Na Mbaraka Kambona,
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba
Ndaki ameiagiza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuwanyang'anya wale wote
walioshindwa kuendeleza vitalu walivyokodishwa
katika ranchi za kampuni hiyo kwa sababu wamekiuka masharti ya mkataba.
Ndaki alitoa agizo hilo alipokutana na
Viongozi wa Chama cha Wafugaji katika kikao cha kujadili Maendeleo ya Sekta ya
Mifugo kilichofanyika jijiji Dodoma Februari 10, 2021.
Alisema kuwa kuna watu wengi
wamekodishwa maeneo katika ranchi za taifa lakini wamezitelekeza na wengine
wamekodisha watu wengine ambao wanatumia maeneo hayo kinyume na makubaliano ya
mkataba.
"Ikifika tarehe 15 mwezi huu, wale
wote waliochukua vitalu na wamekodisha watu wengine wanyang'anywe maeneo hayo
na hatutajali mikataba yao kwani wameshakiuka masharti," alisema Ndaki
Aliongeza kwa kusema kuwa baada ya tarehe
15 kupita wataanza kuwasaka wote waliochukua maeneo hayo na kuwanyang'anya ili
wapewe wafugaji makini waweze kutumia maeneo hayo kuweka mifugo yao.
Kuhusu baadhi ya Wananchi wanaoishi
karibu na ranchi kuvamia maeneo hayo, Ndaki alitumia nafasi hiyo pia kuwataka
waondoke katika maeneo hayo na wasipofanya hivyo wataondolewa.
Aliendelea kusema kuwa wameanza
mikakati ya kuiweka vizuri NARCO ili maeneo makubwa iliyonayo ambayo mengine
hawayatumii vizuri yagawiwe kwa wafugaji watakaoweza kuyatumia kufanya ufugaji
wa kisasa nah atua waliyoanza nayo ni kupunguza bei ya kukodisha vitalu.
"Tumekubaliana kuwa bei ya
kukodisha kitalu iwe ni shilingi elfu tatu mia tano (3500) kwa Ekari moja na
sio zaidi ya hapo," alisema Ndaki
Waziri Ndaki alisema kuwa wameielekeza
NARCO kuwa katika yale maeneo waliyoyatenga kwa ajili ya ukodishaji watenge
asilimia thelathini (30) kwa ajili ya kuwakodisha wafugaji wanaoishi karibu na
maeneo ya ranchi hizo ili kupunguza migogoro na uvamizi wa maeneo hayo.
"Hata maeneo yetu yaliyotengwa kwa
ajili ya kupumzishia mifugo (holding grounds) tutayapunguza ili nayo tuwape
NARCO ili wayakodishe kwa wafugaji wetu, tunaamua kufanya haya ili kutibu
tatizo la malisho na wafugaji waondokane na kutangatanga," alifafanua
Ndaki
Mapema wiki hii Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya NARCO, Paul Kimiti alitangaza kuwa ekari moja ya kitalu katika
ranchi hizo itakodishwa kwa shilingi elfu tatu mia tano (3500).
Katibu Tawala, Mkoa wa
Kagera, Prof. Faustin Kamuzora (wa kwanza kulia) akimueleza jambo Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (wakwanza kushoto) walipokutana katika kikao
cha kujadili Maendeleo ya Sekta ya Mifugo kilichofanyika jijini Dodoma Februari
10, 2021. Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo),
Prof. Elisante Ole Gabriel na wa pili kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha
Wafugaji Tanzania, Jeremiah Wambura.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akifafanua jambo kwa baadhi ya wafugaji waliohudhuria kikao cha kujadili Maendeleo ya Sekta ya Mifugo kilichofanyika jijiji Dodoma Februari 10, 2021.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akiteta jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro walipokutana katika kikao cha kujadili Maendeleo ya Sekta ya Mifugo kilichofanyika jijini Dodoma Februari 10, 2021.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni