Na. Edward Kondela
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewekeza Shilingi Bilioni 60 katika Sekta ya Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2022-2023 ili kuinua kipato cha wananchi kupitia sekta hiyo.
Akizungumza jijini Mwanza (26.01.2023) kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah wakati wa ujio wa mabalozi nane kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya kwenye Kampasi ya Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA), Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Prof. Mohammed Sheikh amesema fedha hizo zimewekezwa kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kwa kununua boti na wavuvi wadogo waweze kufika kwenye maji ya kina kirefu kuvua samaki ili kuongeza kipato.
Prof. Sheikh amebainisha hayo baada ya ziara ya siku moja ya mabalozi hao katika Kampasi ya FETA iliyopo katika Kata ya Nyegezi, Wilaya ya Nyamagana ili kushuhudia majukumu mbalimbali ya FETA na mradi wa ufugaji samaki wanaoufadhili.
Ameongeza kuwa ujio wa mabalozi hao ni wa kawaida ili kujionea namna utekelezaji wa miradi hiyo ambayo wanashirikiana na serikali ili kuwaondoa wavuvi katika uvuvi wa kutumia zana za zamani za uvuvi na kutumia njia ya vizimba kwa kufuga samaki wengi na kujipatia kipato zaidi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) Dkt. Semvua Mzighani amesema ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba unakua kwa kasi na serikali imewekeza pesa, hivyo FETA inawashauri vijana kuchangamkia fursa kupitia Ziwa Victoria.
Dkt. Mzighani ameongeza kuwa FETA inatoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi na kuwashauri wanaohitaji kujifunza namna ya kufuga samaki kwa njia ya vizimba kujiunga na FETA kwenye mafunzo ya muda mfupi ili kujifunza jinsi ya kutengeneza vizimba, namna ya kuviweka ziwani, kupata mbegu bora za samaki, namna ya kukuza samaki na kuwahifadhi ili wasiharibike baada ya kuwavua.
Amefafanua kuwa kumekuwa na muitikio mkubwa wa watu kujifunza namna ya kufuga samaki kupitia vizimba na tayari wapo ambao wameanza kuwekeza kwenye Ziwa Victoria lakini anawasihi watu wengi zaidi kujitokeza hususan vijana kuchangamkia fursa hiyo.
Naye mmoja wa wafugaji samaki kwa njia ya vizimba katika Ziwa Victoria ambaye amepata elimu FETA Bw. Mpanju Elpidius amewaasa vijana wenzake kuchangamkia fursa hiyo kwa kuanza na kidogo walichonacho ili waweze kufikia malengo yao.
Ameipongeza serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutenga fedha ya kuwakopesha vijana kwa masharti nafuu ili kufuga samaki kwa njia ya vizimba na kuziomba benki zilizopo nchini kuiga mfano wa serikali kwa kuwaamini vijana na kuwakopesha kwa masharti nafuu ili kuwekeza kwenye fursa mbalimbali ikiwemo ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba.
Baadhi ya mabalozi kutoka nchi za ulaya waliotembelea miradi inayotekelezwa na FETA ukiwemo wa utoaji elimu ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba kwenye Ziwa Victoria, wamesema wameridhishwa na namna fedha walizowekeza zinavyotumika na kuhamasisha vijana kujitokeza kwa wingi na kuiomba serikali kuwasimamia ili waweze kutumia fedha hiyo kwa malengo yanayotarajiwa.
Umoja wa Nchi za Ulaya umewekeza Shilingi Milioni 800 kwa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA), kwa ajili ya kukuza Sekta ya Uvuvi kupitia ufugaji samaki ambapo wanawekeza kwenye miundombinu, mitaala na kuwawezesha wakufunzi kupata elimu zaidi kwenye ukuzaji viumbemaji kwa njia ya kisasa katika kipindi cha miaka minne ambapo hadi sasa mradi huo umetekelezwa kwa miaka miwili ili kuvutia tasnia ya ufugaji samaki.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Prof. Mohammed Sheikh (wa kwanza kulia), akizungumza na mmoja wa mabalozi kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya waliotembelea Kampasi ya Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) iliyopo Kata ya Nyegezi jijini Mwanza, kushuhudia majukumu mbalimbali ya FETA na mradi wa ufugaji samaki wanaoufadhili. Kulia kwa Prof. Sheikh ni Mtendaji Mkuu wa FETA Dkt. Semvua Mzighani. (26.01.2023)
Mabalozi nane kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya wakikagua shughuli za ufugaji samaki katika Kampasi ya Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) iliyopo Kata ya Nyegezi jijini Mwanza, wakati wakikagua miradi mbalimbali ya Sekta ya Uvuvi wanayoifadhili hapa nchini kupitia FETA. (26.01.2023)
Mabalozi nane kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya wakishuka kutoka kwenye boti baada ya kushuhudia mradi wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba kwenye Ziwa Victoria jijini Mwanza, ambao ni moja ya miradi inayofadhiliwa na umoja huo hapa nchini kupitia Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA). (26.01.2023)
Baadhi ya mabalozi kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya na watumishi wa Jeshi la Polisi nchini wakishuhudia njia mojawapo ya ukaushaji samaki kwenye vichanja, wakati wa ziara ya siku moja ya mabalozi nane kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya waliotembelea Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Nyegezi jijini Mwanza kujionea miradi wanayoifadhili kupitia wakala hiyo hapa nchini yenye thamani ya Shilingi Milioni 800 kwa miaka minne ambapo hadi sasa utekelezaji wake umefikia miaka miwili. (26.01.2023)
Picha ya pamoja ya mabalozi nane kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya na baadhi ya wafanyakazi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo wakati wa ziara ya siku moja ya mabalozi hao jijini Mwanza kutembelea miradi inayofadhiliwa na umoja huo hapa nchini katika Sekta ya Uvuvi kupitia Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA). (26.01.2023)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni