Na Mbaraka Kambona,
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imezindua zoezi la uuzaji wa madume bora ya ng'ombe aina ya Borani ili kuwawezesha Wafugaji nchini kuboresha mifugo yao ili iwe na tija zaidi kuliko hivi sasa ambapo wengi wana makundi makubwa ya ng'ombe huku tija yake ikiwa ni ndogo.
Hafla fupi ya uzinduzi wa zoezi hilo la uuzaji wa madume bora ya ng'ombe aina ya Borani ilifanyika katika Ranchi ya Kongwa iliyopo Wilayani Kongwa, jijini Dodoma Mei 21, 2022.
Wakati akizindua zoezi hilo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi alisema anaimani kuwa uuzaji wa madume hayo bora kutasaidia wafugaji wengi kupata mbegu bora itakayosaidia kuboresha ufugaji wao.
Alisema kuwa wafugaji ni vyema kutumia fursa hiyo vizuri na kuchangamkia madume hayo huku akiwataka kuamini kuwa na mifugo michache iliyobora ndio utajiri kuliko kuwa na kundi kubwa la ng'ombe ambalo tija yake ni ndogo.
Aliendelea kuwakumbusha wafugaji kuwa wakiendelea kuamini kuwa na makundi makubwa ya ng'ombe ndio ufahari jambo hilo halitawasaidia kwa sababu hali ya mabadiliko ya tabia nchi hairuhusu hilo lakini pia hakuna ardhi ya kutosha ya kumuwezesha kila mfugaji kuwa na kundi kubwa la mifugo.
"Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametupa kazi ya kuhakikisha kwamba ng'ombe hawa wanakuwa na tija na kumsaidia mtanzania kuongeza kipato chake na kuchangia kwa sehemu kubwa katika pato la nchi yetu", alisema
Hivyo, aliitaka Kampuni ya NARCO kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu na kuendelea kuuza madume bora mengi kwa bei nzuri ili wafugaji wengi waweze kuyapata kwa urahisi madume hayo na kuboresha mifugo yao.
"Sasa muanze kufikiria namna ambavyo mtazalisha madume haya kwa wingi ili muwe mnayauza kila baada ya miezi sita na tukifanikiwa kufanya hivyo mabadiliko kwa wafugaji wetu yatakwenda kwa haraka sana ," alisisitiza
Waziri Ndaki aliongeza kwa kusema kuwa Serikali imedhamiria kuboresha mifugo ili wafugaji wanufaike na mifugo yao kwa kupata masoko ya uhakika ya kuuza mifugo yao na mazao yake ndani na nje ya nchi.
Aidha, alisema kuwa Serikali imepanga kufanya kampeni kubwa ya uhimilishaji wa mifugo itakayofikia wafugaji wote nchini ili wapate mifugo itakayokuwa na tija katika maisha yao na nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe alisema wameanza kuuza madume 197 kutoka katika Ranchi za Kongwa, West Kilimanjaro na Kalambo na yote wamelenga yauzwe kwa wananchi ili waweze kuboresha mifugo yao.
Alisema madume hayo ya Borani yanafaa sana kwa ajili ya uzalishaji wa nyama huku akisema kuwa dume mmoja anaweza kuzalisha majike mpaka hamsini hivyo kupitia madume hayo itaongeza idadi kubwa ya ng'ombe bora kwa wafugaji.
"Dume wa miaka 2 ambaye atakupa huduma kwa zaidi ya miaka 10 atauzwa kwa shilingi Milioni 3 na dume wa miaka 3 na kuendelea atauzwa kwa shilingi Milioni 3.5", alisema
Naye Mwenyekiti wa Wafugaji wa Wilaya ya Kongwa, Mshando Parutu alisema kuwa hatua hiyo iliyochukuliwa na NARCO ni muhimu kwa mustakabali wa wafugaji nchini huku akiwaomba Wafugaji kuchangamkia fursa hiyo ili kuboresha namna ya ufugaji wao.
Mmoja wa Wafugaji aliyenunua ng'ombe hao, Ibrahim Matiko alisema kuwa kilichomvutia kununua ng'ombe hao ni kuwa kupitia madume hayo ya Borani atapata mbegu iliyobora itakayosaidia kubadilisha mifugo yake ya asili kuwa ya kisasa yenye tija kubwa zaidi.
Baadhi ya Wafugaji waliohudhuria hafla fupi ya uzinduzi wa uuzaji wa madume bora ya ng'ombe aina ya Borani wakikagua ng'ombe hao ambao wanauzwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kwa bei ya kuanzia shilingi Milioni 3 hadi Milioni 3.5. Zoezi hilo la kuuza madume kwa mtindo huo linatajwa kuwa ndio la kwanza tangu kampuni hiyo ianze kazi hapa nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni