Wizara ya Mifugo na Uvuvi, sekta ya uvuvi imeahidi kuanza kufanya mafunzo mbalimbali kwa waelimisha rika ambao watakuwa kiungo muhimu katika kutekeleza jitihada za kutokomeza Ukimwi, MSY na homa ya Ini mahala pa kazi.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alipokuwa akizindua kamati ya VVU, Ukimwi na magonjwa sugu yasiyoambukizwa(MSY) mahali pa kazi, tukio hilo limefanyika leo (20.05.2022) kwenye ukumbi wa ofisi za wizara NBC, Dodoma.
" Sote tunafahamu kuwa Afya ya watumishi ndio msingi mkuu wa uendeshaji wa Taasisi yeyote. Hivyo, suala la afua za UKIMWI na MSY Mahali pa kazi lisipopewa kipaumbele, Utumishi wa umma unaweza kujikuta unapoteza nguvu kazi kutokana na magonjwa na vifo", amesema Dkt. Tamatamah.
Dkt. Tamatamah ameishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora (OR-MUUUB), Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambao wameshirikiana na wizara kuwezesha kufanyika kwa uzinduzi huo.
Aidha, Dkt. Tamatamah amesema kutokana na umuhimu wa ustawi wa watumishi, Wizara imeona ni vema ikaendelea na jitihada za kujenga uelewa juu ya maambukizi na udhibiti VVU, UKIMWI, MSY na homa ya ini ili kuhakikisha hali ya uelewa wa kina miongoni mwa watumishi inaongezeka.
Pia, Dkt. Tamatamah amemalizia kwa kusema ratiba ya majukumu iliyopo itazingatiwa ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa watumishi wote wa wizara, kuhamasisha upimaji wa VVU, MSY na homa ya ini na kuanza chanjo ya homa ya ini pamoja na kuendeleza Jogging Club, Utaratibu wa Basi darasa na Mazoezi ya viungo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni