Nav bar

Ijumaa, 23 Desemba 2022

MABORESHO YA MWONGOZO WA UWEKEJI HERENI YATAMFIKIA KILA MDAU-NDAKI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.  Mashimba Ndaki amebainisha kuwa Wizara yake inaendelea kufanya maboresho ya Mwongozo unaosimamia zoezi la uwekaji wa hereni za kielektroniki kwenye mifugo ili kufanya zoezi hilo kuwa shirikishi kwa pande zote zinazohusiana na sekta ya ufugaji.


Mhe. Ndaki ameyasema hayo jana (20.12.2022) wakati akifunga mkutano wa Wadau wa sekta ya Mifugo uliofanyika kwa siku mbili kwenye jengo la PSSSF, Makole jijini Dodoma ambapo amebainisha kuwa mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuboresha mwongozo huo utakabidhiwa kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu ili atoe hatma ya zoezi hilo.


“Kwenye maboresho ya mwongozo huu tutamfikia kila mdau anayehusika na sekta ya mifugo kwa nafasi yake ili baada ya kukamilika kwake kusiwe na malalamiko ya baadhi ya wadau kutoshirikishwa” Amesisitiza Mhe. Ndaki.


Mhe. Ndaki ametoa rai kwa wafugaji wote walioshiriki kwenye mkutano huo kuwafikishia wafugaji wenzao elimu waliyoipata kupitia mada mbalimbali zilizowasilishwa wakati wote wa mkutano huo ili waweze kutekeleza kwa pamoja maazimio yaliyofikiwa.


“Ni lazima wote kwa pamoja tuelewe sekta ya Mifugo inapaswa kwenda kwenye mwelekeo mpya, hatuwezi kuwa walewale kwa sababu tunalazimishwa kubadilika sasa hivi kwa namna yoyote ile kutokana na mazingira tuliyopo, mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la watu” Amesema Mhe. Ndaki.


Akizungumzia kuhusu marufuku ya uingizwaji wa vifaranga vya kuku kutoka nje, Mhe. Ndaki amesema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo ili kuwalinda wawekezaji na wafanyaiashara wa ndani ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan zinazolenga kuongeza idadi ya wawekezaji nchini.


“Lakini natoa rai kweu mhakikishe mnaboresha mazao yenu ili yawe shindani kwenye masoko ya ndani na nje kwa sababu hivi sasa tupo kwenye ushirikiano wa Afrika Mashariki na hivi karibuni tutaingia kwenye sarafu moja hivyo ni lazima mjipange” Ameongeza Mhe. Ndaki.


Akizungumzia ubora wa nyama inayozalishwa hapa nchini na namna inavyokubalika katika masoko ya nje, Mkurugenzi wa Kiwanda cha kusindika nyama cha Eliya kilichopo mkoani Arusha Bw. Irfhan Virjee amesema kuwa kwa sasa nyama inayozalishwa hapa nchini na kusafirishwa kwenye masoko ya nje ina ubora na kuhitajika hasa kwenye soko la nchi za falme za kiarabu  kiasi cha kushindwa kukidhi mahitaji ya soko hilo.


Naye Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la kimataifa la Heifer ambao ni moja wa wadau wakubwa kwenye sekta ya Mifugo nchini Bw. Mark Tsoxo amesema kuwa ili kufanikisha  mwelekeo mpya wa sekta ya Mifugo ni lazima Serikali na wadau wote kufanya mabadiliko ya teknolojia na mifumo inayoratibu sekta hiyo.  


“Jambo jingine ni muhimu kuhakikisha kwenye mwelekeo huu mpya wa sekta ya Mifugo tunawajumuisha kwa kiasi kikubwa vijana ambao wanakadiriwa kufikia asilimia 31 ya idadi ya watu wote nchini  na wanawake ambao ni asilimia 51 ya idadi ya watu wote waliopo nchini, kinyume na hapo tutatengeneza changamoto kubwa wakati tukitekeleza mwelekeo huu” Amesisitiza Bw. Tsoxo.


Mkutano huo wa wadau wa sekta ya Mifugo ulifunguliwa Disemba 19 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambapo wadau mbalimbali walioshiriki mkutano huo walifanikiwa kutoa maoni mbalimbali yaliyolenga kutekeleza kauli mbiu ya Mkutano huo ya “ Mwelekeo Mpya wa Sekta ya Mifugo nchini”

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda akifafanua moja ya maazimio yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa wadau wa sekta ya Mifugo uliofanyika Disemba 19-20, 2022 kwenye jengo la PSSSF Makole, jijini Dodoma.


Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Mbaraka Stambuli akisoma maazimio yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa wadau wa sekta ya Mifugo uliofanyika Disemba 19-20, 2022 kwenye jengo la PSSSF Makole, jijini Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni