Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki ameagiza maafisa mifugo na madaktari wa mifugo, Wilaya ya
Bariadi Mkoani Simiyu, walioandika au kushuhudia vyeti vya vifo vya ng’ombe
zaidi ya 270 ambao walikamatwa na uongozi wa Pori la Hifadhi la Maswa kusakwa
na kufikishwa katika Baraza la Veterinari Tanzania ili kuchunguzwa.
Waziri Ndaki amebainisha hayo
(16.09.2021) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya za
Itilima na Meatu ambapo akiwa katika Wilaya ya Itilima aliarifiwa baadhi ya
wafugaji walioshinda kesi Mahakama ya Rufaa mwaka 2019, baada ya ng’ombe wao
kudaiwa kuingia katika Pori la Hifadhi la Maswa mwaka 2017, kurejeshewa ng’ombe
51 pekee huku uongozi wa pori hilo ukiwaarifu ng’ombe zaidi ya 270 walikufa,
bila wafugaji hao kushuhudia mizoga ya ng’ombe hao wala vyeti vya vifo ambavyo
inaelezwa viliandikwa na maafisa mifugo ambao pia hawakushudia mizoga hiyo.
Ameongeza kuwa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi kwa sasa inafuatilia taarifa za wafugaji kote nchini, ambao
mifugo yao ilikamatwa na baadaye wafugaji hao kushinda kesi lakini mifugo hiyo
haijareshwa kwao wala fedha walizolipishwa faini, kufuatia agizo la Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kutaka taarifa hiyo
ambayo wizara inakusanya ili kuifikisha kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa
kwa ajili ya maamuzi zaidi.
“Maafisa mifugo na madaktari
wa mifugo nchi nzima mnapaswa kujua nyie ni madaktari wa mifugo siyo kukaa
kwenye meza na kuandika vyeti vya vifo vya ng’ombe bila kushuhudia vifo hivyo,
baadhi yenu wanafanya kazi kiholela.” Amesema Mhe. Ndaki
“Hili jambo siyo dogo ni
kubwa nimeagizwa na Rais nije kufuatilia masuala haya watu wameshinda kesi
lakini ng’ombe hawajarudishwa kwa wenyewe, nimeambiwa nifuatilie nipeleke
orodha yote kwa waziri mkuu ili taarifa itolewe.” Amefafanua Mhe. Ndaki
Kuhusiana na ng’ombe zaidi ya
270 ambao hawajulikani walipo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki
amemjulisha afisa mifugo Mkoa wa Simiyu kwamba wizara inataka kujua aliyeandika
vyeti vya vifo vya ng’ombe hao ambavyo havijulikani vilipo na wala ushahidi wa
kuwa ng’ombe hao walikufa, huku akionya maafisa mifugo na madaktari
watakaobainika kuendelea kufanya kazi bila kufuata taratibu za kazi zao Baraza la
Veterinari Tanzania halitasita kufuta usajili wao.
Aidha, Waziri Ndaki
amewaelekeza wakuu wa Wilaya za Itilima na Meatu kufikia Siku ya Jumanne
(21.09.2021) wawe wamefikisha taarifa rasmi wizarani juu ya idadi ya mifugo
iliyokuwa imekamatwa na kurejeshwa kwa wafugaji, idadi ambayo haijarudishwa
pamoja na majina ya wafugaji ambao wanadai mifugo yao baada ya kushinda kesi
mahakamani kwa madai kuwa mifugo yao iliingia katika Pori la Hifadhi la Maswa.
Katika nyakati tofauti akiwa
katika Wilaya za Itilima na Meatu baadhi ya wafugaji wamelalamikia kitendo cha
baadhi ya maafisa wa serikali, kutoheshimu maamuzi ya mahakama ambapo ndiyo
chombo cha mwisho katika kutoa haki kwani maamuzi yametolewa siku nyingi lakini
baadhi ya wafugaji hawajui hatma ya mifugo yao iliyokamatwa hali iliyosababisha
kuwa na maisha duni.
Pia wamemuomba Waziri Ndaki
kuwa, serikali iangalie namna ya kuwaruhusu wafugaji kuvuna malisho katika
maeneo ya hifadhi badala ya malisho hayo kuchomwa moto ili wafugaji wawe
wanayavuna na kuyatunza kwa ajili ya mifugo yao.
Wamebainisha kuwa wamekuwa
wakipata shida ya malisho kutokana na baadhi ya maeneo kuwa na ukame, hali
ambayo inawapa wakati mgumu kwa mifugo yao kuwa na malisho ya uhakika.
Katika hatua nyingine, Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amewahimiza wafugaji kuiwekea mifugo yao
hereni za kieletroniki ambazo zinatambua mfugo ulipo kuanzia ngazi ya taifa
hadi kijiji hali ambayo itasaidia kuzuia wizi na upotevu wa mifugo.
Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), akizungumza na baadhi ya wafugaji wa
vijiji vya Shishani na Lungalumbogo vilivyopo Kata ya Migato katika Wilaya ya
Itilima Mkoani Simiyu juu ya taarifa ya wafugaji ambao hawajarejeshewa mifugo
yao licha ya kushinda kesi mahakamani kwa madai ya kuingiza mifugo katika Pori
la Hifadhii la Maswa na kuagiza kusakwa kwa maafisa mifugo na madaktari wa
mifugo wa Wilaya ya Bariadi, walioandika au kushuhudia vyeti vya vifo vya
ng’ombe zaidi ya 270 waliokuwa wamekamatwa kwa madai ya kuingia kwenye Hifadhi
ya Pori la Maswa. Waziri Ndaki ameagiza maafisa hao kufikishwa katika Baraza la
Veterinari Tanzania kwa ajili ya uchunguzi zaidi. (16.09.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), (aliyejifunga shuka) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Itilima Mhe. Faiza Sileiman, wakati alipokuwa akiwasili katika vijiji vya Shishani na Lungalumbogo vilivyopo Kata ya Migato na kupokelewa na wafugaji wa kabila la kisukuma waliokuwa wakiimba moja ya nyimbo za kabila hilo kwa ajili ya mapokezi ya Waziri Ndaki alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Simiyu kufuatilia taarifa ya wafugaji ambao hawajarejeshewa mifugo yao licha ya kushinda kesi mahakamani kwa madai ya kuingiza mifugo katika Pori la Hifadhi la Maswa. (16.09.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni