Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki ameiagiza Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kuendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wafugaji ili wafuge kisasa.
Waziri Ndaki ameyasema hayo
leo (28.10.2021) alipotembelea Kampasi ya Tengeru iliyopo mkoani Arusha kwa
lengo la kufungua bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80
ambalo litasaidia kupunguza changamoto ya miundombinu iliyopo.
“Wafugaji bado wanahitaji kupatiwa
elimu ya ufahamu ili waweze kuelewa faida na hasara za kuendelea na njia ya
ufugaji wa asili na njia bora za ufugaji wa kisasa utakaoweza kuwaletea tija
ambapo kwa kuwatumia wataalam tunaowafundisha na waliopo katika maeneo mbalimbali
tutaweza kubadilisha fikra za wafugaji wetu,” alisema Waziri Ndaki
Pia LITA imetakiwa kusaidia
kutatua changamoto ya malisho kwa wafugaji kwa kutoa elimu juu ya umiliki wa maeneo
na upandaji malisho. Waziri Ndaki amesema kupitia mashamba yao ya malisho
ambayo hutumika kuwafundishia wanafunzi, pia wanaweza kuyatumia mashamba hayo
kama mashamba darasa ambapo wafugaji watapata fursa ya kwenda kujifunza.
Aidha, amewashauri Bodi na
Viongozi wa LITA kuangalia namna ya kutoa elimu ambayo itawasaidia wahitimu wa
vyuo hivyo kwenda kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea kuajiriwa. Hili pia
amewaeleza wanafunzi baada ya kufungua bweni la wasichana kuwa ni lazima wasome
kwa nguvu wakilenga kujiajiri.
Waziri Ndaki ameipongeza Bodi
na Uongozi mzima wa LITA kwa kazi nzuri wanayoifanya ikiwemo ya ujenzi wa
miundombinu kama bweni la wasichana licha ya changamoto walizonazo. Pia amewaahidi
kuwa wizara itaendelea kutenga fedha za maendeleo katika bajeti kwa ajili ya
kuendelea kutatua changamoto walizonazo zikiwemo za miundombinu, mitambo na
vifaa mbalimbali na kwamba wizara itaangalia namna ya kuwasaidia ili kutatua
changamoto ya usafiri kwa kununua basi la chuo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya LITA,
Prof. Malongo Mlozi amesema majukumu ya LITA ni kutoa mafunzo ya muda mrefu
katika ngazi ya Stashahada na Astashahada, kutoa huduma za ushauri na mafunzo
ya muda mfupi kwa wafugaji, maafisa ugani pamoja na wadau wengine katika sekta,
kufanya tafiti na huduma za ushauri ili kujitathmini na kuboresha mafunzo
yanayotolewa na kuzalisha na kutunza aina mbalimbali za mifugo na malisho bora
kwa ajili ya mafunzo na kuhudumia jamii ya watanzania.
Mtendaji Mkuu wa Wakalaya ya
Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo, Dkt. Pius Mwambene amesema wakala imepata mafanikio
mbalimbali ikiwemo ongezeko la udahili kutoka 798 mwaka 2012/13 hadi wanafunzi
3,592 mwaka 2020/21, ongezeko la ufikiaji wafugaji kutoka 267 mwaka 2012/13
hadi 2,104 mwaka 2020/21. Pamoja na mafanikio hayo bado wakala inakabiliwa na changamoto
nyingi zikiwemo za miundombinu, upungufu wa walimu na watumishi wengine, uhaba
wa fedha za maendeleo, usafiri, mitambo, lakini pia baadhi ya wanafunzi
wasaidiwe kupata fursa ya mikopo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akifungua bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 katika Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mkoani Arusha ambapo amewataka wanafunzi hao kutunza miundombinu hiyo vizuri. (28.10.2021)
Mwenyekiti wa Bodi ya LITA,
Prof. Malongo Mlozi (kushoto aliyesimama) akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa
majukumu ya bodi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati
alipotembelea Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mkoani Arusha kwa lengo la kufungua
bweni la wasichana lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 80. Prof. Mlozi amesema moja
ya jukumu walilokuwa nalo ni kuhakikisha kuna kuwa na ongezeko la wanafunzi
hivyo kufunguliwa kwa bweni hilo kutasaidia sana. Taarifa hiyo imesomwa katika
ofisi ya meneja Kampasi ya Tengeru mkoani Arusha. (28.10.2021)
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya
Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene akitoa taarifa ya Wakala
hiyo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipotembelea
Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mkoani Arusha kwa ajili ya kuzindua bweni la
wasichana. Dkt. Mwambene amesema licha ya mafanikio wanayoyapata bado wakala
inakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa miundombinu, mitambo, upungufu wa
walimu na watumishi wengine, uhaba wa fedha za maendeleo, usafiri, mitambo, lakini
pia baadhi ya wanafunzi wasaidiwe kupata fursa ya mikopo. (28.10.2021)
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani (WMUV), Dkt. Angello Mwilawa akitoa maelezo kuhusu aina ya malisho ya mifugo yaliyopandwa katika shamba la chuo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipotembelea moja ya shamba la malisho katika Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru. (28.10.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akipanda mti nje ya bweni la wasichana kwenye Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mara baada ya kulifungua. (28.10.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mara baada ya kufungua bweni la wasichana ambapo amewasihi kusoma kwa bidii huku wakilenga zaidi kwenda kujiajiri mara baada ya kuhitimu masomo yao. (28.10.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni