Nav bar

Jumatano, 29 Septemba 2021

ULEGA: TUMEDHAMIRIA KUWAWEZESHA WAVUVI WAONDOKANE NA UVUVI WA KUWINDA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kuwaelimisha Wavuvi na kuwapa vifaa maalum vitakavyowasaidia kujua wapi kuna makundi ya Samaki ili waachane na Uvuvi wa kuwinda ambao umekuwa hauna tija kwao.

Ulega aliyasema hayo katika hafla fupi ya kuwakabidhi Wavuvi na Wakulima wa Mwani vifaa vya kufanyika kazi vikiwemo injini ya boti na Kamba za kulimia zao la Mwani iliyofanyika katika Kijiji cha Mchinga, Mkoani Lindi Septemba 23, 2021.

"Sasa hivi tunatumia njia ya 'Satelite' kujua mavuvi yetu yako wapi, samaki wako wapi, kifaa cha GPS kinamsaidia mvuvi kabla hajatoka Pwani kujua aende umbali gani ambako kuna makundi ya Samaki,"alisema Ulega

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwataka Wavuvi na Wakulima wa zao la Mwani kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwaletea maendeleo.

Katika hafla hiyo, Naibu Waziri Ulega aliwapatia Wavuvi injini moja ya boti yenye thamani ya Shilingi Milioni 11, na Kamba zenye thamani ya Shilingi Milioni 8 kwa Vikundi vitatu vya kina mama Wakulima wa Mwani Mkoani humo.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mama Salma Kikwete alisema kuwa anaishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha wananchi wa Jimbo lake vifaa vitakavyowasaidia kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Aliongeza kuwa yeye kama Mbunge kwa kushirikiana na wananchi ataendelea kuhakikisha maendeleo yanapatiakana kwa kasi katika Jimbo hilo la Mchinga.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akimkabidhi Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mama Salma Kikwete (kushoto) injini ya Boti yenye thamani ya Shilingi Milioni 11 kwa ajili ya kuwapa Wavuvi waitumie katika shughuli zao. Hafla ya kukabidhi injini ilifanyika Katika Kijiji cha Mchinga, Mkoani Lindi Septemba 23, 2021. 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (katikati) akikabidhi kamba za kulimia Mwani kwa wakina Mama Wakulima wa Mwani katika Kijiji cha Mchinga Mkoani Lindi Septemba 23, 2021. Kamba hizo zilizokabidhiwa zina thamani ya Shilingi Milioni 8 Kulia kwake ni Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mama Salma Kikwete. 


Mmoja wa kina Mama wanaojishughulisha na ukulima wa Mwani, Fatuma Selemani akiishukuru Serikali kwa kuwapatia vifaa vitakavyowasaidia kurahisisha utendaji kazi wao. Alitoa shukrani hizo katika hafla ya kukabidhi boti kwa Wavuvi na Kamba kwa Vikundi vya kina mama Wakulima wa Mwani iliyofanyika katika Kijiji cha Mchinga, Mkoani Lindi Septemba 23, 2021. 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni