Serikali ipo katika mchakato wa kufanya mapitio ya sheria na kanuni zinazo simamia sekta ya uvuvi nchini ili kukuza na kuendeleza viumbe maji ikiwemo ufugaji samaki kwa kutumia vizimba.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Mashimba Ndaki amebainisha hayo September 24,2021 jijini Dodoma wakati
alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya kushiriki mkutano wa
kimataifa wa kukuza na kuendeleza ukuzaji viumbe maji ulifanyika kwa njia ya
video.
Mashimba, alisema lengo la kupitia sheria pamoja na kanuni
katika sekta hiyo ni kuhakikisha kuwa zinawezesha uvuvi wa kutumia vizimba
pamoja na mabwawa.
“Sheria pamoja na kanuni zetu awali sekta hii ya uvuvi ilikuwa
imemezwa na uvuvi wa majini tuu hivyo tunafanya mapitio ili kuwezesha uvuvi huu
wa kutumia vizimba unakuwa na mchango katika kuongeza pato la taifa” alisema
Mashimba.
Akizungumzia mkutano huo alisema lengo lake ni kuwezesha nchi
washiriki kukuza na kuendeleza ukuzaji wa viumbe maji kwa kutumia uvuvi wa
vizimba, mabwawa pamoja na njia nyingene.
“Pia katika mkutano huu tunaangalia changamoto pamoja na fursa
zilizopo, vipaumbele na namna ya kuendeleza uvuvi wa viumbe maji” alisema Ndaki.
Alisema uvuvi huo unamchango mkubwa katika usalama wa chakula
ambapo hivi sasa sekta hiyo inachangia pato la taifa kwa asilimia 1.7.
“Kwenye samaki tunapata protini kwa asilimia 21 na takwimu
zinaonyesha kuwa kuna kipindi tulipanda hadi kufikia mtu mmoja kula kilo 14,
kwa mwaka lakini mwaka 2020, tumeshuka hadi mtu mmoja kula kilo 8.5 kwa mwaka”
alisema
Kutokana na hali hiyo alisema Taifa linatakiwa kuwa na uvuvi
endelevu unaochangia usalama wa chakula na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tumekubalina kuwa na ushirikiano wa namna ya kupeana utaalamu wa kukabiliana na
mabadiliko ya tabia nchi ili kuwa na uvuvi endelevu utakao kuza pato letu
lakini pia pato la dunia kupitia sekta hii” alisisitiza
Vilevie, alisema mkakati wa serikali ni kuhakikisha inafanya
utafiti wa maeneo kwa ajili ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba.
“Ili kuwasaidia watu wanaohitaji kufuga samaki kwa njia hii
serikali inafanya utafiti wa mazingira kwa ajili ya ufugaji ili kuwaondolea
gharama wananchi watakao hitaji kwa kuwa gharama zake ni kubwa” alisema
Kadhalika, alisema mkakati mwingine ni kuhakikisha kuwa vituo
vitano vya ukuzaji viumbe maji vinaboreshwa na kuzalisha vifaranga vya samaki
kwa wingi na vyenye ubora.
“Lakini pia serikali inampango wa kuanzisha mashamba darasa kila
wilaya kwa ajili ya kufundisha wakulima pamoja na wafugaji ufugaji wa samaki
kwa kutumia vizimba na mabwawa” alisema
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) September 24,2021. ofisini kwake iliyopo mji wa serikali Mtumba, jijini Dodoma mara baada ya kushiriki mkutano wa kimataifa wa kukuza na kuendeleza ukuzaji viumbe maji ulifanyika kwa njia ya video.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni