Serikali imekabidhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza eneo
lenye ukubwa wa Hekta 6,000 lililotolewa kwa wananchi wa vijiji vya Mpeta na
Chakuru ili ligawiwe kwa wananchi hao kwa ajili ya shughuli za ufugaji baada ya
mgogoro wa muda mrefu wa wananchi hao kuvamia Hifadhi ya Ranchi ya Taifa ya
Uvinza iliyopo Mkoani Kigoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amekabidhi eneo
hilo (23.09.2021), akitekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ameamua eneo hilo kumegwa kutoka Hifadhi ya
Ranchi ya Taifa ya Uvinza baada ya kusikia kilio cha wafugaji hao kutoka mikoa
ya kanda ya ziwa kutokuwa na maeneo kwa ajili ya mifugo yao.
Waziri Ndaki alibainisha kuwa hatua hiyo inakuja kukiwa na
mgogoro mkubwa baina ya wananchi hao ambao ni wafugaji, Halmashauri ya Wilaya
ya Uvinza na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambapo wananchi zaidi ya 5,900
wamevamia eneo la ranchi hiyo kitongoji cha Mwanduhubanhu kijiji cha Mpeta na
eneo la Kazaroho Wilaya ya Uvinza na kuendesha shughuli za ufugaji na kilimo.
Kabla ya hatua ya kukabidhi eneo hilo serikali kupitia Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, watendaji wa Halmashauri za Wilaya za Uvinza na Kasulu kutoka
Idara za Ardhi, Kilimo na Mifugo ambao walifanya sensa ya kujua idadi ya
wavamizi hao kupima eneo ambalo litaweza kutumika kwa wananchi, kuchora ramani
upya na kugawa eneo kuondoa mgogoro huo mchakato uliochukua miezi miwili
kukamilika.
Waziri Ndaki alisema awali Rais Samia alishauriwa kutoa Hekta
4,000 lakini baada ya kufanywa kwa sensa ya watu na mifugo aliamua kutoa Hekta
6,000 ili ziweze kutumiwa na wananchi hao.
“Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa eneo hili naomba
kutangaza kuwa serikali haitaongeza eneo lingine na mgawanyo utafanywa kwa watu
zaidi ya 5,900 waliokuwa wakihusika na mgogoro na kwamba watakaovamia eneo la
ranchi ambalo siyo eneo lililomegwa na kugawiwa sheria itachukua mkondo wake.”
Amesema Waziri Ndaki
Akitoa taarifa kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mkurugenzi Mkuu wa
Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe amesema mchakato
umefanyika kwa kuwa na vikao zaidi ya vitano na viongozi na wananchi waliovamia
eneo hilo ambapo changamoto mbalimbali zilijitokeza.
Prof. Msoffe alisema licha ya mapendekezo na ushauri uliokuwa
ukitolewa na wataalam wananchi hao pia walikuwa na mapendekezo, ushauri na
maamuzi ambayo wakati mwingine yaliegemea kwenye baadhi ya makundi kuona
yananufaika zaidi hivyo maamuzi mengi kuwa na changamoto ya kufikia mwisho kwa
faida ya wote.
“Kwa sasa kumekuwa na idadi kubwa sana ya watu na mifugo na hiyo
inatokana na ongezeko kubwa la wavamizi hao ambapo baada ya kusikia kumeanza
mchakato wa sensa na upimaji baadhi ya watu waliongezeka ambao hapo awali
hawakuwepo kwenye eneo hilo na wengine wameingia kwenye eneo ambalo hapo awali
halikuwa kwenye mgogoro na kuanza kudai waongezewe eneo.” Alisema Mkurugenzi
huyo wa NARCO.
Aliongeza kuwa eneo hilo la Hekta 6,000 limegawanywa kwa Hekta
2,500 kutoa kitongoji cha Kazaroho kijiji cha Mpeta na Hekta 3500 kitongoji cha
Mwanduhubanhu kijiji cha Mpeta wilaya ya Uvinza.
Naye Mkuu wa Wilaya Uvinza, Mhe. Anafi Msabaha akizungumza
katika mkutano huo amesema mgogoro huo umefikia mwisho kwa maamuzi ya Rais
kutoa eneo ambalo litatumiwa na wananchi waliokuwa kwenye mgororo na kwamba
wilaya itasimamia kuona taratibu za ugawaji zinafanyika kwa uwazi na wananchi
ambao ni wafugaji waliohusika wanapatiwa maeneo kulingana na mgawanyo
utakaofanyika.
Baadhi ya wananchi walioongea baada ya taarifa ya Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki kuhusu kutolewa kwa eneo hilo wameishukuru
serikali kwa kukubali kuwamegea eneo hilo, huku wakidai bado eneo walilopewa
haliwezi kutosheleza mahitaji na kuomba waongezewe maeneo zaidi.
Mmoja wa wananchi hao Bw. Masele Mayenga amesema eneo
lililotolewa linaweza kutumika kupatia ufumbuzi wa mgogoro uliokuwepo ambapo
wafugaji walikuwa wakisumbuliwa na kuondolewa eneo la Ranchi kwa kuvamia eneo
hilo ambapo amesema kuwa bado eneo walilopewa haitoshelezi mahitaji yao.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) Prof.
Peter Msoffe (aliyesimama kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
Uvinza Bw. Masumbuko Kechegwa (aliyesimama kushoto) wakikabidhiana nyaraka
ambapo NARCO imekabidhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Hekta 6,000 zilizomegwa
kutoka kwenye Ranchi ya Uvinza kwa ajili ya wananchi ambao ni wafugaji
waliovamia ranchi hiyo. Agizo la kumegwa eneo hilo limetolewa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. (23.09.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki
(aliyesimama kulia) akizungumza na wananchi wa vitongoji vya kijiji cha Mpeta
Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma, kuhusu agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kumega Hekta 6,000 za Ranchi ya Taifa ya
Uvinza na kugawiwa kwa wananchi waliovamia eneo hilo na kuendesha shughuli za
kilimo na ufugaji. (23.09.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyesimama wa
pili kutoka kushoto) na Mkuu wa Wilaya Uviza Mhe. Hanafi Msabaha (wa kwanza
kushoto) wakishuhudia Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO)
Prof. Peter Msoffe (aliyekaa kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya Uvinza Bw. Masumbuko Kechegwa (aliyekaa kushoto) wakisaini nyaraka za
makabidhiano ambapo NARCO inakabidhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Hekta
6,000 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan kwa wananchi waliovamia Hifadhi ya Ranchi ya Taifa ya Uvinza iliyopo
katika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma ili kumaliza mgogoro wa muda mrefu baina
ya pande hizo. (23.09.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni