Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amekitaka kiwanda cha kuzalisha nyavu za kuvulia dagaa cha Ziwa Net kuzalisha nyavu hizo kwa kuzingatia ubora.
Naibu Waziri Ulega ameyasema
hayo leo (25.11.2021) wakati alipotembelea kiwanda hicho kwa lengo la kuona
namna uzalishaji wa nyavu hizo unavyokwenda ambapo uongozi wa kiwanda hicho
umetakiwa kuzingatia ubora katika uzalishaji wa nyavu lakini pia kuhakikisha
wanazalisha nyavu za kutosha ili wavuvi wasipate shida kuzitafuta.
Kwa upande mwingine Naibu
Waziri Ulega amempongeza mwekezaji huyo wa Kiwanda cha Ziwa Net kwa uamuzi wake
wa kujenga kiwanda hicho lakini pia kwa kutoa ajira nyingi kwa wanawake ambapo
kati ya waajiriwa 18 wanaweke ni 15. Vilevile amewasihi kuhakikisha
wanazingatia misingi ya ajira na kuhakikisha hakuna unyanyasaji wa watumishi.
Lakini pia amewashauri kuendelea kuwekeza katika utengenezaji wa nyavu za aina
nyingine zikiwemo za kuvulia samaki pamoja na nyavu maalum za kutengenezea
vizimba vya samaki.
Vilevile amewasihi uongozi wa
kiwanda hicho kuhakikisha wanajitangaza lakini pia kuwaalika wadau kuja kuona
namna nyavu zinavyozalishwa ili pia waweze kutoa maoni yao kuhusu nyavu hizo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu,
Mhe. Salum Kali amesema uwepo wa kiwanda hicho ni muhimu sana kwa wavuvi kwa
kuwa itawarahisishia upatikanaji wa nyavu kwa bei nafuu. Lakini pia itapunguza
uvuvi haramu kwa kuwa wavuvi watakuwa wakitumia nyavu sahihi.
Meneja Masoko wa kiwanda cha
Ziwa Net, Bi. Christina Melkior amesema lengo la kuanzishwa kwa kiwanda hicho
ni kurahisisha upatikanaji wa nyavu za dagaa kwa wavuvi, kukuza na kutangaza
zana bora za uvuvi pamoja na kufungua fursa ya ajira kwa vijana watakao ajiriwa
katika kiwanda hicho. Pia amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha vipande
66 vyenye urefu wa mita 75 na upana wa mita 3.2 kwa siku ambapo uzalishaji kwa
mwezi ni vipande 2000.
Naibu Waziri Ulega pia
ametembelea mwalo wa Ihale kukagua maendeleo ya ujenzi wa mwalo huo na
kuzungumza na wavuvi, Kituo cha kupumzisha Mifugo cha Lamadi wilayani Busega
mkoa wa Simiyu na kiwanda cha kuchakata mabondo cha Pesca Perch wilayani Magu
mkoa wa Mwanza.
Picha ya pamoja ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega na Viongozi na watumishi wa kiwanda cha Ziwa Net kilichopo katika Kijiji cha Kanyama wilayani Magu mkoa wa Mwanza mara baada ya kutembelea kiwanda hicho. (25.11.2021)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akisikiliza maelezo ya namna nyavu za kuvulia dagaa zinavyotengenezwa wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza nyavu cha Ziwa Net kilichopo katika Kijiji cha Kanyama wilayani Magu mkoa wa Mwanza. (25.11.2021)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akikagua ujenzi wa mwalo wa Ihale wilayani Busega mkoa wa Simiyu ambapo amemtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha ujenzi huo kwa wakati. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Gabriel Zacharia na Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Busega, Mhe. Simon Songe. (25.11.2021)
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na wananchi wa Kijiji cha Ihale wilayani
Busega mkoa wa Simiyu mara baada ya kukagua mwalo wa Ihale ambapo amewataka
wananchi kushirikiana na serikali katika kulinda rasilimali za uvuvi.
(25.11.2021)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akikagua miundombinu iliyopo katika Kituo cha kupumzishia Mifugo cha Lamadi wilayani Busega mkoa wa Simiyu ambapo amewaagiza Viongozi kuendelea kulilinda eneo hilo na kwamba uangaliwe uwezekano wa kukiboresha Kituo hicho ili kiweze kufanya kazi kama zamani. (25.11.2021)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiangalia mabondo wakati alipotembelea kiwanda cha kuchakata mabondo cha Pesca Perch kilichopo wilayani Magu mkoa wa Mwanza. (25.11.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni