Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amemuagiza Mkuu
wa Wilaya ya Nanyumbu kuweka utaratibu mzuri wa kugawa kwa muda sehemu ya
shamba la kuendeleza Mifugo la Nangaramo na kuwapatia wananchi wanaoishi karibu
na shamba hilo ili waweze kufanya shughuli zao za kilimo.
Ulega alitoa maelekezo hayo Septemba 24, 2021 kufuatia
malalamiko aliyoyapata kutoka kwa wananchi wanaoishi karibu na shamba hilo
kukosa maeneo ya kulima wakidai kuwa mipaka ya shamba hilo imewekwa ndani ya
maeneo yao ya asili ya kilimo.
Akiwa katika shamba hilo lililopo Wilayani Nanyumbu, Mkoani
Mtwara, Naibu Waziri Ulega alipata fursa ya kusikiliza kero za wananchi hao
ambao wengi wao waliiomba Serikali kuwapatia sehemu ya eneo la shamba hilo ili
waweze kulima zao la mpunga.
Baada ya kusikiliza malalamiko ya Wakulima hao ambao walisema
maeneo yao yamechukuliwa na shamba hilo, Ulega alimuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo
kupitia upya maeneo ya mipaka ya shamba hilo ili waone ni sehemu gani katika
shamba hilo wanaweza kuligawa kwa muda kwa Wakulima hao.
"Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya asipewe mtu kipande cha kulima
bila kuwa na karatasi ya makubaliano itakayothibisha muda wa kulima katika eneo
hilo, maana bila kufanya hivyo kuna wachache wanaweza kugeuka huko mbele
wakauza maeneo hayo wakati yeye alipewa kwa muda tu," alisema Ulega
Naibu Waziri Ulega aliendelea kusema kuwa Serikali ya Awamu ya
Sita inayoongozwa na Rais, Samia Suluhu Hassan inatumia maarifa makubwa sana
katika kuwahudumia wananchi na kuwaletea maendeleo na hivyo aliwataka wananchi
hao kuendelea kulitunza shamba hilo na wasigombane na Uongozi wa shamba hilo,
wakae kwa amani na upendo ili waweze kufanya shughuli zao vizuri.
"Shamba hili ni lenu Watanzania wote litunzeni, muwe na
wivu na shamba hili, msimuone mtu analifanyia ubaya na nyie mkafurahia, hapana,
msifanye hivyo litunzeni ni mali yenu,"alisisitiza Ulega
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Mariam Chaurembo
alimuhakikishia Naibu Waziri kuwa maelekezo yake wameyapokea na watayafanyia
kazi.
"Mheshimiwa Naibu Waziri tunakuahidi tutasimamia maelekezo
yako na tunaamini wakati wa mvua ukifika Wakulima hawa wakianza kulima katika
maeneo tutakayo wagawia lugha itakuwa tofauti hapa," alisema Chaurembo
Awali, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, Yahya Mhata alisema kuwa ni
muhimu Serikali kuangalia upya mipaka ya shamba hilo ambalo sehemu kubwa
kumekuwa pori bila kutumika, huku akimuomba Naibu Waziri Ulega kuona uwezekano
wa kutoa baadhi ya eneo na kuwagawia Wakulima ili waweze kufanya shughuli zao
za Kilimo.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alitoa maelekezo
ya kuboresha shamba la kuendeleza mifugo la Nangaramo kwa Meneja wa Shamba hilo
(kulia kwake- aliyevaa Shari jeupe) alipotembelea katika shamba hilo Septemba
24, 2021. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Mariam Chaurembo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni