Nav bar

TAARIFA ZA MIGOGORO YA WAKULIMA, WAFUGAJI NA WATUMIAJI WENGINE WA ARDHI

MIGOGORO YA ARDHI KIJIJI CHA ELBORKISHU - OLJORO MKOA WA MANYARA, JUMANNE TAREHE 20/04/2015. (ITV HABARI SAA 2 USIKU)
Wanakijiji wawalalamikia Watendaji wa kijiji cha Elborkishu kuuza ardhi kinyemela kwa Wananchi. Watendaji 27 wamegawana wenyewe ardhi kwahiyo mifugo yao inakosa sehemu za malisho, hivyo wanaomba serikali iingilie kati ili kuweza kutatua mgogoro huo.

KIPINDI CHA NIPASHE SAA 12 ASUBUHI RADIO ONE, JUMANNE TAREHE 21/04/2015
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Titus Kamani, alihojiwa na RADIO ONE Kipindi cha NIPASHE saa 12 Asubuhi, na kushauri kuwa " Wafugaji wafuge Mifugo michache yenye tija kuliko kuwa na Mifugo mingi isiyokuwa na tija".


WIZARA YA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI  : Tafadhali wasiliana nasi kwa mawasiliano yafuatayo:


S.L.P 9152 DAR-ES-SALAAM

SIMU +255 22 2861010    
NUKUSHI - +255 22 2861908
BARUA PEPE - ps@mifugouvuvi.go.tz
TOVUTI - www.mifugouvuvi.go.tz


TUPE TAARIFA UKO WAPI MGOGORO, WILAYA,TARAFA,KIJIJI NANI MHUSIKA ILI TUSAIDIANE,TUSHIRIKIANE, TUTATUE MIGOGORO NA KUWA NA TANZANIA YENYE AMANI 

LAKINI TAMBUA MALISHO NI ZAO LA BIASHARA TUNZA VYANZO VYA MAJI ILI MIFUGO IFAIDIKE NA VYANZO HIVYO, NI MUJIBU WETU SOTE KUWA NA ARDHI YA UFUGAJI ,KUITUNZA NA KUIDHAMINI WEKA MIFUGO KULINGANA NA ENEO LAKO.    




WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI











MADA KUHUSU USIMAMIZI WA MIGOGORO YA ARDHI HUSUSAN KWA WAKULIMA NA WAFUGAJI ILIYOWASILISHWA KWENYE MKUTANO WA WAKUU WA MIKOA, MAKATIBU TAWALA WA MIKOA NA WAKUU WA WILAYA




Iliyotolewa na Prof. Anna Tibaijuka (MB)
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi











DODOMA
16 NOVEMBA, 2012






MADA KUHUSU USIMAMIZI WA MIGOGORO YA ARDHI HUSUSAN KATI YA WAKULIMA NA WAFUGAJI ILIYOWASILISHWA KWENYE
MKUTANO WA WAKUU WA MIKOA, MAKATIBU
TAWALA WA MIKOA NA WAKUU WA WILAYA


YALIYOMO
1.0              UTANGULIZI                                                                     
1.1              Maelezo ya Ujumla kuhusu ardhi nchini
1.2              Maelezo ya Ujumla kuhusu mifugo nchini
1.3              Vyanzo Vya Migogoro Ya Ardhi Nchini
1.4              Sera zinazosimamia sekta ya ardhi          
1.4.1        Sera ya Taifa ya Ardhi, 1995          
1.4.2        Sera ya Maendeleo ya Makazi, 2000        

1.5              Sheria zinazosimamia sekta ya ardhi      
1.5.1           Sheria zinazosimamia utawala wa ardhi
1.5.2           Sheria zinazosimamia upangaji mipango ya
matumizi ya ardhi
1.5.3           Sheria inayohusu upimaji ardhi
1.5.4           Sheria zinazohusu usajili wa ardhi na nyaraka
1.5.5           Sheria ya utatuzi wa migogoro ya ardhi                         
1.5.6           Sheria zinazosimamia Mikoa na Serikali za Mitaa
1.5.7           Sheria nyingine zinazohusu ardhi- Misitu, Madini      

2.0              SHUGHULI ZA SEKTA YA ARDHI ZINAZOTEKELEZWA KATIKA NGAZI MBALIMBALI                                            
2.1              Ngazi ya Taifa                                                         
2.2              Ngazi ya kanda                                                       
2.3              Ngazi ya Mikoa                                                                   
2.4              Ngazi ya Halmashauri za Wilaya na Miji                                   
2.5              Ngazi ya Kata                                                                      
2.6              Ngazi ya Kijiji                                                                                 

3.0              MIGOGORO YA ARDHI, HUSUSAN MIGOGORO YA ARDHI KATI YA WAKULIMA NA WAFUGAJI

4.0              WAJIBU WA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA

5.0              CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI SEKTA YA ARDHI
6.0              MIKAKATI YA KUBORESHA UTAWALA WA ARDHI NA KUPUNGUZA MIGOGORO
           
7.0              HITIMISHO

1.0        UTANGULIZI

1.      Wizara ya Ardhi tunamshukuru Mhe Waziri Mkuu kutoa fursa kwetu kushiriki katika Mkutano huu Maalum wa Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Hakika Ardhi ni jukwaa ambalo shughuli zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi zinafanyika. Mathalani; Kilimo, Ufugaji, Viwanda, Biashara, Ujenzi, Miundombinu, Hifadhi za Wanyamapori, Uchimbaji Madini na Vito, Misitu, sanaa, michezo n.k. Ardhi pia ndiyo makazi ya raia wa Vijiji, Miji na Majiji.  Kwa kuwa eneo la ardhi katika nchi yetu haliongezeki pamoja na kuwepo kwa ongezeko kubwa la watu kila mwaka, upo umuhimu mkubwa wa kusimamia ardhi ili kuondoa migogoro inayojitokeza na kudhibiti kasi ya ukuaji wa migogoro mipya  itakayojitokeza.

2.      Mada tuliyopangiwa ni   “Usimamizi wa Migogoro ya Ardhi Hususan Kwa Wakulima na Wafugaji Nchini Tanzania”. Ili kuwa na tija, msingi wa majadiliano ya  mada (conceptual framework) kwa viongozi wakuu wa Tawala za Mikoa unahitajika kujikita na kuwa na mpangilio na uelewa wa mambo muhimu yafuatayo:
a.      Takwimu muhimu kuhusu  matumizi ya ardhi (situational analysis).
b.     Aina ya Migogoro ya Ardhi na sababu zake  (Conflicts typology).
c.          Mifano Kadhaa ya Migogoro Kati ya Wakulima na Wafugaji  (Selected Farmers vs Pastoralists Conflicts).
d.     Sera na Sheria za Ardhi na Matumizi yake (land governance framework).
e.      Mkakati wa Kupunguza na Kuondokana na Migogoro ya Ardhi (land conflicts resolution strategy).
f.          Muhitasari wa mapendekezo (R) kwa  Wakuu wa Wilaya na Mikoa yatokanayo na uchambuzi hapo juu (Summary of Recommendations to District and Regional Administrators/Heads).

A) Takwimu Muhimu Kuhusu Sekta ya Ardhi (Basic Facts and Figures on Land Use)

3.      Eneo la ardhi ya Tanzania ni kilometa za mraba 945,011.7 (Hektari 94.5 milioni) ambapo kati ya hizo kilometa mraba 888,200 (Hektari 88.82milioni) ni eneo la ardhi kavu na kilometa mraba 56,811.7 (hektari 56.8 milioni) ni maji. Mzunguko wa eneo hili ni kilometa 7,940. Tanzania inapakana na nchi 10 bila kuweka mipaka katika Bahari ya Hindi. Nchi hizo jirani ni Comoro, Seychelles, Mozambique, Malawi, Zambia, Congo DRC, Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya. Isipokuwa Congo DRC na Mozambique, ukilinganisha na majirani zetu Tanzania inayo ardhi kubwa na hivyo kuwa kivutio kwa nchi jirani. Kama nitakavyoainisha baadaye tatizo linaanzia hapo. Majirani zetu wanapenda kuhamia Tanzania kutumia ardhi hiyo. Ukosefu wa utulivu na amani katika  karibu nchi nyingi jirani, hasa zile zenye ardhi kubwa kuliko sisi,  hususan Congo DRC na kwa mda mrefu wa  nyuma, Msumbiji, zimeongeza changamoto katika ardhi ya Tanzania na kusababisha migogoro sugu ya ardhi hasa katika mikoa ya mipakani([i]).  (R1) Kwa hiyo kuhimiza na kushirikiana na nchi jirani katika kulinda amani ni mojawapo ya mkakati wa kupunguza migogoro Tanzania. Kwa mfano baada ya Rwanda na Burundi kupata amani raia wake wengi waliokuwa Tanzania wamerejea nyumbani. Wakuu wa Mikoa na Wilaya za Mipakani wanahimizwa kushirikiana na wenzao upande mwingine wa mipaka kupunguza tatizo hili.

Ramani ya kuonesha mipaka 1

4.      Tanzania Bara ina mikoa 21 (kabla ile mipya haijaanzishwa) yenye maeneo kama inavyooneshwa katika Jedwali na 1 hapa chini. Inaonesha kuwa kwa kigezo cha wastani wa taifa ambao ni watu 47 kwa kilometa mraba moja, ufinyu wa ardhi au uwingi wa watu kuanzia juu kwenda chini (descending order) ni kama ifuatavyo: 1) Mwanza, 178; 2) Kilimanjaro, 126; 3) Dar es Salaam, 118; 4) Kagera,  88; 5) Mara,83;   6) Mtwara,  78;   7) Shinyanga, 75;  8) Tanga,  73;  9) Dodoma, 52;  na  10) Kigoma 49. Takwimu hizi zinaungwa mkono na uwingi wa migogoro katika mikoa hiyo ambayo imeoneshwa katika Ramani na 2. Kwa kuwa ardhi haiongezeki bali watu na mifugo na hata wanyama wengine huongezeka, hulka yake ni kuzidi kuwa adimu, kupanda thamani na bila teknologia na kazi mbadala mijini na viwandani, ardhi hugombaniwa. Kwa mfano wakati wa uhuru kila  mtu alirithi haktari takribani 9.76. Hivi sasa kiwango kimeshuka hadi hekta 2.03 kila mtu. (R2) Kwa hiyo hatua ya kwanza kuondoa migogoro ya ardhi ni mapinduzi katika utendaji wa sekta ya KILIMO na MIFUGO.

RAMANI 2




Jedwali 1: Watu katika Mikoa, Eneo na Ujazo wa watu


2002 2010* 2010
Watu "000"

Enoe sq.km
Ujazo/km2



Tanzania Mainland
2002
2010





01 Dodoma

1692
2112
41
52



02 Arusha

1288
1665
36
46



03 Kilimanjaro
1377
1636
13
126



04 Tanga

1636
1967
27
73



05 Morogoro
1753
2115
71
30



06 Pwani

885
1063
33
32



07 Dar es Salaam
2487
3118
13
118



08 Lindi

787
924
66
14



09 Mtwara

1124
1324
17
78



10 Ruvuma

1114
1375
64
21



11 Iringa

1491
1737
57
30



12 Mbeya

2063
2662
60
44



13 Singida

1087
1367
49
28



14 Tabora

1710
2349
76
31



15 Rukwa

1136
1503
69
22



16 Kigoma

1674
1814
37
49



17 Shinyanga
2797
3842
51
75



18 Kagera

2028
2564
29
88



19 Mwanza

2930
3566
20
178



20 Mara

1363
1823
22
83



21 Manyara
1038
1388
46
30



Total - Mainland
33460
41914
897
47



Tanzania Zanzibar







01 North Unguja
137
177
470
377



02 South Unguja
94
113
854
132



03 Urban West
390
483
230
2101



04 North Pemba
185
254
574
443



05 South Pemba
175
247
332
743



Total - Zanzibar
981
1274
2460
518



Total - Tanzania
34441
43188
460
49



Note: Refugees have been excluded and HIV/AIDS assumptions are
incorporated in the projection process.



*








Projections based on 2002 Population and Housing Census.

Source: National Bureau of Statistics Tanzania





5.   KILIMO: Ardhi ya Tanzania imegawanywa katika ardhi za vijiji ambayo ni asilimia 70% ya ardhi yote. Hifadhi asilimia 28%, na miji asilimia 2% tu. Karibu eneo lote la Tanzania linafaa kwa shughuli za kilimo na mifugo kama teknolojia ya kisasa itatumika kuondoa matatizo yanayozikumba sekta hizi mbili na kusababisha migongano kati yake. Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo eneo linalolimwa ni hektari 5.1 million ambayo ni sawa na asilimia 5% ya nchi kavu. Kuna ha 10 milion ambazo zinaweza kulimwa lakini sasa hivi zinatumika kama mbuga kwa kuchungia. Na katika hifadhi kuna takribani ha 4 milioni ambazo zinaweza kulimwa.

6.      MIFUGO: Kati ya hektari 88.6 milioni za nchi kavu, hektari 60 million ni mbuga na zinafaaa kwa ufugaji. Mbuga hizi zina uwezo wa kulisha units za mifugo million 20 (Livestock units) Kipimo hiki uangalia ukubwa wa mnyama na kulinganisha mahitaji ya lishe yake. Unit za mifugo zilizopo nchini ni takriban 17.1milion Hii inatokana na Ng’ombe milioni 18.5, mbuzi 13.1 milioni, kondoo 3.6 milioni na million 30 za kuku wa kienyeji na kisasa. Kwa wastani kila unit ya mifugo inahitaji ekari 3 za ardhi (carrying capacity) kwa hiyo uwezo wetu kufuga ni unit za mifugo 20 million, kama ukomo.



7.      Ni dhahiri kwamba hatuna uhaba wa ardhi bali ufinyu wa mitaji ya kuendeleza ardhi na elimu ya sayansi ya kilimo cha kisasa. Kwa hiyo hatuna budi kukiri kwamba migogoro ya ardhi inatokana na hali yetu ya  kutokuendelea kwetu ipasavyo (underdevelopment). Kwa upande wa KILIMO tunahitaji mapinduzi ya kilimo cha kisasa na chenye umwagiliaji, pembejeo, kuthibiti magonjwa ya mimea. Hii itapunguza kwa kiasi kikubwa mahitaji ya maeneo ya mashamba kwa wakulima wadogowadogo, Kwa mfano badala ya kulima shamba kubwa familia zitalima sehemu ndogo na kupata mavuno zaidi. Wizara ya Kilimo ikifanikiwa katika kazi yake na migogoro ya ardhi itapungua. Kwa hiyo Sera ya Kilimo KWANZA haijakosea kabisa na ikifanikiwa matatizo mengi ya migogoro yatayeyuka.

8.      MIFUGO: Ni muhimu tuelewe aina au utaratibu wake. Ufugaji umejikita katika aina tatu. Kwanza ni ufugaji wa kuhama au  Pastoralism. Huu ni ufugaji wa jadi ambao wafugaji na mifugo yao mingi (asilimia 48%) huhama wakitafuta malisho na maji. Uongezekaji wa watu na mifugo, na ukuaji wa maeneo yanayolimwa unatishia kama siyo tayari umesambaratisha kabisa mfumo huu wa ufugaji. Ni chanzo cha migogoro mikubwa nchini. Kwa mujibu wa Wizara ya MIFUGO hivi sasa kuna kaya 15,488 au asilimia 0.004%) wanaoendelea na utaratibu huu. Pili ni Agro-pastoralism: Ufugaji mseto (mixed agro-pastoralism) ni asilimia 40% ya mifugo. Tangu mwaka 1984 umeongezeka kutoka asilimia 14% za mifugo yote katika Taifa na kufikia 29% mwaka 1995 na sasa ni asilimia 40%. Ufugaji huu ndio muhimili wa lishe Tanzania na chanzo cha 80% ya nyama katika Taifa. Ranchi zina asililima 2% ya mifugo katika TanzaniaTija katika mifugo hutegemeana moja kwa moja utunzaji wa malisho na mbuga.Kwa kuwa umiliki wa ardhi za mbuga au maeneo ya pamoja kama vile maeneo oevu karibu na mito ni wa pamoja (communal tenure) wafugaji wengi hawajali wala kutunza mbuga hizo na kwa kawaida huw hawana mkakati endelevu kuziboresha mbuga hizo. Katika hali hiyo kila mtu anaweka mifugo mingi atakavyo na hakuna mkakati kuboresha. Sehemu ikiharibika anahama. Vile vile wakulima nao wakati mwingine wanalima maeneo oeuvu au vyanzo vya mito na kuviharibu bila kujali athari kwa wenzao au vizazi vijavyo(Tragedy of the Commons).Matatizo yote haya yamebainishwa katika dira ya Taifa ya 2025, sera na sheria mbalimbali  tunapendekeza elimu , Migogoro ya ardhi haiweze kumalizika bila kutatua matatizo haya ya msingi (fundamental and underlying causes of the problem). .  (R3) Kwa kuwa kundi linalohamahama ni dogo lakini lina mifugo wengi ambao wanatumika zaidi kama akiba na kama tulivyoona si chanzo kikubwa cha nyama, faida yake kwa Taifa ni ndogo ukilinganisha na athari inayosababisha katika migogoro na wakati mwingine uvunjifu wa amani. Utatuzi wa chanco hiki unawezekana. Ni vyema sense ya kundi hili na mifugo yao ikafanyika kwa madhumuni ya kuwapatia elimu na kuwashawishi na kuwashauri wafuate sheria kama itakavyofafanuliwa baadaye. Kamishana wa Mifugo ana mamlaka ya kutoa amri kwa mtu yeyote mwenye mifugo kuipunguza kama hana sehemu inayofaa kwa malisho (Compulsory destocking order under the Grazing Act, 2010).

9.   Ukosefu wa Maji na Malisho (Pastures) Sehemu Moja kwa Nyakati zote: Malisho kwa  maana ya nyasi na maji ya kunywa hutegemea na majira. Wakati wa kiangazi nyasi hukosa na kulazimisha wafugaji na mifugo yao kuhama wakitafuta sehemu zisizokame. Pia nyasi nyingi huharibiwa kwa kuchomwa moto ovyo au kukanyagwa na makundi ya ngombe wengi (trampling and uncontrolled burning of grazing lands). Uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji ni mkubwa na hatari. Hali hii husababisha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hizo kwa mfano, wakulima au wachungaji katika ranchi,  Hifadhi za Taifa kama Misitu, Mbuga za Wanyama na maeneo oevu. Tatizo la wafugaji na ufugaji wa asili wa kutangatanga sasa limegeuka suala la Usalama wa Taifa na baadhi ya wananchi wamepoteza maisha yao katika migogoro hiyo.  Ni wakati muafaka kutazama tatizo hili kwa kina zaidi (analytically) kwa uchunguzi wa mtizamo wa kiuchumi kwa kujiuliza: Je, bado ufugaji wa asilia unawezekana tena katika Tanzania yenye watu zaidi ya million arobaini? (Are traditional pastoral farming systems still viable in Tanzania given a rapidly rising population?). Bila kujibu suali hili kiutaalam na kwa kina, tunaweza kujikuta tunashughulikia dalili ya magonjwa na siyo chanzo chake (addressing sysmptoms rather than fundamental and underlying causes of the problem). Mkakati wa kuondoa migogoro ya ardhi sharti uangalie suala hili la ufugaji bora. Juhudi za maksudi zinahitajika katika kuboresha uzingatiaji wa matumizi bora ya ardhi, malisho au uchungaji wa kisasa ikiwemo kupunguza idadi ya mifugo, kuvuna nyasi na kuhifadhi ili kulisha mifugo pale ilipo (ijulikanayo kama “ngitiri” kwa mikoa ya Ziwa, au “alalili” mikoa ya Kaskazini na “milaaga” kwa mikoa ya kati. Pia kuunda vikundi vya ushirika kwa wachungaji (Livestock Keepers Associations), kutunga na kutekekeleza sheria ndogondogo na kanuni za uchungaji bora ikiwemo kwa Kamishana wa Mifugo kutoa amri kwa wachungaji kupunguza mifugo yao inapobidi na kwa mujibu wa sheria ili kuendeleza rangelands na kuondokana na kutangatanga. Serikali itaongeza juhudi zake kuzalisha mbegu za nyasi bora za malisho katika mashamba yake ya mbegu hizo. Pia kwa kushirikiana na Halmashauri kuboresha uvunaji wa maji katika malambo na mabwawa (charcos). Sera ya Wizara ya Mifugo ni kuchangia asilimia hamsini, 50%, Halmashauri asilimia 30% na wafugaji asilimia 20%. Aidha malambo 340 yamekarabatiwa au kujengwa.

10.           Mapinduziya Ufugaji (Transformation of Livestock Husbandry)Mwaka jana Mhe Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, ambaye  ni jirani yangu, na aliishi Wilaya ya Muleba wakati akiwa mkimbizi, alinialika na Wapiga kura wangu wa Wilaya ya Muleba kwenda kushuhudia mapinduzi ya kilimo na ufugaji katika Mkoa wa Mbarara nyumbani kwake huko Unyankole, Rwakitura. Mhe Waziri Mkuu aliniruhusu kufanya ziara hiyo na nilifuatana na  Mkuu wetu wa Mkoa Mhe. Kanali mst Fabian Masawe na viongozi wa Halmashauri na wakulima 134 kutoka kata zote za Uchaguzi katika jimbo langu la Muleba Kusini. Pia nilifuatana na wataalam wa Kilimo na waandisha wa habari wa TBC ili ziara hiyo ya safari darasa (study tour) inufaishe umma wa Tanzania kwa ujumla. Ninaamini labda kuna baadhi mliwahi kuoona tukio hilo la kihistoria lililotangazwa na vyombo vya habari. Tulijifunza yafuatayo. Kwamba kama vile walivyo Wamasai, Wanyankole ni wafugaji na kabla ya mageuzi hayo walikuwa wakihama na kutangatanga, na maisha yao yalikuwa ya taabu sana, migogoro ilikuwa mingi na wizi wa mifugo ilikuwa jadi. Ili kuwabadilisha, Rais Museveni alitatua matatizo yafuatayo, akianzia kwenye shamba la baba yake kama shamba darasa. Polepole aliwafundisha na kuwashawishi majirani na hatimaye wengi walipomuamini, mkoa mzima sasa waliachana na kuhama na wakaanza ufugaji kudumu (sedentary livestock husbandry) kwa kuondoa sababu za kuhama kama ifuatavyo. Kwanza ni kuhakikisha kuna maji safi ya kutosha katika eneo wakati wote. Pili kutokomeza kabisa kupe wanaozaliana sehemu yoyote yenye mifugo na baada ya muda kulazimisha zizi kuhamishwa hata kama maji yapo. Tatu kuboresha nyasi za kuchunga kila  mtu katika eneo lake hivyo malisho yanakuwepo wakati wote (paddocks). Nne kuboresha mifugo yenyewe kwa kuwachuja (screening and crossbreeding, improved breeds). Wanyankole sasa wanauza maziwa Dubai na India, ndege zinawasili kila siku kuyabeba. Migogoro ya ardhi imekwisha. Kila Mfugaji ana shamba lake ngombe wako katika padocks na hawana mchungaji wa wakati wote isipokuwa wanaletwa kwenye zizi kukamuliwa tu. Ninachukua nafasi hii kuwahimiza washiriki wa Mkutano huu kuwa na mtizamo chanya kuhusu ziara darasa (study tours) kama ile niliyofanya Uganda na wapiga kura wangu, na Mhe Waziri Mkuu akaniruhusu. Kuona ni kuamini ilimradi ziara iwe imepangwa kwa umakini na ishirikishe wadau wengi kuliko kakundi ka watu wachache tu ambao wakirudi hawatasimulia na kuwafundisha wenzao. Ziara kama hizi pia zinatakiwa watu wazichukulie kama masomo na siyo nafasi ya kugawana posho. Ili kuhakikisha hilo, kwa mfano katika ziara ya Uganda washiriki wote walilazimika kujitafutia Hati ya Kusafiri (Shs 15,000/-) na hawakupewa posho. Mie nililipia usafiri hadi Uganda. Mhe Rais Museveni akatufadhili Malazi na Chakula. Kwa mantiki hiyo, ninatoa rai tuangalie uwezekano wa kuwapeleka wafugaji wetu Uganda kwenda kujionea mapinduzi katika ufugaji Mbarara Uganda.

11.           UKUAJI WA MIJI KIHOLELA
Ingawaje mada hii imejikita katika kilimo na mifugo, ni vyema tukaangalia pia kwa ufupi mwenendo wa ukuaji wa miji katika mikoa yetu. Sababu kubwa ni kwamba ardhi za maendelezo ya miji zinachukuliwa moja kwa moja kutoka kwa wakulima na wafugaji na hivyo ni sehemu kubwa ya migigoro iliyopo. Kwa ufupi Jedwali na 2 inaonesha hali ya wakazi wa miji katika Tanzania kwa kila mkoa mwaka 2012 na maoteo ya 2020. Watanzania walio mijini, wataongezeka kutoka million 11 za hivi sas had milioni. Muda hauruhusu kujadili kwa kina suala hili la ukuaji wa miji (urbanization) lakini kwa viongozi wa Mikoa na Wilaya yatosha tu kusema sharti kutambua athari za ukuaji kiholela wa miji na uzagaji wa miji (urban sprawl) ambao huchukua ardhi za kilimo bila sababu. Kwa mfano mji wa Arusha sasa unakua kwa kasi lakini ardhi yake (volcanic soils) ina thamani sana kwa maendekeleo ya kilimo. Njia pekee huwa ni kuhakikisha miji yote ina Strategic Master Plans kulinda maslahi ya wadao wote na sekta zote, za uchumi na jamii.

Weka Jedwali na 2

12.          Aina ya Migogoro ya Ardhi

Kwa mtizamo wa Migogoro ya ardhi hapa nchini hujitokeza mijini na vijijini. Migogoro mingi inayojitokeza inahusisha makundi au maeneo yafuatayo:-

(i)           Migogoro kati ya Jamii za Wakulima na Wafugaji

Migogoro ya aina hii husababishwa na muingiliano wa matumizi kati ya makundi haya mawili ambapo mwisho wake huwa ni vurugu. Wachungaji wakati mwingine hulazimika kuingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima na kusababisha mapigano kati yao.  Hii ni kutokana na vijiji kukosa mipango ya matumizi ya ardhi inayoweza kuainisha maeneo kwa ajili ya wafugaji na wakulima.

(ii)       Migogoro kati ya Wanavijiji na Wawekezaji
Baadhi ya migogoro ya ardhi kati ya makundi haya hutokana na vijiji kukalia ardhi yenye hati milki au kutoshirikishwa vyema kwa wananchi pale ardhi inapotolewa kwa ajili ya uwekezaji. Vilevile ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika utoaji wa ardhi ya Kijiji. Kwa mfano fungu la 76 (1-3) la Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999 imeainisha taratibu za idhini ya viwango vya juu vya kumiliki ardhi. Halmashauri ya Kijiji inaruhusiwa kutoa ardhi si zaidi ya hekta 20 sawa na wastani wa ekari 50.  Vilevile maombi kati ya hekta 21 hadi 50 Halmashauri ya Kijiji itawasilisha maombi hayo kwenye Halmashauri ya Wilaya.  Maombi yanayozidi hekta 50 Halmashauri ya Kijiji inatakiwa kuwasilisha maombi hayo kwa Kamishna wa Ardhi. Kwa sasa vijiji vingi vinatoa ardhi bila kuzingatia matakwa ya sheria hiyo.

(iii)      Migororo ya Mipaka baina ya Mamlaka mbalimbali
Migogoro hii hujitokeza hasa kati ya jirani na jirani; kijiji na kijiji; Wilaya na Wilaya; na kati ya Mkoa na Mkoa.

(iv)      Migogoro ya Wamiliki zaidi ya mmoja kwenye kiwanja kimoja
Migogoro hii hutokana na wamiliki wawili au zaidi kugawiwa kiwanja kimoja na pengine wote kuwa na hati za kumiliki kiwanja hicho. Hata hivyo, hili lilikuwa likifanyika sana siku za nyuma kutokana na utunzaji duni wa kumbukumbu uliokuwepo katika ofisi nyingi za ardhi.

(v)         Uvamizi wa mashamba/viwanja
Migogoro ya aina hii hutokea pale baadhi ya wananchi wanapoamua kuvamia mashamba yaliyopimwa zamani na kuachwa kwa muda mrefu bila kuendelezwa. Aidha mmiliki wa shamba au kiwanja anapotaka kuendeleza eneo lake na kuwakuta wananchi inakuwa vigumu kuwatoa wananchi waliovamia mashamba hayo kutokana na wao kuishi kwenye maeneo hayo kwa muda mrefu. Kutokana na hali hii mgogoro mkubwa baina ya pande hizi mbili hujitokeza.

(vi)    Migogoro ya Wananchi kutoridhika na fidia inayolipwa wakati wa utwaaji ardhi

Wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia viwango vya fidia wanavyolipwa pindi ardhi yao inapotwaliwa na serikali kuwa haviendani na hali halisi ya soko. Katika hali kama hii, mgogoro mkubwa kuhusu malipo ya fidia hujitokeza na wakati mwingine kukwamisha ama kuchelewesha utekelezaji wa mradi uliokusudiwa.


1.1           Sababu za Migogoro Ya Ardhi Nchini

Migogoro mingi ya ardhi imetokana na sababu zifutazo:-
(i)              Uelewa  Mdogo wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Utawala wa Ardhi
Uelewa mdogo wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazoongoza utawala wa ardhi umekuwa ni kikwazo kikubwa katika utawala wa ardhi na hivyo kuwa chanzo kikubwa cha migogoro mingi hapa nchini. Uelewa huu mdogo umekuwa ukiwakumba wananchi, baadhi ya watendaji na baadhi ya viongozi mbalimbali na hivyo kufanya au kutoa maamuzi yanayochochea migogoro. Hali hii imekuwa ikichangiwa kwa kiasi kikubwa na kutokuwepo kwa mpango wa kutoa elimu mara kwa mara  kwa wananchi, viongozi  na watendaji wake mbalimbali inayohusu masuala ya ardhi. (R4) Elimu juu ya será na sheria za ardhi kwa Viongozi na umma kwa jumla.

(ii)           Ukosefu wa Uadilifu kwa Baadhi ya Watendaji Katika Sekta ya Ardhi
Baadhi ya watendaji katika Sekta ya ardhi wamekuwa wanakosa uadilifu na hivyo kusababisha migogoro ya ardhi. Vitendo kama uuzaji wa maeneo ya wazi, ugawaji wa kiwanja kimoja kwa watu wawili au zaidi, upokeaji wa rushwa ili kutoa upendeleo wakati wa kugawa viwanja; vilevile kutozingatia taratibu za uhawilishaji ardhi, ubatilisho wa miliki, upimaji ardhi, kuruhusu matumizi ya ardhi kinyume cha sheria na utaratibu; ni baadhi ya vitendo vinavyokiuka sheria na kanuni na hivyo kusababisha migogoro mikubwa ya ardhi. (R5) Usimamizi wa watendaji wa Ardhi katika Halmashauri ni changamoto kubwa. Mapendekezo ya Wizara ya Ardhi kwa Mhe Waziri Mkuu ni kwamba maafisa hawa warejeshwe Serikali kuu kama vile walivyo Mapolisi ili weweze kupata usimamizi wa kitaalam (Professional supervisión). Hili litaiwezesha Wizara kuwasimamia katika utendaji wake Chini ya DAS na RAS kwa hiyo DC na RC. Mkurugenzi wa Halmashauri asiwe Mwenyekiti wa Kamati ya Kagawa Ardhi bali DC. Jambo hili litatuwezesha kuzishauri Halmashauri ni vijiji kulinda maslahi yao ambayo wanapewa kisheria lakini kwa kuwa hawewezi kuwasimamia vizuri Maafisa Ardhi hupotea.

(iii)      Upungufu wa Watendaji (Watumishi) na Vitendea kazi
Halmashauri nyingi pamoja na wizara zinasababisha migogoro ya ardhi kutokana na kutokuwepo kwa watumishi wa kutosha kuendana na ikama. Mfano mzuri ni halmashauri nyingi kutokuwa na maafisa ardhi wateule, maafisa mipango miji, wapima ardhi n.k na hivyo kuchelewesha shughuli za sekta ya ardhi kwa ujumla wake na hii husababisha miji mingi kuendelezwa kiholela. Kwa maene yaliyoendelezwa kiholela wakati unapofika wa kutekeleza mpango mkakati wa kuendeleza miji hii, wananchi wengi wanajikuta makazi yao hayako salama na kulazimika kuhama jambo linalosababisha migogoro mikubwa. Jedwali Na. 3 inaonesha orodha ya maofisa ardhi wateule nchini Tanzania. Katika ya Wilaya 135 ni 86 to au asilimia 64% zilizo na Maafisa ardhi wateule. Hali hii inamaanisha kwamba Halmashauri nyingine hazina watendaji hawa kabisa au zinategemea walio katika Halmashauri jirani. Maafisa Ardhi 2 wamesimamishwa kazi. Wilaya ambazo zina watendaji chini ya asilimia hamsini ni Tabora, 33%, Mwanza Manispaa 43%; Katavi 33%; Lindi 33%.

Jedwali na 2





(iv)      Ukosefu wa Fedha kwa Ajili ya Sekta ya Ardhi
Upatikanaji wa ardhi, uandaaji wa michoro ya mipango miji na upimaji huhitaji kiasi kikubwa cha fedha. Kiasi kidogo kinachotolewa kwenye bajeti ya wizara hufanya shughuli za sekta ya ardhi kama ulipaji fidia na upimaji viwanja kushindikana na hivyo kusababisha wananchi wengi kuingia kwenye maeneo yasiyopimwa na hatimaye kusababisha migogoro. Aidha, wakati mwingine wizara na halmashauri huandaa michoro ya kuongoza uendelezaji wa miji lakini utekelezaji wake hushindikana kutokana na kukosekana kwa fedha kwa ajili ya fidia. Pia ufinyu wa bajeti huifanya Serikali kushindwa kutenga ardhi kwa ajili ya uwekezaji (land bank) ili kuepuka utwaaji wa maeneo yaliyokwisha kaliwa na watu wengi pindi anapojitokeza mwekezaji.

(v)       Utunzaji Hafifu wa Kumbukumbu
Sekta ya ardhi kwa ujumla ina tatizo la utunzaji mzuri wa kumbukumbu hali inayochangia kuwepo kwa migogoro mingi. Utunzaji wa nyaraka za miliki za ardhi umekuwa wa shida kutokana na kutokuwepo kwa masjala nzuri za ardhi na hali hii husababisha nyaraka kutohifadhiwa vizuri hali inayoweza kutoa mwanya kwa watendaji wasiokuwa waadilifu kuharibu nyaraka zilizopo kwa nia ya kutimiza dhamira zao mbovu. Jedwali na 4 inaonesha Taarifa ya Vijiji Vyenye Masjala za Ardhi kwa kila Mkoa na Wilaya zake. Hali hairidhishi kabisa. Masjala za ardhi za vijiji zilizoanzishwa ni 385 kati ya 9,460 zinazohitajika. Hii inamaanisha hati nyingi za vijiji haziwezi kutolewa kama hakuna Masjala. Ingawaje hati 158,030 zimetolewa nyingi zinatokana na Hati zinatokana na Wilaya za Mkurabita kama ifuatavyo: Bariadi 60,151; Babati 28,195 na  Mbozi 17,627. Kata 48 kati 135 hazijatoa hati miliki ya Kimila yoyote.

Jedwali na 4: Masjala za Vijiji



(vi)    Upungufu wa Viwanja Vinavyopimwa ikilinganishwa na mahitaji.
Kumekuwa na idadi ndogo ya viwanja vinavyopimwa ikilinganishwa na mahitaji halisi yanayokua na kuongezeka kila siku, hali ambayo imekuwa ikiwafanya wananchi wengine kutumia mbinu zisizo halali kujipatia viwanja na wakati mwingine kutapeliwa. Tatizo hili lipo zaidi katika Jiji la Dar es salaam hususan manispaa ya Kinondoni.

(vii) Ukosefu wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi katika Vijiji vingi
Ukosefu wa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi husababisha misuguano na migogoro kati ya makundi mbalimbali ya kijamii mathalani wakulima na wafugaji. Kila kundi hujihisi kuwa linakosa haki linayostahili katika ardhi yao na hivyo suluhu kwao huwa ni matumizi ya nguvu na vurugu.

(viii)     Upungufu katika Muundo wa utawala katika Usimamizi wa Ardhi nchini
Kuwepo kwa muundo ambao hauainishi kisheria mamlaka za kusimamia masuala ya ardhi na hivyo kutoa fursa kwa sekta ya ardhi kutokusimamiwa ipasavyo.  Mgawanyo wa majukumu unaotajwa kwenye sheria za ardhi haujaweka bayana wajibu wa mamlaka za Serikali za Mitaa na vilevile ngazi za Mikoa na Wizara. Ningependa kusikia maoni ya Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya juu ya uzoefu wao juu ya tatizo hili.

(ix)    Ukosefu wa Mafunzo kwa Watendaji
Kutokana na ufinyu wa bajeti, watendaji kwenye Halmashauri hushindwa kupelekwa kwenye mafunzo ya muda mafupi ya mara kwa mara yanayoendana na mabadiliko ya kimfumo na sheria na hivyo kupelekea watumishi wengi kufanya kazi kwa mazoea.

(x)      Ukiukwaji wa Masharti ya Uendelezaji kwa Wamiliki na Wawekezaji
Baadhi ya wawekezaji na wamiliki wa ardhi wamekuwa wakihodhi mashamba kwa muda mrefu bila kuyaendeleza na hivyo kusababisha wananchi majirani kuyavamia. Aidha uvamizi huo huweza kukua kwa muda mrefu na mwishoni husababisha mgogoro wakati wa kuwatoa wananchi hao. (R5) Serikali imeridhia kuanzisha será ya ubia katika mashamba makubwa “Land for Equity”. Serikali itajipatia angalau asilimia 25% katika mashamba yote makubwa na kutoa Hati Miliki inayohakikisha hisa hizo za Serikali katika uhai wa miliki hiyo. Tumegundua mapungufu katika mtindo wa derivative rights, ambapo baada ya kutolewa na TIC kwa mwekezaji inakuwa vigumu kwa Kamishana wa Ardhi kuthibiti uchakuchuaji wa Hati miliki hizo wakati zinahamishwa. Hati ya moja kwa moja itaondoa uwezekano kwa Mwekezaji kutumia Miliki hiyo katika vitendo vya speculation. 

(xi)          Ushirikishwaji Mdogo wa Wananchi katika mipango na miradi ya Sekta za Ardhi
Baadhi ya halmashauri zimekuwa haziwashirikishi wananchi vya kutosha katika mipango ya uendelezaji wa ardhi yao na hivyo kusababisha migogoro wakati wa utekelezaji wa mipango hiyo. Ingawaje Sheria inatamka wazi kuhusu umuhimu na hatua za kuwashirikisha wananchi, baadhi ya halmashauri hupuuza ushirikishwaji huo na mwishowe hupata ugumu kwenye utekelezaji na pengine kusababisha migogoro mikubwa. Mfano ni mgogoro wa ardhi eneo la Butengwa Shinyanga ambapo wananchi waligomea uendelelezaji wa mradi wa viwanja katika eneo hilo kutokana na kutoshirikishwa vizuri.

Utaratibu wa Uhawilishaji ardhi umefafanuliwa hatua kwa hatua katika kiambatisho na  1


(xii)       Ukosefu wa Uwazi (Transparency) wakati wa Utekelezaji wa Mipango mbalimbali
Migogoro mingi ya ardhi husababishwa na kutokuwapo uwazi wakati wa utekelezaji wa mipango mbalimbali. Hali hii huwafanya wananchi kuhisi kuwa kuna wingu la rushwa linalozunguka utekelezaji wa mipango au miradi ya ardhi na hivyo kuzusha vurugu na hata uvunjifu wa amani.

(xiii)      Udhaifu wa Vyombo vya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi
Kuwepo kwa vyombo dhaifu vya utatuzi wa migogoro ya ardhi katika ngazi za vijiji, kata na Wilaya (Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji, Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya)

Jedwali na 5: Migogoro ya Ardhi na Maendeleo ya Utatuzi wake katika Kanda ya Kati

13.           Sera Zinazosimamia Sekta ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi

Ardhi ya Tanzania imegawanyika katika makundi matatu ambayo ni ardhi ya jumla (general land), kijiji (village land) na hifadhi (reserved land). Ardhi hii ni jukwaa ambalo shughuli zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi zinafanyika. Shughuli hizo ni pamoja na Kilimo, Ufugaji, Viwanda, Biashara, Ujenzi, Miundombinu, Hifadhi za Wanyamapori, Uchimbaji Madini na Vito, Misitu, sanaa, michezo n.k.  Shughuli zinazofanyika kwenye ardhi zinaongozwa na Sera, Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo. Kwa sababu hiyo, ni muhimu kwa viongozi wa Mikoa na Wilaya kuzifahamu Sera, Sheria, Kanuni na taratibu zinazosimamia sekta ya ardhi na Maendeleo ya Makazi. Kwa kuwa eneo la ardhi katika nchi yetu haliongezeki pamoja na kuwepo kwa ongezeko kubwa la watu kila mwaka, upo umuhimu mkubwa wa kusimamia ardhi ili kuondoa migogoro kati ya watumiaji mbalimbali inayojitokeza na itakayojitokeza.


Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 ni Sera ya msingi inayotoa dira ya Serikali katika usimamizi wa ardhi nchini. Pamoja na Sera hii, ipo Sera ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000 inayotoa dira ya Serikali kuhusu maendeleo ya makazi. Aidha, Wizara ipo katika mchakato wa kuandaa Sera ya Upimaji Ardhi kwa madhumuni ya kutoa dira ya Serikali katika upimaji ardhi na Sera ya Taifa ya Nyumba kwa madhumuni ya kutoa dira ya Serikali katika uendelezaji wa nyumba.

1.1.1           Sera ya Taifa ya Ardhi, 1995
Sera ya Taifa ya Ardhi inasisitiza masuala makuu yafuatavyo:-

(i)     Inatambua kwamba ardhi yote Tanzania ni mali ya umma na imekabidhiwa kwa Rais kama mdhamini kwa niaba ya raia wote;

(ii)  Inahakikisha kwamba haki zote zilizopo katika ardhi na umilikaji wa ardhi kwa muda mrefu unatambuliwa, unafafanuliwa na kulindwa kwa Sheria;

(iii)   Inawezesha ardhi kugawiwa kwa haki na kupatikana na ardhi hiyo kwa raia wote na vilevile imeweka misingi ya kutoa ardhi kwa wawekezaji;

(iv)Inaweka udhibiti wa kiasi cha ardhi ambacho mtu mmoja au taasisi yaweza kumiliki au kuitumia;

(v)   Inahakikisha kwamba, ardhi inatumika kwa manufaa kiuzalishaji na kwamba matumizi hayo yanazingatia misingi ya maendeleo endelevu;

(vi)Inazingatia kwamba maslahi yoyote katika ardhi yana thamani, na kwamba thamani hiyo inazingatiwa wakati wowote katika mapatano yoyote yanayoathiri maslahi hayo;

(vii) Inaelekeza kulipa fidia kamili, ya haki na kwa wakati kwa mtu yeyote ambaye hakimiliki inafutwa, matumizi yake ya ardhi yanayotambulika kutokana na kutumia ardhi hiyo kwa muda mrefu au matumizi yake ya ardhi kwa mujibu wa mila yanafutwa au vinginevyo yanaingiliwa na Serikali na yeye kuathirika kwa mujibu wa Sheria hii au yanatwaliwa kwa mujibu wa Sheria ya Utwaaji wa Ardhi ya mwaka 1967;

(viii)       Inaweka mfumo madhubuti, rahisi na wazi wa kusimamia kwa ufanisi masuala ya ardhi;

(ix) Inawezesha uendeshaji wa soko la ardhi;

(x)   Inadhibiti uendeshaji wa soko la ardhi kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa wakulima wadogo vijijini na mijini pamoja na wafugaji hawawekwi katika hali ngumu ya kuwasababishia hasara;

(xi) Imeweka kanuni za Sheria za Ardhi ambazo zinapatikana kwa urahisi na zinazoeleweka kwa raia wote;

(xii) Imeanzisha mfumo ulio huru, unaofanya kazi kwa haraka na wa haki kwa ajili ya kuamua migogoro ya ardhi, ambao utasikiliza na kuamua migogoro ya ardhi bila ya ucheleweshaji usio wa lazima;

(xiii)  Inahimiza usambazaji wa taarifa za usimamizi wa ardhi na Sheria za Ardhi kama ilivyofafanuliwa na Sheria, kwa kupitia vipindi vya elimu kwa umma na kwa watu wazima na kwa kutumia njia mbalimbali za upashanaji habari;

(xiv) Inaelekeza kwa haki ya kila mwanamke kupata, kumiliki, kutumia na   kuuza au kuigawa ardhi ni sawa na haki ya mwanaume yeyote kwa viwango vile vile na masharti yale yale; na,

(xv)        Inazuia matumizi na makazi katika maeneo oevu; mfano, maeneo yenye mikoko, maeneo kwa ajili ya kutupa taka, ardhi iliyopo ndani ya mita 60 za fukwe za bahari, maziwa, mito n.k, maeneo yenye miteremko mikali n.k.




1.1.2           Sera ya Maendeleo ya Makazi, 2000
Sera ya Maendeleo ya Makazi inaelekeza masuala yafuatayo muhimu:-

(i)                 Kuwezesha uwepo wa ardhi yenye huduma; maji, barabara n.k kwa ajili ya malazi na makazi kwa jamii yote wakiwemo wanawake, vijana, wazee, walemavu na makundi mengine katika jamii.

(ii)              Kuboresha miundombinu na huduma za jamii kwa ajili ya maendeleo endelevu ya makazi.

(iii)            Kuhimiza ongezeko la ajira na kuondoa umaskini.

(iv)            Kuhimiza maendeleo yanayowiana katika mamlaka zinazosimamia makazi kwa ajili ya kusimamia makazi bora.

(v)               Kwa kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za kijamii, mashirika yasiyo ya Kiserikali, ushirika na jamii kuhimiza kupanga, kuendeleze na kusimamia makazi.

(vi)            Kulinda mazingira ya makazi na uwiano wa mifumo ya asili kutokana na uchafuzi, mimomonyoko ili kuleta maendeleo endelevu ya makazi.

(vii)          Kuhimiza kujenga uwezo katika mafunzo ya kitaaluma katika maeneo yanayohusu malazi, maendeleo ya makazi na usimamizi wa mazingira.

(viii)       Kuhimiza kujenga uwezo kwa wadau wote wanaohusika na malazi na maendeleo ya makazi.

(ix)             Kuongeza kiasi cha bajeti kinachotolewa kwa ajili ya malazi na maendeleo ya makazi.

(x)               Kuhakikisha sheria zinazohusu mipango, kanuni za ujenzi na viwango vinaendana uwezo, mahitaji na matarajio ya jamii.

(xi)             Kuhimiza ujenzi wa makazi kwa kutumia vifaa vya kiasili vyenye gharama nafuu.

(xii)          Kusaidia wasio na uwezo kupata makazi yenye hadhi.

(xiii)        Kuhimiza maeneo ya makazi yanayoendelea, mazuri kiafya, na yanayovutia kimazingira.

(xiv)        Kuweka muelekeo mpya wa sheria na kitaasisi kwa ajili ya maendeo ya makazi.

(xv)           Inakataza mabadiliko ya matumizi ya ardhi kwenye maeneo ya wazi, mabondeni na maeneo oevu na hatarishi.

(xvi)        Inaruhusu kilimo mijini ili mradi shamba lisizi ekari tatu.


Sheria na Kanuni mbalimbali. Sheria muhimu katika utawala wa ardhi ni:-
      (i)        Sheria ya Ardhi Na. 4 ya 1999;
     (ii)        Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya 1999;
    (iii)        Sheria ya Mipangomiji Na. 8 ya 2007;
    (iv)        Sheria ya Upangaji wa Matumizi ya Ardhi Na. 6 ya 2007;
     (v)        Sheria ya Upimaji Ardhi Na. 32 ya 1957;
    (vi)        Sheria ya Utwaaji wa Ardhi Na. 47 ya mwaka 1967
  (vii)        Sheria ya Utatumizi wa Migogoro ya Ardhi Na. 2 ya 2002;
 (viii)        Sheria ya Usajili Ardhi Na.36 ya 1953; na
    (ix)        Sheria ya Usajili wa Maafisa Mipangomiji Na. 7 ya 2007
     (x)        Sheria ya Mifugo – Livestock and Grazing Act, 2010
    (xi)        Sheria ya Madini – Mining Act, 2012;
  (xii)        Amendments 2004.



1.2           Sera Zinazosimamia Sekta ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi

Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 ni Sera ya msingi inayotoa dira ya Serikali katika usimamizi wa ardhi nchini. Pamoja na Sera hii, ipo Sera ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000 inayotoa dira ya Serikali kuhusu maendeleo ya makazi. Aidha, Wizara ipo katika mchakato wa kuandaa Sera ya Upimaji Ardhi kwa madhumuni ya kutoa dira ya Serikali katika upimaji ardhi na Sera ya Taifa ya Nyumba kwa madhumuni ya kutoa dira ya Serikali katika uendelezaji wa nyumba.

1.2.1           Sera ya Taifa ya Ardhi, 1995
Sera ya Taifa ya Ardhi inasisitiza masuala makuu yafuatavyo:-

(xvi)                    Inatambua kwamba ardhi yote Tanzania ni mali ya umma na imekabidhiwa kwa Rais kama mdhamini kwa niaba ya raia wote;

(xvii)                  Inahakikisha kwamba haki zote zilizopo katika ardhi na umilikaji wa ardhi kwa muda mrefu unatambuliwa, unafafanuliwa na kulindwa kwa Sheria;

(xviii)               Inawezesha ardhi kugawiwa kwa haki na kupatikana na ardhi hiyo kwa raia wote na vilevile imeweka misingi ya kutoa ardhi kwa wawekezaji;

(xix)                     Inahakikisha kwamba, ardhi inatumika kwa manufaa kiuzalishaji na kwamba matumizi hayo yanazingatia misingi ya maendeleo endelevu;

(xx)  Inazingatia kwamba maslahi yoyote katika ardhi yana thamani, na kwamba thamani hiyo inazingatiwa wakati wowote katika mapatano yoyote yanayoathiri maslahi hayo;

(xxi)                     Inaelekeza kulipa fidia kamili, ya haki na kwa wakati kwa mtu yeyote ambaye hakimiliki inafutwa, matumizi yake ya ardhi yanayotambulika kutokana na kutumia ardhi hiyo kwa muda mrefu au matumizi yake ya ardhi kwa mujibu wa mila yanafutwa au vinginevyo yanaingiliwa na Serikali na yeye kuathirika kwa mujibu wa Sheria hii au yanatwaliwa kwa mujibu wa Sheria ya Utwaaji wa Ardhi ya mwaka 1967;

(xxii)      Inaweka mfumo madhubuti, rahisi na wazi wa kusimamia kwa ufanisi masuala ya ardhi;

(xxiii)                Inawezesha uendeshaji wa soko la ardhi;

(xxiv)                Inadhibiti uendeshaji wa soko la ardhi kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa wakulima wadogo vijijini na mijini pamoja na wafugaji hawawekwi katika hali ngumu ya kuwasababishia hasara;

(xxv)                   Imeweka kanuni za Sheria za Ardhi ambazo zinapatikana kwa urahisi na zinazoeleweka kwa raia wote;

(xxvi)                Imeanzisha mfumo ulio huru, unaofanya kazi kwa haraka na wa haki kwa ajili ya kuamua migogoro ya ardhi, ambao utasikiliza na kuamua migogoro ya ardhi bila ya ucheleweshaji usio wa lazima;

(xxvii)              Inahimiza usambazaji wa taarifa za usimamizi wa ardhi na Sheria za Ardhi kama ilivyofafanuliwa na Sheria, kwa kupitia vipindi vya elimu kwa umma na kwa watu wazima na kwa kutumia njia mbalimbali za upashanaji habari;

(xxviii)          Inaelekeza kwa haki ya kila mwanamke kupata, kumiliki, kutumia na   kuuza au kuigawa ardhi ni sawa na haki ya mwanaume yeyote kwa viwango vile vile na masharti yale yale; na,

(xxix)  Inazuia matumizi na makazi katika maeneo oevu; mfano, maeneo yenye mikoko, maeneo kwa ajili ya kutupa taka, ardhi iliyopo ndani ya mita 60 za fukwe za bahari, na mita 30 maziwa, mito n.k, maeneo yenye miteremko mikali n.k.


1.2.2           Sera ya Maendeleo ya Makazi, 2000
Kuhusu ardhi Sera ya Maendeleo ya Makazi inaelekeza masuala yafuatayo muhimu:-

(xvii)      Kuwezesha uwepo wa ardhi yenye huduma; maji, barabara n.k kwa ajili ya malazi na makazi kwa jamii yote wakiwemo wanawake, vijana, wazee, walemavu na makundi mengine katika jamii.

(xviii)   Inakataza mabadiliko ya matumizi ya ardhi kwenye maeneo ya wazi, mabondeni na maeneo oevu na hatarishi.

(xix)         Inaruhusu kilimo mijini ili mradi shamba lisizi ekari tatu.


1.3             Sheria Zinazosimamia Sekta ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi

Sekta ya ardhi inasimamiwa na Sheria kadhaa. Sheria hizi zimegawanyika katika makundi matano ambayo ni; Sheria zinazosimamia utawala wa ardhi, Sheria zinazosimamia upangaji mipango ya matumizi ya ardhi, Sheria inayohusu upimaji ardhi, Sheria zinazohusu usajili wa ardhi na Sheria inayohusu utatuzi wa migogoro ya ardhi.

1.3.1                                              Sheria Zinazosimamia Utawala wa Ardhi

1.3.1.1                                     Sheria ya Ardhi Na. 4 ya 1999
Sheria hii imeweka utaratibu na mamlaka za usimamizi wa ardhi. Waziri mwenye dhamana na masuala ya ardhi anawajibu wa kuandaa Sera na kuhakikisha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Ardhi na Sheria za Ardhi. Kamishna wa Ardhi anawajibu wa kusimamia ardhi ya jumla pamoja na maelekezo mengine ya kisera yanayotolewa na Serikali kupitia kwa Waziri. Kamishna wa Ardhi katika kutekeleza Sheria hii amekasimu madaraka yake kwa Makamishna wasaidizi wa kanda na Maafisa Wateule waliopo katika Halmashauri za Wilaya na Miji.

RAMANI ZA KANDA

1.3.1.2                                     Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya 1999
Sheria hii imeweka masharti ya usimamizi na uendeshaji wa masuala ya ardhi katika vijiji. Sheria imegatua mamlaka ya usimamizi wa ardhi kwa Halmashauri za vijiji katika kupanga, kugawa na kusimamia matumizi ya ardhi. Katika kutekeleza mamlaka hayo, Halmashauri za vijiji zinatakiwa kupata ridhaa ya wanavijiji kupitia mikutano mikuu ya vijiji. Aidha, Halmashauri za vijiji zinatakiwa kuzingatia maelekezo yo yote yanayotolewa na Halmashauri za Wilaya na Kamishna wa Ardhi katika utekelezaji wa majukumu yake.

1.3.1.3       Sheria ya Utwaaji Ardhi Na. 47 ya 1967
Sheria hii imempa mamlaka Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutwaa milki yo yote ya ardhi pale ardhi hivyo inapohitajika kwa matumizi ya umma (public interest). Hata hivyo sheria inatoa haki ya fidia kwa mwananchi ambaye milki yake ya ardhi imetwaliwa.  

1.3.2                                          Sheria zinazosimamia upangaji mipango ya matumizi ya ardhi

1.3.2.1       Sheria ya Mipangomiji Na. 8 ya 2007
Sheria hii inaweka mamlaka zinazohusika katika kupanga miji na utaratibu mzima wa matumizi ya ardhi. Sheria imetoa mamlaka kwa Mkurugenzi wa Mipangomiji na Vijiji katika kupanga na kuidhinisha mipango ya matumizi ya ardhi. Aidha, inaelekeza kuwa Halmashauri za Wilaya na Miji zitakuwa mamlaka za upangaji katika maeneo yao.

1.3.2.2       Sheria ya Upangaji wa Matumizi ya Ardhi Na. 6 ya 2007
Sheria hii imeweka mamlaka na utaratibu wa kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi. Mipango hii imeelekezwa kuwa katika ngazi ya Taifa, Mikoa, Wilaya na Vijiji. Mamlaka za upangaji zimeanishwa katika Sheria ambapo Halmashauri za Wilaya na Vijiji ni mamlaka za upangaji katika maeneo yao.

1.3.2.3       Sheria ya Usajili wa Maafisa Mipangomiji Na. 7 ya 2007
Sheria hii imeweka utaratibu wa kusajili Maafisa Mipangomiji kwa madhumuni ya kudhibiti maadili ya taaluma ya mipangomiji na kusimamia viwango katika tasnia ya upangaji miji.

1.3.3                                           Sheria Inayohusu Upimaji Ardhi

1.3.3.1     Sheria ya Upimaji Ardhi Na. 32 ya 1957
Sheria hii imeweka mamlaka na utaratibu wa upimaji ardhi, kuweka mipaka ya ardhi na kutengeneza na kuidhinisha ramani za upimaji. Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani anawajibu wa kuidhinisha ramani za upimaji. Usajili na uthibiti wa maadili ya taaluma ya wapima ardhi unasimamiwa na Sheria ya Usajili wa Wapima Ardhi Na. 2 ya 1977 (The Proffessional Surveyors (Registration) Act).

1.3.4                              Sheria Zinazohusu Usajili wa Ardhi na Nyaraka Nyingine

1.3.4.1         Sheria ya Usajili wa Ardhi Na. 36 ya 1953
Sheria hii inahusika na taratibu za kusajili nyaraka zinazohusika na milki za ardhi. Waziri mwenye dhamana na masuala ya ardhi anawajibu wa kuteua Msajili wa Hati ambaye atatekeleza majukumu yaliyoainishwa katika sheria. Katika kutekeleza majukumu yake, Msajili wa Hati atashirikiana na Wasajili wa Hati Wasaidizi ambao baadhi yao wapo katika ofisi za kanda. Kwa ujumla, sheria inaelekeza kuhusu usajili wa awali wa milki za ardhi, namna ya kufanya usajili, masuala ya jumla yanayohusiana na usajili wa milki za ardhi, mathalani; miamala, kubadili milki, kutekeleza amri za Mahakama, usajili wa mazuio na mengineyo.
1.3.4.2        Sheria ya Usajili wa Nyaraka Na. 14 ya 1923
Sheria hii inahusika na usajili wa nyaraka mbalimbali zinazohitaji usajili. Waziri mwenye dhamana na masuala ya ardhi ana wajibu wa kuteua Msajili wa Nyaraka na wasaidizi wake. Wasajili wasaidizi wapo pia katika ngazi ya kanda. Sheria imeainisha nyaraka ambazo ni lazima zisajiliwe (compulsory) na zile ambazo usajili wake ni hiyari (optional). Aidha, sheria imeainisha utaratibu wa kusajili nyaraka, uwezo wa Msajili kukataa kusajili nyaraka na masuala ya jumla yanayohusu usajili wa nyaraka.

1.3.4.3        Sheria ya Usajili wa Mali Zinazohamishika Na.25 ya 1942
Sheria hii inahusika na kusajili mali zinazohamishika. Waziri mwenye dhamana na masuala ya ardhi anawajibu wa kuteua Msajili na Wasajili wasaidizi ambao watafanya shughuli zao kwa maelekezo ya Msajili na baadhi yao wapo katika ngazi ya kanda. Sheria inaainisha utaratibu wa kusajili mali zinazohamishika; mfano, hati za mauzo (bill of sale), rehani (mortgage), pango (lease), zawadi (gift) n.k.

1.3.5      Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi

1.3.5.1                            Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Na.2 ya 2002
Sheria hii inahusu vyombo vinavyohusika na utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa kuvipa mamlaka na kikomo cha mamlaka hayo. Fungu la 167 la Sheria ya Ardhi na fungu la 62 la Sheria ya Ardhi ya Vijiji yameainisha vyombo kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi. Fungu la 3 la Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi limeanzisha vyombo vifuatavyo kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ya ardhi;
           (i)        Baraza la Ardhi la Kijiji;
          (ii)        Baraza la Kata;
        (iii)        Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya;
        (iv)        Mahakama Kuu (Kitengo cha Ardhi); na
          (v)        Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.
Vyombo hivi vimeanza kazi rasmi tarehe 1 Oktoba, 2003 Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi ilipoanza kutumika. Kwa mujibu wa Sheria hii, kesi zote za madai zinazohusu masuala ya ardhi zinatakiwa kushughulikiwa na vyombo hivi.














 

















1.3.6             Sheria Zinazosimamia Mikoa na Serikali za Mitaa

Katika utekelezaji wa shughuli za viongozi wa Mikoa na Wilaya, Sheria hizi zinatakiwa kusomwa pamoja na Sheria zifuatazo:-

1.3.6.1       Sheria ya Tawala za Mikoa Na. 19 ya 1997
Sheria hii imeweka mfumo wa uongozi wa mikoa kwa madhumuni ya kuimarisha na kuhimiza mfumo wa Serikali za mitaa. Sheria inaelekeza kuwa wakuu wa mikoa na wilaya wanawajibu wa kutekeleza Sera za Serikali ikiwemo Sera ya Ardhi katika ngazi za mikoa na wilaya.

1.3.6.2       Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Na. 8 ya 1982
Sheria hii inaanzisha na kusimamia mamlaka za miji kwa maana ya; Miji, Manispaa na Majiji. Aidha, sheria inatoa madaraka kwa wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia shughuli za maendeleo katika maeneo yao ikiwemo sekta ya ardhi.

1.3.6.3       Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Na. 7 ya 1982
Sheria hii inaanzisha na kusimamia mamlaka za miji kwa maana ya; Wilaya, Miji midogo, Vijiji na Vitongoji. Aidha, sheria inatoa madaraka kwa wakurugenzi wa Halmashauri na Halmashauri za vijij kusimamia shughuli za maendeleo katika maeneo yao ikiwemo sekta ya ardhi.

Kwa ujumla sheria hizi ndizo zinazosimamia mamlaka za Mikoa na Wilaya na Halmashauri za Miji na Wilaya na kutoa majukumu kwa mamlaka hizi.

1.4              Sheria Nyingine Muhimu Katika Sekta ya Ardhi na kuepusha migogoro kama zikizingatiwa.

Sheria ya Mazingira, No. 40 ya 2004 (Environmental management act, 2004)
Sheria ya Uwekezaji, 1997 (Investment Act, 1997)
Sheria ya Madini, 2010 (Mining Act, 2010)

Sheria ya Malisho, 2010 9Grazing land and Animal Feeds Resources Act, 2010.


2.0              SHUGHULI ZA SEKTA YA ARDHI ZINAZOTEKELEZWA KATIKA NGAZI MBALIMBALI

Kitaifa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ndiyo yenye dhamana ya kusimamia matumizi endelevu ya ardhi na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anatumia ardhi hiyo kwa manufaa na kujiendeleza kiuchumi na kijamii.

Kama inavyojidhihirisha katika mchoro hapa chini, upo uhusiano wa karibu sana kati ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi za Mikoa na Wilaya katika utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi. Sehemu kubwa ya shughuli za sekta ya ardhi hutekelezwa katika Mikoa na Wilaya; hususan, katika Halmashauri za Wilaya/Miji/Manispaa/Majiji.



MUUNDO WA USIMAMIZI WA ARDHI NCHINI


 


2.1              Ngazi za Taifa

(i)        Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inawajibu wa kuandaa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo na kusimamia utekelezaji wake.
(ii)     Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inawajibu wa kusimamia utekelezaji wa Sera, sheria, kanuni na miongozo.

2.2              Ngazi ya Kanda

Kufuatilia usimamizi wa ardhi kikanda kwa kuhakikisha yafuatayo yanatekelezwa:-
                         (i)          Kuandaa na kuidhinisha mipango ya matumizi ya ardhi.
                        (ii)          Kushughulikia taratibu za upimaji ardhi.
                      (iii)          Kusimamia maandalizi ya hatimiliki na kusaini hati.
                      (iv)          Kusimamia uthamini wa mali.
                        (v)          Kusajili hatimiliki.

2.3              Ngazi za Mikoa

Kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Sera za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, Sheria, Kanuni na Miongozo:-

(i)        Kusimamia na kulinda mipaka ya nchi kwa mikoa iliyoko mipakani.

(ii)     Kuratibu maeneo mbalimbali yanayoandaliwa michoro ya mipangomiji na kukagua michoro ya mipangomiji iliyoandaliwa na Halmashauri kabla ya kuiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Mipangomiji kwa idhini yake.

(iii)   Kuratibu upimaji ardhi unaofanywa katika halmashauri na kuidhinisha ramani za upimaji huo.

(iv)   Kuangalia iwapo umilikishaji ardhi umefanyika kwa kuzingatia sheria.

(v)      Kuchambua na kuhakiki deed plans zinazoandaliwa mkoani kabla ya kuziwasilisha kwa Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kwa ajili ya idhini yake.

(vi)   Kuratibu maeneo yanayofanyiwa urasimishaji mjini na vijijijini.

(vii) Kukagua vitabu vya uthamini kabla ya kuviwasilisha kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa idhini yake.

(viii)                      Kutafsiri sheria na kushauri katika utatuzi wa migogoro ya ardhi inayotokea mkoani.

2.4              Ngazi za Halmashauri za Wilaya na Miji

Halmashauri za Wilaya/Miji/Manispaa/Majiji ni watekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo:-

(i)        Kuhamasisha na kutoa elimu ya Sheria za Ardhi.

(ii)     Kuandaa ramani za mipango miji na vitovu vya vijiji, ramani za urasimishaji wa maeneo yaliyojengwa kiholela na kutoa ushauri kuhusu uaandaji wa mipango ya matumizi ya Ardhi ya Vijiji na kuiidhinisha.

(iii)   Kupima mipaka ya vijiji, viwanja mijini na kutoa ushauri wakati wa uhakiki wa vipande vya ardhi katika Ardhi ya Kijiji.

(iv)   Kuandaa Vyeti vya Ardhi ya Kijiji.

(v)      Kwa kuzingatia sheria, kutwaa na kugawa ardhi kwa matumizi mbalimbali kwa kutumia kamati za ugawaji ardhi wilayani.

(vi)   Kutoa vibali cha uhamisho wa miliki za ardhi.

(vii) Kumshauri Kamishna wa Ardhi viwango ambavyo mtu/taasisi inaweza kumiliki.

(viii) Kutoa vibali vya ujenzi wa nyumba mjini.

(ix)    Kusimamia uendelezaji wa miji na kutoa ushauri wa uendelezaji wa vitovu vya vijiji na kudhibiti ujazo wa majengo katika miji na vitovu vya vijiji hivyo.

(x)      Kuainisha ardhi inayofaa kwa madhumuni ya uwekezaji.

(xi)    Kumshauri Kamishina kuhusu uhawilishaji wa ardhi.

(xii) Kupendekeza mabadiliko ya matumizi ya ardhi.

(xiii)        Kuainisha na kupendekeza ardhi yenye madhara na kuwasilisha mapendekezo hayo kwa Kamishina wa Ardhi.

(xiv)        Kushughulikia taratibu za kuandaa mapendekezo ya ufutaji miliki za ardhi kabla ya kuwasilishwa kwa Kamishna wa Ardhi.

(xv)  Kusimamia uthamini wa mali kwa madhumuni ya kulipa fidia.

(xvi)     Kutoa ushauri kwa Halmashauri za Vijiji kuhusu usimamizi wa ardhi ya vijiji na kuhakikisha zoezi la utoaji wa Hati za Hakimiliki ya Kimila linafanyika vijijini.

2.5              Ngazi ya Kata

Kamati ya Maendeleo ya Kata zina wajibu wa:-

(i)          Kushiriki katika uhamasishaji wa utekelezaji wa Sheria za Ardhi.

(ii)     Kutoa taarifa ya migogoro ya mipaka ya vijiji na kusaidia kutatua migogoro hiyo.

(iii)     Kushauri vijiji kuhusu mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji vyao na mipango ya matumizi ya pamoja ya ardhi ya vijiji.

(iv)      Kupitisha Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kijiji.


2.6              Ngazi ya Vijiji

2.6.1           Mkutano wa Kijiji
(i)        Kuidhinisha ugawaji wa ardhi ya kijiji na mipango ya matumizi ya ardhi ya kijiji.
(ii)     Kuridhia uhakiki wa maslahi katika ardhi ya kijiji.
(iii)   Kuridhia uhawilishaji wa ardhi ya kijiji.

2.6.2           Halmashauri ya Kijiji
(i)        Kusimamia ardhi ya vijiji kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji. Na. 5 ya 1999.
(ii)     Kulinda mipaka ya kijiji na kuhakikisha kijiji kinapata Cheti cha Ardhi ya Kijiji na kutunza cheti hicho.
(iii)   Kugawa ardhi ya kijiji baada ya kuidhinishwa na Mkutano mkuu wa kijiji.
(iv)   Kupendekeza aina ya mpango wa matumizi ya ardhi ya kijiji.

(v)      Kupendekeza kuanza kwa zoezi la uhakiki wa vipande vya ardhi kwa Mkutano wa Kijiji.

(vi)   Kudhibiti kiasi cha ardhi ambacho mtu/taasisi inaweza kumiliki katika kijiji.

14.  MIGOGORO YA ARDHI KATI YA WAKULIMA NA WAFUGAJI

Migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji iliyopokelewa na Wizara na kushughulikiwa kati ya mwaka 2005 – 2012 na ambayo inaendelea kushughulikiwa ni kama ifuatavyo:

2.6.3                    Mgogoro wa Ardhi Ngorongoro/Longido

Mgogoro huu unahusu ardhi ya makazi na hifadhi. Chanzo cha mgogoro ni kuwa ardhi yote ni ardhi ya hifadhi na zipo kazi za kilimo, makazi na ufugaji, uwindaji na utalii zinafanyika katika eneo hili. Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni kutayarisha mipango ya matumizi bora ya ardhi katika eneo hilo na kuunda kamati ya kushughulikia mgogoro huu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ushauri wa Wizara ni kuwa eneola hifadhi ya wanyamapori (GCA) lipunguzwe na wapewe wananchi (wanavijiji).  Aidha, eneo la kijiji na eneo la hifadi lipimwe ili kutambua na kuanza kutumia mipaka mipya. Pia, huduma muhimu kama masoko na bwawa la maji zipelekwe kwenye maeneo hayo.

2.6.4                    Mgogoro wa Ardhi- Kilosa

Mgogoro uliopo katika eneo la Kilosa unatokana na kuwepo kwa vijiji vilivoandikishwa ndani ya mashamba makubwa yenye hatimiliki zilizohai. Chanzo cha migogoro katika eneo hili ni kuwepo kwa ongezeko kubwa la mifugo inayoingia ikitoka nje ya Wilaya hiyo. Kwa hiyo eneo hili limekuwa na uwezo mdogo wa kubeba wingi wa mifugo. Kwa ujumla wafugaji wamekuwa wakiharibu mazao ya wakulima mara kwa mara.
Kutokana na  kuwepo kwa mgogoro huu Serikali ilikwisha kuanza kutayarisha mipango ya matumizi bora ya ardhi katika baadhi ya vijiji Wilayani Kilosa, elimu kwa umma imetolewa kwa wananchi kuhusu madhara ya kuwepo kwa mifugo wengi eneo moja, na kuanza kufanya tathmini ya wamiliki wa mashamba makubwa kwa lengo la kuyatwaa na kuyagawa kwa wamiliki wengine. Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI zimeona upo umuhimu wa kuwatafutia eneo mbadala wafugaji. Pia, wizara inaendelea na hatua ya kufuta milki kwa waliovunja masharti ya umiliki wa mashamba hayo.

2.6.5                    Mgogoro wa Ardhi - Kilombero/Ulanga
Mgogoro huu unatokana na kuwepo kwa kundi kubwa la mifugo katika eneo la Bonde la Mto Kilombero kuliko uwezo wake na kusababisha kuwepo kwa mgogoro kati ya wanavijiji na wafugaji. Serikali imechukua hatua za kupima mipaka ya vijiji 50 Wilayani Kilombero na kuanza kutayarisha mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji vilivyopimwa mipaka yake, kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara yanayotokea kutokana na kuwepo kwa mifugo mingi katika eneo hilo; na kuanza mchakato wa kulitangaza eneo lililo oevu kuwa ramsar site (under Conservation International Heritage).

2.6.6                    Mgogoro wa Ardhi  - Rufiji
Mgogoro katika eneo hili unatokana na kuongezeka kwa mifugo kuliko uwezo wake na kusababisha kuwepo kwa mgogoro kati ya wakulima na wafugaji. Pia, wafugaji wamekuwa wakiingiza mifugo yao kwenye Pori tengefu la Selous na kusababisha uharibifu wa mazingira. Vilevile,  mifugo imekuwa ikiingizwa kwenye marine conservation area (Delta) kinyume na mkakataba wa Umoja wa Mataifa wa kutunza viumbe hai (marine Biodiversity convention treaty).  Pia, yamekuwepo matukio ya wawekezaji kuingia kinyemela kwa wanavijiji na kuanza michakato ya kumilikishwa ardhi bila kufuata sheria.

Hatua zinazochukuliwa na Wizara ni pamoja na kuanza mchakato wa kutangaza eneo hilo kuwa la hifadhi; kuongeza kasi ya utayarishaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi; kusimamia sheria na sheria ndogo zinazolinda mazingira na matumizi ya ardhi.

Migogoro mingine iliyojitokeza kati ya wakulima na wafugaji iko katika Wilaya za Mbarali, Babati, Mbulu, Karatu, Mbinga, Arumeru, Tarime, Geita, Simanjiro Muleba nk kama ilivyoambatishwa (Kiambatisho Na. 1).


15    WAJIBU WA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA

Viongozi wa mikoa na wilaya wanawajibu ufuatao katika kusimamia sekta ya ardhi na kuzuia migogoro ya ardhi katika maeneo yao:-
2.7              Kusimamia mipaka ya nchi na nchi jirani kwa mikoa iliyoko mipakani.
           
5.1              Kuhakikisha kuna mipango ya matumizi ya ardhi iliandaliwa na kukubaliwa na kupitishwa katika maeneo yao kwa mujibu wa Sheria ya Upangaji wa Matumizi ya Ardhi Na. 6 ya 2007.

2.8              Kuhamasisha wananchi kufuata mipango iliyowekwa na kuisimamia kwa pamoja; Mfano, mwananchi akianza kujenga au kuingiza mifugo kwenye msitu wa hifadhi azuiwe mara moja.

2.9              Kuelimisha umma kuhusu ardhi na matumizi yake na kuhakikisha wananchi wanafuata mipango iliyowekwa.

2.10          Kuainisha ardhi kwa ajili ya wawekezaji. Hii itasaidia wawekezaji kupata ardhi kwa urahisi na vilevile kuhakikisha wananchi wanabaki na ardhi ya kutosha.

2.11          Kuhimiza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya matumizi ya umma yanapimwa na kumilikiwa na Halmashauri inayohusika. Mfano; Majiji, Manispaa, Mji, Wilaya na hata Vijiji.

2.12          Kufuatilia kwa kina migogoro inayotokea na kusaidia kuitafutia ufumbuzi kiutawala.

2.13          Kujadili mipango ya matumizi ya ardhi katika vikao ili kudhibiti maendeleo katika ngazi zote. Pamoja na kuwa sheria inatoa mamlaka kwa vyombo mbalimbali katika masuala ya ardhi, taarifa zitolewe kwenye vikao vinavyowekwa kisheria kama vile RCC, DCC, WDC na NDC ili kila ngazi ielewe jinsi ardhi inavyotumika au kugawiwa.

2.14          Kuhakikisha ardhi haitolewi kwa wasio raia isipokuwa kwa kufuata sheria.

2.15          Kuhakikisha Halmashauri zinaweka kwenye mipango yao fedha za kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na upimaji wa viwanja na vijiji ya kutosha kila mwaka.

2.16          Kuhakikisha Halmashauri zinaajiri watumishi wa sekta ya ardhi na kununua vitendea kazi vinavyohusu sekta ya ardhi.

2.17          Kuhakikisha kuwa vijiji vinaanzishwa kwenye maeneo yasiyo ya hifadhi. Hii inawezekana kabisa kuhakikisha kuwa vijiji havianzishwi kiholela. Yaani watu wanaanza kujenga msituni bila kuulizwa na baadaye kijiji kinaandikishwa. Aidha,  ni muhimu kwa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kuwasiliana na Wizara ya Ardhi na Maliasili na Utalii kabla ya kuanzisha na kusajili vijiji vipya.

2.18          Kusimamia mipango ya matumizi ya ardhi kwa madhumuni ya kudhibiti mwingiliano baina ya wakulima na wafugaji.


15.  CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI SEKTA YA ARDHI
Sekta ya ardhi ni sekta muhimu hivyo zipo changamoto nyingi zinazoikabili sekta hii. Miongoni mwa changamoto hizo ni:-

2.19          Kuongezeka kwa idadi ya watu mwaka hadi mwaka wakati ardhi haiongezeki. Hivyo ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii inazidi kuadimika. Kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya watu kutaendelea, na ardhi kwa ajili ya makazi na shughuli za kiuchumi na kijamii itaendelea kuadimika, kuongezeka thamani na kugombaniwa. Kulingana na takwimu za sense ya mwaka 1988 Tanzania ilikuwa na watu 23 milioni. Mwaka 2002 watu 34.4 milioni sawa na ongezeko la asilimia 2.9 wakati mwaka 2027 Tanzania inategemewa kuwa na watu milioni 75.

2.20       Kuwepo kwa uwezo mdogo wa usimamizi wa matumizi ya rasilimali za ardhi unaotokana na ukosefu wa watalaam wa kutosha, vitendea kazi na bajeti ya kutosha. Upungufu wa wataalamu wa sekta ya ardhi katika Halmashauri za Wilaya ni asilimia 76.

2.21          Kuongezeka kwa idadi ya migogoro miongoni mwa watumiaji wa ardhi,        kutokana na ukosefu wa elimu ya sheria za ardhi kwa wananchi, ujenzi holela, uvamizi wa maeneo yaliyopangwa na kupimwa na hata kumilikishwa, uhaba wa viwanja vilivyopimwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

2.22          Kukua kwa migogoro ya ardhi vijijini inayotokana na makundi ya watumiaji wa ardhi kugombania haki ya kutumia ardhi. Mfano ni migogoro kati ya jamii za wakulima na wafugaji; migogoro kati ya wawekezaji au mamlaka za hifadhi mbalimbali kwa upande mmoja na wanavijiji.

2.23          Kugombania mipaka kati ya vijiji au wilaya na hata mkoa kwa mkoa mwingine. Hii inasababisha usimamizi dhaifu wa ardhi katika baadhi ya maeneo.

2.24          Kuwepo kwa migogoro ya ardhi mijini kutokana na mtu zaidi ya mmoja kudai haki ya kumiliki kiwanja kimoja au eneo moja; uvamizi wa maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya matumizi ya umma (ikiwa ni pamoja na maeneo ya wazi au burudani); au watu kutoridhika na taratibu za kutwaa ardhi kwa mujibu wa Sheria, kubadili ardhi toka kundi moja kwenda jingine (kuhawilisha), kubatilisha milki pale mmiliki anapokuwa hajatimiza masharti ya umilikaji.

2.25          Kukiukwa kwa Sheria: Shughuli za sekta ya ardhi zinaongozwa na sheria na kanuni ambazo zinatakiwa kufuatwa katika kupanga na kusimamia matumizi ya ardhi na wakati wa kumilikisha, kuhawilisha, kutwaa, kubatilisha, kupima, kugawa na kuendeleza ardhi, pamoja na kulipa fidia ya ardhi.

2.26          Kutokuwa na Mipango ya Matumizi ya Ardhi: Sehemu kubwa ya ardhi ya nchi yetu bado haijaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Vijiji vyenye mipango hiyo ni kadri ya 1,000 tu kati ya vijiji 11,000 nchini. Kwa upande wa mijini, miji mikuu ya Mikoa yenye mipango ya uendelezaji (master plans) iliyo hai ni kumi tu kati ya miji 25. Miji mikuu ya Wilaya yenye mipango ya matumizi ya ardhi ni 20 kati ya miji zaidi ya 110, na miji midogo yenye mipango hiyo ni 25 tu kati ya miji 95. Hali hii hutoa fursa kwa migongano kutokea kati ya watumiaji wa ardhi kutokana na mwongozo juu ya matumizi halali ya ardhi kutokuwepo.

2.27          Kutozingatia mipango ya ardhi inayoandaliwa na kuidhinishwa kisheria     katika matumizi ya ardhi mfano Dar es salaam inao mpango kabambe ulioidhinishwa mwaka 1979. Hata hivyo mpango huo hauzingatiwi na watendaji wa Halmashauri za Manispaa ambao wamekuwa wakibadilisha matumizi ya ardhi bila kuzingatia mpango.

2.28          Kukosekana kwa bajeti ya kutosha kwa Sekta ya Ardhi katika ngazi zote; hususan, katika Serikali za Mitaa. Kwa miaka mingi sekta ya ardhi imekuwa ikitengewa bajeti isiyokidhi mahitaji ya kujenga uwezo wake kiutendaji ili kuweza kupanga, kupima kumilikisha na kusimamia uendelezaji wa ardhi mijini na vijijini kwa kasi inayoweza kukidhi mahitaji ya wadau mbalimbali. Utaratibu wa sekta ya ardhi kutopewa ruzuku na Serikali kuu umesababisha ukosefu wa bajeti kwani Halmashauri za Miji na Wilaya hazitengi fedha kwa kazi za Sekta ya Ardhi.

2.29          Kukosekana kwa usimamizi thabiti wa wamiliki wa aina mbalimbali za ardhi mfano, wasimamizi wa maeneo ya hifadhi ya wanyamapori, misitu, barabara na huduma za umma kama shule, hospitali, vyuo, na maeneo ya majeshi, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Burudani. Hii inasababisha migogoro kati ya wananchi na asasi zinazohusika.

2.30          Kuwepo kwa mapungufu katika Sera ya ugawaji ardhi kwa ajili ya uwekezaji: Katika miaka ya hivi karibuni wawekezaji wakubwa wameanza kujitokeza kuwekeza katika kilimo cha mazao ya chakula na nishati itokanayo na mimea. Hata hivyo sheria haiwezeshi upatikanaji wa ardhi kwa urahisi wala haionyeshi viwanja vya uwekezaji katika ardhi kwa kila mradi wa mwekezaji.

2.31          Kuwepo kwa mashauri mengi katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ni changamoto kubwa inayoikabili sekta ya ardhi. Mabaraza yaliyoundwa hadi sasa ni sehemu ndogo ya Mabaraza yote yanayotakiwa kuundwa nchini. Kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2011 jumla ya mabaraza 39 yamekwishaanzishwa kati ya Wilaya takribani 140 nchini. Idadi hii ndogo imetokana na ufinyu wa tengeo la fedha katika bejeti inayopata Wizara kwa mwaka.

2.32          Kufunguliwa kwa mashauri mengi katika Mabaraza machache yaliyopo, hivyo kushindwa kumaliza kesi zinazofunguliwa. Takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2010 jumla ya mashauri 46,343 yalifunguliwa kati ya hayo mashauri 32,972 yameamuliwa na mashauri 13,371 yanaendelea kusikilizwa.

2.33          Kuwepo kwa muundo wa utawala wa ambao hauwezeshi usimamizi na uratibu mzuri wa masuala ya ardhi kisheria katika ngazi mbalimbali.


16.  MIKAKATI YA KUBORESHA SEKTA YA ARDHI

Katika kukabiliana na changamoto hizo Wizara imejiwekea mikakati ya kukabiliana nazo. Mikakati hiyo ni:-

6.1       Kuhakikisha uuandaaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi zote mijini na vijijini, kupima ardhi, kuimilikisha na kuiwekea miundo mbinu ya msingi. Hii itawezesha upatikanaji wa ardhi kwa matumizi yote.

Ili kupanga, na kupima ardhi yote nchini, serikali haina budi:

6.1.1    Wizara imeandaa rasimu ya sheria mpya ya uthamini wa mali ili kuwa na vigezo vya uhakika vya kulipa fidia. Pia  viwango vya fidia vimeboreshwa na uanzishaji wa mfuko wa fidia ili kuondoka tatizo la kuchewesha ulipaji fidia.

6.1.2        Hatua za kuanzisha Hazina ya Ardhi (Land bank) zinaendelea.

6.1.3        Kufuatilia na kuhakikisha kuwa Halmashauri zina watumishi na vitendea kazi vya kutosha vinavyohusika katika sekta ya ardhi kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na UTUMISHI. Aidha, kuhimiza ujenzi na ukarabati wa ofisi za ardhi za wilaya na ofisi za Serikali za vijiji ambazo zitatumika pia kuwa Masjala za Ardhi za Vijiji na Wilaya .

6.1.4        Wizara itaendelea kutekeleza mradi wa kuweka mfumo wa alama za upimaji nchini (geodetic network) na kukamilisha maandalizi ya mradi wa ujenzi wa kituo cha kupokea picha za satellite. Lengo la miradi hiyo ni kupunguza gharama za upimaji wa ardhi na kuongeza kasi ya upimaji. Vile vile, Wizara itatoa kipaumbele kwa ununuzi wa vifaa vya upimaji pamoja kubuni na kutathmini taratibu mbadala za kupima ardhi zitakazohusisha ushirikiano na sekta binafsi.


6.2  Kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kutoa elimu kwa watendaji wa Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na Kata ili waweze kushughulikia mashauri ya ardhi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

6.3  Wizara imeandaa mapendekezo ya kurekebisha taratibu za umiliki ardhi kwa wawekezaji wakubwa, ili kuweza kuondoa migongano iliyopo sasa. Aidha Wizara imeanza kutekeleza sera ya Ardhi kama mtaji ’ Land for Equity’ wawekezaji watakuja na mitaji na uendeshaji ’ capital and management’ Utaratibu huu umeanza na Shamba la RAZABA huko Bagamoyo kati ya Serikali na mwekezaji wa Kampuni ya ECO Energy. Utaratibu huo utawasaidia pia wakulima wadogo chini ya mpango wa ’outgrowers scheme’.

6.4  Kusimamia utekelezaji wa Sheria zinazohusu ardhi ili kuhakikisha kuwa ardhi inatumika kwa matumizi yaliyopangwa na kuwa ardhi hiyo inaendelezwa kwa mujibu wa sheria.

6.5  Kuimarisha mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu za ardhi na usimamizi wa watendaji wa sekta ya ardhi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.

6.6  Kuimarisha ukusanyi wa ada za ardhi kwa lengo la kupata fedha za kutosha katika kuendeleza sekta ya ardhi. Kwa sasa Wizara imeongeza viwango vya tozo la huduma za ardhi na kodi ya ardhi ambavyo vimeanza kutumika nchini.

6.7  Kuimarisha utafiti katika masuala yahusuyo ardhi hususani migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa lengo la kupata ufumbuzi wa kudumu.


a.      Kuboresha taratibu za utatuzi wa migogoro ya ardhi na Nyumba: Kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutoa elimu kwa watendaji wa Mabaraza ya Ardhi ya vijiji na Mabaraza ya Kata ili waweze kushughulikia mashauri ya ardhi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

b.      Kuboresha Sera ya ugawaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji: Wizara imeandaa mapendekezo ya kurekebisha taratibu za umiliki ardhi kwa wawekezaji wakubwa, ili kuweza kuondoa migongano iliyopo sasa.

c.       Kuboresha sheria zinazohusu uthamini wa fidia: Wizara imeandaa rasimu ya sheria mpya ya uthamini wa mali na ili kuwa na vigezo vya uhakika vya kulipia fidia. Aidha, viwango vya fidia vinaboreshwa kwa madhumuni hayo hayo.

d.     Kuongeza kasi ya upimaji ardhi: Wizara itaendelea kutekeleza mradi wa kuweka mfumo wa alama za upimaji nchini (geodetic network) na kukamilisha maandalizi ya mradi wa ujenzi wa kituo cha kupokea picha za satellite. Lengo la miradi hiyo ni kupunguza gharama za upimaji wa ardhi na kwa msingi huo kuongeza kasi ya upimaji. Wizara vile vile itatoa kupaumbele kwa ununuzi wa vifaa vya upimaji kwa matumizi ya Wizara, itabuni na kutathmini taratibu mbadala za kupima ardhi zitakazohusisha ushirikiano na sekta binafsi.


e.      Kuwezesha wahitimu wa Vyuo vya Ardhi vya Morogoro na Tabora kuajiriwa moja kwa moja kwenye Halmashauri wanapohitimu masomo yao.




17.  HITIMISHO NA MAPENDEKEZO KWA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA

Mada hii imetoa kwa muhtasari mambo yaliyozingatiwa katika Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi na Sheria zake. Masuala yaliyotolewa hapa ni machache ukilinganisha na hali halisi ya yaliyomo katika Sera, Sheria, kanuni na taratibu. Pia, nimeleza baadhi ya migogoro ya ardhi inayojitokeza mara kwa mara hususan migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Wizara ipo katika mchakato wa kupitia sheria zake kwa madhumuni ya kuziboresha; hususan, kwa kuweka majukumu ya mikoa na wilaya bayana katika usimamizi wa ardhi.

Pia, tupo katika Shirikisho la Afrika Mashariki ambalo limeleta muingiliano mkubwa na nchi jirani na hivyo kusababisha mahitaji makubwa ya ardhi kwa majirani. Vilevile baadhi ya watanzania na nchi mbambali Dunia zimeonyesha nia ya kuwekeza kwa ajili ya kilimo cha mashamba makubwa. Kwa hali hiyo natoa wito kwa viongozi wote tushirikiane kutenga mipango ya matumizi bora ya ardhi, kuzuia kutokea kwa migogoro ya ardhi na inapotokea itafutiwe ufumbuzi wa haraka kwa kuzishirikisha mamlaka mbalimbali.




 ASANTENI KWA KUNISIKILIZA





[i] Kwa mgano kwa vigezo vya Usalama vya Umoja wa Mataifa, Mkoa wa Kagera na Kigoma inahesabiwa kama Security Phase I (yaani unstable, government not in full control of the territory), ambapo viongozi waandamizi wa Umoja wa Mataifa wanapotembelea maeneo hayo inabidi wapewe ulinzi na Serikali na Bima zao za Ajali huarifiwa (Malicious insurance cover to be invoked).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni