Na Elibariki Mafole, MWANZA
WANANCHI wametakiwa kushirikiana katika
suala la kudhibiti uvuvi haramu Ziwa Victoria ili kuendelea kunufaika na
rasilimali za uvuvi.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mashimba Ndaki, katika kikao cha wadau wa Uvuvi kanda ya Ziwa kilichojadili
kuhusu ulinzi na usimamizi wa rasilimali za Uvuvi na kusema suala la
udhibiti wa uvuvi haramu katika mwambao huo ni la kila mmoja.
Mashimba alisema suala la ulinzi wa rasilimali
zilizopo ziwani ni jukumu la kila mmoja katika ngazi zote kuanzia kitongoji
mpaka wilaya hadi wizarani na si jukumu la askari kudhibiti uvuvi haramu.
“Ikiwa uvuvi haramu tutaukumbatia
wenyewe mtajiangamiza wenyewe, ninyi mnaofaidika na ziwa mpo, na athari mnaiona
kwanini waje maaskari kutoka Dodoma au sehemu nyingine kuja kufanya msako
kwenu, ndugu zangu naomba tushirikiane wote, ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Kata
wote hili ni jukumu letu suala la uvuvi haramu halikubaliki,” alisema Ndaki.
Ndaki alisema ipo dhana
inazungumzwa kuwa uvuvi haramu ni dhana tu inayojengwa na wataalamu na serikali
na kuna dhana nyingine kuwa samaki wapo tu ziwani na kuongeza kuwa ikiwa uvuvi
haramu tutaukumbatia tutajiangamiza wenyewe.
“Kuna dhana kuwa uvuvi haramu ni dhana tu
inayojengwa nawataalam na serikali , kwamba uvuvi haramu hamna, na dhana hiyo
inasema kuwa samaki wapo ziwa litaenda wapi, lakini ninyi wenyewe ni mashahidi,
kuna wakati mmeanza kulia ninyi wenyewe kwamba samaki hawapo, mpaka sasa
upungufu upo sasa kwanini isiwaume ninyi imuume zaidi waziri au Katibu Mkuu wa
Uvuvi ambaye nyumbani kwao ni Mtwara bahari pana kuliko ziwa letu, kwanini
lisituume sisi,” alisema Ndaki.
Mwenyekiti wa kikundi cha usimamizi
shirikishi wa rasilimali za uvuvi (BMU) Wilaya ya Rorya Stephano Mchoye alisema
halmashauri ishirikiane na vikundi hivyo ili kudhibiti uvuvi haramu kwa manufaa
ya vizazi vilivyopo na vizazi vijavyo.
Ulinzi shirikishi katika ziwa letu
haujaanza leo, ninaomba Wizara iangalie zana hizi zinazotumika tika uvuvi
haramu zinatoka wapi dawa ya hiyo ikishapatikana naamini uvuvi haramu Tanzania
hautapatikana.
Kwa upande wake Nadhil Sadick msambazaji wa
mazao ya samaki nje ya nchi aliomba serikali kuangalia tozo mbalimbali
wanazotozwa pasipokuangalia madhara yake kwa wanaotoza pamoja na wale
wanaotozwa.
Mashimba amewaagiza halmashauri pamoja na
mabaraza ya madiwani kuangalia upya tozo wanazotoza katika mialo na katika
rasilimali mbalimbali za uvuvi ili kuwapunguzia mzigo wavuvi.
“Niombe halmashauri pamoja na mabaraza yenu
ya madiwani hebu kaangalieni upya tozo mnazowatoza kwenye mialo na mazao
mbalimbali ya uvuvi, mkaangalie upya tuone tutakapowapunguzia, tuwapunguzie
mzigo kwenye hayo maeneo tunayotoka,” alisema Mhe. Ndaki.
“Mimi ni shahidi nimeenda kule Geita tozo
za kwetu ngazi ya wizara kwa upande wa dagaa ni mbili tu royality na leseni,
lakini zipo tozo 8 ambazo halmashauri inatoza, jumla tozo 10 anatozwa mtu mmoja
halmashauri tuangalie pia ustawi wa watu wetu, anaondoka na nini kwenye hicho
tunachotaka kumtoza vinginevyo mtapunguza mapato yeye ninyi wenyewe,” alisema Mhe.
Ndaki.
Baadhi ya viongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na viongozi wa serikali wa Kanda ya Ziwa Victoria wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi (aliyesimama) wakati wa mkutano kuhusu ulinzi na usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. (05.03.2021)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (wa kwanza kulia) akiwa na timu ya wataalam wakati wa kuandaa maazimio ya mkutano wa viongozi wa serikali wa mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria kuhusu ulinzi na usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. (05.03.2021)
Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (aliyekaa katikati), Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah (aliyekaa kulia kwake) na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Viongozi wengine baada ya kumaliza mkutano wa wadau wa sekta ya uvuvi uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. (06.03.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni