Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema katika bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali itajenga bwawa la kunyweshea Mifugo lenye thamani ya Shilingi Milioni 480 katika Kijiji cha Kimambi, Wilayani Liwale, Mkoani Lindi.
Ulega aliyasema hayo Septemba 20, 2021 alipofanya ziara katika
Wilaya ya Liwale, Mkoani Lindi kwa lengo la kusikiliza kero za Wafugaji na
Wakulima ili kuzitatua.
Alisema ujenzi wa bwawa hilo utasaidia kutatua changamoto ya
maji ambayo inawakabili wafugaji wa maeneo hayo na utasaidia pia kutatua
migogoro baina yao na wakulima Wilayani humo.
"Rais Samia Suluhu Hassan anakwenda kuwajengea bwawa lenye
thamani ya Shilingi Milioni 480 hapa Kimambi, ujenzi wa bwawa hilo utasaidia
kuwaondosha katika migogoro," alisema Ulega
Naibu Waziri Ulega alisisitiza kuwa pesa hizo zipelekwe
kufanya kazi iliyopangiwa ya ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo huku
akiwataka viongozi wa Wilaya hiyo kuhakikisha pesa hizo zinatumika vizuri.
Aidha, alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewapa pia Majosho
mawili katika Kijiji cha Kimambi na Kijiji cha Luwele.
"Sasa kwa sababu huku mifugo imekuwa mingi sana, Mimi
nakuongezeeni Josho lingine hapa ili mifugo mingi iweze kuogeshwa ,"
aliongeza Ulega
Naye, Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka alitumia nafasi hiyo
kumshukuru Rais wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea pesa
hizo huku akisema kuwa bwawa hilo likikamilika hawatarajii tena kuona migogoro
katika Vijiji vilivyotengwa kwa ajili ya Wafugaji Wilayani humo.
Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiongea na Wafugaji na Wakulima wa Kijiji cha
Kimambi, Wilayani Liwale, Mkoani Lindi (hawapo pichani) alipofanya ziara katika
Wilaya hiyo Septemba 20, 2021 kwa lengo la kutatua kero zao. Katika ziara hiyo Ulega
alisema Serikali itajenga bwawa la kunyweshea Mifugo Kijijini hapo lenye
thamani ya Shilingi Milioni 480. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Liwale,
Judith Nguli.
Sehemu ya
Wakulima na Wafugaji wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah
Ulega (hayupo pichani) alipokuwa akiongea nao katika Kijiji cha Kimambi,
Wilayani Liwale Mkoani Lindi Septemba 20, 2021.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni