Na Mbaraka Kambona, Kigoma
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba
Ndaki ameielekeza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kutenga Ekari Elfu Kumi na
Tano (15000) na wazigawe kwa Wananchi wa Vijiji viwili vya Mpeta na Chakulu
vilivyopo Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma ili kutatua mgogoro wa ardhi wa muda
mrefu baina ya wananchi hao na Kampuni hiyo.
Ndaki alitoa maelekezo hayo Aprili 25,
2021 katika ziara yake Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma kwa lengo kutatua mgogoro
huo wa ardhi kufuatia wananchi wa vijiji hivyo kuvamia maeneo ya Ranchi ya Uvinza
na kuishi humo kinyume na taratibu.
Akiongea na wananchi wa vijiji hivyo
kwa nyakati tofauti, Waziri Ndaki alisema kuwa Serikali imeamua kufikia maamuzi
hayo ili wananchi hao waweze kujikita katika shughuli za maendeleo na kuachana
na migogoro ya kila siku ambayo haina tija yoyote.
“Hatupendi tuendelee na migogoro kwenye
maeneo yetu, tunataka tumalize migogoro ili tuanze kufanya shughuli za
maendeleo, kila mwananchi afanye shughuli yake bila bughudha yoyote,” alisema
Ndaki
Aliongeza kuwa baada ya ugawaji wa
maeneo hayo kukamilika Mkuu wa Wilaya ya Uvinza na timu yake watakwenda kufanya
tathmini katika maeneo hayo na kuyafanyia mchakato wa kuyarasimisha ili kuwa
Kijiji au Kitongozi.
Alisisitiza kuwa pamoja na wananchi hao
kuvunja Sheria, Serikali imeangalia maslahi mapana na ndio maana imeamua kutoa
sehemu ya eneo katika ranchi hiyo ili wananchi hao waweze kuishi kwa utulivu na
kuendelea na shughuli zao huku akiwaonya kuwa wasijaribu tena kuingia katika
ranchi hiyo baada ya kugawa ekari hizo na atakayefanya hivyo anatafuta kesi.
“Ranchi ni eneo la kufugia mifugo na
sio eneo la kuishi watu au kulima humo, atakayejaribu kuingia tena ananitafuta
kesi, tumewapa maeneo hayo ili mkae humo, atakayetaka kufuga aje sisi tutampa
eneo la kukodisha kwa bei ya Serikali ili aweze kufuga kisasa, kulima malisho
na kuongeza tija ya mifugo yake,” alisisitiza Ndaki
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mwanamvua
Mrindoko baada ya kumshukuru Waziri Ndaki kwa uamuzi huo naye aliwasisitiza
wananchi hao kutoendelea kuvamia maeneo ya ranchi hiyo ili kuepukana na
migogoro isiyo na tija na badala yake watumie maeneo hayo waliyopewa kujiletea
maendeleo yao.
Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chakulu, Mohamed Baswage aliishukuru Serikali kwa tamko hilo la kuwapa eneo wananchi wa Kijiji hicho huku akisema kuwa uamuzi huo utawasaidia wao kusukuma maendeleo yao kwa pamoja wakishirikiana na Serikali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni