Nav bar

Jumanne, 24 Mei 2022

MIRADI YA MAENDELEO MKURANGA IPO KATIKA HATUA NZURI - NZUNDA

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda jana tarehe 20 Mei 2022 alifanya ziara ya kukagua miradi ya Maendeleo inayotekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Mkoani Pwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga na kuridhishwa na kiwango cha utekelezaji wa miradi hiyo mbali ya mapungufu madogomadogo aliyoelekeza kurekebishwa mara moja kabla ya kukamilisha miradi hiyo 30 Mei 2022 .


"Nakupongeza kwa kazi nzuri unayoendelea kufanya pamoja na kwamba ulipatwa na changamoto ya ajali lakini unaendela vizuri na utekelezaji wa mradi huu."

Alisema Nzunda alipokuwa anakagua ujenzi wa kisima katika kijiji cha Matanzi.


Miradi inayotekelezwa Katika Halmashauri ya Mkuranga inayosimamiwa Moja kwa moja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) ni pamoja na ujenzi wa Mnada wa Kisasa wa upili unaojengwa katika kijiji cha Chamgoi wenye thamani ya Tsh. 

300, 274, 584.09 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 45.75.


Aidha, mradi mwingine alioutembelea Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo ni ujenzi wa kisima kirefu cha kunyweshea Mifugo Maji, kisima hicho kinajengwa katika Kijiji cha Matanzi ambapo gharama za ujenzi ni Tsh. 162,309,590.00 ambapo ujenzi wa kisima hicho umefika asilimia 80. 


Vile vile katika Kijiji cha Tundu, Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga  linajengwa Josho lenye thamani ya Tsh.29, 719,500.00 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 70.


Pamoja na kuendelea Vizuri kwa utekelezaji wa Miradi hiyo ya Maendeleo Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Nzunda ameelekeza wakandarasi hao kufanya kazi usiku na mchana ili ifikapo tarehe 30/05/2022  wawe wamemaliza utekelezaji wa Miradi hiyo,vinginevyo kuanzia tarehe 01/06/2022 kama watakuwa hawajamaliza miradi hiyo,wakandarasi hao wataanza kukatwa "LIQUIDATION"kulingana na makubaliano ya Mkataba.


"Fanyeni kazi usiku na mchana,maana siwezi kuwaongezea Muda wa ziada wa utekelezaji wa Miradi hii, ikifika tarehe 01/06/2022 kama mtakuwa hamjakamilisha utekelezaji wa miradi hii nitaanza kuwataka Liquidation". Alisema Nzunda.


Aidha, Nzunda ameelekeza halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kusimamia miradi hiyo ya Maendeleo kwa ukaribu  na kutoa fikra potofu kuwa miradi hiyo ni ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwani wanufaika wa Miradi hiyo ni wananchi wa maeneo husika.


"Simamieni Miradi hii na kuhakikisha kuwa inatekelezwa kwa kiwango kilichokusudiwa  na inakamirika kwa wakati na kwa muda uliopangwa ili wananchi hawa waweza kupata huduma kwa wakati".Alisema Nzunda.


Nzunda alisema kuwa kwa sasa Wizara imeandaa mpango mkakati wa Mabadiliko ya Sekta ya Mifugo ambapo mpango huo utaanza utekelezaji wake mwaka wa fedha 2022/2023, maeneo Muhimu yaliyotiliwa Mkazo katika mpango Mkakati huo ni pamoja na uzalishaji wa Mifugo ya kisasa na yenye tija, uhamasishaji wa uzalizaji wa Malisho, uchimaji wa Malambo na Visima Virefu vya maji kwa kushirikiana na Sekta binafsi.


Aidha, Maeneo mengine yatakayotiliwa mkazo pia ni maeneo ya Utafiti wa mbari za Mifugo, huduma za ugani kwa Sekta ya Mifugo, Masoko pamoja na maeneo yote ya Ranchi za Taifa NARCO ambayo hayatumiki pamoja na holding Ground kuyatafutia namna bora ya kuweza kukodisha kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili yaweza kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Bi. Anna Kiria alimshukuru Katibu Mkuu Mifugo kwa uamuzi wa kupeleka Miradi hiyo ya maendeleo katika Wilaya hiyo, alisema kuwa miradi hiyo itaboresha Ustawi wa Sekta ya Mifugo na Mazao yake pamoja na kurahisisha biashara ya Mifugo.


Vilevile Kiria alisema kuwa changamoto kubwa iliyopekekea kuchelewa kukamilika kwa Miradi hiyo ni pamoja na barabara kutopitika kipindi cha mvua na kupelekea kushindwa kwa mkandarasi kupeleka vifaa vya ujenzi eneo la mradi.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo)Bw.Tixon Nzunda (Kushoto) akisikiliza maelezo ya ujenzi wa Mradi wa kisima kutoka kwa mkandarasi  Bw.Buddy Muhammed (aliyesimama Kulia) unaojengwa katika kijiji cha Matanzi Wilayani Mkuranga.Wengine katika Picha ni kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mkuranga pamoja na wananchi wa kijiji cha Matanzi.


Hiyo ni Miundombinu ya Mabirika ya Kunyweshea maji Mifugo katika kisima cha matanzi kilichopo Wilayani Mkuranga mkoani Pwani.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda akizungumza na Wananchi waliojitokeza katika mnada wa Upili wa Chamgoi jana tarehe 20/05/2022 Mkuranga alipofanya ziara katika Wilaya hiyo. Lengo la ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayosimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo)


Mwonekano wa Kisima cha kunyweshea Mifugo maji katika kijiji cha  Matanzi Wilayani Mkuranga.Lengo la utekelezaji wa Mradi huu wa Kisima ni kusogeza huduma karibu kwa Wafugaji na wananchi wa maeneo husika.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda akiwasili Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga na kupokelewa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo jana tarehe 20/05/2022.Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Bi.Veronica Kinyemi.


Baadhi ya Miundombinu inayojengwa katika mnada wa Upili wa Chamgoi katika halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni