbuzi lipa mbuzi.

"Mwezi Oktoba tutaanza na Vikundi kumi, tutaleta Wilayani hapa kuku elfu mbili (2000) ikiambatana na semina ya kuelekeza namna ya kufuga kuku hao kibiashara," alisema Ulega

Aidha, Waziri Ulega alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma kutafuta eneo zuri ambalo watalitumia kuanza kufanya ufugaji wa Samaki.

"Sasa tafuteni eneo na kikundi kimoja kizuri ili tuje kuweka shamba darasa la ufugaji wa samaki, kikundi hicho kitakuwa kinavuna Samaki hao na watawafundisha na wengine kuhusu ufugaji huo wa samaki," aliongeza Ulega

Waziri Ulega alimuahidi Mkuu wa Wilaya hiyo kuwa atapeleka wataalamu wa shughuli ya ufugaji wa Samaki ili kuwasaidia wananchi hao.

Naye, Mkuu wa Wilaya hiyo alisema kuwa kufuatia kuchipuka kwa shughuli za madini Wilayani humo kumepelekea kuongezeka kwa mahitaji mbalimbali muhimu ikiwemo mahitaji ya nyama, mayai, Samaki na maziwa ambayo mengi yamekuwa yakiagizwa katika maeneo mengine ya nchi na hivyo alimuomba Naibu Waziri kuona hizo fursa na kuwawezesha wananchi wa Wilaya hiyo ili waweze kuzitumia.

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiongea na Wafugaji na Wakulima wa Kijiji cha Nangurugai Kilichopo Wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi Septemba 22, 2021. Lengo la ziara yake hiyo ni kusikiliza kero za Wakulima na Wafugaji na kuzitatua. 



Sehemu ya Wananchi wa Kijiji cha Nangurugai wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (hayupo pichani) alipokuwa akiongea nao Septemba 22, 2021. Ulega alikwenda katika Kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake Wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi. 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni