Nav bar

Jumapili, 7 Machi 2021

WANANCHI WAONDOLEWA HOFU VIFO VYA SAMAKI ZIWA VICTORIA

 

Na Elibariki Mafole, MWANZA

  

WANANCHI wametakiwa kutokuwa na hofu kutokana na vifo vya samaki katika Ziwa Victoria baada ya sampuli zilizopimwa kuonesha kuwa samaki hao Hhawana na sumu.

 

Hayo yalibainishwa na Katibu Mkuu wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk. Rashid Tamatamah alipozungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza na kueleza kuwa mara baada ya taarifa ya uwepo wa vifo vya samaki katika Ziwa Victoria maabara ya ubora wa samaki kwa kusaidiana na taasisi ya uvuvi Tanzania TAFIRI walichukua sampuli zaidi ya 7 kwa ajili ya vipimo na katika hizo hakuna sampuli hata moja iliyobainika kuwa na sumu.                          

 

“Tarehe 15 Januari nilieleza hapa uwepo wa vifo vya samaki katika Ziwa Victoria upande wa Uganda na mara baada kuona taarifa ile tulifanyia kazi kwa kuchukua sampuli zaidi ya saba na kuifanyia vipimo, kati ya hizo hakuna hata moja iliyoonesha kuwa na sumu” alisema Dk. Tamatamah

 

Dk. Tamatamah alisema vifo vya samaki hao vimetokana na mzunguko wa maji katika tabaka la juu na chini kwa vipindi vya mwaka hasa mwezi Julai, Agosti, na Septemba kwa sababu ya hali ya hewa na kuwataka wananchi kutowatumia kama kitoweo samaki hao waliokufa ziwani.

 

Tamatamah alisema tukio la samaki kufa katika ziwa Victoria hutokana na mzunguko wa majira ya mwaka na kwamba samaki aina ya Sangara huishi katika maji ya tabaka la kati na juu ambalo lina hewa ya kutosha ya oksijeni hivyo wanapokosa hewa hukumbwa na kadhia nyingi ikiwemo vifo hasa kwa samaki wakubwa.  

 

Kwa mujibu wa Dk Tamatamah Januari 2 mwaka 2021 walionekana samaki waliokufa katika maeneo ya Masonga-Sota Tarime, Nyamikoma Busega, Geita, pamoja na visiwa vya Misenyi Bukoba.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tatizo la vifo vya samaki aina ya sangara kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. (05.03.2021)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni