Nav bar

Jumatano, 10 Novemba 2021

BILIONI 50 KUANZISHA UJENZI WA BANDARI YA UVUVI KILWA MASOKO

Serikali imetenge fedha shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ambayo itajengwa Wilayani Kilwa mkoani Lindi.

 

Hayo yamesemwa leo (09.11.2021) na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah wakati wa makabidhiano ya eneo hilo la mradi kwa Mshauri Elekezi wa kampuni ya Sering kutoka nchini Italia, kwa ajili ya kukamilisha kandarasi ya upembuzi yakinifu utaopelekea kujulikana kwa gharama za mradi huo na kutangaza zabuni ya ujenzi wa bandari hiyo.

 

Dkt. Tamatamah amesema kuwa ujenzi wa bandari ya uvuvi ni moja ya mkakati wa serikali katika kuhakikisha inaendelea kukuza sekta ya uvuvi hasa katika kuhamasisha uwekezaji na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi  katika pato la taifa.

 

“Ujenzi huu wa bandari ya uvuvi unakwenda sambamba na ununuzi wa meli mbili (2) kubwa za uvuvi  ambazo zitafanya uvuvi katika bahari kuu   lakini serikali pia inalifufua Shirika la Uvuvi (TAFICO) ambalo ndilo litakalokuwa likisisimamia meli hizo,” alisema Dkt. Tamatamah

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Zainabu Kawawa amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalam watakaofika kwa ajili ya kukamilisha mradi huo na kuhakikisha wanaanza kujipanga kutumia fursa zitakazojitokeza kutokana na uwepo wa mradi huo.

 

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kilwa, Kaimu Shekh Mkuu wa Kilwa, Muhidini Matata ameishukuru serikali kwa kuamua kujenga bandari ya uvuvi wilayani Kilwa kwa kuwa itawaletea manufaa mengi kiuchumi. Lakini pia ameiomba serikali kuendelea kupeleka miradi mbalimbali itakayowasaidia wananchi kunyanyuka kiuchumi.

 

Kwa upande wa Mshauri Elekezi Bw. GABRIEL anayeiwakilisha Kampuni Sering Ingegneria kutoka Italia,anasema wanafuraha kubwa kwa kupata nafasi ya kushiriki katika mradi huu muhimu kwa wakazi wa Kilwa na Tanzania kwa ujumla.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Zainabu Kawawa wakikata utepe kama ishara ya kukabidhi mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kwa mshauri elekezi Kampuni ya Sering Ingegneria kutoka Italia kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu. (09.11.2021)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa wakati alipomtembelea ofisini kwake ambapo alimuelezea mpango ulipo kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi. (09.11.2021)


Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Zainabu Kawawa akizungumza na baadhi ya viongozi na wananchi wa Kilwa Masoko ambao walifika kwenye makabidhiano ya ujenzi wa bandari ya uvuvi kwa Mshauri Elekezi Kampuni ya Sering Ingegneria kwa ajili ya kufanya Upembezi Yakinifu ambapo amewataka viongozi na wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalam watakaofanya kazi hiyo. (09.11.2021)


Baadhi ya viongozi na wataalam kutoka Wizarani, Mkoa na Wilaya ya Kilwa wakitembelea eneo la mradi wa ujenzi wa bandari ya Uvuvi. (09.11.2021)


Baadhi ya viongozi na wataalam wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa kuhusu mradi wa ujenzi wa bandari ya uvuvi katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Maendeleo Kilwa Masoko. (09.11.2021)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni