Na Mbaraka Kambona, Pwani
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Pauline Gekul amemsimamisha kazi Mkuu wa Kituo cha Ukaguzi wa Mifugo cha Ruvu
Darajani, Gabriel Lyakurwa kwa tuhuma za kutorosha mifugo na kusababisha
upotevu wa mapato ya Serikali, huku akimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi,
Evarist Ndikilo kuwachukulia hatua Watumishi waliochini ya Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ambao walikuwa wanashirikiana na Mkuu huyo wa
kituo.
Gekul alitoa maamuzi hayo baada ya Mkuu
huyo wa Mkoa wa Pwani kuibua tuhuma hizo katika ziara yake aliyoifanya kwenye
kituo hicho kilichopo Ruvu Darajani, Wilayani Bagamoyo Februari 24, 2021.
Mhandisi Ndikilo alisema uchunguzi
alioufanya umebaini kuwa Mkuu wa kituo hicho amekuwa akishirikiana na wenzake
wasiowaaminifu kutorosha mifugo inayopelekwa katika kituo hicho kwa ajili ya
kukaguliwa kabla ya kuruhusiwa kupelekwa katika maeneo mengine ya minada.
“Mhe. Naibu Waziri nimefanya uchunguzi
wa kina na kugundua kuwa utoroshaji huu unahusisha mtandao wa watu wengi
wakiwemo baadhi ya Wananchi, Wafanyabiashara na Watumishi wa Serikali…, kwa
mfano tarehe 17 mwezi huu wa pili kuna Magari matano yalileta ng’ombe katika
kituo hiki kwa ajili ya kukaguliwa lakini ni gari moja tu lililokwenda Dar es
Salaam kama kawaida ilivyo, huku mengine yaliyobaki yakichepushwa na mifugo
ilipelekwa Kisarawe, Kibaha na Kijiji cha Kidogozero kinyemela,” alisema
Mhandisi Ndikilo
Kufuatia tuhuma hizo, Naibu Waziri
Gekul alitoa maagizo hayo ya kusimamishwa kazi mkuu huyo wa kituo huku akisema
kuwa Wizara itaunda tume maalum kwa ajili ya kwenda kuchunguza tuhuma hizo
ikiwemo kupitia mahesabu yote ili kubaini ni kwa kiasi gani mapato ya Serikali
yamepotea na wale wote watakaoonekana kuhusika katika upotevu huo watachukuliwa
hatua kali.
"Hatuwezi kucheza na maduhuli ya
Serikali, haiwezekani tuwe na ng’ombe zaidi ya milioni 33 lakini mchango wa
sekta ya mifugo katika pato la taifa hauzidi asilimia 7, ni kwa sababu ya
michezo kama hii, hatutakubali, na tutakwenda kukagua katika maeneo yote ya
minada," alisema Gekul
Naye, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani
Kikwete alisema kuwa katika jambo ambalo wamekuwa wakilisemea sana ni kituo
hicho kukithiri kwa vitendo vya ubadhilifu ambavyo vimekuwa vikichangia
Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kupoteza mapato.
Ridhiwani alimuomba Naibu Waziri huyo
kuhakikisha anachukua hatua madhubuti za kudhibiti vitendo hivyo vya ubadhirifu
ikiwemo kuondoa mtandao wote wa waharifu ili halmashauri iweze kupata mapato
yanayostahili.
Msimamizi wa Ujenzi wa Bwawa la Kunyweshea Mifugo la
Chamakweza, Robert Baltazar akimuonesha michoro ya bwawa hilo, Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (wa kwanza kulia) alipotembelea kukagua
maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo lililopo Chalinze, Wilayani Bagamoyo, Mkoani
Pwani Februari 24, 2021. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
Mhandisi, Evarist Ndikilo.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara
ya Uendelezaji Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Rogers Shengoto
akijibu moja ya hoja ziliyoibuliwa katika ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Pauline Gekul aliyoifanya Mkoani Pwani Februari 24, 2021.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Pauline Gekul akijadiliana jambo na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi
Evarist Ndikilo (kushoto) na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (kulia)
alipofanya ziara kukagua Kituo cha Ukaguzi wa Mifugo cha Ruvu Darajani kilichopo
Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani Februari 24, 2021.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni