Nav bar

Jumanne, 24 Mei 2022

SERIKALI YAWATANGAZIA VITA WAVUVI HARAMU

Na Mbaraka Kambona, Mwanza


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema serikali sasa itawekeza nguvu kubwa kukomesha uvuvi haramu katika ziwa viktoria baada ya hatua kadhaa zilizochukuliwa hapo awali ikiwemo kuwashirikisha wavuvi wa kanda ya ziwa kutokuzaa matunda.


Ndaki alitoa kauli hiyo alipokuwa akiongea na wadau wa sekta ya uvuvi katika kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo wavuvi wanaofanya shughuli zao katika ziwa Viktoria kilichofanyika Mkoani Mwanza Mei 16, 2022.


Alisema mwaka jana serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya uvuvi waliandaa mpango shirikishi ambao ulianisha kila mdau na jukumu lake katika ulinzi wa rasilimali za uvuvi katika ziwa viktoria lakini matokeo yake wadau hao hawakujali na sasa uvuvi haramu umeongezeka maradufu.


“Uvuvi haramu sasa hivi ni mkubwa kwenye ukanda wetu wa ziwa viktoria, na sisi wizara tumepewa jukumu la kusimamia rasilimali hizi, Mhe. Rais atatushangaa sana kuona wizara iliyopewa dhamana ya kuhakikisha rasilimali hizi zinalindwa, hazilindwi, sasa wakati tunatafuta mbinu endelevu ya kulinda rasilimali hizi, kuanzia sasa kwenda mbele tutatumia nguvu kuzuia uvuvi haramu”, alisema


Aliongeza kwa kusema kuwa serikali haitavumilia watu wachache wenye kutaka kujinufaisha wao binafsi  huku akiongeza kuwa watawashughulikia wale wote wanaojihusisha na uvuvi haramu kuanzia wavuvi, wasambazaji wa nyavu zisizo halali, na watakamata vyombo vyote vitakavyotumika kubebea au kuhifadhi mazao yaliyovuliwa kwa njia ya haramu katika mikoa yote inayozunguka ukanda wa ziwa viktoria.


Aidha, Waziri Ndaki aliwaeleza wadau wa uvuvi katika kikao hicho kuwa serikali imepokea changamoto zao na watazifanyika kazi lakini nguvu kubwa kwa sasa itawekwa katika kupambana na uvuvi haramu kwa sababu kama rasilimali za uvuvi zikitoweka hizo changamoto nyingine kama za tozo na utafutaji wa masoko hazitakuwa na maana yoyote.


Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia sekta ya uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa serikali imesikiliza kilio cha wavuvi kuhusu tozo na imezishughulikia kwa kiasi kikubwa na hivi karibuni michakato ikikamilika serikali itatoa maelekezo ambayo anaamini yatakuwa na nafuu kubwa kwa wavuvi.


Changamoto kubwa zilizowasilishwa na wadau wa sekta ya uvuvi kwa serikali ni pamoja na uvuvi haramu, matumizi yasiyosahihi ya taa za kuvulia samaki, mlundikano wa tozo kwa mazao ya uvuvi na uhaba wa masoko ya mazao ya uvuvi.


Wadau walioshiriki kikao hicho ni pamoja na viongozi kutoka serikalini, wawakilishi kutoka katika Benki, wavuvi wa Dagaa, wavuvi wa Sangara, wachakataji wa mazao ya uvuvi, wawakilishi wa vyama vya ushirika,wazalishaji wa zana za uvuvi, wafanyabiashara wa taa za sola, wafanyabiashara wa mabondo na wafugaji wa samaki kwenye vizimba.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Sekta ya Uvuvi muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Viktoria kilichofanyika Mkoani Mwanza Mei 16, 2022.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na Wadau wa Sekta ya Uvuvi katika kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Viktoria kilichofanyika Mkoani Mwanza Mei 16, 2022.


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akifafanua baadhi ya mambo katika kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Viktoria kilichofanyika Mkoani Mwanza Mei 16, 2022.

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Emmanuel Bulayi akijibu hoja zilizoibuliwa na wadau wa Sekta ya Uvuvi katika kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Viktoria kilichofanyika Mkoani Mwanza Mei 16, 2022.


Mmoja wa Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Viktoria, Bw. Sospeter Kabongo akionesha moja ya taa ambazo haziruhusiwi kisheria kutumia kuvulia Samaki  na hivyo kumuomba Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki kukomesha matumizi ya taa hizo katika kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Viktoria kilichofanyika Mkoani Mwanza Mei 16, 2022.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni