Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka Wafugaji wa Mkoa wa Pwani kuanza
kuvuna Mifugo yao na kuiuza kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kuwaongezea
kipato na kupunguza migogoro kati yao na watumiaji wengine wa ardhi.
Ulega aliyasema
hayo Septemba 19, 2021 wakati akiongea na Wafugaji na Wakulima wa Wilaya ya
Rufiji alipofanya ziara Wilayani humo ya kusikiliza kero zao na
kuzitafutia ufumbuzi.
Alisema ni
muhimu viongozi wa Wilaya za Rufiji, Mkuranga na Kibiti kukaa na wadau wa
mifugo kutengeneza mkakati wa kuhamasisha uvunaji wa mifugo yao kwakuwa soko
la kuuza lipo mkoani humo na bado hawajalitumia ipasavyo.
"Hapa Mkoa
wa Pwani tuna Kiwanda cha Nyama cha TanChoice lakini pamoja na kiwanda hicho
kuwepo hakuna mifugo inayopelekwa pale kutoka ukanda wetu huu wa
Pwani," alisema Ulega
Aliongeza kwa
kusema kuwa ili faida ya uwepo wa kiwanda hicho ionekane ni vyema wadau wote wa
mifugo mkoani humo waanze uvunaji mkubwa na kupeleka kuiuza kiwandani hapo.
"Tunatamani
kuona mifugo inatoka katika ukanda huu wa Pwani na kwenda kuuzwa jijini Dar es
Salaam ambapo ndipo kwenye biashara kubwa ya nyama, msione fahari kukaa na
makundi makubwa ya mifugo ambayo mwisho wa siku yakaonekana kuwa ni kero na
hayana faida," aliongeza Ulega
Kuhusu
kuboresha huduma za Mifugo, Waziri Ulega alisema kuwa katika Bajeti ya Mwaka
huu 2021/ 2022 Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan imepanga
kununua Pikipiki 300 na itazigawa kwa Maafisa Ugani nchi nzima ili waweze kutoa
huduma ya mifugo kwa ufanisi.
Naye, Mkuu wa
Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowelle alisema kuwa kufuatia migogoro mingi
iliyoibuka katika Wilaya yake ameanzisha zoezi la sensa ya Mifugo na Wafugaji
ili waweze kujua idadi yao halisi na kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi
kulingana na mahitaji.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia)
akimsikiliza Mwenyekiti wa Kijiji cha Chumbi C, Muhidin Mtopa (katikati)
alipokuwa akimuonesha moja ya eneo lililotengwa na Serikali kwa ajili ya
Wafugaji Kijijini hapo lakini baadhi ya Wafugaji wamebadirisha eneo hilo
kuwa makazi na mashamba ya mpunga. Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, kitendo
hicho kimesababisha migogoro ya wakulima na wafugaji kuendelea kushamiri katika
Kijiji hicho. Naibu Waziri Ulega alitembelea Kijiji hicho Kilichopo Wilayani
Rufiji Mkoani Pwani Septemba 19, 2021.
|
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiongea na
Wafugaji na Wakulima wa Wilaya ya Rufiji(hawapo pichani) alipofanya ziara
Wilayani humo Septemba 19, 2021 kwa lengo la kusikiliza kero zao na kuzitatua.
Naibu Waziri Ulega pamoja na mambo mengine aliwataka wafugaji wa Mkoa wa Pwani
kwa ujumla kuvuna Mifugo yao ili kujiongezea kipato na kupunguza migogoro ya
mara kwa mara kati yao na watumiaji wengine wa ardhi. Kulia ni Mkuu wa Wilaya
ya Rufiji, Meja Edward Gowelle.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni