Nav bar

Jumanne, 24 Mei 2022

SERIKALI YAFICHUA ILIVYOPATA MWAROBAINI WA MAGONJWA YA MIFUGO NA MASOKO.

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka wazi namna ilivyofanikiwa kupata suluhu ya changamoto ya ukosefu wa masoko ya mazao ya Mifugo na uhaba wa chanjo za magonjwa mbalimbali ya Mifugo.


Hayo yamebainishwa leo (20.05.2022)  na Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia afya ya jamii ya veterinari, udhibiti wa pembejeo, mifugo na mazao yake kutoka Wizarani hapo ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu (Mifugo)  Dkt. Stanford Ndibalema wakati wa hotuba yake ya kufunga mafunzo ya Siku 3 ya mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi unaojulikana kama “ Mifugo Management Information System (MIMIS)”  kwa wataalam na wadau waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya Mifugo na Uvuvi yaliyokuwa yaliyofanyika kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.


Dkt. Ndibalema amesema kuwa mara baada ya kukamilika kwa Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika nchi za falme za kiarabu, Wizara yake ilipokea wakaguzi ambao walifika katika Viwanda vya kusindika nyama vilivyopo hapa nchini ikiwa ni pamoja na kiwanda cha Chobo kilichopo mkoani Mwanza, Elia kilichopo mkoani Arusha na Tanchoice kilichopo mkoani Pwani.


“Baada ya ukaguzi ule walikubali kuanza kuagiza nyama kutoka Kiwanda cha Tanchoice na Elia na kutoa maoni kadhaa ya kuboresha kwa viwanda vingine ambapo maoni hayo yameshaanza kufanyiwa kazi”  Amesema Dkt. Ndibalema.


Mbali na uwepo wa soko katika nchi za Jamhuri ya falme za kiarabu, Dkt. Ndibalema amesema kuwa tayari nchi za  China, Qatar na Oman zimeshafungua soko la nyama inayozalishwa hapa nchini na wafanyabiashara wa zao hilo wameshaanza kunufaika na fursa hiyo.


Akizungumzia kuhusu hali ya upatikanaji wa kinga  za magonjwa mbalimbali ya Mifugo Dkt. Ndibalema ameeleza kuwa hivi sasa idadi ya  vifo vya mifugo  vinavyotokana na kupe imepungua kwa kiasi kikubwa hasa baada ya Serikali kuanza kutoa bure dawa za kuogeshea mifugo hiyo.


“Sasa kazi iliyobaki ni kwa Halmashauri na kamati za majosho kuhakikisha dawa zote zinazotolewa na Serikali zinaelekezwa kwenye majosho kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji kukinga mifugo yao” Ameongeza Dkt. Ndibalema.


Dkt. Ndibalema amebainisha kuwa hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali katika kulinda afya ya mifugo ni kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa kampuni kutoka nchini India ambayo imejenga kiwanda kikubwa cha kutengeneza chanjo mbalimbali za mifugo kinachojulikana kama “Heister” kilichopo Kibaha mkoani Pwani.


“Kwa sasa Kiwanda hicho kinatengeneza chanjo 3 ambazo ni ile ya homa ya mapafu ya ng’ombe, homa ya mapafu ya mbuzi na chanjo ya Sotoka ya mbuzi na kondoo na kwa kwa Serikali yetu ni sikivu inapokea maoni ya kuboresha eneo lolote ambalo mfugaji au mdau wetu yoyote anadhani linapaswa kurekebishwa” Amesema Dkt. Ndibalema.


Wakizungumzia matarajio yao baada ya kuanza kutumia mfumo huo, baadhi ya wadau walioshiriki mafunzo hayo wamesema kuwa mfumo huo utawasaidia kurahisisha kazi zao, kuongeza faida kwenye biashara zao za mazao ya mifugo na kuokoa muda ambao watautumia kufanya shughuli nyingine za maendeleo.


Mafunzo hayo ya Siku 3 yamelenga kuongeza ufanisi wa biashara ya mazao yanayotokana na mifugo na vyakula samaki na utekelezaji wa mfumo huo unatarajiwa kuanza mapema mwezi juni mwaka huu.


Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi  (Mifugo) ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia afya ya jamii ya veterinari, udhibiti wa pembejeo, mifugo na mazao yake kutoka Wizarani hapo Dkt. Stanford Ndibalema akieleza jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya ufugaji nchini wakati wa hotuba yake ya kufunga mafunzo ya Siku 3 ya mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi  kwa wataalam na wadau waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya Mifugo na Uvuvi yaliyokuwa yaliyofanyika kwa siku 3  (Mei 18-20, 2022)  kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.


Baadhi wa washiriki wa mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi wakimsikiliza Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi  (Mifugo) Dkt. Stanford Ndibalema (hayupo pichani)  wakati wa hotuba yake ya kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku 3 (Mei 18-20, 2022) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni