Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wavuvi kukata bima ya jahazi ili iwasaidie kuwakinga wanapokumbwa na majanga wakati wakitekeleza majukumu yao ya kila siku.
Mhe. Ndaki ameyasema hayo wakati akizindua bima ya Jahazi kwa wavuvi iliyoandaliwa na benki ya NMB kwa kushirikiana na Britam Insurance katika tukio lililofanyika jijini Mwanza Oktoba 31, 2021.
Amesema siku za nyuma bima ilikuwa inawaangalia wavuvi wakubwa pekee na kwamba kwa sasa NMB na Britam wamekuja na aina mpya ya kuwasaidia wavuvi wadogo na wa kati.
"Niwapongeze na kuwashukuru sana benki ya NMB pamoja na washirika wao kuja na hii bima ya jahazi ambayo sasa wavuvi na wote katika Sekta ya Uvuvi wataweza kufanya kazi zao kwa kujiamini kwa kuwa endapo watakumbwa na janga watakuwa na uhakika wa kinga ya vyombo vyao wakitambua kuwa bima ipo na watarejea katika kazi zao," amesema Mhe. Ndaki.
Ameongeza kuwa kwa kutegemea bima kunaongeza kujiamini na kujiamini huko kunaongeza ari ya kufanya kazi zaidi ambapo mwisho wake kunaongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa mtu binafsi na taifa kwa ujumla.
Aidha ametaka wavuvi kuendelea kupewa elimu ya bima ili waijue na kufanya maamuzi kwa kuwa ni njia sahihi ya kuwasaidia katika kipindi chote wanapokuwa katika shughuli zao.
Amesema NMB imedhamiria kuwainua kiuchumi wakulima, wafugaji na sasa ni zamu ya wavuvi na kwamba serikali inatambua mchango wao katika kuhakikisha makundi hayo yananufaika na mikopo inayotolewa na benki hiyo.
Amesema sekta ambazo zilikuwa zinaonekana kuwa na 'risk' kwa sasa zianze kufikiwa na kukatiwa bima kwa kuwa zina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
Waziri Ndaki amesema kuwa sekta ya uvuvi imetoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 202,000 na zaidi ya watanzania milioni 4.5 wameendelea kutegemea kupata kipato chao kupitia Sekta ya uvuvi na kwamba inachangia asilimia 1.7 ya pato la taifa hivyo ni kundi muhimu ambalo linatakiwa kusaidiwa ili liweze kupiga hatua.
Naye Afisa Mkuu wa wateja binafsi na biashara kutoka benki ya NMB, Bw. Filbert Mponzi amesema bima hiyo inawalenga wavuvi wadogo na wa kati hapa nchini na itakuwa bima yenye kusaidia sana wavuvi kama wao binafsi na waliowaajiri lakini pia itahusisha vyombo vyao ambavyo wanatumia wakiwa katika shughuli za Uvuvi.
Amesema wavuvi watakata bima ya asilimia tatu ya chombo husika cha shughuli ya Uvuvi na kwamba wataweza kukingwa na majanga ya ajali, kuungua mitumbwi ama boti, kuvamiwa, kugongwa au kugonga vyombo vingine pamoja na watu watakaokuwa ndani ya vyombo hivyo.
Aidha bima iyo itatoa gharama za matibabu kwa mvuvi pamoja na kulipwa fidia kutokana na ajali yoyote itakayompata atakapokuwa majini kwa ajili ya shughuli za Uvuvi ama kando kando ya ziwa, mto, bwawa na bahari.
Mpozi amewataka wavuvi kufika katika Ofisi za NMB kwa ajili ya kukata bima ambayo itawakinga na majanga mbalimbali wanapokuwa katika shughuli zao za Uvuvi.
Akizungumza katika uzindizi Huo, meneja wa kampuni ya bima ya Britam kanda ya Ziwa, Bw. Said Kadabi amesema bima hiyo itawasaidia wavuvi kuinuka kiuchumi kwa kuwa sasa watafanya kazi zao kwa kujiamini
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), akiongea
na wavuvi, wawakilishi kutoka benki ya NMB na wawakilishi kutoka kampuni
ya Britam Insurance (hawapo pichani) katika hafla ya uzindizi wa Bima ya jahazi
kwa wavuvi na kuwasihi wavuvi kuchangamkia fursa hiyo kwani itaboresha ufanyaji
kazi na kuwaimarisha zaidi. Oktoba 31, 2021 Jijini Mwanza.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) (kushoto)
akishuhudia utiaji saini wa mkataba Kati ya Benki ya NMB na kampuni ya Britam
Insurance leo kwenye uzindizi wa Bima ya jahazi kwa wavuvi Mkoani Mwanza, kulia
ni Mkuu wa Idara ya Bima, Bw. Martine Massawe. Oktoba 31, 2021
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akiwa
kwenye picha ya pamoja na watendaji wa Benki ya NMB, watendaji wa kampuni ya
Britam Insurance, viongozi wa Mkoa wa Mwanza na wadau wa uvuvi mara baada ya
uzindizi wa Bima ya jahazi kwa wavuvi Mkoani humo Oktoba 31, 2021.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni