Nav bar

Jumanne, 27 Desemba 2022

VIFARANGA 62,730 VYAZUILIWA KUINGIA NCHINI

Na Mbaraka Kambona,


Wakaguzi wa Mifugo na Mazao yake kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi walio katika kituo cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wamevizuia vifaranga vya kuku wa mayai 62,730 ambavyo ni mali ya Kampuni ya Phoenix Farms Limited ya Mkuranga, Pwani vilivyofikishwa uwanjani hapo vikitokea nchini Ubeligiji bila ya kuwa na vibali.


Akitoa taarifa ya zuio la vifaranga hivyo wakati akiongea na Waandishi wa Habari jijini Disemba 24, 2022, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga alisema Vifaranga hivyo vilivyowekwa kwenye makasha 697, stakabadhi yake ya mauziano  ya mzigo inaonesha vina gharama ya shilingi 200,262,706.


“Mkurugenzi wa Kampuni pamoja na Wakala wa Mmiliki wa vifaranga hivyo walikiri kutokuwa na kibali cha kuingiza vifaranga hivyo na kwa msingi huo amevunja Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Sura ya 156 na Kanuni za Udhibiti wa Usafirishaji wa Wanyama na Mazao yake ya GN. Na. 28/2007,” alisema Prof. Nonga


Alisema kutokana na tafsiri hiyo vifaranga hivyo vimezuiliwa kuingizwa nchini kwa kuwa ni mzigo hatarishi huku akifafanua kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeutaka uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Tawi la Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam kuielekeza Kampuni ya Phoenix Farms Limited kuvirudisha vifaranga hivyo nchini Ubeligiji kwa sababu vinaweza kuhatarisha usalama wa kuku hapa nchini.


“Vilevile, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kampuni ya Phoenix Farms Limited tunamuelekeza kuviondosha vifaranga hivyo katika maeneo ya uwanja wa ndege na kuvirudisha alikovitoa,”aliongeza


Aidha, alisema kuwa Mwaka 2006 Tanzania iliweka zuio la uingizaji wa kuku na mazao yake kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege duniani na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa salama dhidi ya ugonjwa huo ambao umeathiri nchi nyingi duniani.


Pof. Nonga alitoa wito kwa watanzania wote hususan wadau wa kuku kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo ya kudhibiti kuingia na kuenea kwa magonjwa ya kuku nchini hususan Ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege ili kulinda usalama wa kuku, na ndege wengine pamoja na afya ya jamii ya watanzania kwa ujumla.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga akiwaonesha Waandishi wa habari (hawapo pichani) makasha  yaliyotumiwa kubebea vifaranga 62,730 vilivyoingizwa nchini bila kibali. Akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, Prof. Nonga alitoa tamko la kuzuia vifaranga hivyo visiingie nchini Disemba 24, 2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni