Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali
ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kufanya
mpango wa matumizi bora ya ziwa Victoria ambao utaainisha maeneo ambayo
yatatumika kufanya ufugaji wa vizimba ili kutoa nafasi pia kwa shughuli za
uvuvi wa asili kuendelea bila kuwa na muingiliano.
Ulega aliyasema hayo Septemba 27, 2021 alipotembelea eneo la Kampuni
ya Kichina ya Tangreen iliyowekeza katika mradi wa ufugaji wa Samaki kwa
kutumika vizimba kandokando ya ziwa Victoria, jijini Mwanza.
Alisema kuwa serikali imedhamiria kufanya hivyo ili kupunguza
muingiliano wa shughuli za ufugaji wa Samaki na Uvuvi wa asili ili shughuli
zote zifanyike kwa ufanisi na kuleta tija katika uchumi wa buluu.
"Mpango wa Serikali ni kuhakikisha ufugaji wa vizimba
unafanyika katika maeneo maalum na sio kila mahala, tuwe na maeneo mahsusi ya
kazi hii ili kutoa nafasi pia wavuvi wa asili waweze kuendelea na shughuli
zao," alisema Ulega
Waziri Ulega alisema kuwa mpango huo pia utavutia wawekezaji
wengi kuwekeza katika ziwa Victoria, na wao kama Serikali wanawakaribisha
wawekezaji kama TanGreen kuja kuwekeza nchini.
"Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira
mazuri ya uwekezaji, na hivi karibuni tumemuona akifanya jitihada kubwa kwa
kuitangaza nchi yetu katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kufungua milango
ya uwekezaji, na moja ya maeneo ya uwekezaji aliyokuwa akiyatangaza ni katika
uchumi wa buluu," alisema Ulega
Aliongeza kuwa TanGreen imejikita katika kukuza uchumi wa buluu
kwa kufuga Samaki wa vizimba na wanatarajia kuvuna Tani Elfu kumi (10, 0000)
kwa mwaka, huku akisema kuwa kwa sasa nchini samaki wanaovuliwa kutoka kwenye
mabwawa ni Tani Elfu Ishirini na Mbili (22,000) hivyo TanGreen wanakwenda
kuzalisha nusu ya kile kinachozalishwa sasa nchini.
Aidha, alimuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salim Mkali kuhakikisha muwekezaji
huyo analindwa, na kama kutakuwa na wadokozi wenye nia ya kuirudisha nyuma
kampuni hiyo wawachukulie hatua kali.
Ulega aliendelea kusema kuwa bado kunahitajio kubwa la Samaki
nchini, kiasi kinachohitaji kwa mwaka ni Tani Laki Saba (700, 000) wakati uwezo
uliopo kwa sasa Ni kuzalisha Tani Laki Nne (400, 000) hivyo kufanya pungufu ya
Tani Laki Tatu (300,000) huku akisema ufugaji wa vizimba ukifanyika vizuri
utasaidia kupunguza changamoto hiyo nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Ruhumbi alisema
kuwa wamejipanga kuufanya Mkoa huo kuwa mzalishaji mkubwa wa Samaki wa kufugwa
katika mabwawa.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah
alisema kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameendelea
kuhamasisha uwekezaji wa mitaji na wamehamasisha mabenki kama Benki ya
Maendeleo ya Kilimo (TADB) na imeshaanza kutoa mikopo, huku akisema wanaendelea
kuwashawishi wawekeza wakubwa wa mitaji kuwekeza katika ufugaji wa samaki na
kukuza uchumi wa buluu.
"Hivyo unaweza kuona kuwa ushawishi tulioufanya ndio
umepelekea wawekezaji wakubwa kama TanGreen kujitokeza na kwa kweli imeleta
tija kwa sababu miaka mitatu iliyopita kulikuwa na vizimba 18, lakini kwa sasa
tunavizimba 473 na asilimia 77 ya vizimba vyote vipo hapa ziwa
Victoria," alisema Dkt. Tamatamah
Awali, Daktari wa Samaki wa Kampuni ya TanGreen, Dkt. Mugure
Katwiga Mariwanda akisoma taarifa fupi ya Kiwanda hicho alisema kuwa moja ya
lengo la Kampuni hiyo ni kukuza na kutangaza teknolojia ya ufugaji
ikiwemo kufungua fursa ya ajira kwa vijana.
"Mhe. Naibu Waziri, pamoja na jitihada tunazoendelea nazo
lakini tunakumbana na changamoto kadhaa ikiwemo uhaba wa vifaranga vya Samaki
ndani ya nchi, baadhi ya wavuvi kuingia ndani ya mradi kuiba au kuharibu
miundombinu," alisema Dkt. Katwiga Mariwanda
Aliongeza kwa kuiomba Serikali itoe vibali vya kuingiza
vifaranga vya samaki kutoka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji yaliyopo huku
akiiomba Serikali iendelee kutoa elimu kwa jamii ya wavuvi juu ya uwekezaji wa
vizimba ili waache kufanya shughuli za uvuvi katika mradi huo.
Muonekano
katika picha ni Nyumba ya wafanyakazi wa TanGreen na baadhi ya vizimba vya
kufugia Samaki vilivyowekwa ndani ya Ziwa Victoria. Nyumba hiyo imejengwa
mahususi kwa ajili ya wafanyakazi wanaosimamia vizimba hivyo ndani ya ziwa.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiwapa chakula
Samaki wanaofugwa katika sehemu ya vizimba vya Kampuni ya TanGreen vilivyowekwa
ndani ya ziwa Victoria. Ulega alifanya ziara katika eneo la Kampuni hiyo ya Kichina ambayo
inajishughulisha na ufugaji wa samaki kwa kutumika vizimba Septemba 27,
2021.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni