Nav bar

Jumatano, 21 Desemba 2022

WAWEKEZAJI WATAKIWA KUTOA FURSA ZA AJIRA KWA WAZAWA

Na Mbaraka Kambona, Pwani

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wawekezaji katika sekta ya mifugo kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira kwa vijana ili waweze kufaidika moja kwa moja na uwekezaji wao unaofanyika hapa nchini.

Waziri Ndaki alitoa kauli hiyo wakati akizindua rasmi ujenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL) unaofanyika katika Kata ya Vigwaza, Halmashauri ya Chalinze, mkoani Pwani Disemba 15, 2022.

Alisema ni muhimu sana kwa wawekezaji kutoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi wenye ujuzi na hata wale wasio na ujuzi wakafikiriwe kupewa fursa za ajira ndogo ndogo ili waweze kufaidika na uwekezaji unaoendelea kufanyika katika sekta ya mifugo.

"Ndugu zangu, kiwanda hiki kipo miongoni mwa watu hapa Vigwaza, ni wazi kuwa wananchi watakuwa na matumaini kutokana na uwepo wa  kiwanda hiki, naamini mtawapa kipaumbele mtakapoanza uzalishaji wenu, nimeambiwa mtaajiri watu 1500 na kuna watu 300 pia watapata ajira ambazo sio za moja kwa moja, niwaombe sana mtilie maanani watu wa hapa kwa wenye ujuzi na hata wale ambao hawana ujuzi,"  alisema Ndaki

Aidha, Mhe. Ndaki aliwakumbusha  wawekezaji hao kuzingatia wajibu kwa jamii, kwa maana kufanya shughuli za maendeleo kwa jamii inayowazunguka ili wananchi waone faida ya uwepo wa uwekezaji katika maeneo yao.

"Mtakapoanza uzalishaji niwaombe mfikirie pia wajibu kwa jamii, baada ya kupata faida mrudishe  kwa jamii inayowazunguka hapa, muangalie mahitaji ya jamii inayowazunguka na mkatoa mchango wenu katika kutatua changamoto za wananchi,"aliongeza Ndaki

Halikadhalika, aliwataka wananchi na wafugaji kwa ujumla kutumia fursa ya uwepo wa kiwanda hicho kujiongezea kipato ikiwemo kunenepesha mifugo yao ili waweze kuuza katika kiwanda hicho.

Kiwanda hicho kitapokamilika na kuanza uzalishaji kitakuwa na uwezo wa kuchinja Ng'ombe 2000, Mbuzi na Kondoo  7000 kwa siku.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) akipiga makofi baada ya kuzindua rasmi ujenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL) unaofanyika Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 15, 2022. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL), Bi. Mariam Ng'hwani.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akisalimiana na Mbunge wa Chalinze, ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwan Kikwete(katikati) muda mfupi baada ya kufika katika eneo linalojengwa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL) lililopo Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 15, 2022.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na Wananchi walishiriki katika hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL) uliofanyika Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 15, 2022. Kiwanda hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuchinja Ng'ombe 2000 kwa siku.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL), Bi. Mariam Ng'hwani (kushoto) akimueleza jambo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kulia) alipokuwa akikagua eneo la ujenzi wa kiwanda hicho kinachojengwa  Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 15, 2022.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Meat Abattoirs Limited (UMAL), Bi. Mariam Ng'hwani (kushoto) akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) sehemu ambayo kiwanda hicho kinajengwa alipokuwa akikagua shughuli za ujenzi alipotembelea eneo la ujenzi Disemba 15, 2022.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Nyama na Machinjio ya Kisasa cha Union Abattoirs Limited (UMAL), Bi. Mariam Ng'hwani akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki ramani ya ujenzi wa kiwanda hicho muda mfupi baada ya kufika katika eneo la ujenzi lililopo Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 15, 2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni