Na Mbaraka Kambona, Pwani
Mratibu na Mkurugenzi wa Operesheni,
Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Tina Towo Sokoine amesema kuwa lengo
la kiwanda hicho ni kutumia Wataalam wa ndani lakini uhaba wa Wataalam wa
masuala ya sayansi wenye ujuzi hasa wa vitendo unaelekea kukwamisha dhamira yao hiyo.
Towo aliyasema hayo alipokuwa akitoa
taarifa ya utekelezaji wa kiwanda hicho kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel alipotembelea kiwanda hicho
kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Februari 13, 2021.
Alisema kuwa kwa sasa wana wataalamu
watatu tu kutoka nje ya nchi ambao wamewaajiri katika Kiwanda hicho lakini kwa hali ilivyo wanaona watashindwa na labda
wanaweza kuomba vibali vingine vya kuajiri wataalamu kutoka nje.
“Nia yetu ni kufanyakazi na Watanzania
tu lakini bado vijana wengi tunaowafanyia usahili wanakosa ujuzi hasa wa
vitendo, tunaiomba Serikali na Vyuo vinavyoandaa hawa Wataalam kuhakikisha
wanajikita katika elimu ya vitendo na sio nadharia peke yake ili kukidhi
mahitaji ya sasa na kulinda ajira za Watanzania,” alisema Towo
Kuhusu uzalishaji, Towo alisema kuwa
wanatarajia kuzalisha chanjo ya kwanza mwezi wa nne mwaka huu, huku akiiomba Serikali
kuona uwezekano wa taasisi zinazohusika na kusimamia uwekezaji kuunganishwa
ziwe na lugha ya pamoja ili kumfanya muwekezaji aweze kupata huduma zote sehemu
moja bila kuhangaika kama ilivyosasa.
Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel aliutaka Uongozi wa Kiwanda hicho
kuhakikisha wanazalisha chanjo zenye ubora ili nchi iweze kuondokana na
utegemezi wa chanjo na bidhaa nyingine za mifugo kutoka nchi za nje.
“Lengo la Wizara ni kuhakikisha kuwa
nchi inaondokana na uagizaji wa chanjo kutoka nje, tunatamani kuwa na chanjo
tunazoweza kudhibiti ubora wake na tuwe na uhakika nayo, hivyo uwepo wa kiwanda
hiki kutatusaidia kuzalisha chanjo hapa hapa nchini ili kukidhi mahitaji ya
Wafugaji wetu na Watanzania kwa ujumla,” alisema Prof. Ole Gabriel
Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali
inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili mahitaji ya wafugaji na wananchi yawe
yanashughulikiwa ndani ya nchi.
Aidha, Prof. Ole Gabriel aliwaomba
Wafugaji na Watanzania kuanza kujenga utamaduni wa kuthamini bidhaa za ndani na
waondokane na ile dhana ya kwamba bidhaa bora ni ile inayotoka nje, wakithamini
vya ndani wataongeza pato la Taifa na kukuza uchumi wa nchi.
Katibu Mkuu, Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akibadilishana
mawazo na Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Dkt. Umapati Dasgupta (kushoto) muda mfupi
baada ya kumaliza kutembelea kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani
Pwani Februari 13, 2021.
Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza
Chanjo cha Hester, Dkt. Umapati Dasgupta (kulia) akimueleza jambo Katibu Mkuu,
Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto)
alipotembelea kukagua kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani
Februari 13, 2021.
Mtaalam wa Kuendesha
Mitambo katika Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Geofrey Mahende
(kulia) akitoa maelezo ya namna anavyofanyakazi yake kwa Katibu Mkuu, Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) alipotembelea
kukagua kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Februari 13,
2021.
Katibu Mkuu, Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika
picha ya pamoja na Wataalam wa Kitanzania wanaofanyakazi katika Kiwanda cha
kutengeneza Chanjo cha Hester alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Mkoani
Pwani Februari 13, 2021. Wa kwanza kushoto ni Mratibu na Mkurugenzi wa
Operesheni, Tina Towo Sokoine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni