Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba
Ndaki amekitaka Kitengo cha Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU)
kuhakikisha hadi kufikia Mwezi Agosti Mwaka 2021 kinaweka alama za mipaka
katika maeneo yote ya hifadhi za bahari ili kuondoa migogoro kati yao na
wavuvi.
Akizungumza jana (23.02.2021) na
wananchi katika Kata ya Jibondo iliyopo Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani, Waziri
Ndaki ametaka kuwekwa kwa alama za mipaka hiyo baada ya baadhi ya wananchi
kulalamikia kutozwa faini mara kwa mara kwa tuhuma za kufanya shughuli za uvuvi
kwenye maeneo hayo ambayo hayaruhusiwi kisheria kwa shughuli hizo.
Aidha, Waziri Ndaki akiwa ameambatana
na naibu waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul, amewataka wavuvi kuhakikisha
pindi wanapokamatwa kwa makosa mbalimbali ambayo ni kinyume na sheria ya uvuvi
kuhakikisha wanapatiwa risiti inayotambulika na serikali ya kieletroniki (EFD)
na kuonya watumishi wa serikali wanaopokea fedha za faini bila kutoa risiti
hizo.
“Tuweke mipaka ya hifadhi ieleweke hapa
ndiyo mwanzo na hapa ndiyo mwisho, hadi mwezi wa nane maeneo tengefu yawe na
mipaka yake ya hifadhi ya bahari, pia tushirikishe wananchi na viongozi wao
siyo kuweka tu mipaka, pia kwa mtu anayekutwa na kosa la kwenda kinyume na
sheria ya uvuvi akilipa faini apewe risiti ya serikali ya kieletroniki (EFD).”
Amesema Waziri Ndaki
Pia, waziri huyo ametaka kufanyika kwa
utafiti zaidi ndani ya mwezi mmoja juu ya matumizi ya aina mbalimbali za nyavu
za uvuvi baada ya kupata malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wavuvi ambao
wamekuwa wakilalamikia baadhi ya nyavu ambazo wanatakiwa kuzitumia kisheria kwa
ajili ya uvuvi kutokuwa na sifa ya kukamata mazao ya samaki katika maeneo yao.
Amemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah kuhakikisha
kufikia Tarehe 23 mwezi Machi Mwaka 2021, awe amempatia taarifa hiyo ili iweze
kutoa mwongozo wa maamuzi ya nyavu ambazo zina tija kwa shughuli za uvuvi.
Katika mkutano huo wa hadhara na wananchi
wa Kata ya Jibondo Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Mashimba Ndaki amepiga marufuku kitendo cha baadhi ya maafisa uvuvi kuwakamata
wafanyabiashara wa samaki waliyopo mitaani yakiwemo maeneo ya kuuzia vyakula
kwa madai samaki wanaouzwa katika eneo hilo hawana sifa kisheria badala yake
watafute vyanzo vya maeneo ambayo watu wanavua samaki hao.
“Kuna mambo ambayo sipendi sitaki
kabisa kusikia afisa uvuvi anaenda sokoni kutafuta samaki ambao wapo kinyume
cha sheria na kuwanyanyasa akinamama wanaokaanga samaki, wakiona samaki wa
namna hiyo wanapaswa kuwauliza aliyewauzia ili wapate chanzo halisi cha samaki
walipovuliwa badala ya kumnyanyasa mfanyabiashara ambaye anauza chakula au
kununua samaki anapeleka nyumbani kwa ajili ya mboga.” Amefafanua Waziri Ndaki
Kuhusu kilimo cha zao la mwani Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah
amesema zao hilo limekuwa likilalamikiwa kwa kuuzwa kwa bei ndogo hali ambayo
imekuwa ikiwafanya wakulima hao wasipate mafanikio na kuwataka wakulima
wasiingie mikataba ya kuuza zao la mwani badala yake wauze kwa wafanyabiashara
ambao wanakuwa na bei nzuri yenye tija kwao.
Dkt. Tamatamah amesema wizara
itahakikisha inasimamia zao hilo kwa kuwa limekuwa mkombozi mkubwa kwa
akinamama wengi katika Ukanda wa Pwani pamoja na kuwataka waliongezee thamani
kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo sabuni.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mafia Mhe. Juma Salum Ali amepongeza namna Wizara ya Mifugo na Uvuvi
inavyohakikisha inasimamia maeneo ya hifadhi ya bahari kupitia Kitengo cha
Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) huku akitaka kutatuliwa kwa baadhi
ya changamoto ambazo zinaleta hali ya kitengo hicho kushindwa kushirikiana na
wananchi.
Mhe. Ali amefafanua kuwa baadhi ya
watumishi wa kitengo hicho wamekuwa wakishindwa kufanya kazi kwa kufuata ueledi
wa kazi yao na kuweka maslahi binafsi hali ambayo imekuwa ikizorotesha hali ya
uhifadhi ukizingatia Wilaya ya Mafia bado ina maeneo mengi ambayo yana wingi wa
samaki kwa ajili ya shughuli za uvuvi.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi
waliofika katika mkutano huo wamemuelezea Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Mashimba Ndaki changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo na kuelezea namna
walivyo na imani kubwa na waziri huyo katika kutatua changamoto zao ili waweze
kufanya shughuli za uvuvi bila bughudha na waweze kufuata sheria za nchi.
Aidha, Waziri Ndaki akiwa katika Kata
ya Kilindoni Wilayani Mafia, amezungumza na baadhi ya wavuvi na kuwataka
wafanye shughuli za uvuvi kwa kutumia taa nyakati za usiku wakati Wizara ya
Mifugo na Uvuvi ikiendelea kufanya tafiti ya taa bora zaidi ambazo hazina
madhara wakati wa kuvua samaki.
Mhe. Ndaki amelazimika kutoa ufafanuzi
huo baada ya kulalamikiwa na baadhi ya wavuvi kushindwa kufanya shughuli zao
nyakati za usiku kwa kuzuiwa kutumia taa kama chambo kwa ajili ya kukamatia
samaki.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba
Ndaki amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili katika Wilaya ya Mafia Mkoani
Pwani akiambatana na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul ambapo Waziri Ndaki
amepata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wavuvi na kujionea hifadhi ya bahari
na maeneo tengefu.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya wakazi wa Kata ya Kilindoni
iliyopo Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili
wilayani humo na kutaka wavuvi waendelee na shughuli zao kwa kutumia taa kuvua
samaki nyakati za usiku wakati wizara hiyo ikifanya tafiti zaidi za taa bora
ambazo hazina madhara katika shughuli za uvuvi. (23.02.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akijadiliana jambo na Naibu Waziri Mhe. Pauline
Gekul na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt.
Rashid Tamatamah wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili wilayani humo.
(23.02.2021) Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba
Ndaki (katikati) akijadiliana jambo na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul na
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid
Tamatamah wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili wilayani humo.
(23.02.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akipata maelezo kutoka kwa Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah wakati
wakiwa kwenye boti maalum yenye kioo chini ambayo imewawezesha kujionea maeneo
ya mazalia ya samaki yaliyopo kwenye Bahari ya Hindi, wakati Waziri Ndaki
alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili Wilayani Mafia. Pembeni ya Dkt.
Tamatamah ni Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul. (23.02.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni