Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Sekta ya Uvuvi imeanza kuandaa daftari la viashiria hatarishi katika sekta ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001 iliyofanyiwa marekebosho mwaka 2010 katika sura 348.
Akifungua warsha hiyo leo (16.05.2022) Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Bw. Amosi Machilika amesema kuwa lengo la kuandaa daftari la viashiria hatarishi ni kuiwezesha Sekta ya Uvuvi pamoja na wadau wake wanaotekeleza Sera, Mipango, Mikakati na Programu mbalimbali za kisekta kuweza kufikia Malengo yaliyokusudiwa kwa kiwango kikubwa kwa sababu viashiria hatarishi vitakuwa vimewekewa mikakati ya kudhibitiwa kabla ya kutokea na kukwamisha juhudi za Sekta.
Machilika amesema kuwa watendaji wa sekta ya uvuvi wanajukumu la kubaini viashiria hatarishi vinavyoikabili sekta, kubuni mikakati Madhubuti ya kudhibiti viashiria hivyo na kuandaa daftari la viashiria hatarishi.
Pia amesema kuwa Wakuu wa Idara na Vitengo wanao wajibu wa kuhakikisha kwamba shughuli za sekta zinatekelezwa katika maeneo wanayoyasimami kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali ya usimamizi wa fedha za umma, ununuzi, rasilimali watu, mishahara na mikataba, kwa kusimamia haya kikamilifu kutaiwezesha sekta kufikia malengo yake yaliyokusudiwa.
Vilevile Machilika amesema kuwa matarajio ya Sekta ya Uvuvi kwenye warsha hiyo ni kuwawezesha washiriki kupata uelewa mpana kuhusu viashiria hatarishi, kuvichambua kwa umakini na kuviwekea mikakati ya kuvidhibiti au kuviepuka ili kufikia malengo ya Sekta ya Uvuvi.
Aidha, Machilika amesema kuwa Sekta ya Uvuvi imekuwa kwa asilimia 2.5 ambapo mchango wa Sekta ya Uvuvi kwenye Pato la Taifa ni asilimia 1.8 ikilinganishwa na asilimia 1.7 ya mwaka 2020. Ongezeko hilo limetokana na usimamizi Madhubuti wa shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji. Hivyo sekta ya uvuvi imemamua kuandaa kitabu kitakachosaidia kubaini viashiria hatarishi sna kuvifanyia kazi ili kuyafikia malengo yaliyowekwa.
Naye Msaidizi wa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Abraham Msechu amesema kuwa uwepo wa daftari la viashiria hatarishi una faida zake lakini seta ya uvuvi inatakiwa kuhakikisha inalitumia daftari hilo na sio kuishia kwenye kuliandaa.
Akizungumza kabla ya kufunguliwa kwa warsha hiyo, Mkaguzi Mkuu wa Ndani Sekta ya Uvuvi, Costantino Nyilawila alisema kuwa warsha hiyo imeandaliwa kwa ajili ya kuandaa daftari ambalo litasaidia kubaini viashiria hatarishi na kuweka mikakati ya kukabiliana navyo ikiwa ni pamoja na kuvidhibiti.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni