Nav bar

Ijumaa, 27 Januari 2023

​WAFUGAJI WANAOVAMIA MASHAMBA YA WAKULIMA NI WAHALIFU WASHUGHULIKIWE - NDAKI

Kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wakulima kwenye mikutano ya hadhara aliyoifanya jana (26.01.2023) kwenye kata za Ulaya na Mbwade Wilayani Kilosa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameagiza wafugaji wote wanaovamia mashamba ya wakulima hao wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria.


Mhe. Ndaki amesema kuwa pamoja na kuwa ufugaji ni shughuli halali kama zilivyo nyingine, inapaswa kufanyika kwa kufuata taratibu na sheria bila kuathiri watumiaji wengine wa ardhi.


"Yaani mkulima amelima mazao yake afu kwa makusudi mfugaji anaenda kulisha mifugo yake, huo ni uhalifu na matukio ya aina hii yakithibitishwa kuwa ni kweli basi naomba Mwenyekiti wa Chama cha wafugaji usihangaike hata kunipigia simu kwa sababu na mimi ntasisitiza watu hao wachukuliwe hatua za kisheria" Amesisitiza Mhe. Ndaki.


Aidha Mhe. Ndaki ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Kilosa kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya Sheria wataalam wote wanaopokea rushwa ili kuchochea migogoro hiyo ya wakulima na wafugaji.


"Lakini pia changamoto nayoiona hapa ni wafugaji kutoainishiwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho hivyo ninawaagiza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa mkakae na watu wenu ili muainishe na kuorodhesha maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo na kuyawasilisha ofisini kwangu ili yatangazwe kwenye gazeti la Serikali na hatimaye kurasimishwa rasmi.


Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kilosa Mhe. Palamagamba Kabudi ameishukuru Serikali kwa kuwatengea fedha za kuanzisha mashamba darasa 3 ya malisho ya mifugo ambapo ameongeza kuwa yatawasaidia kuondokana na changamoto ya ukosefu wa malisho ya mifugo hasa msimu wa kiangazi.


"Lakini jambo la pili Wilaya yetu mbali na kuwa na wafugaji ina wafugaji wanaofanya kilimo pia hivyo naomba Wizara iwasaidie hasa kwenye eneo la ugani kwa sababu idadi yao haiendani na wataalam wa ugani waliopo " Amesema Mhe. Kabudi. 


Awali mmoja wa Wakulima walioshiriki kwenye Mkutano huo Bw. Omary Walii alisema kuwa kumekuwa na kiwango cha ongezeko la uvamizi wa wafugaji kwenye maeneo ya wakulima huku akibainisha uharibifu unaofanywa na wafugaji wa kata ya Mbwade kwenye skimu ya umwagiliaji iliyopo kwenye kijiji cha Chanzulu.


Akizungumzia hoja hiyo, mmoja wa wafugaji wa kijiji cha Mbwade Bw. Sozia Zakayo amesema kuwa sababu kubwa inayowafanya kuingia kwenye maeneo ya wakulima ni hali ya mabadiliko ya tabia nchi ambayo inaiathiri mifugo yao hasa kwenye upande wa maji ambapo alimuomba Mhe. Ndaki kuwajengea lambo litakalowatosheleza kupata huduma ya maji wakati wote wa msimu wa kiangazi.


Ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki Mkoani Morogoro inaendelea tena leo ambapo atafanya mkutano na wananchi wa Wilaya ya Kilombero huku lengo la Ziara hiyo likiwa ni kuhamasisha utekelezaji wa Mwelekeo mpya wa sekta ya Mifugo kupitia Mpango wa mabadiliko wa Sekta hiyo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa tatu kutoka kulia) akiongozana na wafugaji wa kijiji cha Mbwade kwenda kukagua shamba darasa la malisho lililopo kijijini hapo muda mfupi baada ya kuwasili katika eneo hilo lililopo Kilosa mkoani Morogoro jana (26.01.2023)

Sehemu ya wananchi wa Kata ya Ulaya iliyopo Kilosa Mkoani Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati wa Mkutano baina yao jana (26.01.2023).

Sehemu ya wananchi wa Kata ya Ulaya iliyopo Kilosa Mkoani Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati wa Mkutano baina yao jana (26.01.2023).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni